Wajenzi wanavyokiuka vibali vya ujenzi, hatari kwa watumiaji

Dar es Salaam. Baadhi ya wamiliki wa majengo jijini Dar es Salaam wamekuwa wakibadilisha mipango ya ujenzi baada ya kupata vibali, ikiwamo kuongeza idadi ya ghorofa, hali ambayo wataalamu wanaonya inaweza kuathiri usalama wa majengo na watumiaji.

Kumbukumbu mbaya ni Novemba 16, 2024, ambapo jengo liliporomoka Mtaa wa Mchikichi na Congo, Kariakoo, Dar es Salaam, na kusababisha vifo vya watu 20, huku zaidi ya 50 wakiokolewa.

Tukio kama hilo lilitokea Machi 29, 2013, Mtaa wa Indira Gandhi, Posta jijini Dar es Salaam, ambapo jengo la ghorofa 16 liliporomoka, ambalo liliombewa kibali cha ghorofa 10. Kuporomoka huko kulisababisha vifo vya watu zaidi ya 15 na kujeruhi wengine.

Aliyekuwa Naibu Meya wa Halmashauri ya Ilala, Kheri Kessy, alisema mwaka 2007 walitoa kibali cha ujenzi wa ghorofa 10 kwa jengo hilo la Posta, ambazo zilikuwa zinafuatiliwa na mkaguzi hadi zilipofikia mwisho, hivyo uongezekaji wa ghorofa sita hawakuutambua.

Novemba 2025, Ofisa wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, aliyeomba jina lake lisitajwe, aliliambia Mwananchi mamlaka hiyo hutoa vibali kwa kuzingatia ramani na michoro inayowasilishwa na mwombaji.

Hata hivyo, alisema baadhi ya wamiliki hubadilisha mipango wanapoanza ujenzi na kuongeza ghorofa tofauti na walizoomba na kupewa kibali.

Alitoa mfano wa jengo moja eneo la Kariakoo, ambalo mmiliki wake aliomba kibali cha kujenga ghorofa tano, lakini wakati wa ujenzi akaongeza hadi ghorofa 10.

“Tumewahi kumpiga faini mmiliki mmoja wa jengo Kariakoo baada ya kubaini aliomba kibali cha ghorofa tano, lakini akajenga ghorofa 10,” alisema ofisa huyo alipozungumza na Mwananchi ilipokuwa ikiandaa habari maalumu kuhusu matumizi ya majengo ya Kariakoo yasiyokamilika.

Hoja hiyo inaakisi kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Albert Chalamila, ya Agosti 6, 2026, kueleza kubaini ukiukaji wa masharti ya ujenzi wakati wa ukaguzi.

Chalamila alisema kuna majengo ambayo vibali vyake vilitolewa kwa idadi ndogo ya ghorofa, lakini yalipofikiwa katika maeneo ya ujenzi yalikuwa yamejengwa zaidi ya idadi iliyoidhinishwa.

Katika mfano alioutoa, alisema jengo moja lilipewa kibali cha ghorofa sita, lakini lilikuwa limejengwa hadi ghorofa 13.

Kutokana na hali hiyo, aliamuru mmiliki na mjenzi wakamatwe, huku uchunguzi wa kitaalamu ukiendelea kubaini kama msingi wa jengo hilo ulikuwa umeandaliwa kuhimili ghorofa hizo.

Itakumbukwa, baada ya jengo la Kariakoo kuporomoka na kuua watu 20, Rais Samia Suluhu Hassan, alipotembelea eneo la tukio saa chache baada ya kuwasili nchini akitokea Brazil, alisema Serikali haitasita kubomoa majengo yote ya Kariakoo iwapo tume iliyoundwa kuchunguza usalama wake itashauri ifanyike hivyo.

Sambamba na hilo, mkuu huyo wa nchi aliwasihi watendaji wa Serikali kuwajibika kwa nafasi zao, hasa katika mchakato wa utoaji vibali vya ujenzi, akitaka visimamiwe.

Rais aliagiza iundwe tume kuchunguza majengo yote, na tayari waziri mkuu wa wakati huo, Kassim Majaliwa, ameunda ikiwa na wajumbe 19, akibainisha matokeo yatakayopatikana yatawekwa wazi kwa wananchi.

