Zijue mbinu za kujenga utajiri wa muda mrefu

Watu wengi wanapotafuta namna ya kujenga maisha bora ya kifedha, mawazo yao huenda moja kwa moja kwenye kuanzisha biashara, kununua kiwanja, kujenga nyumba au kuweka fedha benki. Hizi zote ni njia nzuri za kutumia na kuhifadhi fedha.

Kununua hisa maana yake ni kununua sehemu ndogo ya umiliki wa kampuni. Unaponunua hisa za kampuni, hata kama ni chache, unakuwa mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo kwa kiwango cha hisa ulizonazo. Kampuni inapokua, kupata faida na kuongeza thamani yake, wewe kama mwanahisa unaweza kunufaika pia.

Jambo muhimu hapa ni kuelewa kwamba uwekezaji kwenye hisa si mpango wa kutajirika kwa siku moja. Ni safari inayohitaji muda, maarifa, nidhamu na uvumilivu.

Fikiria mtu mwenye uwezo wa kutenga Sh100,000 kila mwezi. Badala ya kusubiri mpaka siku moja apate Sh10 milioni ndipo aanze kuwekeza, anaweza kuanza taratibu kwa kiasi anachoweza kumudu. Anaweza kujenga utaratibu wa kuweka fedha pembeni na baada ya kufanya uchambuzi unaofaa, kuwekeza kwenye kampuni zenye misingi mizuri ya biashara.

Baada ya miaka kadhaa, uwekezaji huo unaweza kuwa mkubwa kuliko alivyotarajia mwanzoni. Hii ni kwa sababu utajiri wa muda mrefu haujengwi tu na ukubwa wa fedha uliyoanza nayo. Mara nyingi unajengwa na nidhamu ya kuendelea kuwekeza.

Mwekezaji wa hisa anaweza kupata faida kwa njia kuu mbili. Njia ya kwanza ni ongezeko la thamani ya hisa. Kwa mfano, kama mtu amenunua hisa kwa Sh1,000 na baada ya muda thamani yake ikafikia Sh1,500, thamani ya uwekezaji wake imeongezeka. Hata hivyo, bei inaweza pia kushuka, ndiyo maana uwekezaji unahitaji utafiti na uvumilivu.

Njia ya pili ni gawio au dividend. Kampuni inapopata faida, inaweza kuamua kugawa sehemu ya faida hiyo kwa wanahisa wake. Hivyo, mtu anaweza kuendelea kumiliki hisa zake huku akipokea gawio pale linapotangazwa na kulipwa.

Hapa ndipo tunapopaswa kubadili mtazamo wetu kuhusu fedha. Watu wengi tunafanya kazi kwa bidii ili kupata fedha, lakini hatua nyingine muhimu ni kujifunza namna ya kufanya fedha tulizopata nazo zifanye kazi.

Changamoto nyingine ni kwamba baadhi ya watu huingia kwenye soko la hisa wakitarajia bei ipande haraka. Wakiona bei imeshuka kwa muda mfupi, wanaingiwa na hofu na kuuza. Wengine wakisikia hisa fulani inapanda, wanakimbilia kununua bila hata kuelewa kampuni inayohusika. kununua hisa hakupaswi kufanana na kubashiri.

Uwekezaji mzuri huanza na maarifa. Ni muhimu kutoweka fedha zote kwenye kampuni moja. Kampuni yoyote inaweza kukutana na changamoto.

Jambo jingine muhimu ni muda. Mtu aliyeanza kujenga uwekezaji akiwa na miaka 25 ana nafasi tofauti na yule anayesubiri mpaka miaka 50, hata kama wote wana kiasi kinachofanana cha kuanzia. Miaka mingi inatoa nafasi kwa uwekezaji kukua na mapato yanayopatikana kuendelea kuongezwa kwenye uwekezaji.

Ndiyo maana vijana wanapaswa kufundishwa mapema kuhusu kuweka akiba na kuwekeza. Elimu ya uwekezaji isiwe jambo tunaloanza kulifikiria tunapokaribia kustaafu. Hata hivyo, uwekezaji wowote una hatari.

Hakuna uhakika kwamba bei ya hisa itapanda au kampuni italipa gawio kila mwaka. Ndiyo maana ni muhimu kujifunza, kufanya uchambuzi na inapohitajika kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wenye leseni.

Mwisho wa siku, kujenga utajiri si lazima kuanze na mamilioni ya fedha. Kunaweza kuanza na uamuzi mdogo: kutumia chini ya unachopata, kuweka sehemu ya kipato pembeni, kuwekeza kwa maarifa na kufanya hivyo kwa muda mrefu.