MAHUNDI: WAZAZI WANA WAJIBU MKUBWA KULINDA WATOTO DHIDI YA UKATILI

WAZAZI na walezi wametakiwa kuimarisha uangalizi na malezi ya watoto ili kuwakinga dhidi ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji, huku wakisisitizwa kutambua kuwa jukumu la kuhakikisha usalama wa watoto linaanzia katika familia kabla ya kuhitaji hatua za Serikali.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, leo Novemba 2, 2026, jijini Dodoma, wakati akijibu maswali ya Wabunge kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali kutoa elimu kwa mabinti na jamii kuhusu umuhimu wa kuripoti vitendo vya udhalilishaji.

Mahundi amesema wazazi na walezi wanapaswa kutambua nafasi yao katika kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama, yenye malezi bora na ulinzi dhidi ya vitendo vinavyoweza kuathiri maisha na mustakabali wao.

Amesema ni muhimu kwa wazazi kuwa karibu na watoto wao, kuwafuatilia na kuwapatia mwongozo unaozingatia maadili mema, mila, desturi na tamaduni za Kitanzania ili kuwajengea uwezo wa kujitambua na kujilinda.

Ameeleza kuwa jukumu la malezi halipaswi kuachwa kwa Serikali pekee, bali linahitaji ushiriki wa karibu wa familia na jamii katika kutambua, kuzuia na kuripoti vitendo vya ukatili vinavyofanywa dhidi ya watoto.

Akizungumzia hatua za Serikali, Mahundi amesema elimu kwa mabinti na jamii inaendelea kutolewa kupitia Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA).

Amesema mpango huo unatekelezwa kwa kushirikisha kamati za kisekta kuanzia ngazi ya Taifa hadi Vijiji na Mitaa, hatua inayolenga kuhakikisha elimu ya kuzuia ukatili inawafikia wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, amesema kila Kata ina Polisi Jamii wanaoshiriki kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya ulinzi na usalama, ikiwemo namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji.

Mahundi amebainisha kuwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nayo inaratibu wadau wake, wakiwemo viongozi wa kimila na vyombo vya habari, katika kuelimisha jamii kuhusu namna ya kukabiliana na vitendo hivyo.

Amesema ushirikiano wa wadau hao ni muhimu katika kuongeza uelewa wa wananchi na kuimarisha juhudi za kuzuia vitendo vinavyokiuka haki za watoto.

Ameongeza kuwa utoaji wa elimu kwa jamii unapaswa kuambatana na utayari wa wananchi kuripoti vitendo vya ukatili vinapotokea ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.

Mahundi amesisitiza kuwa ulinzi wa watoto ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano wa wazazi, walezi, jamii na Serikali katika kuhakikisha watoto wanakuwa katika mazingira yanayoheshimu haki zao.

Amewataka wananchi wa makundi yote kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutokomeza ukatili wa aina zote, akieleza kuwa watoto wanahitaji mazingira salama yatakayowawezesha kukua vizuri, kupata haki zao na kutimiza ndoto zao.

MWISHO