
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Amani Golugwa, amesema uanaharakati si jambo baya, bali ni sehemu muhimu ya kutetea haki, kudai mabadiliko, kuhimiza uwajibikaji na kusukuma mbele maendeleo ya taifa.
Golugwa ameyasema hayo leo Novemba 5, 2026, alipokuwa akizungumza na wananchi kupitia chaneli ya YouTube ya chama hicho, akieleza kuwa Chadema inatambua umuhimu wa uanaharakati katika kuhakikisha mambo muhimu yanayohusu taifa yanatekelezwa kwa wakati.
Amesema uanaharakati una maana ya kutetea maslahi ya jamii, kushawishi mabadiliko na kudai uwajibikaji kutoka kwa viongozi na taasisi mbalimbali, akisisitiza kuwa chama cha siasa kina wajibu wa kusukuma mbele masuala muhimu kwa manufaa ya wananchi.
“Uanaharakati si jambo baya, uanaharakati katika lugha ya kawaida maana yake ni kutetea, kudai, kushawishi mabadiliko, kuleta uwajibikaji na kutaka kusukuma mambo yaende kwa haraka,” amesema Golugwa.
Amefafanua kuwa msimamo huo pia umeainishwa katika Katiba ya CHADEMA, ambayo inatambua ushupavu na uanaharakati wa kweli katika kutetea maslahi ya chama na jamii kwa ujumla, kwa kuzingatia madhumuni, itikadi na falsafa ya chama hicho.
Aidha, Golugwa amesema kuwa kuwa mwanaharakati ndani ya Chadema si jambo la hiari pekee, bali ni takwa la kimaadili ambalo kila mwanachama anapaswa kuwa nalo ili kutekeleza wajibu wake wa kutetea maslahi ya chama na wananchi.
Amesisitiza kuwa uanaharakati haupaswi kutazamwa kama jambo hasi, kwani ni nyenzo muhimu katika kudai mabadiliko, kuhimiza uwajibikaji na kuhakikisha masuala yanayogusa maisha ya wananchi yanapewa kipaumbele.
