SIRRO : WANAOBEZA TAARIFA ZA TMA KIGOMA KUSHITAKIWA

Na Fadhili Abdallah,Kigoma 

MKUU wa mkoa Kigoma Balozi Simon Sirro amekabidhi misaada kwa waathirika wa mvua za El Nino zinazoendelea kunyesha mkoani Kigomana kuleta madhara kwa watu mbalimbali huku akionya wale wote wanaokaidi kuhama kwenye maeneo hatarishi ambayo yameainishwa na serikali.

 

Mkuu huyo wa mkoa Kigoma amesema hayo akikabidhi misaada kwa wananchi wa kata ya Gungu manispaa ya Kigoma Ujiji ambapo alisema tahadhari imetolewa wananchi kuhama kwenye maeneo hatarishi ambayo yameainishwa lakini wananchi badala ya kufuata maelekezo hayo wengine wanabeza na kusema kuwa ni propaganda kwa ajili ya matumizi ya fedha kwa watendaji kujiilipa posho jambo ambalo serikali imesema haikubaliani nalo na hatua za kisheria kwa watu hao zitachukuliwa.

 

Pamoja na hilo Balozi Sirro alisema kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua na kuwasaidia wananchi watakaoathirika na mvua hiyo kwa sababu mkoa Kigoma umeelezwa kuwa moja ya mikoa ambayo itapata mvua nyingi na kuanzia mwezi Oktoba wilaya za Kigoma, Buhigwem Kakonko, kasulu na Kibondo zimekumbwa na mvua kubwa za upepo ambazo tayari zimeleta madhara kwa wananchi.

 

Awali akitoa taarifa kwa Mkuu wa mkoa kuhusu athari zilizojitokeza Kaimu Mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma Ujiji, Hashim  Mvogogo  alisema kuwa tangu mwezi Oktoba mwaka huu Mvua za El Nino zilipoanza mkoani Kigoma kaya Zaidi ya 100 zimeathirika ambapo nyumba 121 na makanisa manne zimeezuliwa paa na nyingine kuanguka.

 

Mvogogo alisema kuwa kata zilizoathirika na mvua hiyo ni pamoja na Gungu ambapo nyumba 70 zimeathirika, Kibirizi nyumba 47, Mwanga Kusini Nyumba mbili na kata ya Katubuka nyumba mbili.

 

Akieleza msaada uliotolewa kwa wahanga wa mvua hiyo alisema kuwa wamewasilisha tani 2.6 za Mchele, unga wa mahindi tani 1.9, maharage tani moja, sukari, mafuta ya kupikia na  sabuni za kufulia huku wakiendelea kushughulikia mahitaji ya magodoro, shuka, Blanketi na maturubaki huku waathirika wahifadhiwa katika maeneo mbalimbali.

 

Baadhi ya waathirika wa mvua hizo Akiwemo Kobwa Kamana wameishukuru serikali kwa misaada hiyo ya vyakula ingawa alisema kuwa wanaomba serikali ifikirie Zaidi mahitaji ya namna ya kurudi kwenye makazi yao kwa kuwapatia misaada ya bati za kuezekea nyumba zao.

 

Mwisho.

 

Watendaji uchaguzi wasisitizwa uadilifu – HabariLeo

DODOMA: Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele, amewataka watendaji wa uchaguzi kuheshimu viapo vyao na kutekeleza majukumu kwa kuzingatia Katiba, sheria na kanuni za uchaguzi ili kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Mwambegele ametoa wito huo leo, Novemba 2, 2026, katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma, wakati akifunga mafunzo ya watendaji wa uchaguzi yanayolenga kuwaandaa kusimamia uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Chamwino na uchaguzi wa kata 11 za Tanzania Bara.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mwambegele amesema watendaji wanapaswa kuzingatia viapo vyao na kutekeleza majukumu kwa kufuata Katiba, sheria za uchaguzi, kanuni za maadili na maelekezo yanayotolewa na tume.

“Ninawasisitiza kuheshimu viapo vyenu kwa nafasi mlizoteuliwa, tekelezeni majukumu yenu kwa kuzingatia Katiba ya Nchi, sheria za uchaguzi na kanuni zake, kanuni za maadili ya uchaguzi na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na yatakayotolewa na Tume katika kipindi hiki cha uchaguzi,” amesema.

