Chadema Yatangaza Muda wa Hukumu ya Lissu Mahakama Kuu Dar Kesho

Global Publishers
November 5, 2026
0 views
0 Comments

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kuwa hukumu ya kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Antipas Lissu, inatarajiwa kutolewa kesho, Ijumaa, Novemba 6, 2026, saa 3:00 asubuhi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama hicho leo, Novemba 5, 2026, hukumu hiyo itatolewa mbele ya jopo la majaji watatu ambao ni Jaji Dunstan Ndunguru, Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde.

Kupitia taarifa hiyo, CHADEMA kimewataka viongozi, wanachama, wafuasi, asasi za kiraia, watetezi wa haki za binadamu na demokrasia pamoja na Watanzania wote kujitokeza kwa wingi mahakamani kufuatilia mwenendo wa utoaji wa hukumu hiyo.

Chama hicho kimesisitiza umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika misingi ya haki, utawala wa sheria na demokrasia nchini.

Taarifa hiyo imetolewa na Brenda Rupia, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Novemba 5, 2026.

Ndejembi Akutana na Museveni, Maendeleo ya Bomba la Mafuta EACOP Yajadiliwa

Global Publishers
November 5, 2026
78 views
0 Comments

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), linalounganisha Hoima nchini Uganda na Chongoleani mkoani Tanga, Tanzania.

Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ikulu ya Entebbe nchini Uganda, ambapo Ndejembi amemwakilisha Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mkutano huo umelenga kuimarisha ushirikiano wa mataifa hayo mawili katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, hususan katika sekta ya mafuta na gesi, kupitia mradi wa EACOP unaotarajiwa kuwa sehemu muhimu ya usafirishaji wa mafuta ghafi kutoka Uganda kwenda katika soko la kimataifa kupitia bandari ya Tanga.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamejadili maendeleo ya mradi huo pamoja na umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda katika sekta ya nishati.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe; Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Meja Jenerali Marco Gaguti; Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia mafuta na gesi, Dkt. James Mataragio; Kamishna wa Mafuta na Gesi, Goodluck Shirima, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mussa Makame.

Simba Yatawala Tuzo za Oktoba, Barker na Mpanzu Waibuka Kinara

Kiungo mshambuliaji wa Simba, Elie Mpanzu, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Oktoba katika Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/2027, huku kocha wa timu hiyo, Steven Barker, akitwaa tuzo ya Kocha Bora wa mwezi huo.

Mpanzu amefanikiwa kutwaa tuzo hiyo baada ya kuonyesha kiwango bora cha mchezo, aki washinda Iddi Selemani wa Azam FC na Nathaniel Chilambo wa Simba SC, ambao pia waliingia fainali ya tuzo hiyo.

Katika michezo mitatu iliyochezwa mwezi Oktoba, Mpanzu alifunga mabao matatu na kuisaidia Simba SC kupata matokeo mazuri kwenye ligi.

Kwa upande wa tuzo ya Kocha Bora, Steven Barker aliwashinda Florent Ibenge wa Azam FC na Juma Mgunda wa Namungo FC, baada ya kuiongoza Simba SC kushinda michezo yote mitatu iliyocheza mwezi huo na kupanda kutoka nafasi ya pili hadi ya kwanza katika msimamo wa ligi.

Kamati ya Tuzo pia imetangaza mabao matatu bora ya mwezi Oktoba, ambayo yatapigiwa kura na mashabiki ili kumpata mshindi. Mabao hayo yamefungwa na Hassan Mubiru wa Azam FC dhidi ya Mbeya City, Elie Mpanzu wa Simba SC dhidi ya Young Africans na Selemani Bwenzi wa Simba SC dhidi ya Mashujaa FC.

Aidha, Jackson Mwendwa wa Tanzania Prisons ametangazwa kuwa Meneja Bora wa Uwanja wa mwezi Oktoba, kutokana na usimamizi mzuri wa maandalizi ya uwanja na masuala yanayohusu miundombinu ya michezo.

Katika Ligi ya Championship ya NBC, Ramadhan Kalanje wa KMC amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Oktoba baada ya kuwashinda Abdulkariim Segeja wa Kigamboni na Hamdan Ally wa Transit Camp.

Kwa upande wa tuzo ya Kocha Bora wa mwezi Oktoba katika Championship, Awadh Juma wa Mtibwa Sugar ndiye aliyeibuka mshindi, akiwashinda Habibu Kondo wa Bandari na Mohamed Muya wa KMC.

Taarifa hiyo imetolewa Novemba 5, 2026 na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).

Fahamu Marais 3 Tu Kati ya 47 Walioshinda Uchaguzi Midterm Marekani

Katika historia ya siasa za Marekani, uchaguzi wa Midterm umekuwa moja ya mitihani mikubwa kwa marais walioko madarakani. Uchaguzi huu hufanyika kila baada ya miaka miwili, katikati ya muhula wa Rais wa miaka minne.

Kwa kawaida, uchaguzi huu huwa mtihani wa kisiasa kwa chama kinachomiliki Ikulu ya White House. Wananchi hupata nafasi ya kuonyesha kuridhika au kutoridhika kwao na uongozi wa Rais kwa kuchagua upya wajumbe wa Congress.

