Jamhuri Yakamilisha Kumuhoji Lissu Katika Kesi ya Uhaini Leo – Video

Upande wa mashtaka, Jamhuri, umekamilisha zoezi la maswali ya dodoso (cross-examination) kwa shahidi wa kwanza ambaye pia ni mshtakiwa katika kesi ya uhaini, Tundu Lissu.
Zoezi hilo limekamilika leo, Agosti 28, 2026, baada ya Jopo la Majaji kuruhusu upande wa Jamhuri kuendelea na maswali hayo.
Katika swali la mwisho, Wakili wa Serikali Mkuu alimuuliza Lissu iwapo ni kweli au si kweli kwamba nia ya kutenda kosa inathibitishwa na tendo husika. Lissu aliomba ufafanuzi iwapo swali hilo lilihusu nia ya kuthibitisha tendo la uhaini, kabla ya wakili huyo kueleza kuwa alikuwa akiuliza kuhusu tendo lolote na si uhaini pekee.
Baada ya Lissu kujibu, “Si kweli,” Wakili wa Serikali Mkuu aliieleza Mahakama kuwa upande wa Jamhuri umemaliza maswali ya dodoso kwa shahidi huyo.
Baada ya hapo, upande wa Jamhuri uliomba mwongozo wa Mahakama kuhusu namna hatua ya maswali ya ufafanuzi (re-examination) itakavyoendeshwa, kwa kuzingatia kuwa Lissu anajiwakilisha mwenyewe katika kesi hiyo.
Jamhuri ilieleza kuwa kuna haja ya kuweka mwongozo kuhusu namna Lissu atakavyofanya maswali ya ufafanuzi kutokana na majibu aliyoyatoa wakati wa cross-examination, bila kukiuka misingi ya kisheria.
Upande wa Jamhuri ulipendekeza kuwa Lissu aruhusiwe kutoa ufafanuzi katika mambo ambayo yanaweza kuwa na maana zaidi ya moja.
Kwa upande wake, kabla ya kujibu hoja hiyo, Lissu alitaka Jamhuri iweke wazi iwapo suala hilo lilikuwa pingamizi rasmi au ni mapendekezo na ushauri kwa Mahakama.
Baada ya Wakili wa Serikali kufafanua kuwa hawajaweka pingamizi bali wanaomba mwongozo wa Mahakama, Lissu alisisitiza kuwa haki ya kufanyiwa maswali ya dodoso ni ya kisheria chini ya Kifungu cha 156(1) cha Sheria ya Ushahidi, na kwamba kujiwakilisha mwenyewe hakuwezi kumnyima haki hiyo.
Lissu pia alieleza kuwa hofu ya Jamhuri kwamba anaweza kuibua mambo mapya haina msingi, akisema upande wa mashtaka una haki ya kuweka pingamizi wakati wowote atakapovuka mipaka ya maswali ya ufafanuzi.
Akitoa mwelekeo wa Mahakama, Jaji Dunstan Ndunguru alisema jambo la msingi ni kuangalia wigo na mipaka ya dodoso.
Katika maswali ya awali, Jamhuri ilimuuliza Lissu kuhusu maeneo mbalimbali ya ushahidi wake, ikiwemo madai yake kwamba baadhi ya mashahidi wa Jamhuri walitoa ushahidi unaokinzana kwa maelezo na maandishi.
Pia aliulizwa iwapo, baada ya matukio mbalimbali yaliyompata, ikiwemo kushambuliwa kwa risasi, aliwahi kutoa taarifa polisi. Lissu alijibu kuwa alishatoa taarifa na kwamba hakuna hatua iliyochukuliwa.
Lissu anakabiliwa na mashtaka ya uhaini, chini ya Kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code), Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania.