Makonda na Baba Levo Wavutana Kuhusu Ujenzi wa Uwanja wa Arusha – Video


Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Clayton Revocatus Chipando maarufu kama Baba Levo, amepinga maelezo yaliyotolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kuhusu gharama za ujenzi wa Uwanja wa Arusha unaokadiriwa kufikia Shilingi bilioni 338.

Baba Levo amesema hoja ya kuutetea Uwanja wa Arusha kwa kuulinganisha na mapungufu ya Uwanja wa Benjamin Mkapa haina mashiko, akisisitiza kuwa viwanja vyote vinasimamiwa na wizara moja.

Akizungumza na Jambo TV kuhusu ufafanuzi wa Serikali uliotolewa Bungeni, mbunge huyo amesema hapingi ujenzi wala ubora wa Uwanja wa Arusha, bali anataka kuwepo kwa uwazi kuhusu matumizi ya fedha za umma.

Amesisitiza kuwa ndiyo sababu ameomba Serikali iwasilishe mchanganuo wa gharama za mradi huo, unaojulikana kama Bill of Quantities (BOQ), ili kuwezesha kufahamu namna fedha hizo zilivyopangwa na kutumika.

“Huwezi kuutetea Uwanja wa Arusha kwa kuuponda wa Mkapa na viwanja vyote vipo kwenye Wizara yako. Sisi hatujakataa kiwanja cha Arusha siyo bora ila tumehoji kuhusu matumizi ya pesa, mwisho tumeomba BOQ,” amesema Baba Levo.

Hoja hiyo aliitoa pia Bungeni jijini Dodoma Novemba 4, 2026, alipolinganisha gharama za Uwanja wa Arusha unaotarajiwa kuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 30,000 na Uwanja wa Benjamin Mkapa wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000.

Kwa mujibu wa hoja yake, Uwanja wa Benjamin Mkapa, uliokamilishwa kati ya mwaka 2005 na 2007, uligharimu kati ya Shilingi bilioni 40 na 63, huku Uwanja wa Arusha ukikadiriwa kugharimu Shilingi bilioni 338.

Aidha, Baba Levo alirejelea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), akidai kuwa mkandarasi wa mradi wa Uwanja wa Arusha alipatikana kupitia mfumo wa manunuzi wa Single Source, hali aliyoihusisha na ongezeko la gharama za mradi.

Hata hivyo, Waziri Makonda alipojibu hoja hizo Bungeni alieleza kuwa Uwanja wa Arusha hauwezi kulinganishwa moja kwa moja na Uwanja wa Benjamin Mkapa kutokana na tofauti za miundombinu na viwango vilivyotumika.

Makonda alitolea mfano changamoto ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kushindwa kutumika kwa michezo wakati wa mvua kubwa, akisema Uwanja wa Arusha umezingatia mahitaji ya miundombinu ya kisasa.

Kuhusu gharama, Waziri huyo alifafanua kuwa kiasi cha Shilingi bilioni 338 kinajumuisha takribani Shilingi bilioni 52 za kodi, huku makadirio ya awali ya Shilingi bilioni 107 yakiwa hayajajumuisha kodi hiyo.

Aliongeza kuwa ongezeko la gharama limetokana na mabadiliko ya usanifu na kuboresha miundombinu kufikia viwango vya kimataifa vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), ikiwemo ujenzi wa Sky Boxes 21 pamoja na lifti sita.

Kuhusu matumizi ya mfumo wa Single Source, Makonda alisema mfumo huo unatambulika kisheria na unaweza kutumika katika taratibu za manunuzi ya umma.

Hadi sasa, hoja kuu katika mjadala huo inaendelea kuwa uwazi wa gharama za mradi, mchanganuo wa matumizi ya fedha na sababu za tofauti kubwa kati ya makadirio ya awali na gharama ya mwisho ya ujenzi wa Uwanja wa Arusha.

Waziri Mkuu: Serikali ya Samia Kuifufua Rasmi Ajenda ya Katiba Mpya – Video

Global Publishers
November 5, 2026
72 views
0 Comments

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, leo Novemba 5, 2026 amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeipa uzito ajenda ya upatikanaji wa Katiba Mpya, akieleza kuwa dhamira ya kufufua mchakato huo ipo na tayari mwongozo umetolewa.

Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo Bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu, aliyetaka kufahamu ni lini mchakato wa Katiba Mpya utaanza pamoja na utaratibu utakaotumika katika utekelezaji wake.

Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu amesema suala la Katiba Mpya ni muhimu kwa Watanzania na limejumuishwa katika Ilani ya Uchaguzi, jambo linaloonesha kuwa Serikali inalipa kipaumbele.

Amesisitiza kuwa Serikali ina dhamira ya kuendeleza suala hilo, huku akibainisha kuwa tayari hatua za kutoa mwongozo zimechukuliwa ili kuweka msingi wa kufufua mchakato huo.

Kauli hiyo imekuja wakati suala la Katiba Mpya likiendelea kuwa miongoni mwa ajenda muhimu katika mijadala ya kisiasa na kijamii nchini Tanzania, huku wananchi wakisubiri ufafanuzi zaidi kuhusu muda na utaratibu wa kuanza kwa mchakato huo.

Netanyahu Atoa Onyo Kali Dhidi ya Serikali Itakayoungwa Mkono na Vyama vya Kiarabu

Global Publishers
November 5, 2026
0 views
0 Comments

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amepinga uwezekano wa kuundwa kwa serikali ya wachache itakayokuwa madarakani kwa kutegemea uungwaji mkono wa vyama vya Kiarabu, akivitaka vyama vya Kizayuni kuungana na Likud kuunda serikali pana ya kitaifa.

Akizungumza Jumatano jioni Novemba 4, 2026 Netanyahu alisema Israel inakabiliwa na changamoto za kiusalama zinazotokana na Iran na washirika wake, pamoja na kile alichokitaja kuwa ni vitisho vya ndani vinavyohusishwa na vyama vya Kiislamu vinavyounga mkono ugaidi.

Alidai kuwa vyama hivyo vinatishia utambulisho wa Kiyahudi wa taifa la Israel na vinaweza kuathiri uwezo wa serikali kukabiliana na maadui wake.

Netanyahu alionya kuwa serikali yoyote itakayokuwa inategemea uungwaji mkono wa vyama hivyo haitakuwa na uwezo wa kutosha kukabiliana na changamoto za kiusalama.

Alisema wawakilishi wa vyama hivyo wamekuwa wakitoa kauli ambazo, kwa mtazamo wake, zinaonyesha uungwaji mkono kwa wapiganaji wa Nukhba wanaoshikiliwa katika magereza ya Israel.

Badala yake, Netanyahu ametaka kuundwa kwa serikali pana ya kitaifa itakayoongozwa na chama chake cha Likud, ikijumuisha vyama vyote vya muungano wa kitaifa pamoja na vyama vingine vya Kizayuni vitakavyokuwa tayari kujiunga.

Aidha, aliwashutumu viongozi wa kambi ya mrengo wa kushoto kwa kujaribu kuunda serikali nyembamba ya wachache inayotegemea uungwaji mkono wa vyama vya Kiarabu.

Alidai kuwa viongozi hao wanaweka mbele maslahi yao ya kisiasa badala ya maslahi ya taifa.

Kauli za Netanyahu zinaonesha kuendelea kwa mvutano wa kisiasa nchini Israel kuhusu muundo wa serikali ijayo na nafasi ya vyama vya Kiarabu katika siasa za nchi hiyo.

Fenerbahce Yafanya Comeback ya Kishindo, Liverpool Yapigwa 3-2 Istanbul, Uturuki

Liverpool imepata kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Fenerbahce katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliopigwa kwenye Uwanja wa Sukru Saracoglu jijini Istanbul, Uturuki, baada ya kushindwa kulinda faida ya kuongoza mara mbili.

Liverpool ilianza vizuri na kupata bao la kuongoza kupitia kwa kinda Trey Nyoni, ambaye alifunga bao lake la kwanza akiwa na klabu hiyo. Hata hivyo, Fenerbahce ilisawazisha dakika nne baadaye kupitia kwa Mason Greenwood, ambaye mpira wake wa adhabu uligonga mchezaji wa Liverpool Jeremy Jacquet na kuingia wavuni.

Mchezo uliendelea kuwa wa ushindani mkubwa huku Liverpool ikifanikiwa kupata bao la pili dakika ya 69 kupitia kwa Alexander Isak, aliyefunga kwa kichwa na kuipa timu yake matumaini ya kuondoka na ushindi muhimu ugenini.

Hata hivyo, furaha ya Liverpool haikudumu kwa muda mrefu kwani Fenerbahce ilisawazisha kupitia kwa Archie Brown, aliyenufaika na mpira wa kichwa wa Cody Gakpo uliomshinda kipa Alisson na kumkuta akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga.

Dakika sita baadaye, wenyeji walipata bao la ushindi kupitia kwa Vedat Muriqi, aliyefunga kwa kichwa baada ya Liverpool kushindwa kuondoa hatari iliyotokana na mpira mrefu uliorushwa ndani ya eneo la hatari.

Matokeo hayo yamekuwa pigo kwa Liverpool, ambayo ilionekana kuwa na nafasi nzuri ya kupata ushindi baada ya kuongoza mara mbili, lakini makosa ya ulinzi, hasa katika mipira iliyokufa na mipira ya juu, yaliigharimu timu hiyo.

Kocha wa Liverpool, Andoni Iraola, alielezea mabao waliyofungwa kuwa ya kizembe na yenye mkanganyiko, akisisitiza kuwa timu yake ilipaswa kufanya vizuri zaidi katika kuzuia mashambulizi ya aina hiyo.

Kwa upande mwingine, kocha wa muda wa Fenerbahce, Dirk Kuyt, ambaye aliwahi kuitumikia Liverpool kwa miaka sita, aliwapongeza wachezaji wake kwa kupambana hadi dakika za mwisho.

Kuyt alisema aliwakumbusha wachezaji wake kuhusu moyo wa kupambana alioujifunza wakati akiichezea Liverpool, akieleza kuwa walikuwa na nafasi ya kuandika historia mpya jijini Istanbul.

Ushindi huo umekuwa wa kipekee kwa Fenerbahce, huku Kuyt akieleza kuwa ilikuwa mara ya kwanza baada ya miaka 18 kwa klabu hiyo kupata ushindi dhidi ya timu ya England.

Kwa Liverpool, kipigo hicho kimeongeza maswali kuhusu uimara wa safu yake ya ulinzi, hasa baada ya timu hiyo pia kupoteza mchezo dhidi ya Arsenal siku chache zilizopita.

Mchezaji wa zamani wa Liverpool, Stephen Warnock, alisema timu hiyo inaendelea kukumbwa na tatizo la kujirudia la kuruhusu mabao mepesi, licha ya kuonyesha maendeleo katika upande wa ushambuliaji.

Kwa upande wa Fenerbahce, ushindi huo umeipa timu sababu mpya ya kujiamini, huku Kuyt akieleza kuwa matokeo hayo ni usiku wa kipekee kwa mashabiki na wote wanaoipenda klabu hiyo.

The post Fenerbahce Yafanya Comeback ya Kishindo, Liverpool Yapigwa 3-2 Istanbul, Uturuki appeared first on Global Publishers.

WAZIRI MKUU AITAKA NFRA KUHARAKISHA MAUZO YA MAZAO

*_▪︎ Bei ya kununua mahindi yaongezwa hadi shilingi 500_*

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ameitaka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuharakisha taratibu za kuuza mazao pindi masoko yanapopatikana, ili kuepuka kupoteza fursa hizo kutokana na michakato mirefu.

Vilevile, amezitaka taasisi zinazohusika kuendelea kutafuta masoko ya kudumu na kuwezesha uuzaji wa mazao nje ya nchi, huku akieleza kuwa bei ya kununua mahindi kupitia NFRA imeongezwa kutoka shilingi 450 hadi shilingi 500.

Amesema hayo Bungeni, jijini Dodoma leo (Alhamisi, Novemba 05, 2026), wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, katika Mkutano wa Tano, Kikao cha Nane cha Bunge la 13.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Kongwa, Isaya Mngurumi Moses, aliyetaka kufahamu mikakati ya Serikali ya kutafuta masoko na kuboresha bei za mazao ili wakulima wanufaike na uzalishaji wao.

Dkt. Mwigulu amesema NFRA inapopata masoko inapaswa kukamilisha taratibu za mauzo kwa wakati, kwa sababu ucheleweshaji unaweza kuwafanya wanunuzi kupata mazao katika masoko mengine yenye michakato mifupi zaidi.

Amesema Serikali imekuwa ikitumia mazungumzo na viongozi wa mataifa mbalimbali kutafuta masoko ya mazao ya Tanzania na kupanua wigo wa biashara kwa wakulima.

Kuhusu bei ya mahindi, Waziri Mkuu amesema amekutana na Wizara yenye dhamana ya kilimo mara kadhaa kujadili namna ya kuboresha bei ya ununuzi kupitia NFRA.

Amesema bei hiyo iliongezwa kutoka shilingi 200 hadi shilingi 300, baadaye shilingi 450 na sasa shilingi 500.

“Tulikaa tena kwa mara ya mwisho, tukashauriana kwamba kama bado wanaweza kwenda juu zaidi, wafanye hivyo, na tulikubaliana sasa watapeleka iwe shilingi 500,” amesema.

Amewataka wakulima wenye mahindi wanayohitaji kuuza kufika katika ofisi za NFRA za mikoa na kanda ili kutumia fursa ya bei hiyo iliyoboreshwa.

Hata hivyo, amesema NFRA huenda isiweze kununua mahindi yote, hivyo jitihada za kupanua masoko na kuwezesha mauzo nje ya nchi zinapaswa kuendelea.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaelekeza Wakuu wa Mikoa kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaopeleka mifugo katika mashamba ya wakulima bila ridhaa yao, akisisitiza kuwa Serikali haitakubali uvunjaji wa sheria wa makusudi.

Akijibu swali la Mbunge wa Nachingwea, Fadhili Ally Liwaka, kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji, amesema hatua zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya mtu aliyefanya kosa, bila kugeuza tukio hilo kuwa mgogoro kati ya jamii.

“Kama mmoja amefanya kosa hilo, achukuliwe hatua kali huyo huyo. Wala wakulima wasione wafugaji ni adui zao, na wala wafugaji wasione wakulima ni adui zao,” amesema.

Amewataka wananchi kuepuka kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutumia vyombo vya sheria kutafuta haki.

Vilevile, amewaelekeza viongozi katika ngazi mbalimbali kuimarisha mipango ya matumizi bora ya ardhi na kusitisha ugawaji wa maeneo kinyemela. Amesema rushwa, matumizi mabaya ya ofisi na ugawaji wa ardhi usiofuata taratibu vinachochea migogoro katika jamii.

Kuhusu huduma za afya, Waziri Mkuu amesema Serikali itafanya uandikishaji wa awamu ya pili wa bima ya afya kwa wote ili kuendelea kuyafikia makundi ambayo bado hayajafikiwa.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Stella Alex Ikupa, kuhusu matibabu kwa watu wenye ulemavu ambao bado hawajafikiwa na mpango huo, amezitaka taasisi za afya kuendelea kuwahudumia kupitia dirisha la msamaha wa matibabu.

“Pasitokee mtu kukosa matibabu kwa sababu ya hali yake ya ulemavu ama hali yake ya kifedha,” amesema.

Amewahimiza pia Watanzania kuendelea kujisajili katika mfumo wa bima ya afya kwa wote, akisisitiza kuwa mpango huo unalenga wananchi wote, wenye kipato na wasio na kipato.

Nyota 70 Waingia Kinyang’anyiro cha Tuzo za CAF 2026, Hakimi Aongoza Orodha

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limetangaza rasmi orodha ya wachezaji, makocha, timu za taifa na klabu zitakazowania tuzo za CAF Awards 2026, huku nyota mbalimbali wa soka la Afrika wakitajwa katika vipengele saba vya upande wa wanaume.

Miongoni mwa majina makubwa katika kipengele cha Mchezaji Bora wa Mwaka Afrika ni mshindi wa tuzo ya mwaka 2025, Achraf Hakimi wa Morocco, Sadio Mané wa Senegal, Antoine Semenyo wa Ghana, Brahim Diaz wa Morocco na Amad Diallo wa Ivory Coast.

Sherehe za utoaji wa tuzo hizo zinatarajiwa kufanyika Desemba 7, 2026, jijini Lagos nchini Nigeria, zikilenga kutambua mafanikio ya wachezaji na timu katika mashindano ya klabu na timu za taifa.

Orodha hiyo imehusisha wachezaji kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, huku Morocco, Senegal na Afrika Kusini zikiwa na uwakilishi mkubwa katika vipengele tofauti.

1. MCHEZAJI BORA WA MWAKA AFRIKA (CAF MEN’S PLAYER OF THE YEAR)

Achraf Hakimi ataingia katika kinyang’anyiro cha kutetea tuzo aliyoshinda mwaka 2025, akipambana na nyota wengine tisa.

