Namna huduma za mawasiliano zinavyotumiwa na Watanzania

Sekta ya mawasiliano nchini imeendelea kukua kwa kasi katika robo mwaka iliyoishia Juni 2026, huku ongezeko la laini za simu, matumizi ya intaneti na huduma za fedha mtandao likiashiria kukua kwa huduma za kidijitali katika shughuli mbalimbali.

Takwimu zilizotolewa katika ripoti robo mwaka ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa jumla ya laini za simu hai ilifikia milioni 116.95 hadi Juni mwaka huu, sawa na ongezeko la asilimia 4.51 ndani ya robo mwaka ulioishia Juni 2026.

Idadi hiyo imeifanya Tanzania kuwa na kiwango cha upenyaji wa mawasiliano cha zaidi ya asilimia 167, hali inayotokana kwa kiasi kikubwa na matumizi ya laini zaidi ya moja kwa mtu mmoja au taasisi.

Vodacom iliendelea kuwa kinara wa soko ikiwa na asilimia 33 ya usajili huo, ikifuatiwa na Yas yenye asilimia 28.6, Airtel asilimia 20.5, Halotel asilimia 16.4 na TTCL asilimia 1.5.

Hata hivyo pamoja na ukuaji huo takwimu zinaonyesha bado kuna pengo la kijinsia katika matumizi ya huduma hizo kwani wanaume walikuwa na usajili wa P2P milioni 59.48 ikilinganishwa na milioni 56.24 za wanawake.

Kwa upande wa kijiografia, Dar es Salaam iliendelea kuongoza kwa kuwa na usajili milioni 21.53, ikifuatiwa na Mwanza milioni 7.75, Arusha milioni 7.04, Mbeya milioni 6.73 na Dodoma milioni 6.24.

Kupiga simu kuliongezeka ila SMS zinapungua

Licha ya kuongezeka kwa matumizi ya huduma zinazotumia intaneti, simu za sauti bado zimeendelea kuwa muhimu, huku matumizi yake yakiongezeka katika robo mwaka hiyo.

Takwimu zinaonyesha matumizi ya simu za ndani yaliongezeka kwa asilimia 7.44, kutoka dakika bilioni 45.44 katika robo mwaka iliyoishia Machi hadi dakika bilioni 48.82 Juni.

Ongezeko hilo lilitokana na kuongezeka kwa simu zinazopigwa ndani ya mtandao mmoja (on-net) kwa asilimia 5.68 na zile zinazopigwa kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine (off-net) kwa asilimia 9.23. Simu za kimataifa nazo ziliongezeka.

Tofauti na simu za sauti, matumizi ya ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) yalibaki karibu katika kiwango kilekile, huku yakipungua kwa kiasi kidogo.

Matumizi ya SMS za ndani yalishuka kwa asilimia 0.05, kutoka ujumbe bilioni 55.08 Machi hadi bilioni 55.05 Juni.

Mwelekeo huo unaakisi mabadiliko ya tabia za watumiaji, ambao sasa wanazidi kutumia WhatsApp, mitandao ya kijamii na programu nyingine za mawasiliano yanayotumia intaneti.

“Sina haja ya kujiunga na SMS siku hizi maana na chati zaidi kwa kutumia Whatsapp na Telegram, nikishakuwa na bado natuma tu, intaneti ndiyo ya muhimu ukiwa nayo unafanya vingi, unaperuzi pia hata kupiga simu,” anasema Aneth Jackson Mkazi wa Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo matumizi ya intaneti nayo yaliongezeka kwa asilimia 6.48, kutoka milioni 58.97 Machi hadi milioni 62.79 Juni, na kufikisha kiwango cha upenyaji wa intaneti asilimia 89.7.

Huduma za intaneti kupitia mitandao ya simu ya kasi ziliendelea kutawala, zikiwa na usajili milioni 37.58, huku 2G ikiwa na usajili milioni 24.63.

Matumizi ya intaneti yaliongezeka kwa asilimia 11.65, kutoka petabyte 932 hadi petabyte 1,041 katika robo mwaka hiyo. Matumizi makubwa zaidi yalikuwa katika mitandao ya kijamii ya YouTube, TikTok, Facebook, Instagram na WhatsApp.

