Dar/Moshi. Ni mtikisiko. Ndiyo kauli unayoweza kutumia kuelezea kinachoendelea katika wilaya ya kichama ya Moshi Mjini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya uongozi kuagiza ufanyike uchaguzi kujaza nafasi za viongozi wanaoshikilia kofia mbili za uongozi.
Makada mbalimbali waliohojiwa na gazeti hili leo Agosti 19, 2026, wamedai agizo hilo likitekelezwa nchini, litagusa hadi viongozi wa kitaifa na hivyo wameshauri usitishwe na kusubiri uchaguzi wa ndani ya chama mwakani.
“Moshi haijatulia. Unapoleta hoja ya kujaza nafasi kwa wenye kofia mbili ya uenyekiti wa kata na udiwani, unafanya watu wahoji mbona kuna viongozi wa kitaifa wana kofia mbili? Ni wenyeviti na wabunge,” alidai kada mmoja.
“Tayari kuna hisia kwamba ipo agenda ya siri ya hiki kinachoendelea. Kwa nini Moshi Mjini tu ambayo inanyemelewa na bundi? Ili kutuliza mtafaruku na hisia mbaya, CCM Makao Makuu waseme kama hili jambo ni la nchi nzima.”
Agizo hilo la CCM Moshi Mjini limeibua taharuki huku wakihoji kama lina baraka za uongozi wa juu wa chama hicho, kwa kuwa wapo viongozi wa kitaifa kama Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu.
Mbali na Chatanda, wametolea mfano wa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge, ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini, wakihoji kwa nini kushikilia nafasi mbili za uenyekiti na ubunge hakuna uchaguzi unafanyika kujaza nafasi yake.
Orodha hiyo ni ndefu kuanzia viongozi wa kitaifa hadi wale wa ngazi ya kata.
Hata hivyo, uongozi wa CCM mkoani Kilimanjaro umefafanua sababu za uamuzi huo.
Katika wilaya ya Moshi Mjini, Kata ya Kiusa, ambaye diwani wake ni Khalid Shekoloa, na Soweto, ambayo diwani wake ni Paul Maile, ndiyo wanaoshikilia nafasi ya udiwani na wakati huohuo mwenyekiti wa kata, nafasi ambazo zimetakiwa kujazwa.
Barua ya Agosti 12, 2026, yenye kumbukumbu CW/MSM/KK/Vol.V/95 iliyosainiwa na Katibu wa Wilaya, Amos Shimba, inaeleza kuwa maagizo ya kujaza nafasi hizo ni kwa mujibu wa Ibara ya 129 ya Katiba ya CCM, toleo la Mei 2025.
Shimba, kupitia barua hiyo iliyotumwa kwa makatibu wa kata wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, amesema katiba inaelekeza wakati wowote kunapotokea nafasi wazi miongoni mwa viti vyovyote vya CCM, kikao husika kijaze nafasi hiyo bila kuchelewa.
“Mnaelekezwa kusimamia na kuratibu chaguzi za kujaza nafasi wazi za uongozi wa CCM ngazi ya shina, tawi na kata ambazo uchujaji na uteuzi wa mwisho wa wagombea huishia ngazi ya mkoa,” inasema barua hiyo na kuongeza:
“Aidha, mnakumbushwa kuepuka kasoro zote zinazogusa maadili ya chama na za utendaji ambazo zinaweza kusababisha watu wasiostahiki kuchaguliwa, kupenya kwenye nafasi hizi za uongozi ama kwa rushwa, upendeleo au hila.”
“Kanuni na maadili ya chama yazingatiwe kwa ukamilifu na vikao vyote vinavyochuja na kuteua wagombea wa chaguzi za kujaza nafasi wazi katika ngazi husika vinapaswa kukamilika ifikapo tarehe 30.09.2026,” inasisitiza barua hiyo.
Gazeti hili limeona tangazo lililobandikwa Kata ya Kiusa likiwatangazia wanachama wote wenye sifa za uongozi kuanzia Agosti 17 hadi Agosti 23, 2026 kuchukua fomu kwenye ofisi ya kata.
Tangazo hilo linasema nafasi inayogombewa ni mwenyekiti wa CCM kata.
Tangu uchaguzi mkuu wa 2025, Jimbo la Moshi Mjini halijawahi kutulia huku baadhi ya viongozi wa CCM wakituhumiwa kuendekeza makundi na kuanza kutengeneza safu ya uongozi kuelekea uchaguzi wa ndani wa CCM 2027.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja ndani ya CCM, safu hizo zinatengenezwa kwa malengo ya mwaka 2030 na uchaguzi wa ndani wa CCM mwakani.
Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amesema walichokifanya ni kutekeleza maelekezo kutoka mamlaka za juu za chama.
Ameeleza nafasi walizoelekeza zijazwe ni kuanzia tawi, shina hadi kata, akisisitiza maelekezo hayo hayahusu Wilaya ya Moshi pekee, bali Tanzania nzima.
“Siyo Moshi pekee, kila eneo nchi nzima. Sisi tumepokea maelekezo kwamba nafasi zote zilizopo wazi zijazwe kuanzia shina, tawi hadi kata,” amesema.
Alipoulizwa iwapo kujaza nafasi hizo kunahusisha pia nyadhifa za wilaya, mikoa na Taifa, Boisafi amesema hilo si sehemu ya maelekezo na kama litakuwepo, utatangazwa utaratibu wake.
Hata hivyo, Shekoloa ambaye ni mwenyekiti wa CCM wa kata hiyo na diwani wa kata hiyo, alipoulizwa na gazeti hili leo Agosti 19, 2026 amesema:
“Ni kweli kuna uchaguzi wa kujaza nafasi yangu, lakini kwa mujibu wa kanuni na taratibu za chama, hatuna maelekezo yoyote rasmi kutoka ngazi za juu kwa sababu tukiangalia, kwa mfano, Mwenyekiti wa UWT (Chatanda) pia ni Mbunge,” alieleza.
“Nenda kule Mbeya pia. Mwenyekiti wa CCM wa mkoa ndiye Mbunge wa Mbeya Mjini. Mwenyekiti wa UWT Taifa ni mbunge. Kuna watu lukuki, naweza hata kukutumia orodha ya nchi nzima. Hatusikii kama kuna kuachia nafasi moja.”


