Tiseza yawatafutia soko wenye ulemavu wa kusikia 

Dar es Salaam. Ili kuhakikisha makundi yote yanashiriki na kunufaika na fursa zinazotokana na uwekezaji nchini, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum Tanzania (Tiseza) imeingia makubaliano na Ella Foundation kutumia mifuko inayozalishwa na watu wenye ulemavu wa kusikia kama zawadi kwa wawekezaji wanaofika nchini.

Mifuko hiyo inazalishwa na watu wenye uziwi kupitia ujuzi wanaoupata katika taasisi hiyo ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha kujitegemea na kuwapatia soko la uhakika la bidhaa zao.

Mkurugenzi wa Tiseza, Hilead Teri anasema ushirikiano huo ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu la mamlaka kuhakikisha fursa za uwekezaji zinawafikia Watanzania wote wakiwamo watu wenye mahitaji maalumu.

Anasema miongoni mwa bidhaa zinazozalishwa na watu hao ni mifuko yenye ubora ambayo sasa Tiseza itakuwa ikinunua na kuitumia kama zawadi rasmi kwa wawekezaji wanaokuja nchini.

“Tutakuwa washirika wao wa kununua bidhaa ambazo zimetengenezwa na watu wenye makundi maalumu. Mfano ni mifuko hii ambayo tutaendelea kuitumia na kuwapatia wawekezaji mbalimbali,” anasema.

Kwa mujibu wa Teri, hatua hiyo inalenga kutoa soko endelevu kwa bidhaa huku ikiwezesha taasisi za Serikali kutumia mahitaji yao ya kawaida kuchochea matokeo chanya katika jamii.

Anasema awali Tiseza imekuwa ikitumia bidhaa zinazozalishwa nchini, ikiwamo korosho na mvinyo kama sehemu ya zawadi kwa wawekezaji hivyo kuongeza bidhaa zinazotengenezwa na watu wenye mahitaji maalumu kutasaidia kupanua fursa hizo.

“Tumekuwa tukitumia bidhaa za Tanzania kama korosho na mvinyo kwa wawekezaji. Sasa tutaongeza bidhaa hizi ambazo zimetengenezwa na watu wenye mahitaji maalumu. Hatua hii itawasaidia kupata soko endelevu la bidhaa zao na kuongeza fursa za kiuchumi,” anasema.

Anasema ushirikiano huo pia unaonyesha namna taasisi zinavyoweza kutumia shughuli zao za kawaida kusaidia makundi maalumu, huku ukichochea ubunifu, ujuzi na maisha endelevu kwa vijana.

Teri anasema Tiseza inalenga kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu na Ella Foundation katika kuunga mkono na kutangaza ubunifu na ujuzi wa watu wenye mahitaji maalumu.

“Tutaangalia katika sera zetu kwani kuna baadhi ya kazi zinaweza kufundishwa hivyo tutawashawishi wawekezaji kuwa wanapotoa ajira wawafanye watu wenye ulemavu kuwa sehemu ya wanufaika,” anasema.

Kwa upande wake, mwanzilishi wa Ella Foundation, Esther Jaswant anasema ulemavu haupaswi kuwa kikwazo kwa mtu kupata uhuru wa kiuchumi, hivyo taasisi hiyo imeanzisha miradi ya uzalishaji wa bidhaa zenye ubora ili kuwasaidia viziwi kujitegemea.

“Moja ya miradi yetu ni kuzalisha bidhaa zenye ubora ili kusaidia viziwi kujikwamua kiuchumi. Fursa tuliyopata inatoa ujumbe kwamba Tanzania inawathamini watu wenye ulemavu, kwani mifuko yetu ina nembo inayoonyesha imetengenezwa na nani,” anasema.

Aliongeza kuwa matumizi ya bidhaa hizo na Tiseza kama zawadi kwa wawekezaji ni fursa muhimu ya kuitangaza kazi inayofanywa na viziwi, huku ikiwapatia soko na kuongeza thamani ya ujuzi wanaoupata.

Hizi hapa fursa zilizopo wazi sekta ya gesi asilia

Wakati zaidi ya vyombo 20,000 vya usafiri nchini vikitumia gesi asilia, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imebainisha fursa tisa za uwekezaji katika sekta hiyo, zikiwamo ujenzi wa karakana za kubadili mifumo ya magari kutumia nishati hiyo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, hadi Aprili mwaka huu zaidi ya vyombo vya usafiri 20,000 vilikuwa vinatumia gesi asilia, hatua inayoonyesha matumizi ya nishati hiyo yanaendelea kukua nchini kutokana na gharama zake kuwa nafuu na mchango wake katika matumizi ya nishati safi.

Pamoja na ongezeko hilo, idadi ya karakana zilizoidhinishwa kufunga mifumo ya matumizi ya gesi asilia kwenye magari ilikuwa 13 pekee hadi kipindi hicho.

