Msukuma Asimulia Ndejembi Alivyopokea Taarifa za Uteuzi wa Makamu wa Rais – Video

Global Publishers
August 28, 2026
870 views
0 Comments

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku ‘Msukuma’, amesimulia namna Deogratius Ndejembi alivyopokea taarifa za kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Msukuma ametoa simulizi hiyo wakati akizungumza kuhusu uteuzi wa Ndejembi, ambaye Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemteua na kumpendekeza kushika nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa Msukuma, namna Ndejembi alivyopokea taarifa hizo inaonyesha hali aliyokuwa nayo baada ya kupata taarifa za uteuzi huo.

Ndejembi amependekezwa kushika nafasi hiyo baada ya mchakato uliofanywa na CCM, huku hatua inayofuata ikiwa ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupokea na kuthibitisha uteuzi huo kwa mujibu wa Katiba.

Jamhuri Yakamilisha Kumuhoji Lissu Katika Kesi ya Uhaini Leo – Video

Upande wa mashtaka, Jamhuri, umekamilisha zoezi la maswali ya dodoso (cross-examination) kwa shahidi wa kwanza ambaye pia ni mshtakiwa katika kesi ya uhaini, Tundu Lissu.

Zoezi hilo limekamilika leo, Agosti 28, 2026, baada ya Jopo la Majaji kuruhusu upande wa Jamhuri kuendelea na maswali hayo.

Katika swali la mwisho, Wakili wa Serikali Mkuu alimuuliza Lissu iwapo ni kweli au si kweli kwamba nia ya kutenda kosa inathibitishwa na tendo husika. Lissu aliomba ufafanuzi iwapo swali hilo lilihusu nia ya kuthibitisha tendo la uhaini, kabla ya wakili huyo kueleza kuwa alikuwa akiuliza kuhusu tendo lolote na si uhaini pekee.

Baada ya Lissu kujibu, “Si kweli,” Wakili wa Serikali Mkuu aliieleza Mahakama kuwa upande wa Jamhuri umemaliza maswali ya dodoso kwa shahidi huyo.

Baada ya hapo, upande wa Jamhuri uliomba mwongozo wa Mahakama kuhusu namna hatua ya maswali ya ufafanuzi (re-examination) itakavyoendeshwa, kwa kuzingatia kuwa Lissu anajiwakilisha mwenyewe katika kesi hiyo.

Jamhuri ilieleza kuwa kuna haja ya kuweka mwongozo kuhusu namna Lissu atakavyofanya maswali ya ufafanuzi kutokana na majibu aliyoyatoa wakati wa cross-examination, bila kukiuka misingi ya kisheria.

Upande wa Jamhuri ulipendekeza kuwa Lissu aruhusiwe kutoa ufafanuzi katika mambo ambayo yanaweza kuwa na maana zaidi ya moja.

Kwa upande wake, kabla ya kujibu hoja hiyo, Lissu alitaka Jamhuri iweke wazi iwapo suala hilo lilikuwa pingamizi rasmi au ni mapendekezo na ushauri kwa Mahakama.

Baada ya Wakili wa Serikali kufafanua kuwa hawajaweka pingamizi bali wanaomba mwongozo wa Mahakama, Lissu alisisitiza kuwa haki ya kufanyiwa maswali ya dodoso ni ya kisheria chini ya Kifungu cha 156(1) cha Sheria ya Ushahidi, na kwamba kujiwakilisha mwenyewe hakuwezi kumnyima haki hiyo.

Lissu pia alieleza kuwa hofu ya Jamhuri kwamba anaweza kuibua mambo mapya haina msingi, akisema upande wa mashtaka una haki ya kuweka pingamizi wakati wowote atakapovuka mipaka ya maswali ya ufafanuzi.

Akitoa mwelekeo wa Mahakama, Jaji Dunstan Ndunguru alisema jambo la msingi ni kuangalia wigo na mipaka ya dodoso.

