RC MBEYA AONYA WANAOBEZA MVUA ZA ELNINO MITANDAONI

Na  Matukio  Daima Media,Mbeya 

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Jumanne Sagini, amewaonya wananchi wanaofanya mzaha na kudhihaki tahadhari za Serikali kuhusu mvua za El Niño kupitia mitandao ya kijamii, akisema madhara yaliyotokana na mvua zilizonyesha jijini Mbeya ni ushahidi kuwa suala hilo linapaswa kuchukuliwa kwa uzito.

Sagini ametoa onyo hilo Novemba 4, 2026, wakati alipotembelea wananchi walioathiriwa na mafuriko katika Kata ya Nzovwe, jijini Mbeya, ambapo baadhi ya nyumba zimebomolewa na maji huku vyakula na mali nyingine zikisombwa na mafuriko.

Amesema kwa miezi kadhaa Serikali imekuwa ikitoa tahadhari kuhusu uwezekano wa mvua za El Niño, lakini baadhi ya wananchi wamekuwa wakizipokea kwa mzaha na kejeli kupitia mitandao ya kijamii.

“Niendelee kuwaomba wananchi, miezi kadhaa imepita Serikali imekuwa ikizungumzia mvua za El Niño, lakini watu wengine wamekuwa wakileta mizaha kwenye mitandao ya kijamii, wakisema, ‘mbona wameahidi sana, tunaisubiri El Niño yetu’. Sasa mambo mazito watu wanafanya mizaha. Unaisubiri El Niño sasa iliyotokea Novemba 3, tuiite nini?” amehoji Sagini.

Amesema mvua ya Novemba 3, 2026, ilidumu kwa takribani dakika 30 pekee, lakini ilisababisha madhara makubwa kwa wananchi, akiwataka watu kuomba mvua zinyeshe bila kusababisha majanga badala ya kubeza tahadhari zinazotolewa na wataalamu.

Aidha, amewataka wananchi wa Jiji la Mbeya kuchukua tahadhari na kujiandaa kukabiliana na mvua zinazotarajiwa, akieleza kuwa madhara yaliyotokea baada ya mvua ya nusu saa ni ishara ya hatari inayoweza kujitokeza endapo mvua zitadumu kwa muda mrefu.

“Kwa hiyo, niwaombe upande wa Serikali kuhakikisha watu wanapata miundombinu na sehemu za kuhifadhiwa. Mheshimiwa DC na wakurugenzi wako msibweteke, utaratibu uendelee ili watu wapate mahali pa kukimbilia. Lakini wananchi waliopo kwenye maeneo hatarishi, hizi ni salamu za awali tujiandae, zikija mvua nzito zinazohofiwa na wataalamu wetu tuwe na mahali pa kwenda,” amesema.

Sagini amefafanua kuwa wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi wanapaswa kuanza kuondoka kwa muda katika maeneo hayo ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na mafuriko, badala ya kusubiri maji yafike kwenye makazi yao.

Amesisitiza kuwa maji yana nguvu kubwa na hivyo wananchi wanapaswa kuweka usalama wao mbele hata katika kipindi ambacho bado wanakabiliana na majonzi yaliyosababishwa na mafuriko.

Kwa upande wake, Josephat Mwanjesa, amemshukuru Mkuu wa Mkoa pamoja na ujumbe wake kwa kuwafikia mapema na kuwafariji waathirika wa mafuriko hayo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamati ya Maafa, mvua hiyo iliyonyesha kwa muda usiozidi dakika 30 imeathiri nyumba 21 na kaya zisizopungua 43.

Mwisho.

EAC YAWEKA MIKAKATI YA PAMOJA KUKABILI ATHARI ZA EL NIÑO KALI

Na, Matukio Daima Media -Nairobi , Kenya

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zinaendelea na mkutano wao jijini Nairobi, Kenya, kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa za El Niño zinazotarajiwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Siku ya pili ya mkutano huo ulioanza Novemba 04, 2026, Maafisa Wakuu wa Usimamizi wa Maafa wa nchi wanachama wa EAC wamejadili mpango wa pamoja wa namna ya kukabiliana na  athari zinazoweza kujitokeza katika Kanda.

