Wakati zaidi ya vyombo 20,000 vya usafiri nchini vikitumia gesi asilia, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imebainisha fursa tisa za uwekezaji katika sekta hiyo, zikiwamo ujenzi wa karakana za kubadili mifumo ya magari kutumia nishati hiyo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, hadi Aprili mwaka huu zaidi ya vyombo vya usafiri 20,000 vilikuwa vinatumia gesi asilia, hatua inayoonyesha matumizi ya nishati hiyo yanaendelea kukua nchini kutokana na gharama zake kuwa nafuu na mchango wake katika matumizi ya nishati safi.
Pamoja na ongezeko hilo, idadi ya karakana zilizoidhinishwa kufunga mifumo ya matumizi ya gesi asilia kwenye magari ilikuwa 13 pekee hadi kipindi hicho.
Ewura inaeleza hali hiyo inaonyesha bado kuna nafasi kubwa kwa wawekezaji kuingia katika biashara ya kutoa huduma za ubadilishaji wa mifumo ya magari kutoka mafuta kwenda gesi asilia.
Katika Ripoti ya Utendaji wa Sekta Ndogo ya Gesi ya mwaka 2025 iliyotolewa mwaka huu, Ewura imeainisha maeneo tisa yenye fursa za uwekezaji yanayoweza kusaidia kuongeza matumizi ya gesi asilia na kukuza shughuli za kiuchumi nchini.
Miongoni mwa fursa hizo ni ujenzi na uendeshaji wa vituo vikuu vya kuzalisha gesi asilia iliyogandamizwa (Compressed Natural Gas-CNG), ambayo hutumika kama nishati ya magari na matumizi mengine ya kibiashara.
Pia kuna fursa za kujenga na kuendesha vituo vya kujaza CNG vilivyounganishwa na mtandao wa mabomba ya gesi asilia kwa matumizi ya umma na binafsi, pamoja na vituo vinavyopokea gesi kupitia malori maalumu ya CNG kwa ajili ya kuhudumia maeneo ambayo bado hayajafikiwa na miundombinu ya mabomba.
Ripoti hiyo pia imeonyesha nafasi za uwekezaji katika vituo vidogo vya kusambaza CNG kwa matumizi ya viwandani, biashara, uzalishaji wa umeme na majumbani, sambamba na biashara ya usafirishaji wa gesi hiyo kutoka eneo moja kwenda jingine.
Fursa nyingine ni utoaji wa huduma za ukaguzi na uthamini wa mifumo ya CNG inayofungwa kwenye magari ili kuhakikisha inakidhi viwango vya usalama, pamoja na uwekezaji katika biashara ya usafiri kwa kutumia mabasi, malori na teksi zinazotumia gesi asilia.
Mbali na fursa hizo, Serikali inasema imeendelea kuweka mazingira yanayovutia uwekezaji kupitia sera, sheria na mipango mbalimbali inayolenga kuifanya sekta ya gesi kuwa moja ya nguzo za maendeleo ya uchumi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dk James Mataragio alisema uwepo wa Sera ya Taifa ya Nishati ni miongoni mwa sababu zinazotoa uhakika kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika sekta hiyo.
Alisema Serikali pia imeandaa Mpango Kabambe wa Matumizi ya Gesi Asilia (Natural Gas Utilisation Master Plan-NGUMP) unaoainisha maeneo ya kipaumbele ya matumizi ya gesi, ikiwamo uzalishaji wa umeme, maendeleo ya viwanda, matumizi ya majumbani na biashara, viwanda vya petrokemia, uzalishaji wa mbolea pamoja na mauzo ya gesi katika soko la ndani na nje ya nchi.
Dk Mataragio alisema kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, wawekezaji wanapata nafasi ya kushiriki katika kufadhili, kujenga, kuendesha na kutunza miradi mikubwa ya gesi, hatua inayosaidia kuvutia mitaji na teknolojia mpya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Biashara ya Mafuta na Gesi Asilia wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Emmanuel Gilbert alisema bado kuna nafasi kubwa katika shughuli za utafutaji na uzalishaji wa gesi asilia.
“Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) inajiandaa kutangaza zabuni za vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi, jambo litakalofungua fursa zaidi kwa wawekezaji,” alisema.
Gilbert alisema pamoja na shughuli za utafutaji na uzalishaji, bado kuna fursa kubwa katika uwekezaji wa miundombinu ya kujaza gesi kwenye magari, usambazaji wa gesi majumbani, taasisi mbalimbali na viwandani vinavyotumia gesi kama chanzo cha nishati.
Aliwataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali kuwekeza katika sekta hiyo inayokua kwa kasi na ambayo mahitaji yake yanaendelea kuongezeka.
Akizungumzia manufaa ya uwekezaji huo, Profesa wa Miundombinu John Bura alisema matumizi makubwa ya gesi asilia yanaweza kuisaidia Tanzania kupunguza utegemezi wa mafuta yanayoagizwa kutoka nje ya nchi na hivyo kuokoa fedha za kigeni.
“Gesi asilia ni rasilimali tuliyonayo nchini. Kadiri matumizi yake yanavyoongezeka, ndivyo tunavyookoa fedha za kigeni, kupunguza gharama za nishati na kuongeza ushindani wa uchumi,” alisema.
Profesa Bura alisema pamoja na mafanikio yaliyofikiwa, bado kuna haja ya Serikali na wadau wa sekta ya nishati kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za kutumia gesi asilia ili kuongeza idadi ya magari na taasisi zitakazotumia nishati hiyo.