Pamoja na kuwekwa wazi, alieleza iwapo tume hiyo itashauri majengo yote sokoni hapo yavunjwe, hatasita kufanya hivyo. Pia, Rais Samia alisema anatambua uwepo wa ripoti za tume mbalimbali, ikiwemo ya mwaka 2013, akisema uchunguzi unaofanywa utazingatia pia mapendekezo ya tume hiyo.

Mpaka sasa, ripoti ya tume hiyo ya wajumbe 19 haifahamiki kama ilishamaliza kazi na, kama imemaliza, ilibaini kitu gani.

Kifungu cha 33 cha Sheria ya Mipango Miji ya mwaka 2007 kinahusu hitaji la kupata kibali cha ujenzi kutoka mamlaka husika, huku Kifungu cha 36 kikihusu kumbukumbu za maombi na vibali vya ujenzi.

Kanuni za mwaka 2018 zinaweka utaratibu wa udhibiti na ukaguzi wa majengo, hivyo mwenye kibali cha kujenga idadi ya ghorofa husika hawezi kuongeza ghorofa nyingine tofauti na mpango ulioidhinishwa bila kufuata utaratibu wa kufanya mabadiliko na kupata idhini inayotakiwa.

Aidha, Kanuni ya 34 inaweka masharti kuhusu ukaguzi wa jengo lililokamilika na utoaji wa cheti cha matumizi, hatua ambayo inaweza kubaini tofauti kati ya ramani iliyoidhinishwa na jengo lililojengwa.

Wakili Fatma Kibakala anasema kibali hutolewa kwa kuzingatia nyaraka na michoro iliyowasilishwa, hivyo mwenye jengo anapaswa kujenga kulingana na kilichoidhinishwa.

“Ukipata kibali kwa msingi wa ramani fulani, wajibu wako ni kujenga kwa kuzingatia kile kilichoidhinishwa. Kama unataka kubadilisha, unatakiwa kuwasilisha mabadiliko kwa mamlaka husika na kupata idhini inayotakiwa,” anasema Fatma.

Anasema faini pekee haiwezi kuondoa wajibu wa kuhakikisha jengo ni salama.

“Adhabu ya ukiukaji wa masharti ya kibali ni suala moja, lakini usalama wa jengo ni suala jingine. Mmiliki anapaswa kuhakikisha mabadiliko yote yanafuata taratibu na jengo lina uwezo wa kutumika kwa usalama,” anasema.

Mtaalamu wa ujenzi, Dorcas Msabila, anasema kuongeza ghorofa si sawa na kuongeza vyumba ndani ya nyumba kwa sababu kila sakafu mpya huongeza mzigo unaobebwa na msingi, nguzo na mihimili.

Anasema wakati wa usanifu wa jengo, mhandisi hufanya hesabu kulingana na mzigo ambao mfumo wa jengo unatarajiwa kubeba.

“Ukiwa umebuni jengo kwa idadi fulani ya ghorofa, hesabu za kihandisi zinazingatia mzigo wa jengo hilo. Ukiongeza ghorofa bila kufanya tathmini na usanifu mpya, huwezi kusema moja kwa moja kwamba jengo lina uwezo wa kubeba mzigo huo,” anasema Msabila.

Msabila anasema kabla ya kuongeza sakafu, mhandisi anapaswa kuchunguza uwezo wa msingi, nguzo, mihimili na ubora wa vifaa vilivyotumika.

Anasema tathmini inaweza kuonesha kama jengo linaweza kubeba mzigo mpya au linahitaji uimarishaji wa kimuundo kabla ya kuendelea kutumika.

Mtaalamu wa ramani, Herison Amani, naamani ndiyo msingi wa kuhakikisha jengo linajengwa kwa kuzingatia mpango uliothibitishwa.

“Ukiwa umeidhinishiwa ghorofa nne, halafu ukaongeza nyingine bila kurekebisha ramani na kupata idhini, unakuwa umeondoka kwenye mpango uliokuwa umeidhinishwa,” anasema Amani.

Anasema mabadiliko hayo yanapaswa kuonyeshwa kwenye michoro mipya na kuchunguzwa na wataalamu wa usanifu na uhandisi kabla ya ujenzi kuendelea, kwani ubadilishwaji wa idadi ya ghorofa si mabadiliko madogo; ni lazima mfumo mzima wa jengo uangaliwe upya.