Wanaowania:

  1. Amad Diallo (Ivory Coast/Manchester United)
  2. Yoane Wissa (DR Congo/Newcastle United)
  3. Antoine Semenyo (Ghana/Manchester City)
  4. Ismael Saibari (Morocco/Bayern Munich)
  5. Achraf Hakimi (Morocco/Paris Saint-Germain)
  6. Brahim Diaz (Morocco/Real Madrid)
  7. Ismaila Sarr (Senegal/Crystal Palace)
  8. Pape Gueye (Senegal/Villarreal)
  9. Sadio Mané (Senegal/Al-Nassr)
  10. Teboho Mokoena (Afrika Kusini/Mamelodi Sundowns)

2. KIPA BORA WA MWAKA (CAF MEN’S GOALKEEPER OF THE YEAR)

Kipengele hiki kinawakutanisha makipa kumi waliofanya vizuri katika mashindano ya kimataifa na ya klabu.

Wanaowania:

  1. Oussama Benbot (Algeria/USM Alger)
  2. Vozinha (Cape Verde/Colo-Colo)
  3. Yahia Fofana (Ivory Coast/Rizespor)
  4. Lionel Mpasi (DR Congo/Le Havre)
  5. El-Mahdi Soliman (Misri/Zamalek)
  6. Mostafa Shobeir (Misri/Al Ahly)
  7. Ahmed Reda Tagnaouti (Morocco/AS FAR)
  8. Yassine Bonou (Morocco/Al Hilal)
  9. Edouard Mendy (Senegal/Al Ahli)
  10. Ronwen Williams (Afrika Kusini/Mamelodi Sundowns)

3. MCHEZAJI BORA WA MASHINDANO YA VILABU AFRIKA (CAF MEN’S INTERCLUB PLAYER OF THE YEAR)

Katika kipengele hiki, Mamelodi Sundowns ina wachezaji wawili, Teboho Mokoena na Khuliso Mudau, kufuatia mafanikio ya klabu hiyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2025/2026.

Wanaowania:

  1. Abdennour Belhocini (Algeria/CR Belouizdad)
  2. Ahmed Khaldi (Algeria/USM Alger)
  3. Mahmoud Hassan ‘Trezeguet’ (Misri/Al Ahly)
  4. Mohamed Shehata (Misri/Zamalek)
  5. Mohamed Rabie Hrimat (Morocco/AS FAR)
  6. Mounir Chouiar (Morocco/RS Berkane)
  7. Sofiane El Moudane (Morocco/Olympic Safi)
  8. Khuliso Mudau (Afrika Kusini/Mamelodi Sundowns)
  9. Teboho Mokoena (Afrika Kusini/Mamelodi Sundowns)
  10. Abdel Raouf (Sudan/Al Hilal)

4. KOCHA BORA WA MWAKA (CAF MEN’S COACH OF THE YEAR)

Makocha kumi wameteuliwa kuwania tuzo hii kutokana na mchango wao katika mafanikio ya klabu na timu za taifa.

Wanaowania:

  1. Lamine N’Diaye (USM Alger)
  2. Pedro Leitão Brito ‘Bubista’ (Cape Verde)
  3. Sébastien Desabre (DR Congo)
  4. Hossam Hassan (Misri)
  5. Moatamed Gamal (Zamalek)
  6. Alexandre Santos (AS FAR)
  7. Mohamed Ouahbi (Morocco)
  8. Walid Regragui (Morocco)
  9. Pape Thiaw (Senegal)
  10. Miguel Cardoso (Mamelodi Sundowns)

5. MCHEZAJI CHIPUKIZI BORA WA MWAKA (CAF MEN’S YOUNG PLAYER OF THE YEAR)

Kipengele hiki kinatambua vipaji vya vijana vilivyoonyesha uwezo mkubwa katika soka la Afrika na mashindano ya kimataifa.