Ewura inaeleza hali hiyo inaonyesha bado kuna nafasi kubwa kwa wawekezaji kuingia katika biashara ya kutoa huduma za ubadilishaji wa mifumo ya magari kutoka mafuta kwenda gesi asilia.

Katika Ripoti ya Utendaji wa Sekta Ndogo ya Gesi ya mwaka 2025 iliyotolewa mwaka huu, Ewura imeainisha maeneo tisa yenye fursa za uwekezaji yanayoweza kusaidia kuongeza matumizi ya gesi asilia na kukuza shughuli za kiuchumi nchini.

Miongoni mwa fursa hizo ni ujenzi na uendeshaji wa vituo vikuu vya kuzalisha gesi asilia iliyogandamizwa (Compressed Natural Gas-CNG), ambayo hutumika kama nishati ya magari na matumizi mengine ya kibiashara.

Pia kuna fursa za kujenga na kuendesha vituo vya kujaza CNG vilivyounganishwa na mtandao wa mabomba ya gesi asilia kwa matumizi ya umma na binafsi, pamoja na vituo vinavyopokea gesi kupitia malori maalumu ya CNG kwa ajili ya kuhudumia maeneo ambayo bado hayajafikiwa na miundombinu ya mabomba.

Ripoti hiyo pia imeonyesha nafasi za uwekezaji katika vituo vidogo vya kusambaza CNG kwa matumizi ya viwandani, biashara, uzalishaji wa umeme na majumbani, sambamba na biashara ya usafirishaji wa gesi hiyo kutoka eneo moja kwenda jingine.

Fursa nyingine ni utoaji wa huduma za ukaguzi na uthamini wa mifumo ya CNG inayofungwa kwenye magari ili kuhakikisha inakidhi viwango vya usalama, pamoja na uwekezaji katika biashara ya usafiri kwa kutumia mabasi, malori na teksi zinazotumia gesi asilia.

Mbali na fursa hizo, Serikali inasema imeendelea kuweka mazingira yanayovutia uwekezaji kupitia sera, sheria na mipango mbalimbali inayolenga kuifanya sekta ya gesi kuwa moja ya nguzo za maendeleo ya uchumi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dk James Mataragio alisema uwepo wa Sera ya Taifa ya Nishati ni miongoni mwa sababu zinazotoa uhakika kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika sekta hiyo.

Alisema Serikali pia imeandaa Mpango Kabambe wa Matumizi ya Gesi Asilia (Natural Gas Utilisation Master Plan-NGUMP) unaoainisha maeneo ya kipaumbele ya matumizi ya gesi, ikiwamo uzalishaji wa umeme, maendeleo ya viwanda, matumizi ya majumbani na biashara, viwanda vya petrokemia, uzalishaji wa mbolea pamoja na mauzo ya gesi katika soko la ndani na nje ya nchi.

Dk Mataragio alisema kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, wawekezaji wanapata nafasi ya kushiriki katika kufadhili, kujenga, kuendesha na kutunza miradi mikubwa ya gesi, hatua inayosaidia kuvutia mitaji na teknolojia mpya.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Biashara ya Mafuta na Gesi Asilia wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Emmanuel Gilbert alisema bado kuna nafasi kubwa katika shughuli za utafutaji na uzalishaji wa gesi asilia.

“Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) inajiandaa kutangaza zabuni za vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi, jambo litakalofungua fursa zaidi kwa wawekezaji,” alisema.

Gilbert alisema pamoja na shughuli za utafutaji na uzalishaji, bado kuna fursa kubwa katika uwekezaji wa miundombinu ya kujaza gesi kwenye magari, usambazaji wa gesi majumbani, taasisi mbalimbali na viwandani vinavyotumia gesi kama chanzo cha nishati.

Aliwataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali kuwekeza katika sekta hiyo inayokua kwa kasi na ambayo mahitaji yake yanaendelea kuongezeka.

Akizungumzia manufaa ya uwekezaji huo, Profesa wa Miundombinu John Bura alisema matumizi makubwa ya gesi asilia yanaweza kuisaidia Tanzania kupunguza utegemezi wa mafuta yanayoagizwa kutoka nje ya nchi na hivyo kuokoa fedha za kigeni.

“Gesi asilia ni rasilimali tuliyonayo nchini. Kadiri matumizi yake yanavyoongezeka, ndivyo tunavyookoa fedha za kigeni, kupunguza gharama za nishati na kuongeza ushindani wa uchumi,” alisema.

Profesa Bura alisema pamoja na mafanikio yaliyofikiwa, bado kuna haja ya Serikali na wadau wa sekta ya nishati kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za kutumia gesi asilia ili kuongeza idadi ya magari na taasisi zitakazotumia nishati hiyo.

Polisi yawashikilia 18 kwa madai ya kuchoma magari

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata na kuwashikilia watuhumiwa 18 pamoja na pikipiki 23, likiwatuhumu kujihusisha na matukio ya kushambulia, kuchoma na kuharibu magari yanayopata ajali.

