TANGA: MBUNGE wa Jimbo la Mkinga, Twaha Mwakioja, ametekeleza ahadi yake baada ya kukabidhi pampu ya maji kwa ajili ya Shule ya Sekondari Lanzoni, pamoja na kutoa fedha taslimu na vifaa mbalimbali vya maendeleo na michezo katika wilaya hiyo.
Katika ziara yake iliyofanyika katika Kata ya Mhinduro, Mbunge Mwakioja alikabidhi pampu hiyo inayolenga kupunguza kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji shuleni hapo, sambamba na kutoa Sh 300,000 kwa ajili ya ukarabati wa vyoo katika Shule ya Msingi Bamba Mavengero.

”Leo nimekuja kutekeleza ahadi zangu baada ya kubaini changamoto mbalimbali kwenye shule zetu. Ninaamini misaada hii itasaidia kuweka mazingira mazuri ya kujifunzia kwa vijana wetu,” alisema Mwakioja alipokuwa akizungumza na wananchi.
Mbali na sekta ya elimu, Mbunge huyo aligusa nyanja nyingine muhimu kwa jamii ya Mkinga kwa kutoa misaada wa
Viti 20 kwa kikundi cha wanakijiji cha Muheza ili kurahisisha shughuli zao za kijamii na Sh 500,000 kwa Klabu ya Mpira wa Miguu ya St. Augustino FC (inayomilikiwa na Kanisa Anglikana Mhinduro) ikiwa ni hamasa kwa vijana kujihusisha na michezo.
Katika ziara hiyo, Mwakioja alipata fursa ya kusikiliza na kupokea kero mbalimbali za wananchi, kukutana na makundi ya vijana, pamoja na kushiriki katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Kata ya Mhinduro.
Akihutubia wananchi waliojitokeza kwa wingi, aliainisha mafanikio mbalimbali ya kimaendeleo yaliyopatikana jimboni humo tangu alipoingia madarakani. Alisisitiza kuwa siri ya maendeleo ya haraka inatokana na ushirikiano thabiti kati ya wananchi, viongozi wa Chama, na Serikali.