Katika maswali ya awali, Jamhuri ilimuuliza Lissu kuhusu maeneo mbalimbali ya ushahidi wake, ikiwemo madai yake kwamba baadhi ya mashahidi wa Jamhuri walitoa ushahidi unaokinzana kwa maelezo na maandishi.

Pia aliulizwa iwapo, baada ya matukio mbalimbali yaliyompata, ikiwemo kushambuliwa kwa risasi, aliwahi kutoa taarifa polisi. Lissu alijibu kuwa alishatoa taarifa na kwamba hakuna hatua iliyochukuliwa.

Lissu anakabiliwa na mashtaka ya uhaini, chini ya Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code), Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania.

Mafuriko Yaua Watu 100 Nepal, Zaidi ya 1500 Hawajulikani Walipo

Shechambo Chris
August 28, 2026
12 views
0 Comments

 

Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na mafuriko makubwa yaliotokea nchini Nepal imefikia 165, huku wengine 1,300 bado hawajulikani walipo,  mafuriko hayo yamesababisha uharibifu mkubwa katika maeneo ya mpakani mwa Nepal na China.

Mafuriko hayo yalitokea Jumatano, Agosti 26, yakisababisha vifo, uharibifu wa miundombinu na kutoweka kwa mamia ya watu katika maeneo yaliyoathirika. Vifo vingine vitatu pia vimeripotiwa upande wa Tibet, China.

Janga hilo lilisababishwa na kuporomoka kwa barafu kubwa kutoka kwenye milima ya Himalaya, na kusababisha maji mengi, vipande vya barafu, mawe na matope kusukumwa kwa nguvu kuelekea kwenye mfumo wa mito na kuvamia maeneo ya makazi.

Utafiti wa Jiolojia wa Marekani (USGS) umeeleza kuwa ishara ya awali ya mtikisiko iliyodhaniwa kuwa ni tetemeko la ardhi haikusababishwa na tetemeko, bali ilitokana na kuporomoka kwa barafu pamoja na mabaki ya miamba na udongo.

Mafuriko hayo yamesababisha uharibifu mkubwa wa nyumba, barabara na madaraja, huku baadhi ya maeneo yaliyoathirika yakibaki kuwa magumu kufikika kutokana na miundombinu kuharibiwa.

 

Timu za uokoaji zimeendelea na operesheni za kuwatafuta manusura na watu waliopotea kwa kutumia helikopta, ndege zisizo na rubani (drones), mbwa maalumu wa utafutaji na vifaa vingine vya dharura.

Mamlaka zimeripoti kuwa  madaraja 19 na takribani kilomita 40 za barabara zimesombwa na maji nchini Nepal, hali inayozidi kufanya shughuli za uokoaji kuwa ngumu.

Waokoaji wanaendelea na juhudi za utafutaji katika maeneo mbalimbali, huku mamlaka zikionya kuwa idadi ya waliofariki inaweza kuongezeka kutokana na uwepo wa watu wengi ambao bado hawajulikani walipo.



WAZIRI MKUU: NDEJEMBI ANATOSHA KUMSAIDIA RAIS

 

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Mchemba, amewaomba wabunge kuunga mkono na kuthibitisha uteuzi wa Deogratius Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akisema ana sifa na uzoefu unaomwezesha kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza majukumu ya Serikali.

Dkt. Mwigulu amesema Ndejembi ana sifa zote muhimu za kushika nafasi hiyo, akieleza kuwa majukumu ya Makamu wa Rais yanahitaji mtu mwenye busara, mchapa kazi na anayefahamu mwenendo wa Serikali pamoja na mahitaji ya wananchi.

“Sina shaka kwamba tumepata mtu sahihi wa kumsaidia Rais katika majukumu ya kuendesha Serikali,” amesema Dkt. Mwigulu.