Polisi pia limewaonya waendesha bodaboda wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi baada ya ajali, likisema baadhi yao hujiona wamekosewa hata wanapokuwa wahusika au chanzo cha ajali, kisha kuchoma au kuharibu magari yaliyohusika.

Onyo hilo limetolewa baada ya ajali iliyotokea leo, Agosti 19, 2026, katika Barabara ya Kilwa, eneo la Mivinjeni, Temeke, iliyosababisha vifo vya watu wawili na kumjeruhi mmoja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro ajali hiyo ilitokea saa 3:45 asubuhi baada ya lori aina ya DAF lililokuwa na tela kugongana na pikipiki aina ya Boxer.

Lori hilo lilikuwa likitokea eneo la Uhasibu kuelekea Bendera Tatu, wakati pikipiki hiyo ikiendeshwa na Msichoke Mohamed, maarufu Mnyige, mkazi wa Chamazi, Dar es Salaam.

Polisi imesema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa pikipiki kuhama kutoka barabara ya huduma na kuingia katika Barabara ya Kilwa bila kuchukua tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara.

Wakati wa ajali, pikipiki hiyo ilikuwa imebeba abiria wawili.

Ajali hiyo ilisababisha kifo cha dereva wa pikipiki, Msichoke Mohamed, pamoja na mmoja wa abiria, George Luis Nyantora, mfanyabiashara na mkazi wa Mbagala Zakhem, Dar es Salaam.

Abiria mwingine, William Ashery, maarufu Tumbo, mjasiriamali na mkazi wa Mwanza, alijeruhiwa na kupelekwa hospitalini kwa matibabu.

Bodaboda wachoma lori baada ya ajali

Baada ya ajali hiyo, kundi la waendesha bodaboda lilikusanyika eneo la tukio na kudaiwa kuchoma moto sehemu ya mbele ya lori lililohusika katika ajali, maarufu ‘horse’.

Jeshi la Polisi limelaani tukio hilo, likisema kuchoma moto, kupiga au kuharibu magari yanayohusika katika ajali, pamoja na kupora mali zilizomo ndani yake, ni vitendo vya kihalifu na kinyume cha sheria.

Polisi imesema baadhi ya waendesha bodaboda wamekuwa na tabia ya kujiona wao ndio waliokosewa kila ajali inapotokea, hata pale ambapo uchunguzi unaweza kuonyesha kuwa wao ndio waliohusika au kusababisha ajali.

Kwa mujibu wa Polisi, badala ya kuacha mamlaka zinazohusika kufanya uchunguzi na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria, baadhi yao hukusanyika na kuamua kulipiza kisasi kwa kushambulia magari au watu wanaohusishwa na ajali.

Jeshi hilo limeonya kuwa hatua hiyo haiwezi kuvumiliwa na kwamba waendesha bodaboda watakaohusika na uharibifu wa mali au vitendo vya vurugu watachukuliwa hatua za kisheria.

Watuhumiwa 18 washikiliwa

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imesema imewakamata na kuwashikilia watuhumiwa 18 pamoja na pikipiki 23 zinazodaiwa kuhusishwa na matukio ya aina hiyo.

Baadhi ya pikipiki hizo, kwa mujibu wa taarifa hiyo, ziliachwa na watuhumiwa waliokimbia baada ya matukio yaliyotokea maeneo ya Mbopo, Mabwepande, Bunju B, Tegeta, Kunduchi, Kimara na Magomeni Kanisani.

Polisi imesema kukamatwa na kushikiliwa kwa watuhumiwa hao ni sehemu ya hatua zinazochukuliwa kukomesha tabia ya baadhi ya waendesha bodaboda kushambulia magari mara baada ya ajali.

Katika tukio jingine lililotajwa na Polisi, Ally Abdallah (44), fundi rejeta na dereva bodaboda, anadaiwa kuwa miongoni mwa kundi la waendesha pikipiki lililohusika katika tukio la Agosti 15, 2026.

Kwa mujibu wa Polisi, siku hiyo Abdallah akiwa na kundi la wenzake na pikipiki zao, walilishambulia gari lenye namba T 333 EMR, aina ya Harrier, rangi nyeusi, baada ya mmoja wao kuhusika katika ajali.

Gari hilo lilishambuliwa kwa jiwe kubwa lililovunja kioo cha nyuma na kusababisha uharibifu pamoja na hofu kwa mwenye gari.

ACT yalaani Gazeti la MwanaHALISI kusitishiwa leseni

Dar es Salaam. Chama cha ACT- Wazalendo kimepinga uamuzi wa Serikali wa kusitisha kwa miezi sita leseni ya Gazeti la MwanaHALISI kikisema hatua hiyo inakiuka uhuru wa habari na haki ya umma kupata taarifa.

