Sakata la mabasi Stendi ya Magufuli bado moto

Dar es Salaam. Amri ya Serikali ya kuzuia mabasi ya mikoani kupakia na kushusha abiria nje ya Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi Luis, imeanza kung’ata na kuzua mvutano, baada ya viongozi wa kampuni moja ya usafirishaji kukamatwa na kufikishwa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.

Mkurugenzi na meneja wa kampuni ya Tilisho jana, Jumatano Agosti 19, 2026, walifikishwa mbele ya Chalamila wakiwa wamefungwa pingu, wakituhumiwa kukiuka agizo la Serikali na kuendelea na utaratibu wa kupakia abiria nje ya kituo hicho.

Viongozi hao walikamatwa wakati wa ukaguzi uliofanywa na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wa agizo la Chalamila alilolitoa Agosti 11, 2026, likitaka mabasi yote ya mikoani kuanza na kumalizia safari katika Kituo cha Magufuli.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, alisema viongozi hao walikamatwa baada ya mamlaka kubaini basi la kampuni hiyo likifanya shughuli za usafirishaji eneo la Riverside, Ubungo kinyume na agizo la Serikali.

Alisema mamlaka zililifunga basi hilo kwa mnyororo, lakini mmiliki wake alipofika eneo hilo alifungua mnyororo huo na kuliondoa.

Mkurugenzi wa kampuni ya mabasi ya Tilisho na meneja wake wakiwa wanapelekwa kwa Mkuu wa Mkoa na pungu mkononi baada ya kukiuka agizo la mabasi yake kwenda kituo Cha Magufuli.

“Wakati tunafanya ukaguzi tulilikuta basi la Tilisho Riverside. Tulilifunga mnyororo kwa sababu lilikuwa linafanya shughuli ambazo Serikali imeagiza zifanyike Kituo cha Magufuli. Mmiliki alipofika alifungua mnyororo na kuliondoa,” amesema Msando.

Baada ya kusikiliza maelezo ya tukio hilo, Chalamila aliwasamehe viongozi hao, lakini akasema hatua hiyo iwe fundisho kwa kampuni nyingine zitakazojaribu kukaidi agizo la Serikali.

Alisema Serikali haitaruhusu baadhi ya wamiliki wa mabasi kuanzisha vituo vyao katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam kwa masilahi binafsi, wakati Serikali imewekeza zaidi ya Sh50 bilioni kujenga Kituo cha Magufuli.

“Latra, kwa yeyote atakayekaidi kutekeleza agizo la kushusha na kupakia abiria hapa, futa vibali vyote,” amesema Chalamila.

Alisema utekelezaji wa agizo hilo unalenga kuweka utaratibu katika shughuli za usafirishaji wa mabasi ya mikoani, huku akitaka mamlaka husika kuhakikisha hakuna kampuni inayoruhusiwa kuendesha vituo visivyo rasmi katika maeneo mengine ya jiji.

Aidha, Chalamila amepiga marufuku mabasi kuegesha au kushusha abiria katika eneo la Shekilango, akisema kampuni zitakazobainika kufanya hivyo zitachukuliwa hatua za kisheria.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alivyopokelewa leo Agosti 19, 2026 Kituo Kikuu cha mabasi cha Magufuli

Hatua hiyo imekuja wakati utekelezaji wa agizo la kurejesha shughuli zote za mabasi ya mikoani katika Kituo cha Magufuli ukiendelea kuzua mjadala miongoni mwa wamiliki wa mabasi na wadau wa usafirishaji; baadhi wakieleza changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wake.

Hata hivyo, Chalamila amesema Serikali iko tayari kusimamia agizo hilo na kuhakikisha uwekezaji uliofanywa katika Kituo cha Magufuli unatumika ipasavyo kwa manufaa ya abiria na sekta ya usafirishaji.

Abiria washushwa, mabasi madogo yatumika

Utekelezaji wa agizo hilo umeanza kuleta mabadiliko katika usafirishaji wa abiria na baadhi ya mabasi ambayo awali yalikuwa yakipakia au kushusha abiria katika ofisi za kampuni zilizokuwa nje ya Stendi ya Magufuli, sasa yameanza kuwafikisha abiria kituoni hapo.

Katika maeneo ambayo mabasi hayawezi kuingia au kuendelea na safari, abiria wanatumia magbasi madogo na daladala kuwafikisha Kituo cha Magufuli.

Kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa, mabasi yanayotoka mikoani yanatakiwa kuingia Stendi ya Magufuli na kushusha abiria, huku yale yanayoanza safari Dar es Salaam yakitakiwa kupakia abiria ndani ya kituo hicho.

Baadhi ya abiria wameeleza kuwa matumizi ya mabasi magodo yamewasaidia kufika kituoni, hasa wale wanaotoka maeneo ya mbali na Mbezi.

Gema Mshana, mkazi wa Masaki amesema eneo la Shekilango lilikuwa rahisi kwake kufika, lakini anashukuru kwa kuwa baada ya kutumia gari dogo kwenda Kituo cha Magufuli, amelipa nauli inayohusisha safari yake ya kwenda mkoani.

