Polisi Maswa yatoa msaada kwa wagonjwa
Maswa. Jeshi la Polisi wilayani Maswa, mkoani Simiyu, limegeuza maadhimisho ya miaka 20 ya dhana ya Polisi Jamii kuwa fursa ya kuwafikia wananchi kwa vitendo baada ya kutembelea Hospitali ya Wilaya ya Maswa na kutoa misaada kwa wagonjwa, kuchangia damu na kufanya usafi.
Misaada hiyo imetolewa kwa wagonjwa waliolazwa katika wodi za watoto na wazazi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za jeshi hilo kuimarisha uhusiano na jamii na kuonyesha kuwa askari ni sehemu ya wananchi wanaowahudumia.
Akizungumza leo Agosti 19, 2026, wakati wa shughuli hiyo, Mrakibu wa Polisi, Ramadhani Mkimbu amesema maadhimisho hayo yamewapa fursa ya kwenda moja kwa moja kwa wananchi na kushiriki shughuli zenye manufaa kwa jamii.
Askari Polisi, Sajenti Anande Masay (kushoto) akitoa msaada kwa mmoja ya wagonjwa katika wodi ya Wazazi katika hospitali ya Wilaya ya Maswa. Picha na Samwel Mwanga.
Amesema kwa Maswa wameamua kuifikia hospitali hiyo kwa kufanya usafi, kuchangia damu na kutoa mahitaji mbalimbali kwa wagonjwa, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa dhana ya Polisi Jamii.
“Hivi vitu vyote ambavyo tumevileta kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa katika wodi hizi za wazazi na watoto ni michango ya kila askari kutoka katika mfuko wake na hii ndiyo inayodhihirisha dhana hii ya Polisi Jamii,” amesema.
Mkimbu amesema askari hawapaswi kuonekana kama maadui wa wananchi kwa kuwa wao pia ni sehemu ya jamii na wanatoka katika jamii hizo.
“Askari Polisi ni sehemu ya jamii na si maadui kwa raia kwani wametoka katika jamii. Ni vizuri tukashirikiana na wananchi katika shughuli mbalimbali, zikiwemo za kupambana na uhalifu na wahalifu katika jamii,” amesema.
Mrakibu wa polisi, Ramadhani Mkimbu akizungumza leo Agosti 19, 2026 walipofika hospitali ya Wilaya ya Maswa kutoa misaada kwa wagonjwa na kufanya usafi. Picha na Samwel Mwanga
Amesema kazi za Jeshi la Polisi haziwezi kufanikiwa bila ushirikiano wa wananchi na wadau mbalimbali, wakiwamo taasisi za Serikali na sekta binafsi.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Maswa, Dk Deogratius Mtaki amesema ushiriki wa polisi katika shughuli za kijamii umeonyesha namna jeshi hilo lilivyo karibu nao.
Amesema baadhi ya wagonjwa wana uwezo mdogo wa kujihudumia, hivyo misaada iliyotolewa itawasaidia wakati wakiendelea na matibabu.
“Tuna wagonjwa waliolazwa katika hospitali yetu ya wilaya ambao uwezo wao ni mdogo katika kujihudumia, hivyo misaada hii itawasaidia. Hii pia imetufundisha hata sisi wenyewe kujitoa kwa ajili ya kuwahudumia wengine,” amesema.
Beatrice Julius, ambaye mtoto wake amelazwa hospitalini hapo, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa msaada huo, akisema umeonyesha kuwa jeshi hilo linaweza kushirikiana na wananchi katika masuala yanayogusa maisha yao ya kila siku.
Naye Magreth Kadomola, aliyejifungua na kulazwa katika wodi ya wazazi, amesema kutembelewa na polisi na kupatiwa mahitaji mbalimbali kumempa hisia kuwa jeshi hilo lipo karibu na wananchi.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya Wilaya ya Maswa, Dk Deogratius Mtaki akizungumza mara baada ya askari wa jeshi la polisi wilayani humo kufika katika hospitali hiyo kwa lengo la kufanya usafi na kutoa misaada mbalimbali kwa wagonjwa. Picha na Samwel Mwanga
Amesema matukio kama hayo yanaweza kuongeza imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi na kuimarisha ushirikiano katika masuala ya usalama.
“Tunapowaona polisi wakija hospitalini kututembelea na kutusaidia, tunajisikia kuwa wako pamoja nasi. Hii inaongeza imani na ukaribu kati ya wananchi na polisi,” amesema.
Miongoni mwa vitu vilivyotolewa na askari hao ni sabuni za kufulia, mafuta ya kujipaka, pampasi za watoto, dawa za meno, maji na juisi, huku baadhi ya askari wakishiriki pia katika uchangiaji wa damu.

