Benki ya NMB imepata mkopo wa dola za Marekani milioni 30 kutoka Benki ya Maendeleo ya China (CDB) kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa biashara ndogo na za kati nchini Tanzania. Makubaliano hayo yametiwa saini katika Makao Makuu ya NMB jijini Dar es Salaam, yakilenga kuchochea ukuaji wa biashara na kuimarisha ushirikiano wa kifedha kati ya Tanzania na China.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, amesema fedha hizo zitaongeza uwezo wa benki kufadhili wafanyabiashara wanaohitaji mitaji ya kupanua shughuli zao. Amesema upatikanaji wa fedha ni muhimu katika kukuza biashara, kuongeza uzalishaji na kuchochea ajira nchini.
Makubaliano hayo yanafikiwa wakati NMB ikiwa imetambuliwa na jarida la Global Finance kuwa Benki Bora kwa Biashara Ndogo na za Kati Tanzania mwaka 2026. Mkopo huo unatarajiwa kuongeza fursa za mitaji kwa wajasiriamali, kuimarisha biashara kati ya Tanzania na China na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


.jpeg)
.jpeg)