Chadema Yatangaza Muda wa Hukumu ya Tundu Lissu Mahakama Kuu Dar Kesho

Global Publishers
November 5, 2026
96 views
0 Comments

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kuwa hukumu ya kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Antipas Lissu, inatarajiwa kutolewa kesho, Ijumaa, Novemba 6, 2026, saa 3:00 asubuhi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama hicho leo, Novemba 5, 2026, hukumu hiyo itatolewa mbele ya jopo la majaji watatu ambao ni Jaji Dunstan Ndunguru, Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde.

Kupitia taarifa hiyo, CHADEMA kimewataka viongozi, wanachama, wafuasi, asasi za kiraia, watetezi wa haki za binadamu na demokrasia pamoja na Watanzania wote kujitokeza kwa wingi mahakamani kufuatilia mwenendo wa utoaji wa hukumu hiyo.

Chama hicho kimesisitiza umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika misingi ya haki, utawala wa sheria na demokrasia nchini.

Taarifa hiyo imetolewa na Brenda Rupia, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Novemba 5, 2026.