Marekani imekuwa na marais 47 tangu kuanzishwa kwa urais mwaka 1789.

Historia inaonyesha kuwa chama cha Rais mara nyingi hupoteza viti katika uchaguzi huu. Hata hivyo, si kila Rais amepata matokeo hayo.

Fahamu marais watatu walioshinda uchaguzi wa uchaguzi wa Midterm Elections walipokuwa madarakani katika historia ya Marekani

1. Franklin D. Roosevelt (1934)
Mwaka 1934, Rais Franklin D. Roosevelt aliingia katika historia baada ya chama chake cha Democratic kuongeza viti katika uchaguzi wa Midterm. Wakati huo Marekani ilikuwa inapambana na athari za mdororo mkubwa wa kiuchumi uliojulikana kama Great Depression.

Licha ya changamoto za kiuchumi, chama cha Roosevelt kiliendelea kupata uungwaji mkono wa kisiasa na kuongeza uwakilishi wake katika Congress.

2. Bill Clinton (1998)
Mwaka 1998, Rais Bill Clinton naye aliandika historia. Wakati ambapo chama chake cha Democratic kilitarajiwa kukabiliwa na changamoto katika uchaguzi wa katikati ya muhula, badala yake kiliongeza viti vinne katika House of Representatives.

Hii ilikuwa moja ya mifano adimu ambapo chama cha Rais kilipata ongezeko la viti katika House wakati wa Midterm Elections.

3. George W. Bush (2002)
Mwaka 2002, Rais George W. Bush alikuwa miongoni mwa marais wachache walioweza kuona chama chao kikiongeza nguvu katika Congress kupitia Midterm Elections.

Chama cha Republican kiliongeza viti nane katika House of Representatives na viti viwili katika Senate.

Uchaguzi huo ulifanyika mwaka mmoja baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001, ambayo yalibadilisha kwa kiasi kikubwa mazingira ya kisiasa na usalama nchini Marekani.

Kwa nini ushindi huu ni wa kipekee?
Katika mfumo wa Marekani, uchaguzi wa Midterm huwa na umuhimu mkubwa kwa sababu unaweza kubadilisha uwiano wa nguvu kati ya Rais na Congress.

Rais ambaye chama chake kinapoteza udhibiti wa House au Senate anaweza kukabiliwa na changamoto kubwa katika kupitisha miswada, bajeti na ajenda zake za kisiasa.

Kwa upande mwingine, chama kinachoongeza viti kinaweza kuimarisha nafasi yake katika kufanya maamuzi ya kitaifa.

Marais ambao vyama vyao vilipata mafanikio

Rais

Mwaka

Matokeo

Franklin D. Roosevelt

1934

Democrats waliongeza viti 9 House na 9 Senate

John F. Kennedy

1962

Democrats waliongeza viti Senate

Bill Clinton

1998

Democrats waliongeza viti 4 House

George W. Bush

2002

Republicans waliongeza viti 8 House na 2 Senate

Historia ya Midterm Elections: Fahamu Marais 3 Tu Walioshinda Uchaguzi Marekani

Katika historia ya siasa za Marekani, uchaguzi wa Midterm Elections umekuwa moja ya mitihani mikubwa kwa marais walioko madarakani. Uchaguzi huu hufanyika kila baada ya miaka miwili, katikati ya muhula wa Rais wa miaka minne.

Kwa kawaida, uchaguzi huu huwa mtihani wa kisiasa kwa chama kinachomiliki Ikulu ya White House. Wananchi hupata nafasi ya kuonyesha kuridhika au kutoridhika kwao na uongozi wa Rais kwa kuchagua upya wajumbe wa Congress.

Marekani imekuwa na marais 47 tangu kuanzishwa kwa urais mwaka 1789.

Historia inaonyesha kuwa chama cha Rais mara nyingi hupoteza viti katika uchaguzi huu. Hata hivyo, si kila Rais amepata matokeo hayo.

Fahamu marais watatu walioshinda uchaguzi wa uchaguzi wa Midterm Elections walipokuwa madarakani katika historia ya Marekani

1. Franklin D. Roosevelt (1934)
Mwaka 1934, Rais Franklin D. Roosevelt aliingia katika historia baada ya chama chake cha Democratic kuongeza viti katika uchaguzi wa Midterm. Wakati huo Marekani ilikuwa inapambana na athari za mdororo mkubwa wa kiuchumi uliojulikana kama Great Depression.

Licha ya changamoto za kiuchumi, chama cha Roosevelt kiliendelea kupata uungwaji mkono wa kisiasa na kuongeza uwakilishi wake katika Congress.

2. Bill Clinton (1998)
Mwaka 1998, Rais Bill Clinton naye aliandika historia. Wakati ambapo chama chake cha Democratic kilitarajiwa kukabiliwa na changamoto katika uchaguzi wa katikati ya muhula, badala yake kiliongeza viti vinne katika House of Representatives.