Amesema kwa kuzingatia Ibara ya 47(1) ya Katiba, Makamu wa Rais ndiye Msaidizi Mkuu wa Rais katika mambo yote ya Jamhuri ya Muungano kwa ujumla, huku Ibara ya 47(8) ikieleza kuwa Makamu wa Rais hutekeleza madaraka yake chini ya uongozi na usimamizi wa Rais na kuwajibika kwa mambo anayokabidhiwa.

Dkt. Mwigulu amesema Ndejembi si mgeni katikaChama Cha Mapinduzi

(CCM), huku akieleza kuwa tangu aingie Bungeni mwaka 2020 kama Mbunge wa Chamwino, ameendelea kuaminiwa katika majukumu mbalimbali. 

Amesema katika kipindi ambacho amefanya kazi serikalini, Ndejembi ambaye pia ana elimu nzuri, amepata uzoefu katika sekta mbalimbali zenye majukumu muhimu ya kitaifa, pamoja na uzoefu wa uwakilishi wa wananchi.

“Kwa kuzingatia sifa na uzoefu wake mpana wa mfumo wa Serikali na mahitaji ya wananchi, naamini anatosha kuwa Msaidizi muhimu wa Rais,” amesema Waziri Mkuu. 

Waziri Mkuu ametoa ombi hilo wakati wa mchakato wa Bunge kuthibitisha uteuzi wa Makamu wa Rais mpya kwa mujibu wa Ibara ya 50(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Ibara hiyo inaweka utaratibu wa Rais kumteua mtu mwingine kuwa Makamu wa Rais pale nafasi hiyo inapokuwa wazi, na uteuzi huo kuthibitishwa na Bunge.

UEFA Yaandaa Kesi ya Jinai Dhidi ya Infantino, Mashabiki Wamlipua

Global Publishers
August 28, 2026
66 views
0 Comments

Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) linajiandaa kuanzisha mchakato wa kisheria nchini Uswisi dhidi ya Rais wa FIFA, Gianni Infantino, kwa tuhuma za usimamizi mbaya wa fedha, huku mashabiki wakimzomea na kumtukana wakati akiwakabidhi kombe washindi wa mashindano nchini Vietnam.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nyaraka za kisheria zinaonyesha kuwa UEFA pamoja na wahusika wengine wanajiandaa kuwasilisha madai ya jinai dhidi ya Infantino na huenda viongozi au washauri wengine wa FIFA, wakihusisha suala hilo na tuhuma za “criminal mismanagement”.

Hatua hiyo inahusishwa na mpango uliokuwa ukihusisha FIFA kuuza hisa katika Kombe la Dunia, mpango ambao Infantino aliusitisha baada ya UEFA kutishia kususia mashindano hayo.

Wakati huo huo, Infantino alikumbana na hali ya aibu nchini Vietnam baada ya mashabiki waliokuwa kwenye Uwanja wa My Dinh National Stadium, Hanoi, kumtukana kwa lugha chafu alipokuwa akiwasilisha kombe baada ya Vietnam kuifunga Thailand na kutwaa ubingwa wa ASEAN.

Video kutoka uwanjani ilionyesha baadhi ya mashabiki wakimuita Infantino kwa matusi kwa lugha ya Kiingereza, huku rais huyo wa FIFA akitabasamu na kuwapungia mkono.

Infantino mwenye umri wa miaka 56 baadaye alielezea ziara hiyo kupitia Instagram, akisema matukio kama hayo yanaakisi kile ambacho FIFA inasimamia.

Infantino anatarajiwa kugombea tena nafasi ya urais wa FIFA katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Machi 2027.

OUT na Mzumbe Watangaza Nafasi 6 za Kazi, Mwisho wa Maombi Agosti 31

Kwa niaba ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Chuo Kikuu cha Mzumbe (MU), Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma anawakaribisha Watanzania wenye sifa, uwezo, ari ya kufanya kazi, uadilifu na wanaolenga kupata matokeo bora kuomba nafasi sita (6) za kazi zilizoainishwa hapa chini.