Katika taarifa yake ya Jumatano, Agosti 19, 2026, ACT Wazalendo kimekosoa uamuzi huo  na kuitaka Serikali kuondoa kusitishwa kwa leseni hiyo.

“ACT Wazalendo tunalaani kwa nguvu zote uamuzi wa Serikali kusitisha kwa miezi sita leseni ya uchapishaji na usambazaji wa Gazeti la MwanaHALISI kuanzia Agosti 19, 2026,” imeeleza taarifa hiyo iliyosaniwa na waziri kivuli wa habari, mawasiliano na teknolojia ya habari wa chama hicho, Shangwe Shao.

Chama hicho kimeeleza kinautambua wajibu wa vyombo vya habari kuzingatia weledi, lakini kimesisitiza kuwa makosa ya kitaaluma yanapaswa kushughulikiwa kwa namna inayolinda uhuru wa habari, haki ya kusikilizwa na masilahi ya umma.

“Serikali imejipa mamlaka ya kumchunguza, kumsikiliza na kumuadhibu mtoa huduma wa habari,” imeeleza ACT- Wazalendo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Serikali kupitia Idara ya  Habari Maelezo, leseni ya MwanaHALISI imesitishwa kwa miezi sita kuanzia Agosti 19, 2026, baada ya kukiuka sharti la tatu la leseni linalovitaka vyombo vya habari kuzingatia Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, na Kanuni zake za mwaka 2017.

Maelezo imeeleza kosa lilihusisha toleo namba 571 la Agosti 6 hadi 12, 2026, lililokuwa na habari yenye kichwa “Nchimbi agoma kujiuzulu” katika kurasa za kwanza, pili na tatu. 

Idara hiyo imedai habari hiyo haikuzingatia usahihi, mizania na uthibitishaji kabla ya kuchapishwa.

Maelezo pia imesema katika ukurasa wa pili wa gazeti hilo lilichapisha picha ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, lakini maelezo chini ya picha yalimtaja kuwa Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi.

Idara imetaja hilo kuwa dosari ya mwandishi na wahariri.

*Kuhusu mizania* 
Maelezo imesema habari hiyo ilijikita katika madai ya kujiuzulu kwa Nchimbi bila kuonyesha kuwa yeye alihojiwa au kutoa kauli kuhusu suala hilo.

 Aidha, imesema madai yaliyodaiwa kutolewa na Makonda hayakuambatana na uthibitisho wa moja kwa moja kutoka kwake.

Idara pia imesema mwandishi hakufanya jitihada za kuwahoji viongozi wa CCM au wajumbe wa kikao kilichodaiwa kujadili suala hilo, akiwamo Katibu Mkuu, Katibu wa Itikadi na Uenezi au Ofisa Habari, ili kuthibitisha taarifa zilizotokana na vyanzo fiche.

Uamuzi huo, kwa mujibu wa Maelezo, umezingatia pia mwenendo wa gazeti hilo kurudia makosa baada ya kuonywa. 

ACT Wazalendo, hata hivyo, imesema hatua hiyo inapaswa kupingwa kwa kulinda nafasi ya vyombo vya habari katika demokrasia.

“Uhuru wa habari na haki ya kupata, kutoa na kupokea taarifa ni nguzo za Katiba, demokrasia na uwajibikaji wa Serikali. Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 na sheria nyingine zinazompa mamlaka makubwa Mkurugenzi wa Habari juu ya vyombo vya habari zinapaswa kufutwa, na kuondoa vifungu vinavyokandamiza uhuru wa habari,” ACT Wazalendo imeeleza.

Wasira awataka wana-CCM kuhakiki taarifa za mitandaoni

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amewataka wanachama wa chama hicho kukutana mara kwa mara katika vikao rasmi ili kujadili masuala mbalimbali na kuepuka kupotoshwa na taarifa zisizo za kweli zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Wasira ametoa kauli hiyo leo, Agosti 19, 2026, wilayani Ikungi, mkoani Singida, wakati akianza ziara rasmi ya kikazi ya kukagua uhai wa chama hicho.

Amesema vikao vya wanachama ni muhimu kwa kuwa vinatoa fursa ya kupata taarifa sahihi, kubadilishana mawazo na kuambiana ukweli kuhusu masuala yanayohusu chama na nchi.

“Wanachama wetu nchi nzima, kwa mujibu wa Katiba mna vikao vya wanachama. Mkutane muambizane. Siku hizi kwenye mitandao kuna uongo mwingi sana. Usipoangalia unaweza hata wewe kushirikishwa kusema uongo,” amesema.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, akisalimiana na makada wa chama hicho wilayani Ikungi, mkoani Singida, wakati wa ziara rasmi ya kikazi ya kukagua uhai wa chama hicho.

Wasira amesema umuhimu wa wanachama kutokubali taarifa zinazotolewa mitandaoni bila kuzihakiki, badala yake wazijadili katika vikao na kutafuta ufafanuzi kutoka kwa watu wenye ujuzi kuhusu suala husika.