Wanaowania:

  1. Ibrahim Maza (Algeria/Bayer Leverkusen)
  2. Christian Kofane (Cameroon/Bayer Leverkusen)
  3. Christ Inao (Ivory Coast/Fiorentina)
  4. Yan Diomande (Ivory Coast/Real Madrid)
  5. Hamza Abdelkarim (Misri/Barcelona)
  6. Caleb Yirenkyi (Ghana/Coventry City)
  7. Ismael Kamissoko (Mali/Etoiles Mandé)
  8. Abdellah Ouazane (Morocco/Ajax)
  9. Ayoub Bouaddi (Morocco/Manchester City)
  10. Ibrahim Mbaye (Senegal/Aston Villa)

6. TIMU BORA YA TAIFA YA MWAKA (CAF MEN’S NATIONAL TEAM OF THE YEAR)

Mataifa kumi yameingia katika orodha ya wanaowania tuzo hii baada ya kushiriki mashindano ya kimataifa, ikiwemo Kombe la Dunia la FIFA 2026.

Wanaowania:

  1. Algeria
  2. Cape Verde
  3. Ivory Coast
  4. DR Congo
  5. Misri
  6. Ghana
  7. Morocco
  8. Senegal
  9. Afrika Kusini
  10. Tunisia

7. KLABU BORA YA MWAKA (CAF MEN’S CLUB OF THE YEAR)

Klabu kumi zimeingia katika kinyang’anyiro cha tuzo hii, zikiwemo Mamelodi Sundowns iliyotwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2025/2026.

Wanaowania:

  1. CR Belouizdad (Algeria)
  2. USM Alger (Algeria)
  3. AS Maniema (DR Congo)
  4. Zamalek (Misri)
  5. AS FAR (Morocco)
  6. Olympic Safi (Morocco)
  7. RS Berkane (Morocco)
  8. Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini)
  9. Al Hilal (Sudan)
  10. Espérance Sportive de Tunis (Tunisia)

Sherehe za CAF Awards 2026 zitafanyika Jumatatu, Desemba 7, jijini Lagos nchini Nigeria, ambapo washindi wa vipengele hivyo watatangazwa na kutambuliwa kwa mchango wao katika maendeleo ya soka la Afrika.

ATHUMANI AHUKUMIWA MIAKA 20 JELA KWA KUKUTWA NA NYARA ZA SERIKALI

 

Mahakama ya Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro imemhukumu Athumani Issa Rashid, (47), kifungo cha miaka 20 jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kupatikana na nyara za Serikali, zikiwemo nyama za wanyamapori wawili aina ya digidigi, huku pikipiki moja aliyokuwa akitumia ikitaifishwa na Serikali.

Hukumu hiyo imetolewa Novemba 3, 2026, baada ya Mahakama kujiridhisha na ushahidi uliowasilishwa katika kesi ya uhujumu uchumi namba ECO 16343/2026, iliyofunguliwa dhidi ya mshtakiwa huyo.

Kwa mujibu wa taarifa za tukio, mshtakiwa alikamatwa Julai 12, 2026, majira ya saa 08:30 asubuhi katika eneo la Msitu wa Mabilioni, wilayani Same, na askari wa uhifadhi wa TANAPA waliokuwa katika doria ya kudhibiti ujangili na makosa mengine ya jinai.

Wakati wa kukamatwa, alikuwa na nyama za wanyamapori wawili aina ya digidigi bila kuwa na kibali cha kufanya shughuli hiyo. Thamani ya wanyama hao ilikadiriwa kuwa dola za Marekani 600, sawa na shilingi za Tanzania 1,574,100.

Baada ya kukamilika kwa uchunguzi, mshtakiwa alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Same Julai 17, 2026, na kusomewa shtaka la kupatikana na nyara za Serikali.

Baada ya shauri kusikilizwa, Mahakama ilimkuta na hatia na kutoa adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela pamoja na kutaifisha pikipiki moja na kuikabidhi kwa Serikali.

Hukumu hiyo inaendelea kuonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya vyombo vya ulinzi na uhifadhi katika kupambana na ujangili na kulinda rasilimali za wanyamapori nchini.

Watakiwa kujitokeza kujadili miradi ya maendeleo – HabariLeo

MBEYA; Wafanyabiashara na wawekezaji jijini Mbeya wametakiwa kujitokeza katika vikao vya majadiliano ya miradi ya maendeleo wanapoalikwa na serikali ili kupata taarifa za fursa za uwekezaji na kujiandaa kushiriki katika utekelezaji wake,badala ya kusubiri miradi itangazwe ndipo waanze kuzitafuta fursa hizo.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Jiji la Mbeya, Festo Nashon, wakati wa kikao cha majadiliano na wawekezaji pamoja na taasisi za kifedha kuhusu taarifa za upembuzi wa awali wa mradi wa ujenzi wa stendi mpya ya Uyole, unaotarajiwa kutekelezwa kwa ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Nashon amesema ushiriki wa wawekezaji wazawa una umuhimu mkubwa kwa sababu wanafahamu mazingira ya biashara na uwekezaji katika maeneo yao hivyo wana nafasi nzuri ya kutambua fursa na changamoto zilizopo katika maeneo wanayokusudia kuwekeza.