CHUO KIKUU HURIA CHA TANZANIA (OUT)

1.0 MKUFUNZI DARAJA LA II – ELIMU MAALUMU

Nafasi 2

1.1 Majukumu ya Kazi

i. Kusaidia katika kutekeleza majukumu yote ya kitaalamu yanayohitaji uwezo mkubwa wa kupanga na kubuni katika maeneo ya mafunzo kwa vitendo na miradi ya wanafunzi.
ii. Kusaidia katika shughuli za utafiti na maendeleo.
iii. Kusaidia katika kutunza na kufanya matengenezo ya vifaa vya TEHAMA vinavyotumika kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
iv. Kusaidia katika kuandaa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi.
v. Kutekeleza majukumu mengine yanayohusiana na kazi atakayopewa na msimamizi.

1.2 Sifa na Uzoefu

Mwombaji awe na Shahada ya Kwanza ya Elimu Maalumu katika Lugha ya Alama (Sign Language) au sifa inayolingana na hiyo kutoka katika taasisi inayotambuliwa. Mwombaji lazima awe na ujuzi wa matumizi ya kompyuta.

1.3 Mshahara

PUSS 4.1

2.0 FUNDI DARAJA LA II – MIFUMO YA VIYOYOZI NA MAJOKOFU

Nafasi 1

2.1 Majukumu ya Kazi

i. Kukagua mifumo na vipengele vya vifaa vya kupooza.
ii. Kukagua ufungaji wa mifumo na kutoa mapendekezo kuhusu matengenezo ya mifumo ya umeme.
iii. Kuondoa kimiminika cha zamani na kilichochafuliwa cha kupooza na kuweka kimiminika kipya.
iv. Kusaidia katika ukarabati na matengenezo ya mifumo ya umeme katika maabara au karakana.
v. Kusaidia watumishi wakuu katika shughuli zinazohusiana na taaluma yake.
vi. Kutekeleza majukumu mengine atakayopewa na msimamizi.

2.2 Sifa na Uzoefu

Mwombaji awe na Stashahada ya NTA Level 6 au Full Technician Certificate (FTC) katika Uhandisi wa Baharini na Majokofu (Marine and Refrigeration Engineering) au sifa inayolingana na hizo kutoka katika chuo kikuu kinachotambuliwa.

2.3 Mshahara

PGSS 5.1

CHUO KIKUU CHA MZUMBE (MU)

1.0 AFISA TEHAMA DARAJA LA II – VIFAA VYA SAUTI NA PICHA

Nafasi 2

1.1 Majukumu ya Kazi

i. Kusaidia kutunza kumbukumbu sahihi za matokeo yote ya mitihani, mihutasari ya vikao, kanuni na taratibu.
ii. Kusaidia kutunza chumba cha televisheni.
iii. Kutunza kumbukumbu za vifaa vya sauti na picha (Audio-Visual) vinavyohitajika.
iv. Kusaidia katika ukarabati wa vifaa vya sauti na picha pamoja na vifaa vya kituo cha televisheni.
v. Kusaidia katika upigaji wa video kwa kutumia kamera kulingana na matukio mbalimbali.
vi. Kusaidia katika kufunga, kuweka na kurekebisha vifaa vya sauti na picha.
vii. Kutekeleza majukumu mengine atakayopewa na msimamizi.

1.2 Sifa na Uzoefu

Mwombaji awe na Shahada ya Kwanza katika mojawapo ya fani zifuatazo:

  • Teknolojia ya Multimedia na Uhuishaji (Multimedia Technology and Animation);
  • Uendelezaji wa Maudhui ya Multimedia (Multimedia Content Development);
  • Ubunifu wa Mafunzo (Instructional Design);
  • Ubunifu wa Mafunzo na Teknolojia ya Habari (Instructional Design and Information Technology);

au sifa inayolingana na hizo kutoka katika taasisi inayotambuliwa.

