Makamu wa rais mbaroni kwa ulanguzi wa dawa za kulevya

Monrovia. Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Liberia, Jewel Howard Taylor, amekamatwa na Jeshi la Polisi nchini humo na kufunguliwa mashtaka ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, utakatishaji fedha na makosa mengine yanayohusishwa na mtandao wa kimataifa wa usafirishaji wa dawa za kulevya.

Kukamatwa kwa Howard Taylor, kunakuja baada ya mamlaka ya Liberia kutangaza kukamata  kokeini yenye thamani ya takriban dola milioni 317 (Sh808.4 bilioni) iliyokuwa ikielekea barani Ulaya mwezi mmoja uliopita.

Taarifa kutoka  Wizara ya Sheria ya Liberia imeeleza  kuwa, Howard Taylor, aliyekuwa Makamu wa Rais wakati wa utawala wa Rais wa zamani George Weah kuanzia mwaka 2018 hadi 2024, alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Roberts akiwa katika harakati za kuondoka nchini humo.

“Polisi wamewashtaki raia watatu wa kigeni  wawili wa Kroatia na mmoja wa Ukraine ambao walikuwa sehemu ya mtandao na Howard Taylor ili kupisha uchunguzi kwa ajili ya kuwachukuia hatua za kisheria,”imeeleza taarifa hiyo.

Mbali na tuhuma za ulanguzi wa dawa za kulevya na utakatishaji fedha, kiongozi huyo pia anakabiliwa na  tuhuma za kuingiza  dawa zinazodhibitiwa nchini humo bila kibali kutoka mamlaka husika, kushawishi kutendwa kwa uhalifu dhidi ya serikali. Serikali ya Liberia imesema inaendelea na uchunguzi ili kubaini ukweli wa tuhuma hizi ambazo ni  juhudi za kukabiliana na mitandao ya kimataifa ya biashara ya dawa za kulevya huku ikiahidi kuhakikisha mchakato wa kisheria unaendelea bila kuingiliwa kisiasa.

Kwa upande wake, Wakili wa Howard Taylor, Kabineh Ja’neh amekiri kuwa mteja anashikiliwa na mamlaka za kiusalama nchini humo na wataendelea akifikishwa mahakamani.

“Yupo chini ya ulinzi wa polisi wa taifa wa Liberia usiku na  tunategema  kuendelea na suala hilo mara tutakapopata shtaka rasmi,”amesema.

Ikumbukwe kuwa Rais wa Liberia, Joseph Boakai, alipoingia madarakani Januari 2024, aliahidi kuimarisha mapambano dhidi ya ufisadi na kuhakikisha matumizi ya rasilimali za umma yanafanyika kwa uwazi na uwajibikaji.

Ahadi hiyo imekuwa miongoni mwa vipaumbele vya utawala wake katika juhudi za kurejesha imani ya wananchi kwa taasisi za serikali.

Na tangu aingie madarakani, serikali ya Boakai imechukua hatua mbalimbali zinazolenga kuwawajibisha watumishi na viongozi wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ufisadi.

Hatua hizo zimehusisha kuimarisha uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya baadhi ya viongozi wa zamani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kupambana na ufisadi na kuimarisha utawala wa sheria.

Imeandikwa na Elidaima Mangela kwa msaada wa mashirika ya habari.