Matukio Daima Media
NAIBU Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Rahma Salim Mahfoudh, amesema benki hiyo imeongeza nguvu katika kuimarisha uandishi wa habari za uchumi na fedha nchini kwa kuwajengea waandishi wa habari uwezo wa kuchambua sera, takwimu na mifumo ya kifedha ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na zenye manufaa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina kwa wahariri na waandishi wa habari za uchumi na fedha , Dk Mahfoudh alisema uelewa wa kina wa masuala ya uchumi na fedha ni msingi muhimu katika kuboresha ubora wa taarifa zinazotolewa kwa umma.
Alisema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha waandishi kuelewa majukumu ya Benki Kuu, utekelezaji wa sera ya fedha, mifumo ya malipo pamoja na maendeleo mapya katika sekta ya fedha.
Alibainisha kuwa taarifa sahihi za uchumi na fedha zina nafasi kubwa katika kuwasaidia wananchi kuelewa hali halisi ya uchumi, kutambua fursa zilizopo na kufanya maamuzi yenye tija katika maisha yao.
Aidha, alisema BoT imekuwa ikiandaa semina hizo katika ngazi ya kitaifa na kanda kwa lengo la kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari za uchumi na fedha, kuongeza usahihi wa taarifa na kuwajengea waandishi uwezo wa kuchambua takwimu, ripoti na taarifa zinazotolewa na benki hiyo kila wiki, robo mwaka na mwaka.
Dk Mahfoudh, ambaye anasimamia masuala ya Utawala na Udhibiti wa Ndani katika BoT, alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Benki Kuu na vyombo vya habari ni muhimu katika kuhakikisha jamii inapata elimu sahihi kuhusu uchumi na kuelewa mabadiliko yanayotokea katika sekta ya fedha.
Kwa upande wake, Meneja wa Idara ya Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa BoT, Vicky Msina, alisema taasisi hiyo inatambua umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na waandishi wa habari ili kuhakikisha taarifa kuhusu shughuli na majukumu yake zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa usahihi.
Alisema ushirikiano huo ni sehemu muhimu ya kuimarisha uelewa wa umma kuhusu masuala ya uchumi na huduma zinazotolewa na Benki Kuu.
Katika mafunzo hayo, washiriki pia wanapatiwa elimu kuhusu utekelezaji wa sera ya fedha, viwango vya riba, dhamana za Serikali na mchango wake katika kukuza na kuimarisha masoko ya fedha.
Akiwasilisha mada kuhusu utekelezaji wa sera ya fedha kwa kutumia kiwango cha riba cha Benki Kuu, Meneja Msaidizi wa Idara ya Sera ya Fedha ya BoT, John Mero, alisema kiwango cha riba katika soko la mikopo ya siku saba baina ya benki (Seven-Day Interbank Rate) ni kiungo muhimu katika kusambaza athari za mabadiliko ya Kiwango cha Riba cha Benki Kuu (CBR) kwa taasisi za fedha.
Alifafanua kuwa CBR hutumika kama kiashiria kikuu cha mwelekeo wa sera ya fedha, huku kiwango cha riba cha siku saba katika soko la mikopo baina ya benki kikionesha namna maamuzi ya Benki Kuu yanavyoathiri viwango vya riba za muda mfupi.
Aidha, alisema soko hilo huwezesha benki za biashara kukopeshana fedha ili kukidhi mahitaji ya ukwasi wa muda mfupi. Hivyo, mabadiliko ya viwango vya riba katika soko hilo huonesha hali ya upatikanaji wa ukwasi ndani ya mfumo wa benki.
Kupitia mafunzo hayo, BoT inalenga kuongeza uelewa na weledi wa wanahabari katika kuripoti na kuchambua masuala ya uchumi na fedha, hatua inayotarajiwa kuimarisha upatikanaji wa taarifa sahihi na zenye tija kwa wananchi.
Kwa miaka 15 sasa BoT imekuwa ikitoa mafunzo kwa waandishi wa habari nchini katika kanda mbalimbali juu ya masuala ya uchumi na fedha.
….