Mkandarasi wa majengo Kariakoo, Emmanuel Kambi, anasema hali hiyo inachangiwa na mmiliki baada ya kuona mfuko wake unaweza kuongeza idadi ya majengo tofauti na ramani ya awali.

“Tunajua ni kosa kuongeza kitu chochote wakati wa ujenzi tofauti na maelekezo ya ramani, lakini tunafanya kazi kwa matakwa ya mmiliki, kwani kazi yetu ni kutekeleza kile anachohitaji mteja kwa wakati huo,” anasema Kambi.

Anasema kingine kinachochangia ni kutokuwepo kwa ukaguzi wa mara kwa mara, kwani yapo majengo yanakaguliwa mtu akishamaliza hatua fulani, kisha wanakuja kuweka alama za kusimamisha au kubomoa.

Serikali imeonya wamiliki na waendelezaji wa majengo wanaojenga kinyume na michoro na vibali vilivyoidhinishwa, ikisema hatua hiyo ni ukiukaji wa sheria na inaweza kuhatarisha usalama wa majengo.

Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange, anasema kabla ya kuanza ujenzi, mjenzi anatakiwa kufuata taratibu, ikiwamo kupata michoro ya jengo, kuidhinishwa na mamlaka husika na kupata kibali cha ujenzi.

Anasema kibali huzingatia mambo mbalimbali, ikiwamo aina ya jengo, eneo linapojengwa, ukubwa wake, idadi ya ghorofa, aina ya udongo na, kwa baadhi ya miradi, tathmini ya athari za mazingira.

Dk Dugange anasema mjenzi anapaswa kujenga kulingana na kibali alichopewa na hawezi kuomba ghorofa mbili, kisha kuongeza ghorofa nyingine bila kupata idhini ya mamlaka husika.

“Ukiomba kibali cha ghorofa mbili, huwezi kujenga ghorofa tatu. Hilo ni kosa kisheria,” anasema.

Anasema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masharti ya vibali vya ujenzi, huku wataalamu wa Serikali wakifanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali kuhakikisha ujenzi unazingatia sheria, ubora na viwango vinavyotakiwa.

Anasema ikibainika jengo linajengwa kinyume na kibali, hatua huchukuliwa, ikiwamo kusimamisha ujenzi na kuchukua hatua za kisheria kulingana na aina ya ukiukwaji.

Pia, anasisitiza umuhimu wa serikali za mitaa kushiriki katika ufuatiliaji wa ujenzi unaoendelea katika maeneo yao.

Anasema viongozi na watendaji wa serikali za mitaa wana wajibu wa kufuatilia shughuli za ujenzi na kutoa taarifa pale wanapoona ukiukwaji wa taratibu.

Anasema ufuatiliaji hufanyika hatua kwa hatua ili kuhakikisha kile kilichoombwa na kuidhinishwa ndicho kinachojengwa. 

Jamhuri yafunga ushahidi kesi ya Lissu

Dar es Salaam. Jamhuri imefunga ushahidi wake katika kesi ya uhaini  inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu, 

Jamhuri imefunga ushahidi huo leo Jumatatu Agosti 17, 2026 baada ya kuwaita mashahidi 17 kati ya 30 waliokuwa wameorodheshwa.

Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kusudio la kuzuia kufanyika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kwa kutamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi mkuu wa Serikali ya Tanzania, kuwa:-

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko… kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli… tunaenda kukinukisha vibaya sana…”

Kesi hiyo inasikilizwa na Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, ilipangwa kuendelea leo kwa ushahidi wa upande wa Jamhuri.

Hata hivyo baada ya kesi kuitwa Jamhuri kupitia mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali  Mkuu Ajuaye Nzegeli ameieleza Mahakama kuwa baada ya kupitia ushahidi uliokwishawasilishwa na kuangalia ushahidi wa mashahidi waliosalia wameona ushahidi waliokwishawasilishwa unatosheleza.

“Hivyo tunapenda kuitaarifu Mahakama hii tukufu kuwa upande wa Jamhuri unafunga ushahidi wake kwa mashahidi 17”, amesema Wakili Nzegeli.

