Maboresho ya Bandari ya Mtwara yameanza kuleta mabadiliko katika shughuli za usafirishaji na biashara huku ongezeko la shehena likifungua fursa kwa wananchi, madereva, wafanyabiashara na watoa huduma mbalimbali.
Mabadiliko hayo yanatokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ukiwamo upanuzi wa magati, kuongeza mitambo ya kisasa na kuboresha miundombinu inayorahisisha meli na magari kuhudumiwa kwa wakati.
Bandari hiyo sasa inapokea shehena mbalimbali, zikiwamo magari makubwa, vifaa vya ujenzi wa miradi ya kimkakati, saruji, mafuta, makaa ya mawe, mbaazi na korosho. Baadhi ya mizigo hiyo husafirishwa kwenda nchi jirani za Malawi, Zambia, Zimbabwe, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Msumbiji.
Mamalishe wa eneo la bandarini, Rehema Mputa, anasema maboresho ya bandari yamebadili biashara yake na kuongeza kipato.
Anasema awali alikuwa akitumia kilo moja ya ngano kutengeneza chapati kwa siku, lakini sasa anatumia kilo nne na zote zinaisha.
“Yaani mimi kipindi hicho biashara ilikuwa ngumu sana hapa, lakini mpaka leo nimemsomesha mtoto wangu amemaliza kidato cha nne kwa fedha hizihizi za mamalishe,” anasema.
Rehema anasema ongezeko la biashara limemwezesha pia kuwekeza katika kilimo cha mazao mbalimbali, ikiwamo korosho, kwa kuwa na uwezo wa kuwalipa wakulima.
Anasema anaomba maboresho ya bandari yaendelee kwa sababu kuongezeka kwa shughuli kunawapa wananchi fursa zaidi za kujipatia kipato.
Naye kiongozi wa madereva bodaboda katika eneo la matangi ya mafuta bandarini, Issa Mchika, anasema shughuli za bandari zimeongeza abiria na kipato kwa madereva.
“Kiukweli, ujio wa bandari umetusaidia sana sisi wananchi, hususan sisi madereva bodaboda,” anasema.
Mchika anasema uwepo wa depo, magari ya mizigo na magari ya mafuta umeongeza shughuli za usafiri, huku wageni wanaokuja Mtwara wakitumia hoteli, migahawa na huduma za bodaboda.
Anasema awali wananchi wengi, wakiwamo madereva na mama lishe, walitegemea zaidi msimu wa korosho, lakini ongezeko la shughuli za bandari limeleta biashara katika kipindi kirefu zaidi.
Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara, Hekima Ngezi, anasema bandari hiyo iliyoanzishwa mwaka 1950 imeboreshwa kwa kuongeza uwezo wa kuhudumia meli na shehena kubwa.
Ngezi anasema awali Bandari ya Mtwara ilikuwa ya msimu, ikitegemea zaidi karanga na baadaye korosho, lakini Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan iliona umuhimu wa kuiongezea uwezo ili ifanye kazi kwa ufanisi mwaka mzima.
Anasema gati zimeongezwa kutoka tatu hadi nne, huku gati moja likiwa na urefu wa mita 300 na kina cha maji cha mita 13, hali inayowezesha meli kubwa kutia nanga na kupakia au kushusha shehena nyingi zaidi.
“Mpaka sasa, Bandari ya Mtwara inahudumia shehena ya mafuta, korosho, makaa ya mawe, mbaazi na saruji na tunahudumia magari makubwa. Kuanzia Februari mwaka huu hadi sasa, tumehudumia meli 23 na magari 6,390,” anasema.
Anasema saruji kutoka Kiwanda cha Dangote husafirishwa kwenda Zanzibar, Comoro na Msumbiji kwa ajili ya miradi ya Gesi Asilia (LNG).
Ngezi anasema Serikali inaendelea kujenga gati jipya katika eneo la Kisiwa Mpangawe/Kisiwa Mgao, lenye urefu wa mita 300 na kina cha maji mita 15. Ujenzi wake umefikia asilimia 44 na unatarajiwa kukamilika mwakani.
“Bandari hii au gati hili ni maalum kwa ajili ya kusafirisha mizigo michafu. Kwa hiyo, mizigo yote ile ambayo ina asili ya vumbi kama saruji pamoja na makaa ya mawe na aina nyingine itaweza kupelekwa au kuhudumiwa katika gati hilo jipya,” anasema.