Mkuu wa Idara ya Maandalizi na Uendelezaji wa Miradi kutoka Kituo cha Ubia (PPP) Innocent Mauki, amesema taasisi hiyo inaendelea kufanya ziara katika halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya kujadiliana na wadau kuhusu miradi inayotarajiwa kutekelezwa kwa ushirikiano na sekta binafsi.

“Ziara hii imelenga kupata maoni ya wawekezaji na wadau kuhusu mambo yanayopaswa kuzingatiwa na kuboreshwa katika maandiko ya miradi hiyo ili yaendane na mazingira ya uwekezaji pamoja na mahitaji halisi ya wananchi wa Mbeya,”amesema Mauki

Amesema Halmashauri ya Jiji la Mbeya ina miradi miwili inayotarajiwa kutekelezwa kwa mfumo wa ubia na sekta binafsi ukiwemo wa ujenzi wa Stendi mpya ya Uyole huku akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha miradi hiyo inakuwa na tija kwa wananchi , huku ikiwezekana pia kupata ufadhili au mikopo kutoka taasisi za kifedha.

Amesema ushiriki wa sekta binafsi katika miradi ya maendeleo ni nguzo muhimu ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, inayolenga kuifanya sekta binafsi kuwa mshiriki mkuu katika kukuza uchumi wa Tanzania kwa asilimia 70.

Mwakilishi wa wawekezaji, Mkuu wa Masoko wa Kampuni ya Maranatha, Shitindi Venance, amewahimiza Watanzania kutumia fursa zilizopo katika kipindi hiki akisema fursa hizo zinaweza kupungua kadiri muda unavyokwenda huku akiwahimiza vijana kuchangamkia fursa ya kubuni mifumo ya kidigitali katika itakayosaidia uendeshaji miradi hiyo.

Chadema Yatangaza Muda wa Hukumu ya Tundu Lissu Mahakama Kuu Dar Kesho

Global Publishers
November 5, 2026
96 views
0 Comments

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kuwa hukumu ya kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Antipas Lissu, inatarajiwa kutolewa kesho, Ijumaa, Novemba 6, 2026, saa 3:00 asubuhi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama hicho leo, Novemba 5, 2026, hukumu hiyo itatolewa mbele ya jopo la majaji watatu ambao ni Jaji Dunstan Ndunguru, Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde.

Kupitia taarifa hiyo, CHADEMA kimewataka viongozi, wanachama, wafuasi, asasi za kiraia, watetezi wa haki za binadamu na demokrasia pamoja na Watanzania wote kujitokeza kwa wingi mahakamani kufuatilia mwenendo wa utoaji wa hukumu hiyo.

Chama hicho kimesisitiza umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika misingi ya haki, utawala wa sheria na demokrasia nchini.

Taarifa hiyo imetolewa na Brenda Rupia, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Novemba 5, 2026.

Chadema Yatangaza Muda wa Hukumu ya Lissu Mahakama Kuu Dar Kesho

Global Publishers
November 5, 2026
0 views
0 Comments

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kuwa hukumu ya kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Antipas Lissu, inatarajiwa kutolewa kesho, Ijumaa, Novemba 6, 2026, saa 3:00 asubuhi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama hicho leo, Novemba 5, 2026, hukumu hiyo itatolewa mbele ya jopo la majaji watatu ambao ni Jaji Dunstan Ndunguru, Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde.

Kupitia taarifa hiyo, CHADEMA kimewataka viongozi, wanachama, wafuasi, asasi za kiraia, watetezi wa haki za binadamu na demokrasia pamoja na Watanzania wote kujitokeza kwa wingi mahakamani kufuatilia mwenendo wa utoaji wa hukumu hiyo.

Chama hicho kimesisitiza umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika misingi ya haki, utawala wa sheria na demokrasia nchini.

Taarifa hiyo imetolewa na Brenda Rupia, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Novemba 5, 2026.