Emil Jonas wa Gongo la Mboto amesema kampuni zote zenye ofisi nje ya kituo zinapaswa kuweka utaratibu wa kuwapeleka abiria Magufuli badala ya kuwaambia wakutane kituoni bila msaada wa usafiri.

Hata hivyo, baadhi ya abiria wameonyesha wasiwasi kuhusu muda wa kusubiri mabasi madogo. Luhende Jandika, aliyekuwa akisafiri na familia yake yenye watu 14, amesema alifika kituoni asubuhi akitokea Lindi kuelekea Singida kwa ajili ya mazishi, lakini alilazimika kusubiri muda mrefu hadi basi kuondoka.

Amesema alifika saa tatu asubuhi na kuambiwa gari lao lingeondoka saa sita mchana, hali iliyowaongezea gharama za chakula na mahitaji mengine.

Ameomba kampuni za mabasi kupanga ratiba vizuri ili abiria wanaofikishwa kituoni kwa mabasi madogo wasikae muda mrefu kusubiri mabasi waliyoahidiwa.

Katika utekelezaji wa utaratibu huo, huduma za usafiri wa bodaboda pia zimetajwa kuwa sehemu ya kuwasaidia abiria wanaofika au kuondoka Kituo cha Magufuli.

Bodaboda wanaruhusiwa kubeba abiria pamoja na mizigo yao, hasa katika maeneo yanayohitaji usafiri wa haraka kuelekea au kutoka kituoni.

Hata hivyo, huduma hizo zinatakiwa kuendeshwa kwa kuzingatia taratibu za kituo na usalama wa abiria.

Bodaboda hawatakiwi kuingia maeneo yasiyoruhusiwa ndani ya kituo, bali kuwapokea au kuwashusha abiria katika maeneo yaliyopangwa.

Utaratibu huo unalenga kuwasaidia abiria wanaotumia usafiri wa mabasi, hasa wale wenye mizigo au wanaotoka maeneo ambayo hayana usafiri wa moja kwa moja hadi Kituo cha Magufuli.

Kwa upande mwingine, Chalamila amewataka madereva wa mabasi kukataa maagizo kutoka kwa waajiri wao ya kupakia au kushusha abiria nje ya Kituo cha Magufuli.

Amesema dereva atakayelazimishwa kufanya hivyo anapaswa kukataa kwa kuwa utekelezaji wa agizo la Serikali ni wa lazima.

“Madereva ambao watalazimishwa na mabosi wao kupakia abiria nje ya stendi wakatae, la sivyo wataishia gerezani,” amesema.

Amesema hatakuwa tayari kufanya mazungumzo na wamiliki wa mabasi kuhusu kubadili agizo hilo, akisisitiza kuwa ni msimamo wa Serikali.

Abiria katika kituo Kikuu Cha Mabasi Cha Magufuli kilichopo Mbezi Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam wakiwa wanashushwa katika magari madogo kwa ajili ya kuanzia safari katika kituo hicho.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustapha Mwalongo amesema wamiliki hawajakataa kutekeleza agizo hilo.

Amesema Taboa imeandika barua kwa Mkuu wa Mkoa ikiomba kukutana naye kwa ajili ya majadiliano, kwa kuwa uamuzi huo haukushirikisha chama hicho.

Katika utekelezaji huo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando amesema Serikali imeweka vituo vinne vya ukaguzi ili kudhibiti mabasi yanayoweza kukiuka agizo hilo.

Ametaja vituo hivyo kuwa Kiluvya, Goba Njia Nne, Shekilango na Barabara ya Sam Nujoma.

Amesema tangu Agosti 17, 2026, yeye pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya wamekuwa wakifanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali, hasa Shekilango.

Kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Serikali pia imeagiza hifadhi za barabara ziendelee kuwa wazi na hatua zichukuliwe kwa kampuni zinazopakia abiria katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Msando amesema Jeshi la Polisi limepewa jukumu la kukagua mabasi yanayoenda mikoani kabla hayajaanza safari, huku ukaguzi huo ukifanyika ndani ya Kituo cha Magufuli.

Abiria, wafanyabiashara wanufaika

Baadhi ya wafanyabiashara wadogo katika Kituo cha Magufuli, wakiwemo wamachinga, wabeba mizigo na wapiga debe, wameipongeza Serikali kwa kusimamia matumizi ya kituo hicho.

Wamesema awali baadhi ya mabasi yalikuwa yakipita moja kwa moja bila kupakia au kushusha abiria, hali iliyopunguza wateja na mapato yao.

Mbunge wa Kibamba na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesema kituo hicho kina uwezo wa kuhudumia zaidi ya abiria 33,000 kwa siku, lakini kwa sasa kinahudumia takribani 16,000.

Amesema kuna zaidi ya kampuni 40 za mabasi na kutotumia kituo hicho kumekuwa kukiiingizia halmashauri hasara ya zaidi ya Sh2 bilioni kwa mwaka.

Kwa mujibu wa Kairuki, kituo hicho pia kinatoa ajira kwa zaidi ya watu 7,000, wakiwemo mamalishe, wauza tiketi na wabeba mizigo.