Amewaasa watendaji hao kutofanya kazi kwa mazoea licha ya baadhi yao kuwa na uzoefu wa kusimamia chaguzi zilizopita, akieleza kuwa kila uchaguzi una mazingira na taratibu zake zinazopaswa kuzingatiwa.

Uchaguzi huo mdogo unatarajiwa kufanyika Novemba 4, 2026, katika Jimbo la Chamwino na kata 11 za Tanzania Bara.

Kata hizo ni Nonde katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Lugenge (Halmashauri ya Mji Njombe), Bargish (Halmashauri ya Mji Mbulu), Makole (Halmashauri ya Wilaya ya Muheza), Mwera (Halmashauri ya Wilaya ya Pangani) na Oldonyosambu (Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro).

Nyingine ni Igalula katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Shelui (Halmashauri ya Wilaya ya Iramba), Mvumi (Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa), Nyarero (Halmashauri ya Wilaya ya Tarime) na Ilolangulu (Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe).

MAHUNDI: WAZAZI WANA WAJIBU MKUBWA KULINDA WATOTO DHIDI YA UKATILI

WAZAZI na walezi wametakiwa kuimarisha uangalizi na malezi ya watoto ili kuwakinga dhidi ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji, huku wakisisitizwa kutambua kuwa jukumu la kuhakikisha usalama wa watoto linaanzia katika familia kabla ya kuhitaji hatua za Serikali.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, leo Novemba 2, 2026, jijini Dodoma, wakati akijibu maswali ya Wabunge kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali kutoa elimu kwa mabinti na jamii kuhusu umuhimu wa kuripoti vitendo vya udhalilishaji.

Mahundi amesema wazazi na walezi wanapaswa kutambua nafasi yao katika kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama, yenye malezi bora na ulinzi dhidi ya vitendo vinavyoweza kuathiri maisha na mustakabali wao.

Amesema ni muhimu kwa wazazi kuwa karibu na watoto wao, kuwafuatilia na kuwapatia mwongozo unaozingatia maadili mema, mila, desturi na tamaduni za Kitanzania ili kuwajengea uwezo wa kujitambua na kujilinda.

Ameeleza kuwa jukumu la malezi halipaswi kuachwa kwa Serikali pekee, bali linahitaji ushiriki wa karibu wa familia na jamii katika kutambua, kuzuia na kuripoti vitendo vya ukatili vinavyofanywa dhidi ya watoto.

Akizungumzia hatua za Serikali, Mahundi amesema elimu kwa mabinti na jamii inaendelea kutolewa kupitia Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA).

Amesema mpango huo unatekelezwa kwa kushirikisha kamati za kisekta kuanzia ngazi ya Taifa hadi Vijiji na Mitaa, hatua inayolenga kuhakikisha elimu ya kuzuia ukatili inawafikia wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, amesema kila Kata ina Polisi Jamii wanaoshiriki kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya ulinzi na usalama, ikiwemo namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji.

Mahundi amebainisha kuwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nayo inaratibu wadau wake, wakiwemo viongozi wa kimila na vyombo vya habari, katika kuelimisha jamii kuhusu namna ya kukabiliana na vitendo hivyo.

Amesema ushirikiano wa wadau hao ni muhimu katika kuongeza uelewa wa wananchi na kuimarisha juhudi za kuzuia vitendo vinavyokiuka haki za watoto.

Ameongeza kuwa utoaji wa elimu kwa jamii unapaswa kuambatana na utayari wa wananchi kuripoti vitendo vya ukatili vinapotokea ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.

Mahundi amesisitiza kuwa ulinzi wa watoto ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano wa wazazi, walezi, jamii na Serikali katika kuhakikisha watoto wanakuwa katika mazingira yanayoheshimu haki zao.

Amewataka wananchi wa makundi yote kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutokomeza ukatili wa aina zote, akieleza kuwa watoto wanahitaji mazingira salama yatakayowawezesha kukua vizuri, kupata haki zao na kutimiza ndoto zao.

