Shigongo Ahoji Serikali Kuhusu Barabara za Mitaa Nyehunge – Video
Global Publishers
August 27, 2026
12 views
0 Comments

Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo, amehoji Bungeni jijini Dodoma kuhusu hatua za Serikali katika kuboresha barabara za mitaa katika eneo la Nyehunge, Buchosa mkoani Mwanza, ambazo kwa sasa hazikidhi viwango vinavyohitajika.
Shigongo ametoa hoja hiyo Bungeni akiitaka Serikali kueleza ni lini itachukua hatua za kuzirekebisha barabara hizo ili ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi na kurahisisha usafiri katika eneo hilo.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, amesema Serikali inalifahamu suala hilo na tayari inalishughulikia.
Prof. Shemdoe amesema kuwa Serikali itaendelea kutafuta na kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo, huku akieleza kuwa fedha zitakapopatikana, barabara hizo zitajengwa kwa kiwango cha lami.
Kauli hiyo imekuja ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha miundombinu ya barabara za mitaa na kuongeza ubora wa huduma za usafiri kwa wananchi.
Uboreshaji wa barabara hizo unatarajiwa kuwa na mchango katika kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi katika eneo la Buchosa.