“Kwa hiyo ni vizuri kukutana mkasema hili jambo limesemwa sana, maana yake ni nini? Mkamwita mtu anayejua akawasaidia kufafanua,” amesema.

Amesema vikao hivyo pia vinapaswa kutumika kujadili masuala mbalimbali yanayoendelea nchini ili kuwajengea wanachama uelewa na kuwawezesha kukitetea chama kwa hoja sahihi.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, akisalimiana na makada wa chama hicho wilayani Ikungi, mkoani Singida, wakati wa ziara rasmi ya kikazi ya kukagua uhai wa chama hicho.

Katika hatua nyingine, Wasira amesema CCM itaendelea kulinda uhuru na umoja wa Tanzania, akieleza kuwa mambo hayo ni sehemu ya misingi ambayo chama hicho kimepewa jukumu la kuilinda.

 “Hii ndiyo CCM. Kazi ya kwanza tulipewa ni uhuru na tunalinda. Ya pili ni umoja na tunahakikisha unabaki. Yeyote anayetaka kuubomoa anabomoa msingi ambao hawezi. Anaweza kutikisa matawi lakini mizizi itabaki chini,” amesema.

Wasira pia amekosoa kauli za baadhi ya watu wanaodai kuwa CCM haijafanya chochote tangu Tanzania ipate uhuru, akisema madai hayo hayana uhalisia.

“Wanasema hatujafanya chochote tangu uhuru. Lakini uhuru wa kusema ndio huo walionao. Mdomo una kazi mbili: kusema na kula. Mtu akisema hakuna chochote tangu uhuru, muache tu. Huyo ana matatizo anahitaji msaada,” amesema.

DIT MWANZA YAONESHA NGUVU YA TEKNOLOJIA NA UZALISHAJI WA BIDHAA TANGA

   Na Mwandishi Wetu

Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Kampasi ya Mwanza imeendelea kudhihirisha nafasi yake katika kukuza elimu ya ufundi na teknolojia nchini kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Usagara jijini Tanga.

Maonesho hayo, yanayoratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, yanawakutanisha taasisi za Serikali, taasisi za elimu na utafiti, wabunifu, wanafunzi, wataalamu pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu, sayansi na teknolojia.

Kupitia maonesho hayo, DIT Kampasi ya Mwanza imewasilisha bunifu mbalimbali zinazolenga kuonesha uwezo wa wanafunzi na wataalamu wa taasisi hiyo katika kutatua changamoto za jamii kupitia teknolojia, ujuzi na ubunifu.

Miongoni mwa bidhaa zilizovutia wageni waliotembelea banda la DIT ni pamoja na bidhaa za ngozi zinazozalishwa na kampasi hiyo, zikiwemo viatu, mikoba na bidhaa nyingine zenye thamani ya kibiashara zinazotengenezwa kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya soko.

Mbali na kuonesha bunifu hizo, DIT Kampasi ya Mwanza imekuwa ikitoa huduma mbalimbali kwa wananchi, ikiwemo huduma za udahili kwa wanafunzi wanaotaka kujiunga na taasisi hiyo pamoja na kutoa elimu kuhusu programu mbalimbali za mafunzo zinazotolewa katika ngazi tofauti.

Wananchi waliofika katika banda la DIT wamepata fursa ya kujifunza kuhusu kozi za teknolojia, uhandisi na ufundi zinazotolewa na taasisi hiyo, huku wakihamasishwa kuchangamkia elimu ya ujuzi kama njia ya kujiajiri na kuchangia maendeleo ya taifa.

Ushiriki wa DIT katika Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu umeendelea kuonesha dhamira ya taasisi hiyo katika kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kutumia maarifa yao kuzalisha bidhaa na huduma zenye tija katika jamii.

Aidha, maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wanafunzi, wabunifu, wajasiriamali, taasisi za elimu na wadau mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuibua fursa mpya za maendeleo kupitia elimu na teknolojia.

Kwa upande wake, DIT Kampasi ya Mwanza imeeleza kuwa itaendelea kuwekeza katika ubunifu, utafiti na mafunzo ya vitendo ili kuhakikisha vijana wanapata maarifa yanayoweza kuwasaidia kujiajiri na kushindana katika soko la ajira la ndani na kimataifa.

Kupitia ushiriki wake katika maonesho hayo, DIT imeendelea kuthibitisha kuwa elimu ya ufundi na teknolojia ni nguzo muhimu katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

Hakika, uwepo wa DIT Kampasi ya Mwanza katika Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026 umeendelea kuwa ushahidi kwamba taasisi hiyo siyo tu kitovu cha elimu, bali pia ni chachu ya ubunifu, uzalishaji na maendeleo endelevu ya Taifa.