Hii ilikuwa moja ya mifano adimu ambapo chama cha Rais kilipata ongezeko la viti katika House wakati wa Midterm Elections.

3. George W. Bush (2002)
Mwaka 2002, Rais George W. Bush alikuwa miongoni mwa marais wachache walioweza kuona chama chao kikiongeza nguvu katika Congress kupitia Midterm Elections.

Chama cha Republican kiliongeza viti nane katika House of Representatives na viti viwili katika Senate.

Uchaguzi huo ulifanyika mwaka mmoja baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001, ambayo yalibadilisha kwa kiasi kikubwa mazingira ya kisiasa na usalama nchini Marekani.

Kwa nini ushindi huu ni wa kipekee?
Katika mfumo wa Marekani, uchaguzi wa Midterm huwa na umuhimu mkubwa kwa sababu unaweza kubadilisha uwiano wa nguvu kati ya Rais na Congress.

Rais ambaye chama chake kinapoteza udhibiti wa House au Senate anaweza kukabiliwa na changamoto kubwa katika kupitisha miswada, bajeti na ajenda zake za kisiasa.

Kwa upande mwingine, chama kinachoongeza viti kinaweza kuimarisha nafasi yake katika kufanya maamuzi ya kitaifa.

Marais ambao vyama vyao vilipata mafanikio

Rais

Mwaka

Matokeo

Franklin D. Roosevelt

1934

Democrats waliongeza viti 9 House na 9 Senate

John F. Kennedy

1962

Democrats waliongeza viti Senate

Bill Clinton

1998

Democrats waliongeza viti 4 House

George W. Bush

2002

Republicans waliongeza viti 8 House na 2 Senate

PSSSF YAKABIDHI MIRADI YA MAJI SHULE MBILI DODOMA

*Miradi Kunifaisha zaidi ya Watu 1000

*Wanafunzi Waanzisha Bustani Kuboresha Lishe

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umekabidhi miradi miwili ya visima vya maji vyenye thamani ya Shilingi milioni 55 katika Shule ya Sekondari Kimaghai, Mpwapwa, na Shule ya Msingi Uhuru, jijini Dodoma, inayotarajiwa kunufaisha zaidi ya watu 1,000.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mradi wa Kimaghai A, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Bw. Ally Akida, aliishukuru PSSSF kwa kutatua changamoto ya muda mrefu ya maji, akieleza kuwa mradi huo utanufaisha zaidi ya watu 600.

Naye Kaimu Afisa Elimu wa Jiji la Dodoma, Bw. Yasin Mponda, aliipongeza PSSSF kwa kukubali  ombi la Shule ya Msingi Uhuru, akieleza kuwa Mfuko umeifanya shule hiyo kujiona inathaminiwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru, Bi. Agatha Mosha, aliishukuru PSSSF kwa mradi huo ambao umewezesha kuanzishwa kwa kilimo cha mbogamboga kwa ajili ya kuboresha lishe ya wanafunzi na unatarajiwa kunufaisha zaidi ya watu 500.

Makabidhiano ya miradi hiyo yalifanyika tarehe 3 na 4 Novemba 2026, yakiongozwa na Meneja wa PSSSF Kanda ya Kati, Bw. Lulyaya Sayi, aliyewataka wanafunzi, walimu na wananchi kutunza visima na miundombinu yake ili iendelee kutoa huduma kwa muda mrefu.

MWISHO.

Yaya Touré Akabiliwa na Presha Baada ya Slovan Kupoteza Mechi 14 Mfululizo

BRATISLAVA, Slovakia – Klabu ya Slovan Bratislava inayofundishwa na nyota wa zamani wa Ivory Coast, Yaya Touré, imeweka rekodi isiyopendeza katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League) baada ya kupoteza mechi 14 mfululizo katika hatua kuu ya mashindano hayo.

Slovan Bratislava iliweka rekodi hiyo Jumanne baada ya kuchapwa mabao 4-0 na LASK ya Austria, ikiwa ni kipigo cha 14 mfululizo tangu kuanza kwa rekodi za hatua kuu ya mashindano hayo mwaka 1992.

Matokeo hayo yameifanya Slovan kuvunja rekodi ya awali iliyokuwa ikishikiliwa na Marseille ya Ufaransa, iliyopoteza mechi 13 mfululizo kati ya Machi 2012 na Novemba 2020.

Hata hivyo, rekodi ya muda wote ya kushindwa mechi nyingi mfululizo katika historia ya mashindano ya vilabu bingwa Ulaya bado inashikiliwa na Jeunesse Esch ya Luxembourg, iliyopoteza mechi 16 mfululizo katika mfumo wa zamani wa European Cup.

Akizungumza baada ya kipigo dhidi ya LASK, Touré, ambaye alitwaa ubingwa wa Champions League akiwa na Barcelona mwaka 2009, alikiri kuwa hali hiyo ni ngumu kwa kikosi chake.

Alisema wapinzani wao walikuwa na nguvu na uchu mkubwa zaidi wa ushindi, huku akitambua kuwa timu yake ilihitaji kupambana zaidi.

