UWEKEZAJI wa kampuni ya Saudi Gold Refinery kutoka Saudi Arabia unatarajiwa kuongeza kasi ya utafiti wa madini nchini baada ya Serikali kuipatia kampuni hiyo leseni tisa, huku ikitangaza mpango wa kuwekeza Sh bilioni 26 katika shughuli za utafiti na uwekezaji.
Hatua hiyo inaashiria kuongezeka kwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Saudi Arabia, huku Serikali ikielekeza nguvu katika kuvutia wawekezaji wenye uwezo wa kuendeleza maeneo ya madini na kuyageuza kuwa vyanzo vya uzalishaji na ajira.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alisema uwekezaji huo umefuatia mazungumzo yaliyofanyika katika mkutano wa kibiashara kati ya Tanzania na Saudi Arabia, ambapo kampuni hiyo ilieleza nia yake ya kuingia katika sekta ya madini nchini.
Amesema baada ya mazungumzo hayo, Serikali ilichukua hatua za haraka kuhakikisha kampuni hiyo inapata leseni za awali ndani ya siku saba za kazi kama ilivyoahidiwa, jambo lililoiwezesha kuendelea na taratibu za kupata maeneo mengine ya utafiti kupitia Tume ya Madini.
Mavunde amesema Serikali inalenga kuvutia wawekezaji ambao hawataishia kumiliki leseni na maeneo ya madini, bali watakaotekeleza shughuli za utafiti na kuanzisha shughuli za uchimbaji kwa kutumia mitaji, vifaa na utaalamu walionao.
Amesema kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wamiliki wa leseni kushikilia maeneo makubwa ya madini bila kuyaendeleza, hali inayozuia maeneo hayo kutumiwa na wawekezaji wengine wenye uwezo wa kuyafanyia kazi.
“Kutokana na hali hiyo, amesema Serikali imekuwa ikifuta leseni za wale wanaoshindwa kutekeleza masharti ya umiliki na kurejesha maeneo hayo ili yatolewe kwa wawekezaji wengine watakaoyaendeleza, ” Amesema
Na Kuongeza kuwa “Si maeneo yote yanayorejeshwa yanatolewa kwa kampuni kubwa, kwani mengine huandaliwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo kupitia programu ya Mining for Brighter Tomorrow inayowalenga wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ” Amesema Mavunde.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha makundi mbalimbali yanapata nafasi ya kushiriki katika shughuli za uchimbaji na kunufaika na fursa zinazotokana na rasilimali za madini.
Aidha, Mavunde amesema Tanzania ina mazingira mazuri na rafiki kwa uwekezaji, hivyo Serikali itaendelea kutumia fursa za mikutano ya kimataifa na majukwaa ya kibiashara kutangaza fursa zilizopo nchini na kuvutia mitaji kutoka mataifa mbalimbali.
Akizungumzia mwenendo wa mapato, alisema katika kipindi cha Julai hadi Oktoba mwaka huu, sekta ya madini imekusanya Sh bilioni 500.2 dhidi ya lengo la Sh bilioni 351, sawa na utekelezaji wa asilimia 117.8.
Amesema kwa mwaka huu wa fedha, sekta hiyo imejiwekea lengo la kukusanya Sh trilioni 1.4, akieleza kuwa uwekezaji mpya katika utafiti na uchimbaji ni miongoni mwa hatua zitakazosaidia kuongeza uzalishaji na mapato ya Serikali.
Kwa upande wake, mwakilishi wa kampuni ya Saudi Gold Refinery, Faisal Suleiman, amesema kampuni hiyo imepanga kuelekeza Sh bilioni 26 katika shughuli za utafiti na uwekezaji wa madini nchini ili kutimiza malengo yake.
Suleiman ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwapa nafasi ya kuwekeza na kueleza kuwa kampuni hiyo inalenga kushirikiana na Watanzania katika kutekeleza shughuli zake.
Ameahidi kuwa uwekezaji huo utatoa nafasi za ajira kwa wazawa, hatua itakayowawezesha kupata kipato, kuboresha maisha yao na kushiriki katika manufaa yatokanayo na sekta ya madini nchini.
Mwisho.
