MWISHO

SERIKALI YASISITIZA UHURU WA WAANDISHI WA HABARI NCHINI

NA MATUKIO DAIMA MEDIA

IRINGA.Serikali imesisitiza umuhimu wa kulinda usalama na uhuru wa waandishi wa habari nchini ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uwajibikaji na bila vitisho, huku ikivitaka kutumia ipasavyo taaluma yao kwa kuzingatia miiko na maadili ya uandishi wa habari katika kutangaza fursa mbalimbali zilizopo nchini, hususan za kiuchumi na uwekezaji.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James wakati wa ufunguzi wa   maadhimisho ya siku ya  kimataifa ya kukomesha kutoadhibiwa kwa wahalifu dhidi ya waandishi wa habari  ,kongamano lililoandaliwa   na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), mkoani Iringa.

Akifungua kikao hicho kilichowakutanisha wawakilishi wa klabu za waandishi wa habari kutoka maeneo mbalimbali, Heri James alisema serikali inatambua mchango wa vyombo vya habari katika kuhabarisha umma na kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa taifa.

“Waandishi wa habari wanapaswa kupata mazingira rafiki yatakayowawezesha kuripoti mafanikio na changamoto za jamii kwa uhuru, huku wakizingatia weledi, usahihi wa taarifa na uwiano wa kimaadili”alisema na kuongeza kuwa 

“vyombo vya habari vina jukumu muhimu katika kulinda haki, amani na mshikamano wa taifa,kuwa taarifa sahihi na zenye uwiano zinaweza kusaidia kupunguza uvumi, kuondoa kutokuelewana na kujenga uelewa miongoni mwa makundi mbalimbali ya kijamii”

Awali, Katibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, alisema hali ya usalama wa waandishi wa habari nchini inaendelea kufuatiliwa kwa karibu, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi za kulinda uhuru wa habari na kuhakikisha wanahabari wanafanya kazi katika mazingira salama yanayoheshimu haki na misingi ya taaluma hiyo.

Sungura alisema MCT inaendelea kufuatilia matukio ya ukiukwaji wa haki na vitisho dhidi ya waandishi wa habari ili kutathmini hali halisi ya usalama wao na kubaini changamoto zinazohitaji hatua za pamoja kutoka kwa wadau wa sekta ya habari.

Kwa mujibu wa takwimu alizowasilisha, matukio 12 ya ukiukwaji wa haki dhidi ya waandishi wa habari yalikuwa yamethibitishwa katika kipindi cha mwaka 2026 , ikilinganishwa na matukio 51 yaliyoripotiwa mwaka 2025 na matukio 33 yaliyorekodiwa mwaka 2024.

Aidha, Sungura alieleza kuwa pamoja na umuhimu wa kulinda usalama wa waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao, masuala ya mazingira ya ajira bado ni changamoto inayohitaji kushughulikiwa ili kuimarisha uhuru na weledi wa taaluma hiyo.

Alibainisha kuwa takwimu zilizotajwa zinaonyesha asilimia 62 ya waandishi wa habari barani Afrika hawana mikataba rasmi ya ajira, huku hali ya Tanzania ikitajwa kuwa na changamoto kubwa zaidi, ambapo takwimu za kipindi cha miaka mitatu iliyopita zinaonyesha kuwa asilimia 80 ya waandishi wa habari hawana mikataba rasmi ya ajira.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa UTPC Keneth Simbaya amewataka Wadau wa masuala ya ajira na haki za binadamu kuimarisha ushirikiano katika kuhakikisha usalama na ustawi wa waandishi wa habari, kwa kuweka mfumo rasmi utakaosaidia kubaini changamoto na vihatarishi vinavyowakabili pamoja na kuboresha usimamizi wa haki zao.

Simbaya alisema kuwa maamuzi yanayofikiwa Novemba 2, 2026 yameweka msingi muhimu wa kuimarisha usalama wa waandishi wa habari, huku akisisitiza umuhimu wa kutathmini maeneo ambayo tayari yanafanya vizuri na yale yanayohitaji kuongezewa nguvu ili kupata matokeo bora zaidi.