Mgambo wazunguka soko la mitumba, wafanyabiashara ‘wafungiwa’ biashara

Musoma. Wafanyabiashara katika soko la mitumba la Mlango Mmoja, Kata ya Nyasho, Manispaa ya Musoma, wameingia katika taharuki baada ya askari wa Jeshi la Akiba la manispaa hiyo, maarufu mgambo, kuzingira soko hilo na kuwazuia kufungua vibanda vyao.

Hali hiyo imetokea leo, Jumatano, Agosti 19, 2026, baada ya wafanyabiashara hao kufika sokoni asubuhi kwa ajili ya kuendelea na biashara zao, lakini wakawakuta mgambo wametanda katika maeneo mbalimbali ya soko.

Wafanyabiashara hao wamesema walizuiwa kufungua vibanda vyao hadi watakapolipa Sh10,000 kila mmoja, kiasi kilichoelezwa kuwa ada ya maombi ya kibanda.

Baadhi yao wamesema wameshangazwa na hatua hiyo kwa kuwa walitumia fedha zao kujenga vibanda hivyo baada ya manispaa kutenga eneo hilo kwa ajili ya soko.

“Tunaambiwa tujaze fomu kwa Sh10,000, ambayo ni ada ya maombi. Mbaya zaidi, ukiomba huna uhakika wa kupewa hicho kibanda, wakati tumetumia gharama zetu kujenga vibanda. Huu ni unyanyasaji, tunaomba msaada,” amesema Jenifa Yusufu.

Amesema pia kumekuwa na ongezeko la kodi ya vibanda bila kuzingatia hali ya biashara, jambo analodai linawaweka katika wakati mgumu, hasa kwa kuwa wengi wao hutegemea mikopo.

Baadhi ya wafanyabiashara wa Soko la Mitumba la Mlango Mmoja, Manispaa ya Musoma, wakiwa nje ya soko hilo baada ya mgambo kuwazuia kufungua vibanda vyao hadi walipie Sh10,000 kwa ajili ya maombi ya upangaji. Picha na Beldina Nyakeke.

Kwa mujibu wa Jenifa, awali walilipa Sh12,000 kwa mwezi kama kodi ya kibanda, lakini Aprili mwaka huu ilipanda hadi Sh15,000 na sasa imefikia Sh24,000.

Mfanyabiashara mwingine, Yohana Simon, amesema wanaendelea kutozwa kodi na tozo, huku soko likikosa baadhi ya huduma muhimu, ikiwamo vyoo vya kutosha.

“Hapa mazingira ni sisi ndio tunapambana nayo. Hivi vibanda tumejenga kwa gharama zetu. Hatuna huduma ya ulinzi kutoka manispaa na hata choo kipo kimoja, ambacho hakikidhi mahitaji,” amesema.

Katibu wa soko hilo, David Machera, amesema wafanyabiashara walifikisha malalamiko yao kwa mkuu wa mkoa wa Mara, ambaye ameahidi kukutana nao kesho kusikiliza na kujadili changamoto hiyo.

“Leo tumekuja tunakuta mgambo wamezingira eneo lote, wakati tuna ahadi ya kukutana na Mkuu wa Mkoa kesho. Tuna mikopo tunatakiwa kurejesha, unapotuzuia kufanya biashara unategemea nini?” amehoji.

Mbunge wa Musoma Mjini (CCM), Mgore Miraji, alifika sokoni na kuwasiliana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma, akimtaka kuwaondoa mgambo ili wafanyabiashara waendelee na shughuli zao.

“Hii si sawa kabisa. Serikali kila siku inatafuta namna ya kuwawezesha watu wake kujiimarisha kiuchumi. Inakuwaje mfanyabiashara anafungiwa kibanda chake? Mkurugenzi, waondoe mgambo wako hapa ili shughuli ziendelee, kisha tutakutana tufanye kikao kama tulivyokubaliana,” amesema.

Mgore amesema malalamiko hayo aliyapokea tangu juzi na jana walikubaliana kufanya kikao pamoja na mkurugenzi, ofisa biashara na wafanyabiashara hao.

Amesema wafanyabiashara hawajapata elimu ya kutosha kuhusu malipo hayo, akieleza kuwa wanapaswa kuwa na namba ya utambulisho wa mlipa kodi ili kusajiliwa katika mfumo wa Serikali wa Tausi na kupewa control namba za malipo.

“Mnatakiwa kusajiliwa kwenye mfumo wa Tausi ili kila mmoja apewe control namba awe analipa kodi yake kama kawaida. Kwa kuwa wote ni wafanyabiashara wenye vibanda hapa, msiwe na hofu kwani hakuna atakayeondolewa,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, amekiri kutokea kwa hali hiyo na kusema ameitisha kikao cha pamoja cha wafanyabiashara, viongozi wao, manispaa na mbunge kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa kudumu.

“Ni kweli hiyo hali imetokea. Tayari tumechukua hatua na hivi tunavyoongea biashara zinaendelea pale sokoni. Lengo la kikao ni kupata ufumbuzi wa kudumu juu ya suala hili,” amesema.