Anasema gati hilo litaongeza uwezo wa bandari kuhudumia shehena nyingi zaidi, akieleza eneo la Kisiwa Mgao lina uwezo wa kuhudumia tani 100,000 kwa pamoja.
Kwa mujibu wa Ngezi, zaidi ya magari 6,000 yaliyohudumiwa bandarini tangu Februari yameelekezwa katika nchi zinazozunguka Tanzania, zikiwamo Malawi, Msumbiji, Zambia, Zimbabwe, DRC, Burundi na Rwanda.
Anasema lengo la TPA ni kuendelea kuongeza uwezo wa Bandari ya Mtwara ili iweze kuhudumia wateja wengi zaidi, akisisitiza kuwa mitambo bora na ya kisasa ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa upakiaji na upakuaji wa shehena.
Kiungo cha Ushoroba wa Kusini
Ngezi anasema Bandari ya Mtwara ipo katika Ushoroba wa Kusini unaounganisha mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma, hivyo ina nafasi muhimu katika kukuza biashara ya ndani na kuvuka mipaka.
Anasema malengo ya TPA ni kuhakikisha bandari hiyo inakuwa kiunganishi na chachu ya kukuza ushoroba huo, ambako mizigo itatoka Mtwara kupitia Lindi na Ruvuma hadi Bandari ya Mbamba Bay na baadaye kwenda Malawi.
“Kwa hiyo malengo ya mamlaka ni kuhakikisha Bandari ya Mtwara inakuwa kiunganishi na chachu ya kukuza ushoroba wa kusini ambapo mizigo yetu itatoka hapa Bandari ya Mtwara ikipitia mikoa ya Lindi na Ruvuma mpaka Bandari ya Mbamba Bay, ambapo katika bandari ile mizigo hiyo itaweza kuvuka kwenda nchi jirani ya Malawi,” anasema.
Anasema kuimarika kwa ushoroba huo kutachochea biashara katika mikoa ya kusini na kuongeza fursa kwa wananchi na wafanyabiashara.
Ngezi anasema Bandari ya Dar es Salaam ina mzigo mkubwa, hivyo TPA imeona ni muhimu baadhi ya mizigo ipitie Mtwara ili kupunguza mzigo katika bandari hiyo na kutoa huduma kwa wakati.
“Nafuu iliyopo ya kupitishia mizigo katika Bandari ya Mtwara, tunao uwezo wa kuitumikia kwa wakati na kuweza kuokoa muda ambao unatumika katika kuisafirisha mizigo kwenda Burundi, Rwanda, Zambia, Zimbabwe na Malawi,” anasema.
Anasema kutumia Mtwara kunaweza kupunguza muda wa kusafirisha mizigo kwa nchi zinazotumia njia hiyo, huku pia kukiwa na nafasi ya kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo yanayopitiwa na ushoroba.
Kuhusu fursa zinazotokana na maboresho hayo, Ngezi anasema wananchi wanaozunguka bandari tayari wanaanza kunufaika kutokana na ongezeko la shehena na mahitaji ya huduma mbalimbali.
Anasema ongezeko la magari yanayoingia na kutoka bandarini limeongeza mahitaji ya madereva, hasa wale wanaosafirisha magari na mizigo kwenda nchi jirani.
“Tulipoanza kupitisha shehena ya magari, magari haya yanahitaji madereva. Madereva ambao watayatoa magari haya kwenye yadi zetu, lakini madereva watakayosafirisha magari haya kuyatoa Mtwara kuyapeleka nchi husika au kwenye mipaka ya mataifa husika hiyo ni fursa,” anasema.
Kuhusu mradi wa LNG wa Lindi, Ngezi anasema bandari imejipanga kuhudumia vifaa mbalimbali vitakavyotumika katika miradi ya gesi, kwa kutumia mitambo ya kisasa.
“Tunafahamu miradi hii ya gesi lazima itakuwa na shehena ya vifaa mbalimbali ambavyo vitatumika katika uchimbaji wa gesi, sisi tumejipanga mitambo ya kisasa, ambayo ni kitu cha kwanza kabisa, bandari haiwezi kufanya kazi bila mitambo,” anasema.