Maafisa hao pamoja na mambo mengine wanatathmini uwezo wa nchi wanachama katika kukabiliana na majanga, kubaini mapungufu yaliyopo na kuweka mikakati ya uratibu wa pamoja ili kulinda maisha ya wananchi, huduma muhimu na shughuli za kiuchumi, hususan biashara katika ukanda huo.

Mkutano huo utahitimishwa na Mkutano wa Dharura wa pamoja wa Mabaraza ya Kisekta ya Mawaziri wa Ushirikiano katika Ulinzi, Amani na Usalama na Uratibu wa Sera za Mambo ya Nje wa EAC, utakaofanyika Novemba 06, 2026 kwa ajili ya kuimarisha maandalizi ya kikanda ya kukabiliana na majanga hayo.

=MWISHO=

 

e-GA YAWATAKA MAAFISA TEHAMA KUHAKIKISHA TAASISI ZAO ZINAKUWA NA NYARAKA MUHIMU ZA USIMAMIZI WA TEHAMA

MENEJA wa Usimamizi na Udhibiti na Viwango vya Serikali Mtandao (e-GA) Bi. Sultana Seiff amewataka Maafisa TEHAMA kuhakikisha taasisi zao zinakuwa na nyaraka muhimu za TEHAMA zinazosaidia kusimamia na kutekeleza ipasavyo Jitihada za Serikali Mtandao 

Bi. Sultana ameyasema hayo wakati wa mafunzo ya siku tano yanayoendelea jijini Dodoma, yanayolenga kutoa uelewa wa pamoja kuhusu Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Usimamizi na Utekelezaji wa Teknolojia Zinazoibukia, ikiwemo Akili Unde (AI), kwa Maafisa TEHAMA.

Meneja huyo amesema kuwa, nyaraka hizo ni pamoja na Sera ya TEHAMA, Mkakati wa TEHAMA, Sera ya Usalama wa TEHAMA, Mpango wa Urejeshaji wa Huduma baada ya Maafa, Sera ya Matumizi Sahihi ya Rasilimali za TEHAMA, Taratibu za Usimamizi wa Huduma za TEHAMA, Taratibu za Usimamizi wa Miradi ya TEHAMA, Taratibu za Uendelezaji, Ununuzi, Uendeshaji na Matengenezo ya Mifumo ya TEHAMA pamoja na Muundo wa Jumla wa Usanifu wa Mifumo ya Taasisi (Enterprises Architecture). 

Amesisitiza kuwa uwepo wa nyaraka hizo ni muhimu katika kuhakikisha shughuli za TEHAMA zinafanyika kwa kuzingatia taratibu, viwango na miongozo iliyowekwa, sambamba na kuimarisha usalama wa mifumo na taarifa za taasisi za umma.

Aidha, amewahimiza Maafisa TEHAMA kutumia mafunzo hayo kuongeza ujuzi na uelewa kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia zinazoibukia, hususan Akili Unde, ili kuweza kuzitumia kwa tija katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Afisa TEHAMA kutoka Bohari ya Dawa (MSD), Bw. Erick Makabali, amesema mafunzo hayo yamemwezesha kupata uelewa wa namna ya kuandaa nyaraka ya Usanifu wa Jumla wa TEHAMA wa Taasisi (Enterprise Architecture), ambayo itasaidia taasisi yake kupanga na kusimamia uwekezaji wa TEHAMA kwa ufanisi.

Ameeleza kuwa uwepo wa nyaraka hiyo utasaidia MSD kuepuka kujenga au kununua mifumo ya TEHAMA inayotekeleza majukumu yanayofanana, kupunguza gharama zisizo za lazima na kuhakikisha bajeti ya TEHAMA inaelekezwa katika maeneo yenye vipaumbele na mahitaji halisi ya taasisi.