Mfululizo wa matokeo mabaya ya Slovan ulianza Oktoba 1992 ilipopoteza mechi mbili dhidi ya AC Milan katika raundi ya pili ya mashindano hayo.

Katika mwaka 2024, timu hiyo ilipoteza mechi nane katika mfumo mpya wa ligi ya Champions League, kabla ya kuongeza vipigo vingine vinne msimu huu.

Slovan bado ina michezo miwili muhimu nyumbani dhidi ya Real Betis na Shakhtar Donetsk, ambayo itakuwa na umuhimu mkubwa katika kujaribu kuzuia kufikia rekodi ya Jeunesse Esch ya vipigo 16 mfululizo.

Mbali na changamoto za Champions League, Slovan pia inakabiliwa na hatari ya kushindwa kufuzu hatua za mchujo za mashindano hayo msimu ujao, jambo ambalo halijatokea kwa klabu hiyo katika misimu tisa iliyopita.

Kwa sasa, timu ya Touré inazidiwa kwa pointi nane na vinara wa ligi ya Slovakia, FC DAC, ambao bado hawajapoteza mchezo.

Touré ameeleza kuwa ratiba ngumu ya michezo, ambapo timu yake hulazimika kucheza kila baada ya siku mbili au tatu katika mashindano mbalimbali, imechangia uchovu kwa wachezaji.

Hata hivyo, kocha huyo amesema bado msimu ni mrefu na kikosi chake kitaendelea kupambana licha ya changamoto zinazowakabili.

BoT YAWANOA WANAHABARI KUCHAMBUA MASUALA YA UCHUMI NA FEDHA

Matukio Daima Media 

NAIBU Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Rahma Salim Mahfoudh, amesema benki hiyo imeongeza nguvu katika kuimarisha uandishi wa habari za uchumi na fedha nchini kwa kuwajengea waandishi wa habari uwezo wa kuchambua sera, takwimu na mifumo ya kifedha ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na zenye manufaa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina  kwa wahariri na waandishi wa habari za uchumi na fedha , Dk Mahfoudh alisema uelewa wa kina wa masuala ya uchumi na fedha ni msingi muhimu katika kuboresha ubora wa taarifa zinazotolewa kwa umma.

Alisema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha waandishi kuelewa majukumu ya Benki Kuu, utekelezaji wa sera ya fedha, mifumo ya malipo pamoja na maendeleo mapya katika sekta ya fedha.

Alibainisha kuwa taarifa sahihi za uchumi na fedha zina nafasi kubwa katika kuwasaidia wananchi kuelewa hali halisi ya uchumi, kutambua fursa zilizopo na kufanya maamuzi yenye tija katika maisha yao.

Aidha, alisema BoT imekuwa ikiandaa semina hizo katika ngazi ya kitaifa na kanda kwa lengo la kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari za uchumi na fedha, kuongeza usahihi wa taarifa na kuwajengea waandishi uwezo wa kuchambua takwimu, ripoti na taarifa zinazotolewa na benki hiyo kila wiki, robo mwaka na mwaka.

Dk  Mahfoudh, ambaye anasimamia masuala ya Utawala na Udhibiti wa Ndani katika BoT, alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Benki Kuu na vyombo vya habari ni muhimu katika kuhakikisha jamii inapata elimu sahihi kuhusu uchumi na kuelewa mabadiliko yanayotokea katika sekta ya fedha.

Kwa upande wake, Meneja wa Idara ya Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa BoT, Vicky Msina, alisema taasisi hiyo inatambua umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na waandishi wa habari ili kuhakikisha taarifa kuhusu shughuli na majukumu yake zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa usahihi.

Alisema ushirikiano huo ni sehemu muhimu ya kuimarisha uelewa wa umma kuhusu masuala ya uchumi na huduma zinazotolewa na Benki Kuu.

Katika mafunzo hayo, washiriki pia wanapatiwa elimu kuhusu utekelezaji wa sera ya fedha, viwango vya riba, dhamana za Serikali na mchango wake katika kukuza na kuimarisha masoko ya fedha.

Akiwasilisha mada kuhusu utekelezaji wa sera ya fedha kwa kutumia kiwango cha riba cha Benki Kuu, Meneja Msaidizi wa Idara ya Sera ya Fedha ya BoT, John Mero, alisema kiwango cha riba katika soko la mikopo ya siku saba baina ya benki (Seven-Day Interbank Rate) ni kiungo muhimu katika kusambaza athari za mabadiliko ya Kiwango cha Riba cha Benki Kuu (CBR) kwa taasisi za fedha.

Alifafanua kuwa CBR hutumika kama kiashiria kikuu cha mwelekeo wa sera ya fedha, huku kiwango cha riba cha siku saba katika soko la mikopo baina ya benki kikionesha namna maamuzi ya Benki Kuu yanavyoathiri viwango vya riba za muda mfupi.

Aidha, alisema soko hilo huwezesha benki za biashara kukopeshana fedha ili kukidhi mahitaji ya ukwasi wa muda mfupi. Hivyo, mabadiliko ya viwango vya riba katika soko hilo huonesha hali ya upatikanaji wa ukwasi ndani ya mfumo wa benki.