“Masuala ya usalama wa waandishi wa habari si jukumu la kundi moja pekee, bali ni suala linalohusu jamii nzima na linahitaji ushiriki wa wadau mbalimbali, kwa kuwa changamoto zinazowakabili waandishi zinaweza kuwa na athari pana zinazogusa haki za binadamu, demokrasia na jamii kwa ujumla.

Aidha, amesema rasimu ya mfumo huo inalenga kuweka utaratibu usioegemea upande wa kisiasa utakaoleta uwiano na mwendelezo katika kushughulikia masuala ya waandishi wa habari, kubaini vihatarishi vinavyowakabili na kuziba mapengo yaliyopo katika usimamizi wa haki na usalama wao.

Kikao hicho kinatarajiwa kusaidia wadau wa habari kutathmini changamoto zinazowakabili waandishi wa habari na kuweka mikakati ya kuimarisha usalama wao, uhuru wa habari na mazingira bora ya utekelezaji wa majukumu yao.

Naye Peter Kivuyo kutoka ofisi ya kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa kitengo cha dawati la sheria na upelelezi alisema kuwa waandishi wa habari wanaowajibu wa kutekeleza majukumu yao bila woga wala vitisho kwa sababu jeshi hilo lipo kwa ajili ya kulinda usalama wa wananchi na mali zao.

MWISHO.

Eva Godwin Atwaa Taji la Miss Africa International 2026 Nigeria

Global Publishers
November 2, 2026
6 views
0 Comments

Tanzania imeendelea kung’ara katika mashindano ya urembo ya kimataifa baada ya mrembo Eva Godwin kutwaa taji la Miss Africa International 2026 katika mashindano yaliyofanyika nchini Nigeria.

Eva alitangazwa mshindi usiku wa kuamkia Novemba 2, 2026, ushindi uliopokelewa kwa pongezi na timu iliyokuwa ikiratibu ushiriki wake, akiwemo Mkurugenzi wa Miss Grand Tanzania, Nazimizye Adam Mdolo.

Mafanikio hayo yanaongeza idadi ya warembo wa Tanzania wanaofanya vizuri katika majukwaa ya kimataifa mwaka huu, huku warembo wengine wakipata nafasi mbalimbali katika mashindano tofauti.

Safari ya Eva kuelekea kwenye ushindi huo ilianzia katika mashindano ya Miss Grand Tanzania 2026 yaliyofanyika Agosti 8, 2026, ambapo Jihan Dimack alitwaa taji la taifa na baadaye kuwakilisha Tanzania katika Miss Grand International 2026 nchini Thailand.

Jihan aliandika historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza na Mwafrika wa kwanza kutwaa taji hilo tangu mashindano hayo yaanzishwe mwaka 2013.

Katika mashindano hayo ya Miss Grand Tanzania, washiriki wengine waliopata mataji ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa ni:

  • Prisca Lyimo – Miss Cosmo Tanzania 2026.

  • Celine Edson – Miss Earth Tanzania 2026.

  • Agape Anthony – Miss International Tanzania 2026.

  • Rossie Uisso – Miss Global Tanzania 2026.

  • Zulfa Yazid – Miss Africa Golden Tanzania 2026.

  • Namala Patrick – Miss Tourism Tanzania 2026.

Kwa upande mwingine, Rossie Uisso aliingia 12 bora katika Miss Global International, huku Sharon Julius akishika nafasi ya tatu katika Miss Elite World yaliyofanyika nchini Misri.

Eva Godwin, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA), aliwahi kutwaa taji la Miss TIA 2026 kabla ya kupata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika Miss Africa International.

Ushindi na nafasi zilizopatikana na warembo hao zimeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazofuatiliwa katika mashindano ya urembo ya kimataifa mwaka 2026.

Video: Samia Atoa Maelekezo Mazito kwa Tume Za Haki na Migogoro ya Kazi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

DODOMA: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameitaka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi wa Migogoro ya Kazi kusimamia sheria na kutenda haki kwa waajiri na waajiriwa bila upendeleo, chuki wala hila katika maamuzi yake.