Aidha, amesema mafunzo ya uandaaji wa nyaraka hiyo yatamsaidia kuboresha uratibu na muunganiko wa mifumo ya TEHAMA, kurahisisha usimamizi wa rasilimali za teknolojia na kuimarisha utoaji wa huduma kwa ufanisi.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia e-GA za kuimarisha uwezo wa rasilimali watu katika usimamizi na matumizi ya TEHAMA, pamoja na kuendeleza utekelezaji wa Serikali Mtandao nchini

RC MBEYA AONYA WANAOBEZA MVUA ZA ELNINO MITANDAONI

Na  Matukio  Daima Media,Mbeya 

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Jumanne Sagini, amewaonya wananchi wanaofanya mzaha na kudhihaki tahadhari za Serikali kuhusu mvua za El Niño kupitia mitandao ya kijamii, akisema madhara yaliyotokana na mvua zilizonyesha jijini Mbeya ni ushahidi kuwa suala hilo linapaswa kuchukuliwa kwa uzito.

Sagini ametoa onyo hilo Novemba 4, 2026, wakati alipotembelea wananchi walioathiriwa na mafuriko katika Kata ya Nzovwe, jijini Mbeya, ambapo baadhi ya nyumba zimebomolewa na maji huku vyakula na mali nyingine zikisombwa na mafuriko.

Amesema kwa miezi kadhaa Serikali imekuwa ikitoa tahadhari kuhusu uwezekano wa mvua za El Niño, lakini baadhi ya wananchi wamekuwa wakizipokea kwa mzaha na kejeli kupitia mitandao ya kijamii.

“Niendelee kuwaomba wananchi, miezi kadhaa imepita Serikali imekuwa ikizungumzia mvua za El Niño, lakini watu wengine wamekuwa wakileta mizaha kwenye mitandao ya kijamii, wakisema, ‘mbona wameahidi sana, tunaisubiri El Niño yetu’. Sasa mambo mazito watu wanafanya mizaha. Unaisubiri El Niño sasa iliyotokea Novemba 3, tuiite nini?” amehoji Sagini.

Amesema mvua ya Novemba 3, 2026, ilidumu kwa takribani dakika 30 pekee, lakini ilisababisha madhara makubwa kwa wananchi, akiwataka watu kuomba mvua zinyeshe bila kusababisha majanga badala ya kubeza tahadhari zinazotolewa na wataalamu.

Aidha, amewataka wananchi wa Jiji la Mbeya kuchukua tahadhari na kujiandaa kukabiliana na mvua zinazotarajiwa, akieleza kuwa madhara yaliyotokea baada ya mvua ya nusu saa ni ishara ya hatari inayoweza kujitokeza endapo mvua zitadumu kwa muda mrefu.

“Kwa hiyo, niwaombe upande wa Serikali kuhakikisha watu wanapata miundombinu na sehemu za kuhifadhiwa. Mheshimiwa DC na wakurugenzi wako msibweteke, utaratibu uendelee ili watu wapate mahali pa kukimbilia. Lakini wananchi waliopo kwenye maeneo hatarishi, hizi ni salamu za awali tujiandae, zikija mvua nzito zinazohofiwa na wataalamu wetu tuwe na mahali pa kwenda,” amesema.

Sagini amefafanua kuwa wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi wanapaswa kuanza kuondoka kwa muda katika maeneo hayo ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na mafuriko, badala ya kusubiri maji yafike kwenye makazi yao.

Amesisitiza kuwa maji yana nguvu kubwa na hivyo wananchi wanapaswa kuweka usalama wao mbele hata katika kipindi ambacho bado wanakabiliana na majonzi yaliyosababishwa na mafuriko.

Kwa upande wake, Josephat Mwanjesa, amemshukuru Mkuu wa Mkoa pamoja na ujumbe wake kwa kuwafikia mapema na kuwafariji waathirika wa mafuriko hayo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamati ya Maafa, mvua hiyo iliyonyesha kwa muda usiozidi dakika 30 imeathiri nyumba 21 na kaya zisizopungua 43.

Mwisho.

 

EAC YAWEKA MIKAKATI YA PAMOJA KUKABILI ATHARI ZA EL NIÑO KALI

Na, Matukio Daima Media -Nairobi , Kenya

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zinaendelea na mkutano wao jijini Nairobi, Kenya, kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa za El Niño zinazotarajiwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Siku ya pili ya mkutano huo ulioanza Novemba 04, 2026, Maafisa Wakuu wa Usimamizi wa Maafa wa nchi wanachama wa EAC wamejadili mpango wa pamoja wa namna ya kukabiliana na  athari zinazoweza kujitokeza katika Kanda.

