Lissu alivyoishawishi Mahakama hana kesi ya kujibu, aomba fidia

Written by

in

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amewasilisha hoja za kisheria akiishawishi Mahakama Kuu kuwa hana kesi ya kujibu katika shtaka la uhaini linalomkabili, akiiomba imuachilie huru na iamuru alipwe fidia.

Lissu amewasilisha hoja hizo leo Jumatatu, Agosti 17, 2026, baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wake katika kesi hiyo.

Jamhuri imefunga ushahidi baada ya kuwaita mashahidi 17 kati ya 30 waliokuwa wameorodheshwa kutoa ushahidi.

Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyodaiwa kuyatamka kuhusu kusudio la kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025, kwa kutamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi mkuu wa Serikali, akisema: “Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”

Kesi hiyo inasikilizwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, mbele ya jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Baada ya kesi kuitwa leo, Wakili wa Serikali Mkuu, Ajuaye Nzegeli, aliiambia Mahakama kuwa baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa na ushahidi wa mashahidi waliosalia, Jamhuri imeona uliopo unatosheleza.

“Hivyo tunapenda kuitaarifu Mahakama hii tukufu kuwa upande wa Jamhuri unafunga ushahidi wake kwa mashahidi 17,” amesema Nzegeli.

Baada ya Jamhuri kufunga ushahidi, iliomba fursa ya kuwasilisha hoja za kisheria iwapo kwa kuzingatia ushahidi uliowasilishwa Lissu ana kesi ya kujibu. Ombi hilo liliungwa mkono na Lissu na Mahakama ikatoa fursa kwa pande zote kuwasilisha hoja, huku Lissu akiwa wa kwanza kabla ya Jamhuri kujibu.

Katika hoja zake, Lissu amesema ushahidi wa mashahidi 17 umeshindwa kujenga kesi dhidi yake kiasi cha kumlazimisha kujitetea.

Ameanza kwa kurejea maamuzi ya Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki katika kesi za Grey Likungu Mataka na wenzake dhidi ya Jamhuri na Hatibu Gandhi na wenzake.

Amesema kesi hizo ziliweka masharti matatu ya kuthibitisha uhaini: kwanza, mshtakiwa kuwa na utiifu kwa Jamhuri ya Muungano; pili, kuwa na nia ya kutenda uhaini; na tatu, nia hiyo ithibitishwe kwa maandishi au matendo ya wazi.

Amesema suala la utiifu halina mjadala kwa kuwa amekubali kuwa ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo hoja ni iwapo kulikuwa na nia ya kutenda uhaini na kama nia hiyo ilithibitishwa kwa maandishi au matendo ya wazi.

Amesema katika kesi ya Grey Likungu, Jaji Mkuu wa wakati huo, Francis Nyalali, alisisitiza kuwa hatia ya uhaini inahitaji uthibitisho wa matendo ya wazi, nia ya kutenda uhaini na utiifu wa mtuhumiwa kwa Jamhuri ya Muungano.

Kwa mujibu wa Lissu, katika kesi ya Hatibu Gandhi, Mahakama ya Rufani ilijiuliza iwapo maneno matupu ya mshtakiwa yanaweza kutengeneza kosa la uhaini na ikaweka msimamo kuwa maneno matupu si matendo ya wazi, isipokuwa yanaelezea kitendo cha uhaini.

Amesema kitendo cha uhaini kinaweza kuwa ni kuelekeza namna ya kupindua Serikali na hatua za kutekeleza hilo, si kusema tu mtu anataka kupindua Serikali. Hata hivyo, amesema Mahakama ilieleza kuwa msimamo wa maneno matupu hautumiki kwa mshtakiwa mmoja bali unaweza kuwa tofauti kwa watu wengi ambapo maneno yanaweza kujenga njama ya kufanya uhaini.

Akirejea ushahidi uliotolewa katika kesi yake, Lissu amesema Jamhuri haijathibitisha nia ya kutenda uhaini.