Rais Samia ametoa maelekezo hayo leo, Novemba 2, 2026, wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi wateule iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, ambapo amempongeza Jaji mstaafu Wilfred Sobera, Mwenyekiti wa tume hiyo, pamoja na makamishna walioapishwa.

Amesema tume hiyo inapaswa kuhakikisha maamuzi yake yanazingatia sheria na ushahidi uliopo, akibainisha kuwa baadhi ya maamuzi yanapowasilishwa kwake kupitia rufaa huwa na hoja zinazohitaji kukubaliwa au kukataliwa.

Amesisitiza kuwa hali hiyo inaonesha umuhimu wa viongozi wa tume kuwa makini, waadilifu na wenye weledi katika kushughulikia migogoro inayojitokeza baina ya waajiri na waajiriwa.

Aidha, Rais Samia amesema ongezeko la uwekezaji na kuingia kwa kampuni binafsi nchini kumeongeza shughuli za kiuchumi pamoja na uwezekano wa kujitokeza kwa migogoro ya kikazi, hivyo tume inapaswa kuhakikisha pande zote zinapata haki kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ameitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kufuatilia na kujibu shutuma zinazotolewa dhidi ya Tanzania kuhusu masuala ya haki za binadamu, kwa kuzingatia ukweli na hali halisi ya mambo.

Akizungumza katika hafla hiyo hiyo, Rais Samia amesema tafsiri ya masuala ya haki za binadamu katika dunia ya sasa imekuwa na changamoto, akibainisha kuwa baadhi ya nchi hukosolewa kutokana na mitazamo ya wengine, huku nyingine zikikabiliwa na tuhuma bila kupewa uzito unaolingana.

Amewataka makamishna wa tume hiyo kutumia uwezo na mamlaka yao kufuatilia taarifa zinazochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na majukwaa mbalimbali kuhusu Tanzania, kuzichambua na kutoa majibu yanayozingatia ukweli.

Amesisitiza kuwa jukumu la tume hiyo halipaswi kuishia kusubiri malalamiko kutoka kwa wananchi wanaodai kuvunjiwa haki zao, bali linapaswa pia kujumuisha ufuatiliaji wa masuala ya utawala bora na namna haki za binadamu zinavyotekelezwa nchini.

Rais Samia amesema matarajio yake ni kuona tume hiyo ikitekeleza majukumu yake kwa upana, ikiwemo kushughulikia malalamiko ya wananchi, kufuatilia masuala ya utawala bora na kutoa ufafanuzi kuhusu hoja zinazotolewa kimataifa kuhusiana na hali ya haki za binadamu nchini.

Maelekezo hayo yametolewa wakati wa kuwaapisha viongozi wateule wa taasisi hizo, yakilenga kusisitiza wajibu wa tume hizo katika kusimamia haki, uwajibikaji na utawala bora nchini.

Rais Samia Akutana na Mwalimu Wake wa Zamani Baada ya Miaka 40

Global Publishers
November 2, 2026
18 views
0 Comments

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amekutana na mwalimu wake wa zamani, Mzee George Mpelumbe, aliyemfundisha alipokuwa akisoma katika Chuo cha Usimamizi wa Maendeleo (IDM) mwaka 1986.

IDM kwa sasa kinajulikana kama Chuo Kikuu cha Mzumbe.

Rais Samia amekutana na mwalimu huyo leo, Jumatatu, Novemba 2, 2026, katika hafla ya kuwaapisha viongozi aliowateua, iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma.

Watendaji uchaguzi watakiwa wasisitizwa uadilifu – HabariLeo

DODOMA: Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele, amewataka watendaji wa uchaguzi kuheshimu viapo vyao na kutekeleza majukumu kwa kuzingatia Katiba, sheria na kanuni za uchaguzi ili kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Mwambegele ametoa wito huo leo, Novemba 2, 2026, katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma, wakati akifunga mafunzo ya watendaji wa uchaguzi yanayolenga kuwaandaa kusimamia uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Chamwino na uchaguzi wa kata 11 za Tanzania Bara.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mwambegele amesema watendaji wanapaswa kuzingatia viapo vyao na kutekeleza majukumu kwa kufuata Katiba, sheria za uchaguzi, kanuni za maadili na maelekezo yanayotolewa na tume.

“Ninawasisitiza kuheshimu viapo vyenu kwa nafasi mlizoteuliwa, tekelezeni majukumu yenu kwa kuzingatia Katiba ya Nchi, sheria za uchaguzi na kanuni zake, kanuni za maadili ya uchaguzi na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na yatakayotolewa na Tume katika kipindi hiki cha uchaguzi,” amesema.

Amewaasa watendaji hao kutofanya kazi kwa mazoea licha ya baadhi yao kuwa na uzoefu wa kusimamia chaguzi zilizopita, akieleza kuwa kila uchaguzi una mazingira na taratibu zake zinazopaswa kuzingatiwa.

Uchaguzi huo mdogo unatarajiwa kufanyika Novemba 4, 2026, katika Jimbo la Chamwino na kata 11 za Tanzania Bara.

Kata hizo ni Nonde katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Lugenge (Halmashauri ya Mji Njombe), Bargish (Halmashauri ya Mji Mbulu), Makole (Halmashauri ya Wilaya ya Muheza), Mwera (Halmashauri ya Wilaya ya Pangani) na Oldonyosambu (Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro).

Nyingine ni Igalula katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, Shelui (Halmashauri ya Wilaya ya Iramba), Mvumi (Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa), Nyarero (Halmashauri ya Wilaya ya Tarime) na Ilolangulu (Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe).

YAS Yakabidhi Vifaa Tiba Hospitali ya Wete, Kuimarisha Huduma za Mama na Mtoto

PEMBA: Kampuni ya mawasiliano ya YAS Tanzania imekabidhi vifaa tiba mbalimbali kwa Hospitali ya Wilaya ya Wete Kinyasini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuboresha huduma za afya na kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Wete, Abdalla Rashid Ali, ameipongeza kampuni hiyo kwa kujitolea kusaidia jamii kupitia huduma mbalimbali za kijamii.

Amesema msaada huo utasaidia kuimarisha huduma za afya, hususan kwa akinamama wajawazito wanaofika hospitalini hapo kupata huduma za uzazi, pamoja na kupunguza changamoto zinazowakabili wahudumu wa afya.

Amesema hatua hiyo inaonesha kuwa YAS si kampuni inayojihusisha na huduma za mawasiliano pekee, bali pia ina dhamira ya kushiriki katika maendeleo ya jamii.

“Nyinyi si watu wa mawasiliano pekee, kumbe mna upande mwingine ambao bado haujajulikana. Leo mmekuja kutuonesha mfano kwa kukabidhi baadhi ya vifaa muhimu kwa hospitali yetu, hususan katika kuwahudumia akinamama wajawazito,” alisema.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amesema uwekezaji katika afya ya mama na mtoto ni uwekezaji katika maisha ya kizazi kijacho, huku akiwataka wafanyakazi wa hospitali hiyo kuhakikisha vifaa vilivyotolewa vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kampuni ya YAS Zanzibar, Mohamed Wakid, ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa juhudi zake za kuimarisha huduma za afya nchini.

Amesema kupitia kampeni ya Tumaini, kampuni hiyo imeamua kutoa vifaa tiba kwa Hospitali ya Wete Kinyasini ili kusaidia kuboresha huduma za uzazi kwa akinamama wanaofika hospitalini hapo.

Ameeleza kuwa kampeni hiyo ni ya kipekee kwa kuwa wazo lake lilitokana na wafanyakazi wenyewe wa kampuni hiyo kuguswa na changamoto zinazowakabili akinamama wakati wa kujifungua.

“Kampeni hii ya Tumaini ni ya kipekee, kwani wazo lake limeanzia kwa wafanyakazi wenyewe baada ya kuguswa na changamoto zinazowakabili akinamama wanapofika hospitalini kujifungua,” alisema Wakid.

Akitaja baadhi ya vifaa vilivyokabidhiwa, alisema ni pamoja na vitanda, viti mwendo, vitanda vya kujifungulia, kanga, mashuka na vifaa vingine mbalimbali vinavyohitajika katika utoaji wa huduma za afya.