Maafisa hao pamoja na mambo mengine wanatathmini uwezo wa nchi wanachama katika kukabiliana na majanga, kubaini mapungufu yaliyopo na kuweka mikakati ya uratibu wa pamoja ili kulinda maisha ya wananchi, huduma muhimu na shughuli za kiuchumi, hususan biashara katika ukanda huo.

Mkutano huo utahitimishwa na Mkutano wa Dharura wa pamoja wa Mabaraza ya Kisekta ya Mawaziri wa Ushirikiano katika Ulinzi, Amani na Usalama na Uratibu wa Sera za Mambo ya Nje wa EAC, utakaofanyika Novemba 06, 2026 kwa ajili ya kuimarisha maandalizi ya kikanda ya kukabiliana na majanga hayo.

=MWISHO=

Vijana waomba ushiriki ngazi za maamuzi – HabariLeo

DAR ES SALAAM: CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimesema changamoto za ajira na kipato ni miongoni mwa sababu zinazochochea vijana kudai nafasi na mahitaji yao katika jamii.

Pia, kimeeleza kuwa vijana wanapaswa kupewa nafasi ya kushiriki katika maamuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ili kutumia uwezo wao katika maendeleo badala ya kujieleza kupitia vitendo vinavyoharibu mali na miundombinu.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Utafiti), Profesa Nelson Boniface, amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tisa wa Kimataifa wa Sauti ya Sayansi za Jamii ulioandaliwa na Ndaki ya Sayansi za Jamii ya chuo hicho, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo wa siku mbili ulikuwa na kaulimbiu isemayo ‘Kutafakari Upya Leo na Kesho: Kizazi cha Gen Z na Harakati za Kijamii Barani Afrika’, ukiwakutanisha watafiti na washiriki kutoka nchi mbalimbali kujadili changamoto na nafasi ya vijana katika jamii.

Alisema harakati za vijana zinaonekana duniani kote kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa ajira zinazoweza kuwachukua wahitimu wa vyuo vikuu na vijana wengine wanaotafuta kipato.

Alisema: “Idadi ya watu duniani imeongezeka na kuzidi uwezo wa uchumi kuzalisha ajira. Hivyo, sekta ya elimu, serikali na wafanyabiashara wanapaswa kushirikiana kutafuta shughuli za kuwawezesha vijana kupata kipato.”

Hata hivyo, alisema ingawa vijana wana haki ya kudai mahitaji yao, njia zinazohusisha uharibifu wa mali na miundombinu si sahihi, hivyo wazazi, walezi na wanataaluma wana wajibu wa kuwaelimisha njia bora za kufikisha madai yao kwa wenye mamlaka.

Alisema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka masuala ya vijana, ujasiriamali, elimu na ujuzi kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya maendeleo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Ndaki ya Sayansi za Jamii ya UDSM, Profesa Christine Noe, alisema harakati za Gen Z ni suala la kimataifa linalohusisha masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, hivyo zinahitaji kueleweka kupitia tafiti zinazozingatia mazingira tofauti ya vijana.

Alisema mabadiliko ya sayansi na teknolojia pamoja na tabianchi yanaathiri maisha ya vijana, yakiwapatia fursa mpya lakini pia changamoto zinazohitaji jamii na watunga sera kuzitambua.

Alisema hakuna sababu moja inayoweza kueleza harakati zote za vijana kwa kuwa changamoto na fursa wanazokutana nazo hutofautiana kulingana na mazingira wanayoishi.

Aliongeza kuwa mjadala huo utasaidia kupata mawazo ya vijana wenyewe kutoka nchi mbalimbali ili kuelewa wanachopitia na namna ya kuwawezesha kushiriki katika maendeleo ya mataifa yao.

Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa UDSM, Mwakigoye Diamond Stephen, alisema mkutano huo ni fursa muhimu kwa vijana kutoa maoni yao na kushiriki katika mijadala ya maamuzi yanayohusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Alisema vijana wamekuwa wakionekana kutokuwa na uwezo wa kujieleza na kuwakilisha maslahi yao, jambo linalofanya baadhi yao kuamua kusimamia hoja zao wenyewe.

