Shauri la uhaini namba 19605/2025 linalomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, linaendelea leo Agosti 24, 2026 katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.
Kesi hiyo inaendelea katika hatua ya ushahidi wa utetezi, mbele ya jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru.
Hatua hiyo ilianza Ijumaa, Agosti 21, baada ya Mahakama kumkuta Lissu ana kesi ya kujibu na kumpa nafasi ya kuanza kujitetea dhidi ya mashtaka yanayomkabili.
Lissu, ambaye ameamua kujitetea mwenyewe, alianza kutoa ushahidi wake siku hiyo na pia akawasilisha orodha ya mashahidi anaotarajia kuwaita mahakamani.
Miongoni mwa mashahidi aliowataja ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan; Makamu wa Rais mstaafu, Philip Isdor Mpango; pamoja na Waziri Mkuu mstaafu, Kassim Majaliwa.
Aidha, Lissu amewataja baadhi ya viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na viongozi wa CHADEMA, akiwemo Makamu Mwenyekiti John Heche, Katibu Mkuu John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Amani Golugwa na Brenda Rupia.
Leo, Lissu anatarajiwa kuendelea na ushahidi wake wa kujitetea kama shahidi wa kwanza. Baada ya kukamilisha ushahidi wake, mashahidi wengine wa upande wa utetezi wanatarajiwa kuanza kutoa ushahidi wao.
Hata hivyo, suala la kuwaita viongozi wa Serikali, wakiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, limezua mvutano kati ya pande hizo mbili.
Upande wa mashtaka umepinga wito wa viongozi hao kufika mahakamani, ukieleza kuwa Jamhuri tayari imekamilisha ushahidi wake na kwamba si jambo la busara kumtaka Rais kufika mahakamani kutoa ushahidi katika kesi hiyo.
Kwa upande wake, Lissu amepinga hoja hiyo akisisitiza kuwa sheria inapaswa kutumika kwa kila mtu bila kujali cheo au nafasi yake.
Kesi hiyo inaendelea huku ikifuatiliwa kwa karibu kutokana na uzito wa mashtaka na majina ya viongozi wakuu wa Serikali yaliyotajwa kuwa sehemu ya mashahidi wa utetezi.
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania kuendelea kuliombea Taifa na kudumisha amani, akisema amani ni msingi unaowezesha wananchi, taasisi za dini na Taifa kwa ujumla kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo.
Amesema dunia inaendelea kushuhudia mabadiliko na mitikisiko katika maeneo mbalimbali, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kumwomba Mungu ailinde Tanzania na kuendeleza amani ambayo imeiwezesha nchi kutekeleza shughuli zake kwa utulivu.
Waziri Mkuu amesema hayo leo (Jumapili, Agosti 23, 2026) aliposhiriki ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), Usharika wa Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.
“Tuendelee kuiombea nchi yetu. Leo hii tunaweza kufanya ibada kwa sababu nchi yetu ipo na amani. Tuna mipango mbalimbali kama nchi, katika ngazi ya familia, taasisi, Dayosisi na Kanisa, lakini hayo yote tunaweza kuyafanya kama nchi yetu ipo na amani,” amesema.
Dkt. Mwigulu amewafikishia waumini salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Serikali kwa ujumla, huku akitambua na kuenzi mchango mkubwa unaofanywa na Kanisa katika maendeleo ya nchi.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kusonga mbele.
“Hauwezi ukataja maendeleo ya nchi yetu bila kutaja mchango wa Kanisa,” amesema.
Naye Katibu Mkuu wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Bw. Goodluck Nkini, alimshukuru Waziri Mkuu kwa kuchagua kuabudu katika Usharika wa Kijitonyama na kwa kuendelea kujumuika na waumini katika maeneo mbalimbali.
Ibada hiyo iliongozwa na Mchungaji Anna Kuyonga wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Usharika wa Kijitonyama.
Viongozi wengine waliohudhuria ibada hiyo ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mhe. Aggrey Mwanri; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya; Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila; Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule; Mbunge wa Same Magharibi, Dkt. David Mathayo; na Mbunge wa Makete, Mhe. Festo Sanga.
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amefanya ziara ya kushtukiza leo Jumapili, Agosti 23, 2026, katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa Mwananyamala, jijini Dar es Salaam, kukagua hali ya utoaji wa huduma kwa wananchi.
Alipowasili hospitalini hapo, Dkt. Mwigulu ametembelea wodi mbalimbali, zikiwemo Wodi ya Mama na Mtoto na Wodi ya Upasuaji, ambako amezungumza na wagonjwa pamoja na ndugu zao na kusikiliza maoni yao kuhusu huduma zinazotolewa hospitalini hapo na changamoto wanazokabiliana nazo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wanaopata huduma hospitalini hapo wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Serikali kwa ujumla kwa kuendelea kuboresha huduma za afya na mazingira ya utoaji wa huduma hospitalini hapo.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila; Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule; pamoja na viongozi wa Hospitali hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi, wageni mbalimbali pamoja na wananchi waliohudhuria hafla ya Uzinduzi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP), chenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2115 katika eneo la Rufiji mkoani Pwani tarehe 22 Agosti, 2026.
PWANI: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kukamilika kwa Mradi wa Kufua Umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) ni utekelezaji wa ndoto ya muda mrefu ya Tanzania ya kuwa na nishati ya uhakika kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Rais Samia amesema hayo leo, Jumamosi, Agosti 22, 2026, wakati akizindua rasmi mradi huo uliopo mkoani Pwani.
Amesema Serikali ilipa mradi huo uzito unaostahili kutokana na umuhimu wake kwa Taifa, akisisitiza kuwa haukuwa mradi wa kuachwa kwa sababu una mchango mkubwa katika kuongeza umeme kwenye Gridi ya Taifa.
Rais Samia akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP).
Rais Samia amekumbusha kuwa Desemba 22, 2022 alifika eneo la mradi kushuhudia hatua ya kufungwa kwa njia ya kuchepusha maji ya Mto Rufiji na kuanza kujazwa kwa bwawa.
Alisema awali ilitarajiwa bwawa hilo kujazwa ndani ya miaka mitatu, lakini kwa neema ya Mungu lilijaa ndani ya mwaka mmoja na nusu, jambo lililowezesha majaribio ya uzalishaji umeme kuanza mapema.
Katika hafla hiyo, Rais Samia alizindua rasmi kituo cha kuzalisha umeme na kukagua maeneo mbalimbali ya mradi, yakiwemo mitambo ya uzalishaji, tuta kuu pamoja na kituo cha kupokea na kusafirisha umeme kwenda kwenye Gridi ya Taifa.
Amesema maeneo hayo yanafanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kwamba mradi huo ni jambo la kujivunia kwa Taifa.
JNHPP ina uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115, hali inayoongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa Tanzania katika kuhudumia mahitaji ya nishati kwa shughuli za uzalishaji, viwanda, uwekezaji na maendeleo ya wananchi.
Samia awakumbuka viongozi waliotangulia
Rais Samia amesema kukamilika kwa mradi huo kunatoa somo kuhusu umuhimu wa kuwa na nidhamu katika ufuatiliaji wa miradi, ustahimilivu katika kukabiliana na changamoto na uimara wa kusimamia malengo ya miradi ya kimkakati.
Amesema kuanzisha mradi pekee hakutoshi, bali matokeo yake hutegemea namna Serikali inavyofuatilia utekelezaji wake hatua kwa hatua hadi kufikia malengo yaliyowekwa.
Rais Samia pia amewashukuru viongozi wa awamu zilizopita kwa kuendeleza maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ya kutumia rasilimali za Mto Rufiji kwa ajili ya kuzalisha umeme.
Miongoni mwa viongozi aliowataja ni Hayati Ali Hassan Mwinyi, Hayati Benjamin Mkapa na Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete, kwa mchango wao katika kuendeleza dira hiyo.
Aidha, amemkumbuka na kumshukuru Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa msimamo wake wa kuhakikisha fedha zinapatikana na ujenzi wa mradi unaanza licha ya changamoto na upinzani uliokuwepo.
Samia atoa tahadhari kuhusu mvua kubwa
Katika hatua nyingine, Rais Samia amewataka Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Taasisi za Serikali kujiandaa mapema kukabiliana na uwezekano wa mvua kubwa zinazotabiriwa kunyesha nchini.
Amesema taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) zinaonyesha uwezekano wa mvua kubwa zinazohusishwa na mfumo wa hali ya hewa wa El Niño.
Rais Samia amesisitiza kuwa taarifa hizo zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito na hatua za tahadhari zichukuliwe kabla ya madhara kujitokeza.
Ameagiza viongozi kuhakikisha mifereji inasafishwa, mifumo ya uokoaji inaandaliwa na wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi wanatambuliwa na kuondolewa mapema.
“Niwaombe nendeni mkajitayarishe, mkaweke mazingira sawa ili mvua hizo zitakapoanza zisilete maafa makubwa kwa wananchi wetu,” amesema Rais Samia.
Amesisitiza kuwa tahadhari zinazotolewa na TMA zinapaswa kufanyiwa kazi kwa wakati ili kulinda maisha na mali za wananchi.
Maelekezo hayo yametolewa muda mfupi baada ya Rais Samia kukamilisha uzinduzi rasmi wa JNHPP, mradi unaotarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji wa umeme na kuimarisha upatikanaji wa nishati nchini.