Tanzania yaandaa ziara ujumbe wa ADDI – HabariLeo
DAR ES SALAAM: Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeandaa ziara maalumu ya ujumbe kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Diaspora wa Kiafrika (ADDI) katika Makumbusho ya Taifa la Tanzania, jijini Dar es Salaam.
Ziara hiyo iliyofanyika Agosti 26, 2026, imelenga kuwapa wageni fursa ya kujifunza historia, utamaduni na urithi wa Tanzania, pamoja na kuimarisha diplomasia ya utamaduni.

Ujumbe huo uliongozwa na Mwanzilishi na Rais wa ADDI, Balozi Arikana Chihombori-Quao kutoka Zimbabwe, ambaye amewataka Waafrika kuwa wamoja, kushikamana na kudumisha amani, akisisitiza umuhimu wa umoja katika kulinda na kuendeleza urithi wa Afrika.

Kwa upande wake, Muhifadhi Kiongozi wa Makumbusho na Nyumba za Utamaduni, Dk. Aloyce Mwambwiga, amewahimiza wananchi na wageni kutoka nje ya nchi kutembelea Makumbusho ya Taifa ili kujifunza zaidi kuhusu historia, utamaduni na urithi wa Tanzania.

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za kuendeleza diplomasia ya utamaduni na kuitangaza Tanzania kupitia historia na urithi wake kwa wageni kutoka ndani na nje ya nchi.