1.3 Mshahara

PGSS 7.1

2.0 MHUSIKA WA USAFISHAJI WA NGUO DARAJA LA II

Nafasi 1

2.1 Majukumu ya Kazi

i. Kukusanya mashuka na neti za vitanda zilizotumika kutoka wodini.
ii. Kuhakikisha vifaa vya kufulia vinawekwa katika hali safi na salama ya kufanya kazi.
iii. Kuhakikisha eneo la kufulia linakuwa katika hali salama.
iv. Kuwapatia idara mbalimbali mashuka na neti za vitanda zilizo safi.
v. Kufua na kupiga pasi nguo za hospitali.
vi. Kuripoti nguo, mashuka na neti za vitanda zilizochakaa au kuharibika.
vii. Kutekeleza majukumu mengine atakayopewa na msimamizi.

2.2 Sifa na Uzoefu

Mwombaji awe amehitimu Kidato cha Nne na awe na Cheti cha Usimamizi wa Huduma za Ukarimu (Hospitality Management) au fani inayolingana na hiyo kutoka katika taasisi inayotambuliwa.

2.3 Mshahara

PMOSS 1.1

MASHARTI YA JUMLA YA MAOMBI

  1. Waombaji wote lazima wawe raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wasiwe na umri unaozidi miaka 45. Hata hivyo, kwa nafasi zilizo katika taasisi za kijeshi/paramilitary, waombaji wa nafasi zisizohitaji shahada hawapaswi kuzidi miaka 25, na waombaji wa nafasi zinazohitaji shahada hawapaswi kuzidi miaka 30.
  2. Waombaji wanapaswa kuomba kwa kuzingatia sifa na taarifa zilizotolewa katika tangazo hili.
  3. Waombaji wanapaswa kuambatanisha nakala zilizothibitishwa za vyeti vifuatavyo:
    • Vyeti vya Uzamili/Shahada/Stashahada ya Juu/Stashahada/Vyeti;
    • Nakala za matokeo ya masomo (transcripts);
    • Vyeti vya usajili wa kitaaluma na mafunzo kutoka katika mamlaka husika za usajili au udhibiti, pale inapohitajika;
    • Cheti cha kuzaliwa.
  4. Hairuhusiwi kuwasilisha:
    • Karatasi za matokeo (results slips) za Kidato cha Nne na Kidato cha Sita;
    • Testimonials;
    • Nakala za matokeo ambazo hazijakamilika (partial transcripts).
  5. Mwombaji anatakiwa kupakia picha yake ya hivi karibuni ya ukubwa wa passport katika Mfumo wa Ajira.
  6. Watumishi walioajiriwa katika Utumishi wa Umma hawaruhusiwi kuomba nafasi hizi. Wanapaswa kuzingatia Waraka Na. CAC.45/257/01/D/140 wa tarehe 30 Novemba, 2010.
  7. Mtumishi aliyestaafu katika Utumishi wa Umma kwa sababu yoyote ile haruhusiwi kuomba.
  8. Kila mwombaji anatakiwa kutaja wadhamini (referees) watatu wenye sifa nzuri pamoja na mawasiliano yao yanayoweza kupatikana.
  9. Vyeti vyote vya elimu vilivyotolewa nje ya Tanzania lazima vitambuliwe na mamlaka husika, ambazo ni TCU, NECTA na NACTVET. Waombaji wa nafasi zinazohitaji GPA wanapaswa kuambatanisha cheti cha ukokotoaji wa GPA kutoka TCU.
  10. Barua ya maombi iliyosainiwa inaweza kuandikwa kwa Kiswahili au Kiingereza na ielekezwe kwa:

Katibu,
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma,
S.L.P. 2320,
Mtaa wa Mahakama, Tambukareli,
Dodoma.