Kupitia mafunzo hayo, BoT inalenga kuongeza uelewa na weledi wa wanahabari katika kuripoti na kuchambua masuala ya uchumi na fedha, hatua inayotarajiwa kuimarisha upatikanaji wa taarifa sahihi na zenye tija kwa wananchi.

Kwa miaka 15 sasa BoT imekuwa ikitoa mafunzo kwa waandishi wa habari nchini katika kanda mbalimbali juu ya masuala ya uchumi na fedha.

….

Nandy vs Zuchu: Fahamu Ukweli wa Mafanikio Unaofichwa na Followers na Views – Video


Katika eneo hilo, Nandy, anayefahamika pia kama The African Princess, ana safari inayostahili kuangaliwa kwa jicho tofauti.

Kwa zaidi ya miaka 10 tangu aanze kujijengea jina katika muziki, Nandy ameendelea kupanua wigo wa shughuli zake kutoka kuwa mwimbaji hadi kuwa mjasiriamali, mmiliki wa lebo na mwandaaji wa matamasha.

Hata hivyo, hilo halimaanishi kuwa Zuchu hana mafanikio yake. Msanii huyo naye amejijengea jina kubwa ndani na nje ya Tanzania, akitumia muziki na ushirikiano wa kibiashara kujenga chapa yake.

SAFARI ZAO ILIVYOANZA

Nandy na Zuchu wana historia inayogusana tangu waliposhiriki mashindano ya TECNO Own The Stage mwaka 2015 nchini Nigeria.

Nandy alifanikiwa kushika nafasi ya pili katika mashindano hayo, hatua iliyomfungulia milango ya kujenga jina lake katika muziki wa Afrika Mashariki. Mwaka 2016 aliingia rasmi kwenye soko la muziki kupitia wimbo wake Nagusagusa.

Msanii wa label ya WCB, Zuhura Othman almaarufu Zuchu.

Kwa upande wa Zuchu, jina lake lilipata umaarufu mkubwa zaidi mwaka 2020 baada ya kusainiwa na lebo ya WCB Wasafi inayomilikiwa na Diamond Platnumz.

Alitambulishwa rasmi sokoni kupitia EP yake ya I Am Zuchu, iliyokuwa mwanzo wa safari yake kubwa katika muziki.

Tofauti ya mazingira hayo ya kazi imekuwa sehemu muhimu ya mjadala kuhusu safari zao, hasa katika suala la umiliki na uendeshaji wa biashara ya muziki.

NANDY NA UMILIKI WA LEBO YAKE

Moja ya hatua kubwa katika safari ya Nandy ni kuanzisha lebo yake ya muziki, The African Princess Label, mwaka 2023.

Kupitia lebo hiyo, Nandy alijitanua kutoka kuwa msanii anayefanya muziki wake pekee hadi kuwa mtu anayeshiriki katika kukuza na kusimamia vipaji vya wasanii wengine.

Miongoni mwa wasanii walioingia kwenye mfumo huo ni Yammi, ambaye alianza safari yake kupitia EP ya Three Hearts.

Hatua hii inampa Nandy nafasi mbili ndani ya tasnia kuwa msanii anayezalisha kazi zake na wakati huohuo kuwa mmiliki wa biashara inayoweza kuwekeza katika vipaji vingine.

Kwa upande wa Zuchu, yeye ni msanii aliyesainiwa chini ya WCB Wasafi. Hivyo, tofauti inayoweza kuonekana hapa ni kwamba Nandy ameanzisha na kuendesha lebo yake, wakati Zuchu anafanya kazi ndani ya mfumo wa lebo ambayo hamiliki.

MITANDAO YA KIJAMII: NANDY ANAONGOZA INSTAGRAM, ZUCHU TIKTOK NA YOUTUBE

Katika zama ambazo mitandao ya kijamii imekuwa sehemu muhimu ya biashara ya muziki, idadi ya wafuasi inaweza kuonyesha ukubwa wa ushawishi wa msanii katika jukwaa husika.

Nandy amefikisha wafuasi milioni 10.7 Instagram, huku Zuchu akiwa na milioni 7.6.

Hata hivyo, hali ni tofauti katika majukwaa mengine.

Zuchu anaongoza TikTok akiwa na takribani wafuasi milioni saba, dhidi ya milioni 2.7 wa Nandy.

Katika YouTube, Zuchu naye anaongoza kwa kuwa na subscribers takribani milioni tano, wakati Nandy akiwa na milioni 1.9.

Takwimu hizi zinaonyesha kuwa kila msanii ana eneo ambalo amejijengea nguvu zaidi. Nandy ana ushawishi mkubwa Instagram, huku Zuchu akiwa na  ushawishi mkubwa zaidi TikTok na YouTube.

ALBAMU NA KAZI ZILIZOJENGA MAJINA YAO

Nandy amekuwa na safari ndefu katika utoaji wa kazi za muziki. Mwaka 2018 alitoa albamu yake ya The African Princess, iliyosaidia kuimarisha utambulisho wake katika soko la muziki.