Alisema: “Kupitia mkutano huu, vijana watapata fursa ya kuonyesha kuwa wana uwezo wa kujisemea wenyewe na kushiriki katika kufanya maamuzi yanayohusu maisha yao na maendeleo ya taifa.”

Aliongeza kuwa harakati za Gen Z zinajitokeza katika maeneo mbalimbali, yakiwemo siasa, uchumi na jamii, hivyo mkutano huo unaweza kuongeza nidhamu na kujiamini kwa vijana katika kutekeleza majukumu yao.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa UDSM, Zuleha Mohammed, alisema vijana wanapaswa kupewa elimu ya kutosha ili waweze kuleta mabadiliko chanya katika jamii bila kusababisha vurugu.

Alitoa wito kwa viongozi na jamii kwa ujumla kuwapa vijana kipaumbele katika masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi ili wajione kuwa sehemu muhimu ya maendeleo.

Katika mhadhara mkuu wa mkutano huo, Profesa Mette Olwig wa Chuo Kikuu cha Roskilde nchini Denmark, alieleza namna mitandao ya kijamii inavyowasaidia vijana kujenga mitandao ya kimataifa, kupata fursa za kitaaluma na kuendeleza ushirikiano unaovuka mipaka.

Hata hivyo, alisema matumizi ya mitandao hiyo yanaweza kuleta shinikizo kwa vijana kujenga taswira fulani ili kuvutia wafuasi na kupata nafasi za kushiriki katika mafunzo na mikutano ya kimataifa.

Alisema baadhi ya vijana walieleza kuwa picha na machapisho ya matukio wanayohudhuria huwasaidia kutambulika na kupata fursa nyingine, lakini pia huongeza shinikizo la kuwa hai muda wote kwenye mitandao ya kijamii.

Profesa Olwig alisema changamoto nyingine ni matumizi ya mifumo ya kimataifa kama Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), ambayo wakati mwingine haizingatii tofauti za mazingira, uzoefu na uwezo wa vijana wa Kaskazini na Kusini mwa dunia.

Alisema ingawa mitandao ya kijamii na malengo ya pamoja vinaweza kuwaunganisha vijana duniani, havipaswi kufuta tofauti zao za ndani au kuendeleza mifumo ya ukosefu wa usawa iliyojengwa katika historia ya ukoloni.

Alisisitiza kuwa mshikamano wa vijana duniani unapaswa kujengwa kwa kuzingatia mazingira na uzoefu wao halisi ili kuhakikisha sauti zao zinawakilishwa kwa usawa.

Mpanzu, Barker wachomoza tuzo Oktoba – HabariLeo

DAR ES SALAAM; Kiungo mshambuliaji wa Simba ya Dar es Salaam, Elie Mpanzu amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Oktoba wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2026/27, huku Steve Barker pia wa Simba akichaguliwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.

Taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), imesema Mpanzu alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiwashinda Idd Selemani wa Azam FC na Nathaniel Chilambo wa Simba, alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

“Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo mitatu ambayo  ilicheza mwezi huo na kushinda yote, huku nyota huyo akifunga mabao matatu.

“Kwa upande wa Barker aliyeingia fainali na Florent Ibenge wa Azam na Juma Mgunda wa Namungo, aliiongoza Simba kushinda michezo yote mitatu iliyocheza mwezi huo na kupanda kutoka nafasi ya pili hadi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi yenye timu 16,” imesema taarifa hiyo.

Taarifa imesema Kamati pia imeteua magoli matatu bora, ambayo yatapigiwa kura na mashabiki ili kupata goli bora la mwezi Oktoba. Magoli hayo ni  Hassan Mubiru (Azam v Mbeya City), Elie Mpanzu (Simba v Yanga) na  Selemani Bwenzi (Simba V Mashujaa).

Kamati ya Tuzo pia imemteua Meneja wa Uwanja wa Kwaraa, Jackson Mwendwa  kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Oktoba kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.

“Pia Kamati ya Tuzo imemchagua Ramadhan Kalanje wa KMC kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Oktoba wa Ligi ya Championship, akiwashinda Abdulkarim Segeja wa Kigamboni na Hamdani Ally wa Transit Camp alioingia nao fainali.

