ATHUMANI AHUKUMIWA MIAKA 20 JELA KWA KUKUTWA NA NYARA ZA SERIKALI

 

Mahakama ya Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro imemhukumu Athumani Issa Rashid, (47), kifungo cha miaka 20 jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kupatikana na nyara za Serikali, zikiwemo nyama za wanyamapori wawili aina ya digidigi, huku pikipiki moja aliyokuwa akitumia ikitaifishwa na Serikali.

Hukumu hiyo imetolewa Novemba 3, 2026, baada ya Mahakama kujiridhisha na ushahidi uliowasilishwa katika kesi ya uhujumu uchumi namba ECO 16343/2026, iliyofunguliwa dhidi ya mshtakiwa huyo.

Kwa mujibu wa taarifa za tukio, mshtakiwa alikamatwa Julai 12, 2026, majira ya saa 08:30 asubuhi katika eneo la Msitu wa Mabilioni, wilayani Same, na askari wa uhifadhi wa TANAPA waliokuwa katika doria ya kudhibiti ujangili na makosa mengine ya jinai.

Wakati wa kukamatwa, alikuwa na nyama za wanyamapori wawili aina ya digidigi bila kuwa na kibali cha kufanya shughuli hiyo. Thamani ya wanyama hao ilikadiriwa kuwa dola za Marekani 600, sawa na shilingi za Tanzania 1,574,100.

Baada ya kukamilika kwa uchunguzi, mshtakiwa alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Same Julai 17, 2026, na kusomewa shtaka la kupatikana na nyara za Serikali.

Baada ya shauri kusikilizwa, Mahakama ilimkuta na hatia na kutoa adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela pamoja na kutaifisha pikipiki moja na kuikabidhi kwa Serikali.

Hukumu hiyo inaendelea kuonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya vyombo vya ulinzi na uhifadhi katika kupambana na ujangili na kulinda rasilimali za wanyamapori nchini.