Aidha, amesema kampuni hiyo imeendelea kupanua huduma zake za mawasiliano Zanzibar, ambapo kwa mujibu wa maelezo yake imefikia takribani asilimia 99 ya wananchi wa visiwa hivyo.

Nao baadhi ya akinamama waliokuwepo hospitalini hapo wameishukuru YAS Tanzania kwa msaada huo, wakisema utasaidia kuboresha mazingira ya huduma na kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za uzazi.

Fatma Juma Hamad ameipongeza kampuni hiyo kwa kujitokeza kusaidia hospitali hiyo, huku akizitaka kampuni na taasisi nyingine kuiga mfano huo kwa kuchangia katika kuboresha huduma za afya.

Kwa upande wake, Raya Seif Abdalla amesema vifaa vilivyotolewa vitakuwa na mchango mkubwa katika kusaidia akinamama wanaofika hospitalini hapo kupata huduma wakati wote.

Msaada huo kupitia kampeni ya Tumaini unaonesha mchango wa sekta binafsi katika kuunga mkono juhudi za kuboresha huduma za afya na ustawi wa jamii nchini Zanzibar.

MWISHO.

Rita Moreno Afichua Siri ya Kutunza Tuzo Zake Zote Katika Chumba Maalumu Nyumbani

Mwigizaji mkongwe wa Hollywood, Rita Moreno, mwenye umri wa miaka 94, amefichua kuwa ana chumba maalumu nyumbani kwake ambacho hutumia kutunza tuzo zote alizojinyakulia katika safari yake ya zaidi ya miaka 80 kwenye tasnia ya burudani.

Moreno ametoa kauli hiyo alipohudhuria hafla ya 2026 Día de Muertos Gala iliyofanyika jijini Los Angeles, Marekani, Oktoba 27, ambapo alizungumza kuhusu namna anavyohifadhi kumbukumbu za mafanikio yake.

“Nimeshinda vitu vingi sana. Tuzo zangu ziko nyumbani, nina chumba kimoja ambacho zote zimewekwa,” alisema Moreno.

Mwigizaji huyo ni miongoni mwa wasanii wachache duniani waliotunukiwa heshima ya EGOT, inayotolewa kwa watu waliofanikiwa kushinda tuzo kuu nne za burudani nchini Marekani, ambazo ni Emmy, Grammy, Oscar na Tony.

Alikamilisha mafanikio hayo mwaka 1977 baada ya kushinda tuzo ya Primetime Emmy kutokana na ushiriki wake katika kipindi cha televisheni cha The Muppet Show.

Safari yake ya mafanikio ilianza mwaka 1962 aliposhinda tuzo ya Oscar ya mwigizaji bora msaidizi kupitia filamu ya West Side Story Mwaka 1972 alitwaa tuzo ya Grammy kupitia kazi yake ya The Electric Company, kabla ya kushinda tuzo ya Tony mwaka 1975 kutokana na uigizaji wake katika tamthilia ya The Ritz.

Mwaka 1978 aliongeza tuzo nyingine ya Emmy baada ya kutambuliwa kama mwigizaji bora wa kike katika kipindi cha televisheni kupitia nafasi yake katika tamthilia ya The Rockford Files.

Mbali na tuzo hizo nne kubwa, Moreno amepokea heshima na tuzo nyingine nyingi katika kipindi chote cha kazi yake iliyohusisha maigizo ya jukwaani na filamu.

Kwa sasa, mwigizaji huyo anajiandaa kutimiza miaka 95 ifikapo Desemba 11, 2026, ambapo amesema anatarajia kusherehekea siku hiyo kwa kupata chakula cha jioni pamoja na marafiki zake wa karibu.

Akizungumzia hatua hiyo ya maisha yake, Moreno amesema anashangazwa na safari yake ya kufikia umri huo na kujiona bado anaendelea kuwa imara.

Pia amesema anajisikia mwenye heshima kubwa kuwa miongoni mwa wasanii wachache waliosalia kutoka kizazi cha dhahabu cha Hollywood (Hollywood’s Golden Age).

Amesema anafurahia kuendelea kuwa hai na kupata nafasi ya kushuhudia safari ndefu ya maisha yake katika tasnia ya burudani.