Baadaye aliendelea kutoa EP mbalimbali zikiwemo Taste, Maturity na Wanibariki, huku akiendelea kujenga lebo yake kupitia jina la The African Princess.

Kwa upande wa Zuchu, EP yake ya I Am Zuchu ya mwaka 2020 ilikuwa hatua muhimu katika kumtambulisha rasmi kwa mashabiki. Kupitia kazi hiyo na nyimbo zilizofuata, aliweza kujenga nafasi yake katika muziki wa Tanzania na Afrika Mashariki.

YOUTUBE: ZUCHU ANA NGUVU KUBWA YA WATAZAMAJI
Licha ya Nandy kuwa na mafanikio katika umiliki wa lebo na biashara, Zuchu ana takwimu kubwa zaidi katika upande wa watazamaji wa YouTube.

Kwa mujibu wa takwimu zilizoripotiwa Novemba 2025, Zuchu alikuwa amefikisha zaidi ya watazamaji bilioni moja katika video zake, wakati Nandy akiwa na zaidi ya milioni 306.

Takwimu zilizotajwa za Novemba 2026 zinaonyesha Zuchu akiwa amefikisha zaidi ya watazamaji bilioni 1.3 kwenye chaneli yake, huku Nandy akiwa na zaidi ya milioni 375.

Hizi ni takwimu zinazoonyesha ukubwa wa matumizi ya kazi za Zuchu kwenye jukwaa hilo la kidijitali.

Hivyo, mafanikio ya Zuchu kwenye YouTube ni sehemu muhimu ya mjadala huu na hayawezi kupuuzwa.

MAISHA YA NANDY NJE YA MUZIKI
Moja ya mambo yanayovutia katika safari ya Nandy ni namna ambavyo amejaribu kupanua shughuli zake nje ya muziki.

Mbali na The African Princess Label, amekuwa akihusishwa na biashara ya vipodozi kupitia chapa ya Shushi Products.

Pia amehusishwa na biashara ya malazi kupitia NayVilla, inayotangaza huduma za nyumba za kifahari za kupangisha kwa muda mfupi.

Nandy pia ameendesha tamasha lake la Nandy Festival, ambalo limekuwa jukwaa la kukutanisha wasanii, burudani na kukuza vipaji mbalimbali.

Kwa hatua hiyo, ameongeza nafasi yake ndani ya tasnia kutoka kuwa mtu anayehusika na utengenezaji wa muziki hadi kuwa sehemu ya uandaaji wa majukwaa ya burudani.

MAGARI NA MALI ZA NANDY
Katika upande wa mali binafsi, Nandy amewahi kuhusishwa na umiliki wa magari mbalimbali ya kifahari.

Taarifa zilizochapishwa na Global Publishers mwaka 2019 na 2021 zilimtaja kuwa na magari yakiwemo, Range Rover Evoque, Land Rover Discovery, BMW X1, Mercedes-Benz E-Class, Toyota Alphard, Toyota Harrier na Toyota Noah na kwa sasa anamiliki Mercedes-Benz AMG G63 (G-Wagon) Linatajwa kuwa na thamani kuanzia Milioni 600 hadi Milioni 800 za Kitanzania (TSh 600M – 800M+).

Hata hivyo, taarifa hizo ni za miaka iliyopita na hazithibitishi kuwa magari yote hayo bado yako chini ya umiliki wake.

Pia Nandy aliwahi kuripotiwa kuwazawadia wazazi wake nyumba, hatua iliyotajwa kuwa sehemu ya mafanikio yake na namna alivyotumia matunda ya kazi yake kuwasaidia watu wa karibu.

Ni muhimu kutofautisha taarifa za mali zilizowahi kuripotiwa na thamani halisi ya utajiri wa mtu, ambayo inahitaji nyaraka na taarifa za kifedha zilizothibitishwa.

MAFANIKIO YA ZUCHU NJE YA MUZIKI

Kwa upande wa Zuchu, mafanikio yake hayaishii kwenye muziki pekee. Tangu alipoingia rasmi kwenye soko mwaka 2020, ameendelea kujijengea thamani kupitia kazi za muziki na mikataba ya kibiashara.

Mwaka 2021 Zuchu alikuwa amekataa mkataba wa matangazo ya pombe uliokuwa na thamani ya Sh milioni 250.

Pia amekuwa akihusishwa na ushirikiano wa kibiashara na makampuni mbalimbali, zikiwemo Darling Hair na Tridea Cosmetics.

Katika upande wa magari, Zuchu aliwahi kujinunulia Range Rover mwaka 2023.

Pia anahusishwa kuendesha au kutumia magari ya kifahari kupitia familia na mpenzi wake Diamond Platnumz, kama vile Range Rover na mara kwa mara kuonekana akitumia au kupanda magari ya kifahari ya WCB kama Cadillac Escalade ya Diamond Platnumz.

Novemba 3,  2026 Zuchu ametangaza kujinunulia gari aina ya Bentley Continental GT V8 Azure (Takribani TSh milioni 148-250 kwa gari ambayo imetumika), akieleza kuwa gari hilo lilikuwa ndoto yake ya muda mrefu na mafanikio yaliyotokana na muziki.

Pia mwaka 2025 alionyesha nyumba ya vyumba vitano aliyomjengea mama yake, Khadija Kopa, ikiwa ni sehemu ya kutimiza ndoto yake ya kumzawadia mzazi wake makazi bora.

Taarifa nyingine za mwaka 2026 zimemhusisha na uwekezaji wa vyumba ya kifahari Zanzibar, ingawa umiliki na thamani ya uwekezaji huo haukuwekwa wazi.

Mafanikio hayo yanaonyesha namna Zuchu anavyotumia muziki kujenga maisha na kupanua vyanzo vya mapato.

Nandy yupo kwenye ndoa na msanii mwenzake, Billnass.

MAISHA YA MAPENZI: NANDY NA BILLNASS, ZUCHU NA DIAMOND
Mbali na mafanikio ya muziki na biashara, maisha yao binafsi pia yamekuwa sehemu ya mijadala ya mashabiki.

Nandy yupo kwenye ndoa na msanii mwenzake, Billnass, ambaye pia ni sehemu ya tasnia ya muziki. Muunganiko wao umekuwa ukivutia kutokana na namna wanavyounganisha maisha ya familia na shughuli zao za kisanii na kibiashara.

Kwa upande wa Zuchu, ameolewa na Diamond Platnumz, ambaye ni mmiliki wa WCB Wasafi, lebo anayoifanyia kazi. Uhusiano wao umekuwa ukivuta hisia za mashabiki na kuendelea kuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii na wamepata mtoto mmoja mwaka huu.

NANDY NA ZUCHU NANI ANAPASWA KUHESHIMIWA ZAIDI?
Kwa kuangalia safari zao, ni wazi kuwa Nandy na Zuchu wana mafanikio katika maeneo tofauti.

Nandy ana historia ndefu zaidi katika muziki, ameanzisha lebo yake, amejihusisha na biashara ya vipodozi na malazi, ameandaa tamasha lake na kuendelea kujenga chapa ya The African Princess.

Kwa upande mwingine, Zuchu ana mafanikio makubwa katika YouTube na TikTok, amejenga ushawishi mkubwa wa kidijitali, amefanya mikataba ya kibiashara na kuonyesha mafanikio yake kupitia ununuzi wa mali mbalimbali.

Hata hivyo, kuna jambo moja ambalo mara nyingi husahaulika katika mijadala ya aina hii si kila msanii ana safari inayofanana na ya mwingine.

Nandy amekuwa akijenga mfumo wake wa biashara na lebo yake, wakati Zuchu amefanya safari yake kubwa ndani ya mfumo wa WCB Wasafi, ambao imekuwa na mchango katika kukuza kazi zake.

Hiyo haimaanishi kuwa mafanikio ya mmoja yanapaswa kupunguza thamani ya mwingine.

Siri ya Mauaji ya Laurent Kabila, Askari wa Miaka 18 Ashangaza Dunia -Video

Tarehe 16 Januari 2001 ilikuwa siku ambayo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ilikumbwa na tukio lililobadilisha historia ya taifa hilo. Rais Laurent-Désiré Kabila alipigwa risasi ndani ya ofisi yake katika Ikulu ya Palais de Marbre, jijini Kinshasa, na mtu aliyekuwa anadaiwa kuwa mmoja wa walinzi wake wa karibu.

Kilichofanya tukio hilo kuwa la kushangaza zaidi ni kwamba mshambuliaji hakuwa mwanajeshi wa taifa adui, wala mpinzani wa kisiasa aliyeingia kwa nguvu ndani ya ikulu. Alikuwa askari aliyekuwa sehemu ya mfumo wa ulinzi wa rais mwenyewe.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa, mshambuliaji huyo alifahamika kwa jina la Rashidi Mizele, pia akitajwa kama Rachidi Kasereka. Tukio hilo limeendelea kuibua maswali kuhusu usalama wa rais, mazingira ya mauaji na watu walioweza kuwa nyuma ya mpango huo.

Siku hiyo, Kabila alikuwa akiendelea na shughuli zake za kawaida katika ofisi yake iliyokuwa Palais de Marbre, eneo la Ma Campagne, katika wilaya ya Ngaliema jijini Kinshasa.

Katika muda wa asubuhi, alikuwa amepokea wageni mbalimbali, wakiwemo wafanyabiashara na wanasiasa.

Ilipofika majira ya saa saba mchana kwa saa za Kinshasa, askari kijana wa kikosi cha ulinzi wa rais aliyejulikana kwa jina la Rachidi alifika katika eneo la ofisi ya rais na kuomba kuingia ili kumsalimia.

Kwa kuwa alikuwa mmoja wa askari waliokuwa sehemu ya ulinzi wa rais, ombi lake halikuonekana kuwa na hatari yoyote. Aliruhusiwa kuingia.

Alipofika ndani, alimkuta Kabila akiwa kwenye mazungumzo na mshauri wake wa masuala ya uchumi, Émile Mota.

