SANGU AWAONYA MAWAKALA WA AJIRA NJE YA NCHI

 

Na Matukio DaimaMedia

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amewaonya mawakala binafsi wa ajira wanaotangaza nafasi za kazi nje ya nchi bila kufuata taratibu za Serikali, akisisitiza kuwa matangazo yote ya fursa hizo lazima yapitie Ofisi ya Waziri Mkuu ili kulinda usalama na haki za Watanzania wanaokwenda kufanya kazi ughaibuni.

Akizungumza katika hafla ya kuwaaga Watanzania 985 wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi, Sangu amesema baadhi ya mawakala wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kutangaza nafasi za ajira bila kupata idhini ya Serikali, jambo linaloweza kuhatarisha usalama wa vijana wanaotafuta fursa hizo.

Amesema Serikali imeweka utaratibu wa matangazo ya ajira nje ya nchi kuratibiwa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na mawakala husika, huku akionya kuwa fursa zinazotangazwa nje ya utaratibu huo hazitatambuliwa na mawakala watakaokiuka masharti watachukuliwa hatua.

Aidha, amewataka mawakala kuhakikisha vijana wanapata mafunzo kabla ya kusafiri, yakiwemo elimu kuhusu haki na wajibu wao, mazingira ya kazi na namna bora ya kusimamia fedha wanazozipata ili wanapokuwa nje ya nchi waweze kujilinda na kutumia vizuri kipato chao.

Sangu amesisitiza umuhimu wa mikataba ya ajira kubainisha wazi mishahara, maslahi, haki na wajibu wa mwajiri na mwajiriwa, akionya dhidi ya mawakala wanaowapa vijana mikataba tofauti na masharti wanayokutana nayo wanapofika katika nchi husika.

Ameonya pia dhidi ya tabia ya baadhi ya mawakala kutoza gharama zisizoruhusiwa na Serikali, akieleza kuwa tayari hatua zimechukuliwa kwa baadhi yao, ikiwemo kusitishiwa leseni kutokana na ukiukwaji wa taratibu zilizowekwa.

Akizungumzia mafanikio ya mpango huo, Sangu amesema katika kipindi cha mwaka mmoja vijana 10,471 wameunganishwa na fursa za ajira nje ya nchi, huku Serikali ikiendelea kufanyia kazi nafasi zaidi ya 4,000 zilizopatikana wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba, nchini Qatar.

Amesema Serikali inahitaji ushirikiano wa mawakala binafsi katika kutafuta na kuunganisha vijana na fursa hizo, akisisitiza kuwa ushirikiano huo unapaswa kuzingatia sheria na taratibu ili kuhakikisha ajira zinazopatikana zinakuwa salama na zenye kulinda maslahi ya Watanzania.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdallah Kilima, amewashauri vijana wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi kuwa na nidhamu, kufanya kazi kwa bidii na kuweka akiba kwa ajili ya uwekezaji watakaoufanya watakaporejea nchini.

Kilima amewataka pia kujifunza ujuzi mwingine utakaowaongezea uwezo, kuwa makini wanapotuma fedha kwa watu wengine na kuzingatia sheria za nchi wanazokwenda, akisisitiza kuwa wanapokuwa nje ya nchi wanaiwakilisha Tanzania.

Naye, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Robert Kadege, amewahimiza Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi kujiunga na mifumo ya hifadhi ya jamii ili kujijengea kinga ya kifedha na kuwa na uhakika wa kupata mafao kwa mujibu wa masharti ya mfuko.

Kadege amesema ni muhimu wafanyakazi hao kuendelea kuchangia na kufuatilia haki zao za hifadhi ya jamii hata wanapokuwa nje ya nchi, akieleza kuwa utaratibu huo ni sehemu ya maandalizi ya maisha yao ya baadaye na usalama wao wa kifedha.

Naye, Mwenyekiti wa TRAA, Abdallah Mohamed, amesema ushirikiano kati ya Serikali na mawakala binafsi ni muhimu katika kutafuta fursa za ajira nje ya nchi na kuwaunganisha vijana na waajiri, akieleza kuwa mawakala wana mchango mkubwa katika kufanikisha upatikanaji wa ajira hizo.

Mohamed amesisitiza kuwa mawakala wanapaswa kuendelea kushirikiana na Serikali na kuzingatia taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha vijana wanaopata nafasi za kazi nje ya nchi wanasafiri kwa utaratibu unaotambuliwa na unaolinda haki na maslahi yao.