Ndejembi Akutana na Museveni, Maendeleo ya Bomba la Mafuta EACOP Yajadiliwa

Global Publishers
November 5, 2026
78 views
0 Comments

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), linalounganisha Hoima nchini Uganda na Chongoleani mkoani Tanga, Tanzania.

Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ikulu ya Entebbe nchini Uganda, ambapo Ndejembi amemwakilisha Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mkutano huo umelenga kuimarisha ushirikiano wa mataifa hayo mawili katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, hususan katika sekta ya mafuta na gesi, kupitia mradi wa EACOP unaotarajiwa kuwa sehemu muhimu ya usafirishaji wa mafuta ghafi kutoka Uganda kwenda katika soko la kimataifa kupitia bandari ya Tanga.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamejadili maendeleo ya mradi huo pamoja na umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda katika sekta ya nishati.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe; Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Meja Jenerali Marco Gaguti; Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia mafuta na gesi, Dkt. James Mataragio; Kamishna wa Mafuta na Gesi, Goodluck Shirima, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mussa Makame.