Kwa mujibu wa simulizi la Mota, askari huyo alimkaribia rais kwa utulivu kana kwamba alikuwa na jambo la kumwambia. Ghafla, akatoa bastola yake na kumfyatulia risasi Kabila akiwa karibu kabisa naye.

Kwa mujibu wa taarifa za Radio Okapi, Kabila alijeruhiwa katika maeneo ya shingo na sehemu ya chini ya tumbo. Mshambuliaji alijaribu kutoroka, lakini aliuawa na Kanali Eddy Kapend, aliyekuwa msaidizi wa karibu wa rais.

Baada ya tukio hilo, Kabila alikimbizwa katika Hospitali ya Ngaliema jijini Kinshasa kwa ajili ya matibabu.

Habari kuhusu hali yake zilikuwa za kutatanisha. Baadhi ya taarifa zilidai kuwa alikuwa amefariki dunia, huku nyingine zikisema bado alikuwa hai na alikuwa amehamishiwa Zimbabwe kwa matibabu zaidi.

Hali ya sintofahamu iliendelea nchini humo, huku wananchi wakisubiri taarifa rasmi kutoka serikalini.

Hatimaye, Januari 18, 2001, serikali ya Kongo ilitangaza rasmi kifo cha Laurent-Désiré Kabila akiwa nchini Zimbabwe.

Kifo chake kilitikisa taifa hilo na kuibua maswali mengi kuhusu namna ambavyo mtu aliyekuwa sehemu ya ulinzi wa rais aliweza kufanya shambulio hilo ndani ya ofisi ya mkuu wa nchi.

Rashidi alikuwa nani?

Rashidi Mizele, ambaye jina lake pia limeandikwa Rachidi Kasereka katika baadhi ya taarifa, alitajwa kuwa mwanajeshi kijana aliyekuwa sehemu ya walinzi wa rais.

Simulizi mbalimbali zinamhusisha na kundi la wanajeshi vijana waliofahamika kama Kadogo.

Neno Kadogo lilitumika kuelezea watoto na vijana waliokuwa wamejiunga na makundi ya kijeshi wakati wa mapambano yaliyomuwezesha Laurent Kabila kuingia madarakani mwaka 1997 baada ya kuuangusha utawala wa Mobutu Sese Seko.

Kabila alikuwa amepata uungwaji mkono wa vikosi vilivyotoka katika nchi jirani, hasa Rwanda na Uganda, katika mapambano yake ya kumuondoa Mobutu.

Hata hivyo, umri kamili wa Rashidi na maelezo yote kuhusu nafasi yake katika mauaji hayo hayajathibitishwa kwa uhakika na vyanzo vyote vya kihistoria.

Mauaji hayo yalikuwa na watu wengine nyuma yake?

Hili ndilo swali ambalo limeendelea kuisumbua historia ya kisiasa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Baada ya mauaji hayo, serikali ilifanya uchunguzi na kuwafikisha mahakamani watu 135 waliotuhumiwa kuhusika kwa namna mbalimbali na njama za kumuua rais.

Miongoni mwa waliokamatwa alikuwa Kanali Eddy Kapend, ambaye alikuwa amemuua mshambuliaji ndani ya ikulu.

Hata hivyo, miaka mingi baadaye, bado kumekuwa na maswali kuhusu kama watu waliopatikana na hatia walikuwa wahusika halisi wa kupanga mauaji hayo au kama kulikuwa na watu wengine wenye ushawishi waliohusika nyuma ya pazia.

Radio Okapi imeeleza kuwa hadi miaka 24 baada ya tukio hilo, maswali kuhusu waandaaji halisi wa mauaji hayo yalikuwa bado hayajajibiwa kikamilifu.

Joseph Kabila achukua madaraka

Baada ya kifo cha Laurent-Désiré Kabila, mwanawe Joseph Kabila alichukua nafasi ya kuongoza nchi hiyo.

Joseph aliingia madarakani katika kipindi kigumu ambacho Kongo ilikuwa bado inakabiliwa na vita vilivyohusisha makundi ya waasi na majeshi ya nchi jirani.

Alirithi taifa lililokuwa katika mazingira magumu ya kisiasa na kiusalama, huku vita vya pili vya Kongo vikiendelea.

Siri ambayo historia bado inaisubiri

Mauaji ya Laurent-Désiré Kabila yanabaki kuwa moja ya matukio yenye utata mkubwa katika historia ya kisiasa ya Afrika.

Rais aliyekuwa ameiongoza nchi baada ya kuuangusha utawala wa Mobutu aliishia kupoteza maisha ndani ya ofisi yake mwenyewe, katika mazingira ambayo mshambuliaji alitoka ndani ya kikosi kilichokuwa na jukumu la kumlinda.

Na jambo linaloacha maswali mengi zaidi ni hili: Je, Rashidi Mizele alitenda peke yake, au alikuwa sehemu ya mpango mkubwa zaidi wa kumuondoa Laurent Kabila madarakani?

Hilo ndilo fumbo ambalo limeendelea kuandamana na historia ya mauaji ya rais huyo wa zamani wa Kongo.