Upatikanaji wa 5G kwa wakazi uliongezeka kutoka asilimia 32.83 Machi hadi asilimia 34.18 Juni, huku upatikanaji wake kijiografia ukiongezeka kutoka asilimia 11.04 hadi 11.34.

Kwa upande wa 4G, upatikanaji kwa wakazi ulifikia asilimia 94.39, kutoka asilimia 94.32, wakati upatikanaji kijiografia ulifikia asilimia 77.53.

Hata hivyo pamoja na upatikanaji mpana wa mitandao, umiliki wa simu janja bado ni kikwazo katika kuongeza matumizi ya huduma za kidijitali.

Upenyaji wa simu janja uliongezeka kutoka asilimia 42.50 Machi hadi asilimia 44.74 Juni, huku simu janja milioni 31.34 zikiwa zimeunganishwa kwenye mitandao ya waendeshaji huku simu za kawaida zikiwa bado kwenye soko, zikiwa milioni 58.40 na kiwango cha upenyaji cha asilimia 83.38.

Miamala ya simu yashika kasi

Eneo lililoonyesha ukuaji mkubwa zaidi ni huduma za fedha mtandao. Idadi ya akaunti hai za fedha mtandao iliongezeka kwa asilimia 7.5, kutoka milioni 80.98 Machi hadi milioni 87.05 Juni.

M-Pesa iliendelea kutawala soko kwa ukubwa ikiwa na asilimia 40.6 ya usajili (Yaani kila kati ya watu 10 wanaotumia huduma za miamala wanaotumia M-Pesa ni wanne), ikifuatiwa na Mixx by Yas yenye asilimia 32, Airtel Money asilimia 16.4 na HaloPesa asilimia 10.1.

Kwa pamoja, M-Pesa, Mixx by Yas na Airtel Money zilidhibiti takriban asilimia 89 ya usajili wa huduma za fedha mtandao. Ukuaji huo haukuishia kwenye idadi ya akaunti. Jumla ya miamala ya fedha mtandao iliongezeka kwa asilimia 5.38 katika robo mwaka, kufikia bilioni 2.10, kutoka bilioni 1.99 Machi.

Kwa mwezi Juni pekee, watoa huduma walirekodi miamala milioni 710.99, kutoka milioni 679.19 Aprili, katika miamala hiyo M-Pesa pia iliongoza kwa miamala milioni 286.41, ikifuatiwa na Mixx by Yas milioni 228.59 na Airtel Money milioni 129.14.

Akizungumzia ripoti ya kipindi kama hicho ya Vodacom Mkurugenzi wake Philip Besiimire alisema huduma za miamala ya simu na ongezeko la matumizi ya intaneti katika soko la Mawasiliano vimekuwa na mchango mkubwa katika mapato ya kampuni hiyo.

Alisema katika kipindi hiki cha mwaka uliopita, wateja wa M-Pesa waliongezeka kwa asilimia 22.6, jambo linalodhirisha namna matumizi ya fedha kidijitali yanavyozidi kusimika mizizi katika maisha ya kila siku.

“M-Pesa ni nyenzo muhimu katika kuendeleza ujumuishaji wa kifedha nchini Tanzania kupitia suluhisho za kisasa kama mikopo ya kidijitali, usimamizi wa uwekezaji na utajiri, akiba za vikundi na huduma za malipo ya kidijitali,” alieleza Besiimire.

Kwa upande mwingine alisema mapato yatokanayo na huduma za intaneti yaliongezeka kwa asilimia 29.5, yakichochewa zaidi na ongezeko la mamilioni ya watumiaji wa huduma za data, ikiwa ni zaidi ya asilimia 25 ya data ikilinganishwa na ripoti ya mwaka uliopita.

“Matumizi ya simu janja pia yameendelea kuongezeka kwa kasi kubwa kupitia mkakati wetu endelevu wa kuongeza matumizi ya simu janja nchini Tanzania, tumefanikisha kufikisha mtandao wetu kwa watumiaji wa simu janja milioni 11.5,” Alisema Besiimire.