Amesema kifungu alichoshtakiwa nacho kinahusu kuhamasisha watu waitishe Serikali, Bunge au Mahakama, na nia hiyo lazima ithibitishwe kwa maandishi au matendo ya wazi.

Amesema katika maneno yanayodaiwa kuwa ya uhaini, Serikali, Bunge wala Mahakama havikutajwa.

“Katika mashahidi wote 17 kila aliyezungumzia maneno hayo nilimuuliza Serikali imetajwa humo? Haimo,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali ina maana ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Halmashauri, huku akisema kila shahidi aliulizwa kama alimtaja Rais, waziri mkuu au mkuu wa mkoa na hakuna aliyethibitisha.

Amesema uchaguzi unasimamiwa na Tume ya Uchaguzi, si Serikali, hivyo kwa kuangalia hati ya mashtaka, Serikali haiwezi kutishiwa kwa kuzuia uchaguzi.

Pia amedai maneno ya kuzuia uchaguzi na kukinukisha hayamo katika orodha ya makosa ya jinai chini ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2025, Sheria ya Kanuni ya Adhabu au sheria nyingine nchini.

“Kwa hiyo uthibitisho wa uhaini kama ilivyowekwa kwenye kesi ya Grey na Gandhi haupo na kwa hakika hakuna ushahidi wa nia ya kutenda kosa lolote kwa mujibu wa sheria zinazojulikana Tanzania,” amesema.

Lissu amesema katika kesi hiyo anashtakiwa peke yake kwa kutoa maneno, ilhali Mahakama ya Rufani katika kesi ya Gandhi ilisema hakuna kosa la maneno kwa mshtakiwa mmoja.

“Kwa hiyo waheshimiwa majaji kama ushahidi uliotolewa umeshindwa kuthibitisha kesi ya kutenda kosa la uhaini, nitajitetea kwa lipi? Kwa hoja hiyo peke yake sina kesi ya kujibu,” amesema.

Kuhusu madai ya uchapishaji wa maneno hayo kwenye Jambo TV, Lissu amesema Jamhuri ilipaswa kuwasilisha video na ripoti ya uchunguzi wa video hizo, lakini hakuna shahidi kati ya 17 aliyewasilisha vielelezo hivyo.

Amesema Jamhuri iliahidi kuwasilisha nyaraka tisa, zikiwemo video clips na ripoti ya uchunguzi, lakini havikuwasilishwa. Kwa hiyo, amesema mashahidi walieleza tu kuwa waliona video bila kuiwasilisha mahakamani.

Lissu amesema kati ya mashahidi 17, shahidi wa 17 pekee ndiye aliyekuwepo kwenye mkutano ambako alitamka maneno hayo, huku wengine 16 wakiwa mashahidi wa kusikia.

Amesema shahidi huyo alisema yeye na wenzake watano walirekodi na kuchapisha video, hivyo hakuna ushahidi kwamba Lissu ndiye aliyeichapisha.

Kuhusu madai kwamba yeye ndiye aliyeitisha mkutano, Lissu amesema shahidi huyo alieleza kuwa mwaliko ulitolewa na Ofisa Habari wa Chadema, Brenda Lupia, na kwamba hakumuona Lissu akifanya maandalizi ya mkutano huo.

Kwa sababu hizo, Lissu ameiomba Mahakama imuachilie huru bila kumtaka kujitetea na, ikiwa itaridhika kuwa hana kesi ya kujibu, itoe uamuzi huo leo ili asirudi gerezani, huku uamuzi wa maandishi ukitolewa baadaye.

Pia ameiomba Mahakama iamuru alipwe fidia, akisema amekaa gerezani kwa siku 496 kwa mashtaka anayodai hayana msingi wa kisheria na kwamba sheria inaipa Mahakama mamlaka ya kutoa fidia.

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *