Mbegu bora, chachu ya kilimo cha ushindani – HabariLeo

IRINGA: Wakulima mkoani Iringa wametakiwa kuanza maandalizi ya msimu mwingine wa kilimo kwa kuchagua na kutumia mbegu bora, zilizoidhinishwa na zenye uwezo wa kuongeza uzalishaji, huku wakisisitizwa kuachana na mbegu zinazoweza kuathiri mavuno na kipato.

Wito huo umetolewa katika kijiji cha Mawala, kata ya Ilole katika halmashauri ya wilaya ya Kilolo, wakati wakulima wakijiandaa kwa msimu mwingine wa kilimo na kupewa elimu kuhusu umuhimu wa matumizi ya mbegu bora katika kuongeza tija na ubora wa mazao.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Mgongolwa Agrovet and Seeds, ambayo ni wakala mkuu wa mbegu zinazozalishwa na Taasisi ya Mbegu Tanzania (ASA) kwa Mkoa wa Iringa na Nyanda za Juu Kusini, Joseph Mgongolwa, amesema maandalizi mazuri ya msimu yanapaswa kuanzia kwenye uchaguzi wa mbegu, kwa kuwa ubora wa mbegu una nafasi kubwa katika kuamua kiwango na ubora wa mavuno.

Amesema Serikali imeweka utaratibu wa kuwawezesha wakulima kupata mbegu bora zenye ruzuku kwa bei nafuu, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa mbegu bora na kuwasaidia wakulima kupunguza gharama za uzalishaji.

“Wakati huu ambao wakulima wanaelekea kuanza maandalizi ya msimu mwingine, ni muhimu wasisubiri mpaka muda wa kupanda ufike. Wanapaswa mapema kupanga aina ya zao watakalolima, kutafuta mbegu bora na kushauriana na wataalamu ili kuhakikisha wanakwenda shambani wakiwa wamejiandaa,” amesema Mgongolwa.

Amesema ASA huzalisha mbegu za mazao mbalimbali, ikiwemo mahindi, maharage, alizeti na ufuta, ambazo zinaweza kuwasaidia wakulima kuongeza tija na kuzalisha mazao yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko.

Amesema matumizi ya mbegu bora yanapaswa kwenda sambamba na kuzingatia kanuni nyingine za kilimo, ikiwemo muda sahihi wa kupanda, nafasi za kupanda, matumizi sahihi ya mbolea, udhibiti wa magonjwa na wadudu pamoja na usimamizi mzuri wa shamba.

“Lengo si kupata mavuno mengi pekee, bali kupata mazao yenye ubora unaokubalika katika masoko. Tunataka mkulima aweze kuzalisha kwa ajili ya chakula, lakini pia awe na uwezo wa kuuza na kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mawala, Vedasto Mbuta, amewataka wakulima kutumia mbegu zinazotambulika na kuthibitishwa na Wizara ya Kilimo na kuhakikisha wanazinunua kutoka kwa wauzaji wanaoaminika.

Amesema baadhi ya wakulima wamekuwa wakikumbwa na hasara kutokana na kununua mbegu zisizojulikana, jambo linaloweza kusababisha mbegu kutoota vizuri, mavuno kuwa madogo au mazao kutofikia ubora unaotarajiwa.

“Tunapokwenda kwenye msimu mwingine, mkulima anatakiwa kujiandaa mapema. Asiangalie bei ya mbegu pekee, aangalie ubora na chanzo chake. Mbegu bora ni uwekezaji unaoweza kumrudishia mkulima faida kubwa wakati wa mavuno,” amesema Mbuta.

Baadhi ya wakulima walioshiriki katika zoezi hilo wamesema elimu waliyoipata imewasaidia kutambua umuhimu wa kuanza maandalizi ya msimu mapema, hususan katika kuchagua mbegu sahihi na kupata ushauri wa wataalamu.

Wamesema wamejifunza kuwa kuongeza uzalishaji hakutegemei ukubwa wa eneo la shamba pekee, bali pia ubora wa mbegu, matumizi ya teknolojia sahihi na kufuata kanuni bora za kilimo.

Mwisho.

Simba Yakiri Singida Black Stars ni Bora, Lakini Yalenga Pointi Tatu Kesho

Global Publishers
August 21, 2026
60 views
0 Comments

Simba SC imekiri kuwa Singida Black Stars ni timu yenye ubora mkubwa kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/27, lakini imeweka wazi kuwa inalenga kupata ushindi.

Timu hizo zinatarajiwa kukutana kesho, Agosti 22, katika Uwanja wa Airtel, zikiwa zote zimecheza michezo miwili katika mwanzo wa msimu.

Singida Black Stars imeanza msimu kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate, kabla ya kutoka sare ya 1-1 na Kagera Sugar ugenini.

Kwa upande wa Simba SC, kikosi hicho kilianza kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar na kufuatiwa na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Pamba Jiji FC.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amesema wanatambua ubora wa Singida Black Stars na kwamba mchezo hautakuwa rahisi.

“Malengo yetu ni kuona kwamba tunashinda mchezo wetu na tunatambua kwamba hautakuwa mchezo rahisi kutokana na ubora wa wapinzani wetu,” alisema Barker.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa wa ushindani mkubwa kutokana na rekodi nzuri ya timu hizo katika michezo yao ya mwanzo wa msimu, huku Simba ikitegemea uwezo wa washambuliaji wake akiwemo **Libasse Gueye**, wakati Singida Black Stars ikiwa na mshambuliaji wake kinara **Jonathan Sowah**.

Hii itakuwa mara ya pili kwa Singida Black Stars na Simba SC kukutana katika Uwanja wa Airtel, baada ya mchezo wao wa kwanza katika uwanja huo kumalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Luizer ampongeza Asha Baraka – HabariLeo

MSANII wa muziki wa dansi nchini, Luizer Nyoni Mbutu amempongeza Asha Baraka kwa mchango wake katika kuendeleza muziki wa dansi, akisema kupitia Bendi ya Twanga Pepeta imeweza kutoa ajira kwa zaidi ya familia 40.

Luizer amesema Asha ni mwanamke mwenye juhudi na asiyekata tamaa, akimtaja kama mmoja wa watu walioendelea kupigania maendeleo ya bendi hiyo na muziki wa dansi kwa ujumla. “Ni mwanamke na nusu, ni mpambanaji asiyekata tamaa. Leo hii ni Mbunge wa Viti Maalumu, amepambana kwa miaka mingi hadi kupata nafasi hiyo, lakini pia ameipigania Bendi ya Twanga Pepeta kwa muda mrefu,” amesema Luizer.

Amesema mchango wa Twanga Pepeta hauishii katika burudani pekee bali pia umekuwa chanzo cha ajira kwa wasanii na wafanyakazi mbalimbali, hivyo kusaidia familia nyingi kupata kipato. Kwa mujibu wa Luizer amesema juhudi alizofanya Asha Baraka ni mfano wa namna sanaa inavyoweza kuchangia katika uchumi na kuwasaidia watu kujipatia kipato kupitia vipaji na ajira zinazotokana na sekta hiyo. SOMA: Bella, El Saadat, Twanga Pepeta kukiwasha Valentine Day

 

Ray Kigosi Atoa Siri ya Familia, Chuchu Hansy Atarajia Mtoto wa Pili – Video

Global Publishers
August 21, 2026
420 views
0 Comments

Mwigizaji mkongwe wa filamu Bongo, Vincent Kigosi, maarufu kama Ray, amefichua kuwa mzazi mwenzake, Chuchu Hansy, anatarajia kupata mtoto wao wa pili.

Ray ametoa taarifa hiyo kupitia ukurasa wake wa Instagram, akieleza furaha na shukrani alizonazo moyoni kutokana na ujio wa mtoto huyo, huku akimshukuru Mungu kwa baraka hiyo katika familia yao.

Katika ujumbe wake, Ray ameandika:
“MY LOVELY MZUNGU, maneno hayatoshi kueleza furaha na shukrani nilizonazo moyoni. Unakaribia kunipa zawadi ya thamani kuliko zote, mtoto wetu wa pili.

Namshukuru Mungu kwa ajili yako na kwa baraka hii kubwa katika familia yetu.

Asante kwa upendo wako na kwa kunipa furaha isiyo na kipimo. Nakupenda sana MY LOVELY MZUNGU. Mungu ailinde familia yetu na abariki familia yetu daima.

Nakuahidi kuthamini familia yetu, kukupenda sana na kusimama na wewe katika kila hatua ya maisha yetu.”

Ray pia ametumia ujumbe huo kuwashukuru watu mbalimbali waliohusika katika maandalizi ya picha zao, huku akiwataja wauzaji wa mavazi pamoja na mpiga picha.

Ujio wa mtoto huyo unakuwa hatua nyingine katika maisha ya familia ya Ray na Chuchu Hansy, huku mashabiki wao wakituma pongezi na kuwatakia safari njema kuelekea kumpokea mtoto wao wa pili.

Ray ni miongoni mwa waigizaji waliodumu kwa muda mrefu katika tasnia ya filamu Tanzania na amejijengea jina kubwa kupitia kazi zake mbalimbali katika Bongo Movies.

Lissu Aanza Kujitetea Kesi ya Uhaini, Ushahidi Waahirishwa hadi Jumatatu

Baada ya Jopo la Majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, kumkuta Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Antiphas Lissu, ana kesi ya kujibu katika shauri la uhaini namba 19605/2025, utetezi wake umeanza rasmi leo, Agosti 21, 2026.

Kesi hiyo iliendelea saa 9:48 Alasiri baada ya mahakama kutoa mapumziko mafupi. Jopo la majaji lilipoingia ukumbini, upande wa mashtaka ulieleza kuwa uko tayari kusikiliza utetezi wa Lissu, huku yeye pia akithibitisha kuwa yuko tayari kuanza kutoa ushahidi.

Kabla ya kuanza utetezi, Lissu aliomba maelekezo kuhusu utaratibu wa mashahidi wake ambao wamepangwa kutoa ushahidi, akitaka kujua kama wanapaswa kubaki ndani ya ukumbi au kutoka nje.

Majaji walielekeza kuwa mashahidi wengine hawapaswi kuwepo ndani ya ukumbi wakati shahidi mwingine akitoa ushahidi.

Kutokana na maelekezo hayo, viongozi waandamizi wa CHADEMA waliopangwa kuwa mashahidi, akiwemo John Mnyika, Amani Golugwa na John Heche, waliondoka ukumbini kusubiri kuitwa kutoa ushahidi wao.

 

Baada ya hapo, Lissu alisimama kizimbani na kula kiapo kama shahidi wa kwanza wa utetezi.

Akianza ushahidi wake, Lissu alisema sehemu ya kwanza ya utetezi wake inahusu maisha yake binafsi, akieleza kuwa maelezo hayo yatasaidia mahakama kumuelewa yeye ni mtu wa aina gani.

Lissu alijitambulisha kama kiongozi wa chama cha siasa kilichosajiliwa kisheria na kueleza kuwa amekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa tangu Januari 22, 2025.

Alisema alidumu katika nafasi hiyo kwa takribani wiki tano au sita kabla ya kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uhaini.

Katika ushahidi wake, Lissu pia alieleza historia ya uongozi wake ndani ya CHADEMA, akibainisha kuwa aliwahi kuwa Naibu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia Desemba 2019 hadi Januari 22, 2025.

Aidha, alieleza kuwa aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama kuanzia mwaka 2010 hadi Septemba 7, 2017.

Utetezi wa Lissu sasa unaendelea mbele ya jopo hilo la majaji, huku akianza kueleza historia yake binafsi na kisiasa kama sehemu ya ushahidi wake katika kujibu mashtaka yanayomkabili.

Baada ya kuanza kutoa ushahidi wake leo, shauri hilo limeahirishwa hadi Jumatatu, Agosti 24, 2026 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa utetezi.

WAZIRI KOMBO APOKEA NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO KWA BALOZI MTEULE WA UBELGIJI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb), amepokea Nakala za Hati  za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Ubelgiji nchini Mhe. Lot Debruyne, katika Ofisi ndogo za Wizara, Jijini Dar es Salaam. 

Baada ya tukio hilo viongozi hao walijadili namna bora ya kuendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano kati ya Tanzania na Ubelgiji.

Akizungumza na Balozi Mteule wa Ubelgiji Mhe. Waziri Kombo alisisitiza azma ya kuhamisha ushirikiano kutoka kwenye misaada na kuelekea katika kufanya biashara na uwekezaji.

Mhe. Waziri Kombo ameeleza juu ya fursa za ushirikiano katika kilimo na umwagiliaji, uhamishaji wa maarifa na ujuzi, pamoja na mitambo na teknolojia za kisasa za kilimo. 

Pia alihimiza kuongezwa kwa biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Ubelgiji akitaja ongezeko la watalii kupitia safari za moja kwa moja za Shirika la Ndele la Ubelgiji (Brussels Airlines) kwenda Kilimanjaro na Zanzibar kama fursa ya kukuza sekta ya utalii.

Viongozi hao walibainisha maeneo ya ushirikiano ikiwemo ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, nishati safi na jadidifu, mapishi safi, mabadiliko ya kidijitali na afya. 

Aidha, viongozi hao walisisitiza juu ya ushirikiano kati ya Bandari za Antwerpen na Dar es Salaam, pamoja na fursa za ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Ghent na taasisi za Tanzania katika kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili.

 

Lissu: Hakuna Mtu Asiyeweza Kuitwa Kuwa Shahidi Mahakamani – Video

Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu leo Agosti 21, 2026 amekataa hoja kwamba Rais wa Tanzania hawezi kupelekewa wito wa mahakama, akisema Rais anaweza kupelekewa wito huo kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Lissu amesema kwa upande wa Rais, wito unaweza kupelekwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi au Katibu Binafsi wa Rais, ambaye anaweza kusaidia mahakama kumfikishia Rais wito huo.

Amesema ni kweli kwamba wito wa mahakama hauwezi kumpelekea Rais moja kwa moja, bali unaweza kuwasilishwa kupitia katibu wake.

Lissu amekiri kwamba mahakama haiwezi kumlazimisha Rais kufika mahakamani, lakini inaweza kumpelekea wito kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

“Na Rais ndiye ataamua kuuheshimu wito huo au la,” amesema Lissu.

Kuhusu Makamu wa Rais mstaafu na Waziri Mkuu mstaafu, Lissu amesema tayari wamestaafu na hivyo hawawezi kutumia hoja kwamba wanamsaidia Rais katika utekelezaji wa majukumu yake.

Vilevile, Lissu ametoa hoja kuhusu Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mkurugenzi wa Ujasusi, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkuu wa Majeshi, akisema wote wanaweza kuitwa mahakamani kama mashahidi.

Lissu amesema hakuna mtu au afisa yeyote ambaye hawezi kupelekewa wito wa mahakama, akiwamo Rais, Makamu wa Rais mstaafu, Mkuu wa Majeshi au Mkuu wa Jeshi la Polisi.

Amesema mahakama inaweza kutoa wito kwa Rais, ingawa haina uwezo wa kutoa hati ya kukamatwa dhidi yake.

Hata hivyo, kwa mujibu wa hoja zake, Makamu wa Rais mstaafu, Waziri Mkuu mstaafu, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mkuu wa Majeshi na Mkuu wa Ujasusi wanaweza kupewa hata hati ya kukamatwa iwapo mazingira ya kisheria yatatimia.

Lissu ameiambia mahakama kwamba ikiwa haiwezi kutoa wito kwa mashahidi aliowaomba kutoka upande wa Serikali ili wafike mahakamani, basi haki katika kesi hiyo inaweza kuathirika.

“Kama kwenye kesi kubwa kama hii mahakama haiwezi kupeleka wito, basi sijui itaonekanaje. Lindeni haki yangu ili kuweka haki katika kesi na uadilifu,” amesema Lissu.

Ameeleza kuwa hakuna shauri linalozuia mashahidi kupelekewa wito wa mahakama, akisisitiza kuwa mashahidi hao wanaweza kuitwa na kwamba ushahidi wao ni muhimu katika kesi hiyo.

Arsenal vs Coventry: Arteta Aanza Msimu na Mtihani wa Lampard

Kabla ya mchezo wa leo Ijumaa Emirates Stadium, hebu tuangalie undani zaidi wa kile kinachotarajiwa kutokea kimbinu na kikikosi katika mechi hii ya kufungua msimu wa 2026/27. Kwa upande wa mbinu, Arsenal ya Mikel Arteta wanatarajiwa kutumia mfumo wao wa kawaida wa 4-3-3.

Kikosi kinachotarajiwa kuanza ni Raya; White, Mosquera, Gabriel, Calafiori; Lewis-Skelly, Odegaard, Guimaraes; Saka, Havertz, Tzolis. Muundo huu unaonyesha jinsi Arteta anavyotaka kuchanganya uzoefu wa wachezaji wa zamani kama Odegaard na Saka na nguvu mpya za waliojiunga hivi karibuni kama Guimaraes na Tzolis.

Hata hivyo, Arsenal wana upungufu fulani wa ulinzi kwani William Saliba hatapatikana kutokana na jeraha, jambo linalomlazimu Arteta kutegemea muungano mpya wa waliopo nyuma.

Coventry City nao wanapanga kucheza kwa mfumo unaofanana, 4-3-3, wakijaribu kuzuia mashambulizi ya Arsenal huku wakitafuta nafasi za kushtukiza kupitia mabao ya kukimbiza mpira.

Kikosi kinachotegemewa ni Rushworth; Van Ewijk, Thomas, Amenda, Dasilva ukiwa na viungo wapya walioongezwa msimu huu. Frank Lampard, ambaye ana uzoefu mkubwa wa kucheza dhidi ya Arsenal enzi za Chelsea, atajaribu kutumia maarifa yake kubuni mkakati wa kuwabana Wagunners hasa maeneo ya kati ya uwanja ambako Odegaard na Guimaraes hupenda kudhibiti mchezo.

Meridianbet inasema kuna michezo kama Keno, Aviator, Poker, Roulette, Wild Icy Fruits, Super Heli. Ingia katika kasino ya mtandaoni ya Meridianbet na ujiokotee mkwanja mapema.  Jiunge sasa au Tembelea tovuti ya meridianbet.co.tz au piga *149*10# kisha uanze safari yako ya ushindi.

Suala la majeraha linaweza kubadilisha kabisa mwelekeo wa mchezo huu upande wa Coventry. Kukosekana kwa Haji Wright, ambaye alikuwa mfungaji muhimu aliyewasaidia kupanda daraja, kunawaacha Coventry bila silaha kuu ya mbele. Hali kadhalika, Frank Onyeka na Jack Rudoni pia hawapo kwa sababu za majeraha, jambo linalodhoofisha zaidi uwezo wao wa kudhibiti sehemu ya kati ya uwanja dhidi ya kikosi chenye ubora wa hali ya juu cha Arsenal.

Kwa mtazamo wa takwimu za awali, ubashiri unaonyesha wazi jinsi mchezo huu unavyotarajiwa kwenda. Wachambuzi wanaona uwezekano mkubwa wa Arsenal kufunga angalau mabao mawili au zaidi, kutokana na mwenendo wao mzuri wa kufunga nyumbani msimu uliopita.

Coventry, licha ya kuwa na msimamo wa kujilinda, watahitaji ubunifu mkubwa kutoka kwa washambuliaji wapya kama Tchaouna ili kuweza kuleta tishio lolote dhidi ya ulinzi wa Arsenal unaoongozwa na David Raya kwenye kiremba.

Kwa ujumla, mchezo huu unatarajiwa kuwa mtihani mkubwa wa mapema kwa Coventry City kuonyesha kama wanaweza kushindana katika kiwango cha ligi kuu, huku Arsenal wakitarajiwa kutumia fursa hii kuweka msingi imara wa msimu wao wa kutetea ubingwa.

Serikali Yamjibu Lissu: Sheria Haipo kwa Ajili ya Kumfurahisha Mtu

Dar es Salaam — Mvutano wa hoja umeendelea katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, huku upande wa mashtaka wa Serikali ukisisitiza kuwa mahakama haiwezi kufanya maamuzi kwa misingi ya huruma au shinikizo kutoka kwa upande wowote.

Upande wa Serikali umesema sheria haipo kwa ajili ya kumfurahisha mtu yeyote wala kufuata maombi ya upande fulani, bali mahakama ina wajibu wa kusimamia na kutafsiri sheria.

Mwendesha mashtaka amesema kitendo cha kuielekeza mahakama kwenye hoja za huruma si msingi wa kufanya uamuzi, akidai kuwa Lissu alipaswa kufuata sheria na vifungu vilivyotajwa badala ya kuwaomba majaji wamuone huruma.

Hata hivyo, Lissu amepinga madai hayo na kuwataka mawakili wa Serikali kuonyesha kwenye rekodi sehemu ambayo aliomba kuhurumiwa au kuwatisha majaji.

“Kama nina sehemu yoyote nimesema, ‘Nionee huruma,’ au nimewatisha majaji, basi nionyesheni rekodi,” Lissu amesema, akisisitiza kuwa hakutoa kauli hizo.

Katika hoja nyingine, upande wa Serikali umehoji kauli inayodaiwa kutolewa kuhusu mahakama kushindwa kuwaita mashahidi kwa sababu ya kuihofia Serikali.

Mwendesha mashtaka amesema kauli hiyo inaweza kutafsiriwa kama jaribio la kuishinikiza mahakama na kujenga mazingira ya hofu ambayo yanaweza kuathiri utekelezaji wa majukumu yake.

Serikali pia imesema haikupata hoja yoyote ya msingi katika rekodi za kesi kuhusu mashahidi hao, ikidai kuwa majina yao yalitajwa tu kama sehemu ya mambo mengine yaliyowasilishwa mahakamani.

Kwa msingi huo, upande wa Serikali umesisitiza kuwa Lissu alipaswa kuwasilisha rasmi hoja yake mbele ya mahakama ili majaji waamue kama wana mamlaka ya kuwaita mashahidi hao au la.

Aidha, Serikali imesema suala la iwapo iliogopa au haikuogopa halipaswi kuwa msingi wa uamuzi katika shauri hilo, bali kinachopaswa kuzingatiwa ni sheria, ushahidi na hoja zilizowasilishwa mbele ya mahakama.

*DKT. MWIGULU AAGIZA KASI YA UJENZI WA VIWANJA VYA MAZOEZI VYA AFCON IONGEZEKE*

*_▪︎ Ataka kazi ifanyike usiku na mchana inapowezekana;_*

*_▪︎ Asisitiza mashindano hayo ni fursa kubwa ya kiuchumi kwa Tanzania;_*

*_▪︎ Awataka wakandarasi kukamilisha mikataba ya wafanyakazi na kushughulikia stahiki zao ndani ya wiki moja._*

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba ameagiza kuongezwa kasi ya ujenzi wa viwanja vya mazoezi vitakavyotumika katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ili vikamilike kwa wakati na kukidhi viwango vinavyotakiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Amesema kazi hiyo inapaswa kufanyika kwa kasi, ikiwemo kuongeza muda wa kufanya kazi pale inapobidi, ili viwanja vikamilike kwa wakati na Tanzania iwe tayari kabla ya ukaguzi wa maandalizi unaotarajiwa kufanywa na CAF.

Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo leo (Ijumaa, Agosti 21, 2026) baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa viwanja vya mazoezi vya Farasi na Leaders Club jijini Dar es Salaam, ambavyo ni miongoni mwa viwanja vitakavyotumika katika maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027 yatakayofanyika kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda.

Amesema Tanzania haipaswi kusubiri hadi dakika za mwisho kukamilisha maandalizi yake kwa sababu CAF inahitaji kujiridhisha mapema kuwa miundombinu inayohitajika iko tayari.

“Twendeni tufanye kazi usiku na mchana tumalizie asilimia iliyosalia. Wenzetu wanaosimamia mashindano hawawezi kurisk tu kwamba tuko tayari, wanataka wajionee kwamba tuko tayari kukiwa bado kuna muda wa kutosha,” amesema.

Dkt. Mwigulu amesema mashindano ya AFCON hayapaswi kutazamwa kama tukio la michezo pekee, bali ni fursa kubwa ya kiuchumi ambayo Tanzania inapaswa kujiandaa kuitumia kikamilifu.

“Hii si michezo tu, bali pana uchumi ndani yake,” amesema na kuongeza kuwa baada ya kukamilisha miundombinu, nchi inapaswa kuelekeza nguvu katika kujiandaa kimkakati ili kunufaika na fursa za kiuchumi zitakazoambatana na mashindano hayo.

Katika ukaguzi huo, Waziri Mkuu pia ametoa maelekezo ya kushughulikia malalamiko ya wafanyakazi wanaoshiriki ujenzi wa viwanja hivyo, hususan kuhusu mikataba ya ajira, malipo ya muda wa ziada na stahiki nyingine.

Ameagiza Wizara yenye dhamana, wasimamizi wa miradi na wadau wengine kuhakikisha wafanyakazi wanapatiwa mikataba yao ndani ya wiki moja, huku hesabu za mishahara, malipo ya muda wa ziada na stahiki nyingine zikihakikiwa kwa kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa.

“Suala la mikataba lishughulikiwe haraka, lakini pia wazingatie hizi hesabu walizozisema wafanyakazi. Hoja yao inaeleweka,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua uzalendo uliooneshwa na wafanyakazi hao kwa kuendelea na kazi licha ya changamoto walizozieleza, hivyo akaagiza masuala yao yashughulikiwe kwa mujibu wa sheria na makubaliano yaliyopo.

Aidha, amesisitiza kuwa mikataba hiyo izingatie kipindi ambacho wafanyakazi wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwenye miradi hiyo.

Katika uwanja wa Leaders Club, Waziri Mkuu amewapongeza wafanyakazi kwa kuendelea kuchapa kazi na kuwataka waongeze juhudi ili miradi ikamilike ndani ya muda uliopangwa.

Amesema Serikali itaendelea kusimamia changamoto za wafanyakazi sambamba na kuhakikisha kasi ya ujenzi wa miundombinu inaongezeka, kutokana na umuhimu wa AFCON kwa uchumi, michezo na maendeleo ya nchi.

“Tusimwangushe Mheshimiwa Rais. Amejitoa sana kuhakikisha nchi yetu inakuwa mwenyeji wa mashindano haya. Twendeni tukamilishe kwa wakati,” amesema.

Awali, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamisi Mwinjuma, alisema viwanja vya Farasi na Leaders Club ni sehemu ya miundombinu inayojengwa ili kukidhi mahitaji ya CAF kwa ajili ya AFCON 2027.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gerson Msigwa, amesema Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa karibu, sambamba na kushughulikia masuala ya wafanyakazi kwa kushirikiana na taasisi zinazohusika na masuala ya ajira na hifadhi ya jamii.

Kwa mujibu wa taarifa ya wataalamu, ujenzi wa uwanja wa Farasi ulikuwa umefikia asilimia 74 na unatarajiwa kufikia zaidi ya asilimia 80 ifikapo mwisho wa mwezi huu, wakati ujenzi wa uwanja wa Leaders Club ukiendelea kwa kasi kuelekea hatua zinazotakiwa katika ratiba ya maandalizi.

Uwanja wa Farasi unajengwa kama uwanja wa mazoezi wenye vyumba vya kubadilishia nguo, vyumba vya waamuzi, madaktari na huduma nyingine muhimu, pamoja na mfumo wa kisasa wa kuondoa maji uwanjani.

Kwa upande wa Leaders Club, pamoja na huduma hizo, uwanja huo utakuwa na jukwaa lenye uwezo wa kuchukua takribani watazamaji 2,500.