Polisi Maswa yatoa msaada kwa wagonjwa

Maswa. Jeshi la Polisi wilayani Maswa, mkoani Simiyu, limegeuza maadhimisho ya miaka 20 ya dhana ya Polisi Jamii kuwa fursa ya kuwafikia wananchi kwa vitendo baada ya kutembelea Hospitali ya Wilaya ya Maswa na kutoa misaada kwa wagonjwa, kuchangia damu na kufanya usafi.

Misaada hiyo imetolewa kwa wagonjwa waliolazwa katika wodi za watoto na wazazi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za jeshi hilo kuimarisha uhusiano na jamii na kuonyesha kuwa askari ni sehemu ya wananchi wanaowahudumia.

Akizungumza leo Agosti 19, 2026, wakati wa shughuli hiyo, Mrakibu wa Polisi, Ramadhani Mkimbu amesema maadhimisho hayo yamewapa fursa ya kwenda moja kwa moja kwa wananchi na kushiriki shughuli zenye manufaa kwa jamii.

Askari Polisi, Sajenti Anande Masay (kushoto) akitoa msaada kwa mmoja ya wagonjwa katika wodi ya Wazazi katika hospitali ya Wilaya ya Maswa. Picha na Samwel Mwanga.

Amesema kwa Maswa wameamua kuifikia hospitali hiyo kwa kufanya usafi, kuchangia damu na kutoa mahitaji mbalimbali kwa wagonjwa, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Polisi Jamii.

“Hivi vitu vyote ambavyo tumevileta kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa katika wodi hizi za wazazi na watoto ni michango ya kila askari kutoka katika mfuko wake na hii ndiyo inayodhihirisha dhana hii ya Polisi Jamii,” amesema.

Mkimbu amesema askari hawapaswi kuonekana kama maadui wa wananchi kwa kuwa wao pia ni sehemu ya jamii na wanatoka katika jamii hizo.

“Askari Polisi ni sehemu ya jamii na si maadui kwa raia kwani wametoka katika jamii. Ni vizuri tukashirikiana na wananchi katika shughuli mbalimbali, zikiwemo za kupambana na uhalifu na wahalifu katika jamii,” amesema.

Mrakibu wa polisi, Ramadhani Mkimbu akizungumza leo Agosti 19, 2026 walipofika hospitali ya Wilaya ya Maswa kutoa misaada kwa wagonjwa na kufanya usafi. Picha na Samwel Mwanga

Amesema kazi za Jeshi la Polisi haziwezi kufanikiwa bila ushirikiano wa wananchi na wadau mbalimbali, wakiwamo taasisi za Serikali na sekta binafsi.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Maswa, Dk Deogratius Mtaki amesema ushiriki wa polisi katika shughuli za kijamii umeonyesha namna jeshi hilo lilivyo karibu nao.

Amesema baadhi ya wagonjwa wana uwezo mdogo wa kujihudumia, hivyo misaada iliyotolewa itawasaidia wakati wakiendelea na matibabu.

“Tuna wagonjwa waliolazwa katika hospitali yetu ya wilaya ambao uwezo wao ni mdogo katika kujihudumia, hivyo misaada hii itawasaidia. Hii pia imetufundisha hata sisi wenyewe kujitoa kwa ajili ya kuwahudumia wengine,” amesema.

Beatrice Julius, ambaye mtoto wake amelazwa hospitalini hapo, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa msaada huo, akisema umeonyesha kuwa jeshi hilo linaweza kushirikiana na wananchi katika masuala yanayogusa maisha yao ya kila siku.

Naye Magreth Kadomola, aliyejifungua na kulazwa katika wodi ya wazazi, amesema kutembelewa na polisi na kupatiwa mahitaji mbalimbali kumempa hisia kuwa jeshi hilo lipo karibu na wananchi.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya Wilaya ya Maswa, Dk Deogratius Mtaki akizungumza mara baada ya askari wa jeshi la polisi wilayani humo kufika katika hospitali hiyo kwa lengo la kufanya usafi na kutoa misaada mbalimbali kwa wagonjwa. Picha na Samwel Mwanga

Amesema matukio kama hayo yanaweza kuongeza imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi na kuimarisha ushirikiano katika masuala ya usalama.

“Tunapowaona polisi wakija hospitalini kututembelea na kutusaidia, tunajisikia kuwa wako pamoja nasi. Hii inaongeza imani na ukaribu kati ya wananchi na polisi,” amesema.

Miongoni mwa vitu vilivyotolewa na askari hao ni sabuni za kufulia, mafuta ya kujipaka, pampasi za watoto, dawa za meno, maji na juisi, huku baadhi ya askari wakishiriki pia katika uchangiaji wa damu.

Pande mbili utekelezaji agizo la Chalamila kuhusu malori

Dar es Salaam. Agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila la kutaka malori yasiegeshwe kwenye hifadhi za barabara limeendelea kuzua mjadala, huku baadhi ya wananchi wakiliunga mkono na wengine wakionesha shaka kuhusu utekelezaji wake.