Anasema bandari ina mitambo ya kupakua na kushusha shehena ambayo inaweza kutumika katika shughuli zinazohusiana na miradi ya gesi.
Kuhusu kuzuia msongamano wa magari, Ngezi anasema bandari imejipanga kutumia Bandari Kavu (ICDs) endapo kutakuwa na ongezeko kubwa la magari au shehena.
Anasema maeneo ya bandari ambayo hayajatumika kikamilifu yanaweza kutumika kuhifadhi mizigo, huku ICD ya Mangachini ikiwa ni miongoni mwa maeneo yanayoweza kusaidia kupunguza msongamano.
Wakala wa Meli wa Joyous Shipping Service Ltd, Esthersia Mallya, anasema mazingira ya Bandari ya Mtwara yamebadilika, huku idadi ya meli ikiongezeka na huduma kutolewa kwa wakati.
“Hapa Mtwara hakuna kabisa,” anasema wakati akizungumzia changamoto ya foleni.
Anasema Serikali na uongozi wa bandari wamefanya juhudi kuboresha mazingira yanayozunguka bandari, ikiwamo barabara zinazorahisisha magari kuingia na kutoka.
“Uboreshaji ambao umefanyika pamoja na mifumo ya namna ya kuhifadhi mizigo, kiasi kwamba mzigo wako utakavyoingia ndivyo utakavyoupata,” anasema.
Mallya anasema hali hiyo ni manufaa kwa wafanyabiashara na mawakala kwa sababu meli zinapofika hupata huduma kwa wakati, hivyo mizigo kushushwa na kupakiwa bila kuchelewa.
Anashauri wafanyabiashara na mawakala ambao wamekuwa wakitegemea zaidi Bandari ya Dar es Salaam kuangalia uwezekano wa kutumia Mtwara kutokana na kutokuwapo kwa foleni kubwa.
Madereva wachangamkie fursa
Wakala wa Baruti International Limited, Abdulrahman Upete, anasema Bandari ya Mtwara imewekeza katika mitambo mbalimbali inayorahisisha utendaji wa kazi na kuzipa nafuu Bandari za Dar es Salaam na Tanga.
Anasema kampuni yao, yenye ofisi Dar es Salaam na Tanga pia inatarajia kuwa na tawi Unguja, imeweza kuwahudumia wateja wake kwa kutumia Bandari ya Mtwara.
Aidha, Upete anasema maboresho hayo yameifanya Mtwara kuwa kiungo kwa nchi zinazozunguka Tanzania, zikiwamo Msumbiji, Malawi, Congo na Zambia, huku ikianza kupokea mizigo ya magari, mashine na vifaa vya ujenzi kutoka mataifa mbalimbali.
Anashauri Serikali kuendelea kuwekeza katika mitambo na miundombinu ili kuongeza ufanisi wa bandari.
Anasema uwekezaji zaidi utaifanya Mtwara kuwa lango kuu la kusini katika kuingiza na kusafirisha mizigo kwenda maeneo mbalimbali.
Upete amewataka wadau wa usafirishaji wa magari na mitambo pamoja na wananchi kuchangamkia fursa za udereva na huduma zinazohusiana na usafirishaji.
“Magari mengi yanapita hapa, mahitaji ya madereva yameongezeka, mahitaji ya magari ya kusaidia nayo yanahitajika, kwa sababu mara nyingine yanakuja ‘matrailer’ hapa yanatakiwa magari ya kuvuta,” anasema.
Anasema baadhi ya magari yanayopita Mtwara yanaendelea na safari kwenda nje ya Tanzania, hivyo kuna umuhimu kwa madereva wa eneo hilo kupata ujuzi na uzoefu wa usafirishaji wa kimataifa.
Anasema madereva wengi waliopo Mtwara hawana uzoefu wa kuvuka mipaka, jambo linaloweza kuwa changamoto wakati wa kusafirisha magari au mitambo kwenda Malawi, Zambia, Congo na nchi nyingine.
“Kwa hiyo kuna haja ya madereva waliopo hapa Mtwara sasa kuingia vyuoni kama Veta ili kupata uzoefu na ujuzi zaidi kwa sababu unapotoka nje ya mipaka ya Tanzania kuna taratibu zake,” anasema.