Baada ya Jamhuri kufunga ushahidi wake sasa kesi imeingia katika hatua ya pili ambapo pande zote zinawasilisha hoja kuishawishi mahakama kama mshtakiwa kwa ushahidi huo ana kesi ya kujibu au la.

Kwa sasa ameanza mshtakiwa Lissu kuwasilisha hoja zake kuishawishi Mahakama kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuonesha kuwa kuna kesi ya kumfanya ajitetee, kabla ya upande wa mashtaka kujibu hoja hizo kuionesha Mahakama kuwa imeweza kujenga kesi kiasi cha kumlazimu mshtakiwa kujitetea kabla ya kutoa hukumu.

Lissu alivyoishawishi Mahakama hana kesi ya kujibu, aomba fidia

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amewasilisha hoja za kisheria akiishawishi Mahakama Kuu kuwa hana kesi ya kujibu katika shtaka la uhaini linalomkabili, akiiomba imuachilie huru na iamuru alipwe fidia.

Lissu amewasilisha hoja hizo leo Jumatatu, Agosti 17, 2026, baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wake katika kesi hiyo.

Jamhuri imefunga ushahidi baada ya kuwaita mashahidi 17 kati ya 30 waliokuwa wameorodheshwa kutoa ushahidi.

Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyodaiwa kuyatamka kuhusu kusudio la kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025, kwa kutamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi mkuu wa Serikali, akisema: “Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”

Kesi hiyo inasikilizwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, mbele ya jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Baada ya kesi kuitwa leo, Wakili wa Serikali Mkuu, Ajuaye Nzegeli, aliiambia Mahakama kuwa baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa na ushahidi wa mashahidi waliosalia, Jamhuri imeona uliopo unatosheleza.

“Hivyo tunapenda kuitaarifu Mahakama hii tukufu kuwa upande wa Jamhuri unafunga ushahidi wake kwa mashahidi 17,” amesema Nzegeli.

Baada ya Jamhuri kufunga ushahidi, iliomba fursa ya kuwasilisha hoja za kisheria iwapo kwa kuzingatia ushahidi uliowasilishwa Lissu ana kesi ya kujibu. Ombi hilo liliungwa mkono na Lissu na Mahakama ikatoa fursa kwa pande zote kuwasilisha hoja, huku Lissu akiwa wa kwanza kabla ya Jamhuri kujibu.

Katika hoja zake, Lissu amesema ushahidi wa mashahidi 17 umeshindwa kujenga kesi dhidi yake kiasi cha kumlazimisha kujitetea.

Ameanza kwa kurejea maamuzi ya Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki katika kesi za Grey Likungu Mataka na wenzake dhidi ya Jamhuri na Hatibu Gandhi na wenzake.

Amesema kesi hizo ziliweka masharti matatu ya kuthibitisha uhaini: kwanza, mshtakiwa kuwa na utiifu kwa Jamhuri ya Muungano; pili, kuwa na nia ya kutenda uhaini; na tatu, nia hiyo ithibitishwe kwa maandishi au matendo ya wazi.

Amesema suala la utiifu halina mjadala kwa kuwa amekubali kuwa ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo hoja ni iwapo kulikuwa na nia ya kutenda uhaini na kama nia hiyo ilithibitishwa kwa maandishi au matendo ya wazi.

Amesema katika kesi ya Grey Likungu, Jaji Mkuu wa wakati huo, Francis Nyalali, alisisitiza kuwa hatia ya uhaini inahitaji uthibitisho wa matendo ya wazi, nia ya kutenda uhaini na utiifu wa mtuhumiwa kwa Jamhuri ya Muungano.

Kwa mujibu wa Lissu, katika kesi ya Hatibu Gandhi, Mahakama ya Rufani ilijiuliza iwapo maneno matupu ya mshtakiwa yanaweza kutengeneza kosa la uhaini na ikaweka msimamo kuwa maneno matupu si matendo ya wazi, isipokuwa yanaelezea kitendo cha uhaini.