  1. Mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 31 Agosti, 2026.
  2. Waombaji watakaofaulu katika hatua ya usaili wa awali pekee ndio watakaotaarifiwa kuhusu tarehe ya usaili.
  3. Kuwasilisha vyeti vya kughushi au taarifa za uongo kutasababisha hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya mwombaji.
  4. Maombi yote yanapaswa kutumwa kupitia Mfumo wa Ajira (Recruitment Portal) kwa kutumia anwani: http://portal.ajira.go.tz. Anwani hii pia inaweza kupatikana kupitia tovuti ya PSRS kwa kubofya sehemu ya “Recruitment Portal.”
  5. Maombi yatakayotumwa kwa njia nyingine yoyote hayatapokelewa au kuzingatiwa.

Imetolewa na:
KATIBU
SEKRETARIETI YA AJIRA KATIKA UTUMISHI WA UMMA

Bunge la Tanzania leo: Deogratius Ndejembi Kuthibitishwa Kuwa Makamu wa Rais – Video

Global Publishers
August 28, 2026
402 views
0 Comments



Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo, Ijumaa, Agosti 28, 2026, linatarajiwa kupokea na kuthibitisha uteuzi wa Deogratius Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa ratiba ya shughuli za Bunge kwa siku ya leo, wabunge wanatarajiwa kutekeleza jukumu hilo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya jina la Ndejembi kupendekezwa kwa nafasi hiyo.

Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Agosti 27, 2026, kumteua na kumpendekeza Ndejembi kwa nafasi ya Makamu wa Rais.

Iwapo Bunge litathibitisha uteuzi huo, Ndejembi ataapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuanza rasmi kutekeleza majukumu ya kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Uteuzi huo unatajwa kuwa hatua muhimu katika mchakato wa kuunda uongozi wa juu wa Serikali, huku macho ya Watanzania yakiwa kwenye hatua itakayochukuliwa na Bunge leo.

Endelea kufuatilia taarifa zaidi kuhusu mchakato huo.

Inashangaza! Simba Yashinda, Lakini Mashabiki Watoa Lawama Kwa Doumbia – Video

Global Publishers
August 28, 2026
78 views
0 Comments


Baadhi ya mashabiki wa Simba wameonekana kutoridhishwa na kiwango cha mshambuliaji wa klabu hiyo, Ibrahim Doumbia, licha ya timu hiyo kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union FC.

Mchezo huo umechezwa katika Uwanja wa Isamuyo, ambapo shabiki wa Simba, wametoa maoni yao kuhusu kiwango cha Doumbia wakati akizungumza na mtangazaji wetu Official Diana, mara baada ya mchezo kumalizika.

Watu Wawili Wafariki Baada ya Kujinyonga Dagailoi, Babati – Video

Global Publishers
August 28, 2026
6 views
0 Comments

Watu wawili, wakazi wa Kijiji cha Dagailoi, Kata ya Sigino, Wilaya ya Babati, mkoani Manyara, wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti baada ya kujinyonga.

Tukio la kwanza lilitokea Agosti 22, 2026, ambapo mwanaume aliyefahamika kwa jina la Petro Moya anadaiwa kujinyonga baada ya kutokea mvutano kuhusu bili ya maji ya Shilingi 6,000 kati yake na mama yake mzazi.

Inadaiwa kuwa Petro alipewa fedha hizo na mama yake kwa ajili ya kulipia bili ya maji, lakini alizitumia kwa shughuli nyingine. Baada ya mama yake kumdai fedha hizo, Petro alichukua uamuzi wa kujinyonga.

Tukio la pili limetokea asubuhi ya leo, Agosti 27, 2026, ambapo mwanaume mwingine aliyefahamika kwa jina la Mohamed Abdilai amefariki dunia baada ya kujinyonga.

Inadaiwa kuwa Mohamed alichukua uamuzi huo baada ya baba yake mzazi kumtaka arejee nyumbani, kufuatia kushindwa kulipa kodi ya nyumba ya Shilingi 10,000.

Mwandishi wa Global TV, Hosea El Nino, amefika katika Kitongoji cha Dagailoi kufuatilia undani wa matukio hayo.

