WARAGHABISHI WACHOCHEA MAENDELEO KIGOMA – Matukio Daima Habari
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mkakati wa uraghabishi unaotekelezwa na wananchi wa mitaa 10 ya manispaa ya Kigoma Ujiji kwa uratibu wa Shirika lisilo la kiserikali la TWAWEZA unaelezwa kuchochea wananchi kwenye mitaa hiyo kushiriki kwenye mikutano ya maendeleo sambamba na kushiriki kwenye utekelezaji wa miradi inayoibuliwa kwenye mtaa yao.
Mthamini Binafsi aliyepewa kazi na TWAWEZA kutathmini utekelezaji wa mradi huo uliotekelezwa kwa miaka minane katika manispaa ya Kigoma Ujiji, Kapongola Nganyanyuka alisema hayo akiwasilisha taarifa yake ya tathmini wakati wa kufunga mradi huo ambao umefikia mwisho.
Nganyanyuka alisema kuwa katika utekelezaji wa mtadi huo wananchi wamekuwa na hamasa ya kuhudhuria mikutano ya mitaa yao, kuibua mawazo mbalimbali yakiwemo ya miradi ya maendeleo, kupanga na kushiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo huku wakiwa na uwezo wa kuomba taarifa ya hali ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Baadhi ya wananchi (waraghabishi) walioshiriki katika mpango wa kutoa elimu kwa jamii kiwemo Mwenyekiti wa Waraghabishi (WAMCU) mkoa Kigoma, John Edward alisema kuwa baada ya kuona mradi unafikia mwisho waliamua kuunda umoja huo ili kuendeleza kazi hiyo kwa kuendelea kutafuta fedha kutoka vyanzo vingine.
Edward alisema kuwa kwa kipindi cha uratibu wa TWAWEZA walichofanya kazi kumekuwa na mabadiliko makubwa na mwamko kwa jamii kujitokeza kwenye mikutano na shughuli za maendeleo.
Naye Shekhe Omari Hussein kutoka kata ya Buzebazeba alisema kuwa mradi huo umeleta mabadiliko makubwa kwenye fikra za wananchi kuhusu dhana ya kuibua,kupanga na kutekeleza miradi na kuwa chachu ya kuwafanya wananchi kuwa na umiliki kamili wa miradi kwa kuifanya miradi hiyo kama sehemu ya maisha yao.
Akieleza kuhusu utekelezaji wa mradi huo ambao umefikia mwisho Mratibu wa mkoa Kigoma wa mradi huo, Esther Prosper alisema kuwa mradi ulilenga kuwajengea uwezo waraghabishi kuifikia jamii kubwa wanaoishi nayo kuwa na uwezo wa kushiriki mikutano, kuchangia mada na kuwa washiriki wa maamuzi wa mikutano hiyo ikiwemo kuibua, kupanga na kushiriki shughuli za maendeleo na kwamba miaka minane ya mradi huo wameridhika na mafanikio yaliyofikiwa.
Mwisho.