“Kwa upande wa Kocha Bora wa ligi hiyo, kamati ilimchagua Awadh Juma wa Mtibwa Sugar aliyewashinda Habibu Kondo wa Bandari na Mohmed Muya wa KMC alioingia nao fainali katika mchakato huo,” imesema taarifa hiyo.

Shigongo Ahoji Hatima ya Rasilimali za Madini, Mwigulu Aeleza Hatua za Serikali – Video

Global Publishers
November 5, 2026
0 views
0 Comments

Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Eric Shigongo.

Mbunge wa Jimbo la Buchosa, Eric Shigongo, ameitaka Serikali kueleza hatua zinazochukuliwa kuhakikisha kuwa vizazi vijavyo vinanufaika na utajiri wa rasilimali za madini zinazopatikana nchini Tanzania.

Katika hoja yake, Shigongo ameibua wasiwasi kuhusu hatima ya rasilimali hizo, akitaka kuhakikisha kuwa madini yanapokwisha, vizazi vijavyo havibaki na mashimo pekee badala ya kunufaika na utajiri wa taifa.

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba.

Swali hilo amelielekeza kwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, akitaka kufahamu mikakati ya Serikali katika kusimamia rasilimali za madini kwa kuzingatia maslahi ya muda mrefu ya Watanzania.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba ameeleza hatua mbalimbali ambazo Serikali tayari imezichukua ili kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania wa sasa na vizazi vijavyo.

Majibu ya Waziri Mkuu yamelenga kueleza namna Serikali inavyosimamia matumizi ya rasilimali hizo ili kuhakikisha utajiri wa madini unachangia maendeleo endelevu ya taifa.

Hoja hiyo imeibua mjadala muhimu kuhusu usimamizi wa rasilimali za taifa, uhifadhi wa mazingira na umuhimu wa kuhakikisha mapato yanayotokana na madini yanabadilishwa kuwa manufaa ya kudumu kwa Watanzania.

CRDB yazindua kampeni kidijitali zaidi – HabariLeo

DAR ES SALAAM: Benki ya CRDB imeboresha huduma zake za Internet Banking kwa kuweka mifumo inayowawezesha wateja kufanya miamala kwa haraka, urahisi na usalama zaidi, huku ikitoa fursa ya kujisajili wenyewe na kuanza kutumia huduma hiyo bila kulazimika kufika katika matawi ya benki hiyo.

Maboresho hayo ni sehemu ya jitihada za benki hiyo kuendelea kuboresha huduma za kidijitali na kuwapa wateja urahisi wa kufanya miamala yao wakati wowote na mahali popote.

Akizungumza kuhusu maboresho hayo, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Benki ya CRDB, Bonaventure Paul, amesema hatua hiyo inalenga kuondoa changamoto zilizokuwa zikijitokeza kwa watumiaji wa Internet Banking na kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa huduma za kibenki.

Amesema huduma hiyo sasa inawawezesha wateja kufanya miamala saa 24 kwa siku na siku saba za wiki, hali inayowapa uhuru wa kupata huduma za kibenki muda wowote bila kutegemea saa za kazi za matawi au mawakala.

Paul amesema moja ya maboresho muhimu ni kuanzishwa kwa mfumo wa kujisajili mwenyewe (Self-registration), unaomwezesha mteja mwenye akaunti ya CRDB iliyounganishwa na kadi ya ATM kujisajili na kuanza kutumia Internet Banking bila kufika katika tawi la benki.

Amesema hatua hiyo itapunguza muda na gharama ambazo wateja wamekuwa wakitumia kufuata huduma hiyo kwenye matawi, huku ikiongeza urahisi wa kupata huduma za kidijitali.

Aidha, amesema maboresho mengine ni kuwepo kwa uwezo wa mteja kurejesha huduma yake (Unlock) pale akaunti ya Internet Banking inapozuiwa kutokana na kuingiza nywila isiyo sahihi mara kadhaa.

Amesema kupitia mfumo huo, mteja anaweza kurejesha huduma yake bila kulazimika kufika katika tawi la benki kwa ajili ya kuhakikiwa upya.