Amesema kitendo cha uhaini kinaweza kuwa ni kuelekeza namna ya kupindua Serikali na hatua za kutekeleza hilo, si kusema tu mtu anataka kupindua Serikali. Hata hivyo, amesema Mahakama ilieleza kuwa msimamo wa maneno matupu hautumiki kwa mshtakiwa mmoja bali unaweza kuwa tofauti kwa watu wengi ambapo maneno yanaweza kujenga njama ya kufanya uhaini.

Akirejea ushahidi uliotolewa katika kesi yake, Lissu amesema Jamhuri haijathibitisha nia ya kutenda uhaini.

Amesema kifungu alichoshtakiwa nacho kinahusu kuhamasisha watu waitishe Serikali, Bunge au Mahakama, na nia hiyo lazima ithibitishwe kwa maandishi au matendo ya wazi.

Amesema katika maneno yanayodaiwa kuwa ya uhaini, Serikali, Bunge wala Mahakama havikutajwa.

“Katika mashahidi wote 17 kila aliyezungumzia maneno hayo nilimuuliza Serikali imetajwa humo? Haimo,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali ina maana ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Halmashauri, huku akisema kila shahidi aliulizwa kama alimtaja Rais, waziri mkuu au mkuu wa mkoa na hakuna aliyethibitisha.

Amesema uchaguzi unasimamiwa na Tume ya Uchaguzi, si Serikali, hivyo kwa kuangalia hati ya mashtaka, Serikali haiwezi kutishiwa kwa kuzuia uchaguzi.

Pia amedai maneno ya kuzuia uchaguzi na kukinukisha hayamo katika orodha ya makosa ya jinai chini ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2025, Sheria ya Kanuni ya Adhabu au sheria nyingine nchini.

“Kwa hiyo uthibitisho wa uhaini kama ilivyowekwa kwenye kesi ya Grey na Gandhi haupo na kwa hakika hakuna ushahidi wa nia ya kutenda kosa lolote kwa mujibu wa sheria zinazojulikana Tanzania,” amesema.

Lissu amesema katika kesi hiyo anashtakiwa peke yake kwa kutoa maneno, ilhali Mahakama ya Rufani katika kesi ya Gandhi ilisema hakuna kosa la maneno kwa mshtakiwa mmoja.

“Kwa hiyo waheshimiwa majaji kama ushahidi uliotolewa umeshindwa kuthibitisha kesi ya kutenda kosa la uhaini, nitajitetea kwa lipi? Kwa hoja hiyo peke yake sina kesi ya kujibu,” amesema.

Kuhusu madai ya uchapishaji wa maneno hayo kwenye Jambo TV, Lissu amesema Jamhuri ilipaswa kuwasilisha video na ripoti ya uchunguzi wa video hizo, lakini hakuna shahidi kati ya 17 aliyewasilisha vielelezo hivyo.

Amesema Jamhuri iliahidi kuwasilisha nyaraka tisa, zikiwemo video clips na ripoti ya uchunguzi, lakini havikuwasilishwa. Kwa hiyo, amesema mashahidi walieleza tu kuwa waliona video bila kuiwasilisha mahakamani.

Lissu amesema kati ya mashahidi 17, shahidi wa 17 pekee ndiye aliyekuwepo kwenye mkutano ambako alitamka maneno hayo, huku wengine 16 wakiwa mashahidi wa kusikia.

Amesema shahidi huyo alisema yeye na wenzake watano walirekodi na kuchapisha video, hivyo hakuna ushahidi kwamba Lissu ndiye aliyeichapisha.

Kuhusu madai kwamba yeye ndiye aliyeitisha mkutano, Lissu amesema shahidi huyo alieleza kuwa mwaliko ulitolewa na Ofisa Habari wa Chadema, Brenda Lupia, na kwamba hakumuona Lissu akifanya maandalizi ya mkutano huo.

Kwa sababu hizo, Lissu ameiomba Mahakama imuachilie huru bila kumtaka kujitetea na, ikiwa itaridhika kuwa hana kesi ya kujibu, itoe uamuzi huo leo ili asirudi gerezani, huku uamuzi wa maandishi ukitolewa baadaye.

Pia ameiomba Mahakama iamuru alipwe fidia, akisema amekaa gerezani kwa siku 496 kwa mashtaka anayodai hayana msingi wa kisheria na kwamba sheria inaipa Mahakama mamlaka ya kutoa fidia.