Baadhi ya wanaounga mkono wamesema hatua hiyo itasaidia kurejesha utaratibu wa matumizi ya barabara na kupunguza msongamano wa magari, huku wenye shaka wakisema Serikali ilipaswa kujadiliana na wadau wa malori kabla ya operesheni.

Agosti 11, 2026, Chalamila aliliagiza Jeshi la Polisi kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuendesha operesheni ya kuwaondoa madereva wanaoegesha malori kwenye maeneo yaliyotengwa kwa matumizi mengine.

Kwa mujibu wa Chalamila, hatua hiyo inalenga kurejesha nidhamu ya matumizi ya barabara na kukabiliana na uholela unaochangia msongamano na usumbufu kwa watumiaji wengine wa miundombinu ya usafiri jijini.

Kutokana na agizo hilo, Agosti 18, 2026 Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Elias Lukumay alitishia kusitisha shughuli za usafirishaji endapo Serikali haitashughulikia changamoto zinazowakabili wanachama wake.

“Mnatupitisha kwenye njia ngumu kila kukicha, lakini kero ni zilezile. Tunaamini maelewano ndiyo njia bora. Yakishindikana, tuko tayari kuyaegesha malori hadi hapo tutakapokubaliana,” alisema Lukumay.

Hata hivyo, tayari Tanroads wameshaanza utekelezaji wa oparesheni hiyo.

Akizungumza na Mwananchi, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Alinanuswe Kyamba, amesema wameshaianza operesheni hiyo na wamekamata malori kadhaa yaliyokutwa yameegeshwa katika hifadhi ya barabara.

“Ni kweli tumekamata malori kadhaa yaliyokuwa katika hifadhi za barabara. Ni vigumu kukupa takwimu hapa labda nitafute kesho asubuhi (Agosti 20) nitakuwa na idadi kamili,” amesema.

Mkazi wa Dar es Salaam, Mfaume Ramadhani amesema utekelezaji wa agizo hilo utakumbana na vikwazo iwapo Serikali haitadhibiti utoaji wa vibali vya bandari kavu katikati ya jiji.

Malori yakiwa yameegeshwa kando ya barabara ya Mandela eneo la Tabata TOT hadi Tabata Mwananchi leo, Agost 19, 2026, licha ya maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kutaka yasiwepo magari yanayoegeshwa pembezoni mwa barabara. Picha na Said Powa

“Ili kumaliza tatizo, vibali vya ICD vinapaswa kudhibitiwa na shughuli nyingi zihamishiwe nje ya mji. Hifadhi za barabara zinapaswa kubaki kwa matumizi ya watembea kwa miguu,” amesema.

Mkazi wa Temeke, Shaaban Ibrahim amesema baadhi ya bandari kavu zimejaa makasha kiasi cha kukosa maeneo ya kupokelea mizigo, jambo linalochangia malori kuegeshwa barabarani.

Amesema mazungumzo kati ya Serikali na wadau ni muhimu ili kupata suluhisho linalotekelezeka bila kuathiri shughuli za usafirishaji na biashara zinazotegemea huduma za malori.

Mkazi wa Tabata,  Muhidini Athuman amesema operesheni hiyo itasaidia kuondoa usumbufu kwa watembea kwa miguu ambao mara nyingi hulazimika kutumia sehemu za magari kutokana na njia kuzibwa na malori.

Jabiri Khatibu amesema malori yanachangia msongamano katika baadhi ya barabara za jiji, hivyo ni muhimu kutengwa maeneo maalumu ya maegesho na shughuli za usafirishaji kuhamishwa pembezoni mwa mji.

Mwananchi ilipita katika barabara mbalimbali zikiwamo za Mandela na Nyerere na kubaini baadhi ya malori yaliyokuwa yemegeshwa katika kinyume cha utaratibu yameondolewa.

Maeneo ya Sokota, Uwanja wa Taifa kuelekea bandari ambayo siku za nyuma yalikuwa sehemu ya kuhifadhi malori, hali imekuwa tofauti baada ya hifadhi ya barabara katika sehemu hizo kuonekana hazina magari.

Hata hivyo, baadhi yameendelea kuwepo hasa katika maeneo yenye bandari kavu, yakiwa yameegeshwa katika hifadhi ya barabara.

Miongoni mwa maeneo ambayo yameonekana malori yakiegeshwa ni Tabata TOT, Matumbi, Mchicha, Mabibo Msikiti, ingawa kulionekana maofisa wa Tanroads na polisi wakiyashughulikia.

Makamu Mwenyekiti wa Tatoa, Rahim Dossa amesema chama hicho kimeitwa katika kikao kazi cha wadau kujadili suala hilo.

Amesema pia viongozi wa Serikali wameanza kusikiliza hoja zao na kuahidi kuzifanyia kazi changamoto zilizowasilishwa.