TANESCO NA MAHAKAMA NYANDA ZA JUU KUSINI ZAIMARISHA MAHUSIANO KULINDA MIUNDOMBINU YA UMEME

Dodoma

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeeleza umuhimu wa kuwa na ushirikiano wa karibu na Mahakama katika kushughulikia changamoto zinazohusu miundombinu ya umeme, ikiwemo matukio ya uharibifu na hujuma dhidi ya miundombinu hiyo.

Akizungumza Agosti 27, 2026, baada ya watumishi wa Idara ya Mahakama, akiwemo Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Wasajili, Mahakimu, Watendaji na wafanyakazi wengine kufanya ziara katika Kituo cha Kufua Umeme cha Mtera kwa lengo la kujifunza namna umeme unavyozalishwa, kusafirishwa na kusambazwa kwa wananchi, Meneja wa Huduma za Usalama wa TANESCO, Bw. Lenin Kiobya, amesema ziara hiyo imewapa watumishi hao uelewa wa namna Shirika linavyotekeleza majukumu yake, kuanzia uzalishaji, usafirishaji hadi usambazaji wa umeme kwa wananchi.

Amebainisha kuwa uelewa huo ni muhimu kwa Mahakama katika utekelezaji wa majukumu yake ya kutafsiri na kusimamia sheria, hususan inaposhughulikia kesi zinazohusiana na miundombinu ya umeme, ili masuala yanayogusa maslahi ya taifa yaweze kupewa uzito unaostahili.

Aidha, amesema kuwa TANESCO itaendelea kujenga ushirikiano na Mahakama katika kushughulikia changamoto zinazojitokeza kwenye miundombinu yake, hatua inayolenga kusaidia kupunguza uhalifu na hujuma zinazoweza kuathiri huduma ya umeme nchini.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Fahamu Mtulya, amesema ziara hiyo katika Kituo cha Kufua Umeme cha Mtera imewasaidia Majaji na Mahakimu kuelewa kwa kina umuhimu wa kulinda miundombinu yenye maslahi ya kitaifa, ikiwemo miundombinu ya TANESCO.

Amesema kuwa wamebaini kuwa ucheleweshaji wa mashauri yanayohusiana na uwekezaji na miundombinu ya TANESCO unaweza kuwa na gharama kubwa, hivyo wamekubaliana kuyapa kipaumbele mashauri yanayohusu miundombinu hiyo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Pia, amebainisha kuwa uharibifu wa miundombinu yenye maslahi ya kitaifa, ikiwemo miundombinu ya umeme na reli, huhusisha makosa ya uhujumu uchumi yenye adhabu kali, huku akisisitiza umuhimu wa wadau wa sheria, ikiwemo Bunge, kushirikiana kubaini na kuziba mianya ya kisheria inayoweza kujitokeza.

Aidha, amewataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya taasisi za umma, ikiwemo ya TANESCO, akieleza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda mali za taifa. Amesema Mahakama pia itatumia Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kulinda miundombinu ya umeme.

Naye, Kaimu Meneja wa Kituo cha Kufua Umeme cha Mtera, Mhandisi William Modest, amesema kituo hicho kina uwezo wa kuzalisha megawati 80 kupitia mashine mbili, kila moja ikiwa na uwezo wa kuzalisha megawati 40. Umeme huo huingizwa kwenye gridi ya taifa kwa matumizi ya wananchi na shughuli za kiuchumi.

Aidha, ametoa wito kwa Majaji kusaidia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji na madhara ya kilimo holela kinachoweza kuzuia mtiririko wa maji kuelekea Bwawa la Mtera.

Amebainisha kuwa Kituo cha Mtera kina umuhimu mkubwa katika upatikanaji wa umeme nchini, huku kikihudumia zaidi ya vijiji 12. Bwawa la Mtera pia lina umuhimu katika shughuli za uvuvi na kilimo, huku Mto Ruaha ukitoa maji kwa skimu mbalimbali za kilimo katika Nyanda za Juu Kusini.