Maboresho hayo yanatarajiwa kuongeza matumizi ya huduma za kibenki kupitia njia za kidijitali, kupunguza utegemezi wa huduma za ana kwa ana na kuwezesha wateja wa CRDB kupata huduma kwa urahisi zaidi.

Makonda na Baba Levo Wavutana Kuhusu Ujenzi wa Uwanja wa Arusha – Video


Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Clayton Revocatus Chipando maarufu kama Baba Levo, amepinga maelezo yaliyotolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kuhusu gharama za ujenzi wa Uwanja wa Arusha unaokadiriwa kufikia Shilingi bilioni 338.

Baba Levo amesema hoja ya kuutetea Uwanja wa Arusha kwa kuulinganisha na mapungufu ya Uwanja wa Benjamin Mkapa haina mashiko, akisisitiza kuwa viwanja vyote vinasimamiwa na wizara moja.

Akizungumza na Jambo TV kuhusu ufafanuzi wa Serikali uliotolewa Bungeni, mbunge huyo amesema hapingi ujenzi wala ubora wa Uwanja wa Arusha, bali anataka kuwepo kwa uwazi kuhusu matumizi ya fedha za umma.

Amesisitiza kuwa ndiyo sababu ameomba Serikali iwasilishe mchanganuo wa gharama za mradi huo, unaojulikana kama Bill of Quantities (BOQ), ili kuwezesha kufahamu namna fedha hizo zilivyopangwa na kutumika.

“Huwezi kuutetea Uwanja wa Arusha kwa kuuponda wa Mkapa na viwanja vyote vipo kwenye Wizara yako. Sisi hatujakataa kiwanja cha Arusha siyo bora ila tumehoji kuhusu matumizi ya pesa, mwisho tumeomba BOQ,” amesema Baba Levo.

Hoja hiyo aliitoa pia Bungeni jijini Dodoma Novemba 4, 2026, alipolinganisha gharama za Uwanja wa Arusha unaotarajiwa kuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 30,000 na Uwanja wa Benjamin Mkapa wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000.

Kwa mujibu wa hoja yake, Uwanja wa Benjamin Mkapa, uliokamilishwa kati ya mwaka 2005 na 2007, uligharimu kati ya Shilingi bilioni 40 na 63, huku Uwanja wa Arusha ukikadiriwa kugharimu Shilingi bilioni 338.

Aidha, Baba Levo alirejelea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akidai kuwa mkandarasi wa mradi wa Uwanja wa Arusha alipatikana kupitia mfumo wa manunuzi wa Single Source, hali aliyoihusisha na ongezeko la gharama za mradi.

Hata hivyo, Waziri Makonda alipojibu hoja hizo Bungeni alieleza kuwa Uwanja wa Arusha hauwezi kulinganishwa moja kwa moja na Uwanja wa Benjamin Mkapa kutokana na tofauti za miundombinu na viwango vilivyotumika.

Makonda alitolea mfano changamoto ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kushindwa kutumika kwa michezo wakati wa mvua kubwa, akisema Uwanja wa Arusha umezingatia mahitaji ya miundombinu ya kisasa.

Kuhusu gharama, Waziri huyo alifafanua kuwa kiasi cha Shilingi bilioni 338 kinajumuisha takribani Shilingi bilioni 52 za kodi, huku makadirio ya awali ya Shilingi bilioni 107 yakiwa hayajajumuisha kodi hiyo.

Aliongeza kuwa ongezeko la gharama limetokana na mabadiliko ya usanifu na kuboresha miundombinu kufikia viwango vya kimataifa vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), ikiwemo ujenzi wa Sky Boxes 21 pamoja na lifti sita.

Kuhusu matumizi ya mfumo wa Single Source, Makonda alisema mfumo huo unatambulika kisheria na unaweza kutumika katika taratibu za manunuzi ya umma.

Hadi sasa, hoja kuu katika mjadala huo inaendelea kuwa uwazi wa gharama za mradi, mchanganuo wa matumizi ya fedha na sababu za tofauti kubwa kati ya makadirio ya awali na gharama ya mwisho ya ujenzi wa Uwanja wa Arusha.