Masaji si tiba ya kila maumivu, wataalamu waonya

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wameonya wananchi dhidi ya kukimbilia huduma za masaji wanapopata maumivu ya mgongo, shingo, miguu au misuli bila kwanza kufahamu chanzo cha tatizo, wakisema kufanya hivyo kunaweza kutoa nafuu ya muda huku ugonjwa ukiendelea kukua.

Wamesema baadhi ya maumivu yanayodhaniwa kuwa ya uchovu au mkazo wa misuli yanaweza kuhitaji tathmini ya kitaalamu ili kubaini chanzo na kupewa matibabu au mazoezi yanayolenga kurejesha uwezo wa mwili.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani wa Hospitali ya Medinova, Selestine Mpiri, anasema dhana inayowachanganya wananchi ni kuamini kuwa fiziotherapia na masaji ni huduma moja.

“Massage mara nyingi inalenga kutoa unafuu wa muda mfupi. Misuli ikikaza ukafanyiwa masaji utajisikia vizuri, lakini hiyo inaweza kuwa ni ya muda mfupi. Fiziotherapia inalenga kutafuta mzizi wa tatizo na kuhakikisha unafanyiwa mazoezi au utaratibu unaoweza kusaidia tatizo liondoke na lisirudi tena,” anasema.

Anasema tatizo si masaji yenyewe, bali kuitumia kama tiba ya kila aina ya maumivu bila kufanyiwa tathmini ya kitaalamu.

Kwa mfano, anasema baadhi ya wagonjwa waliowahi kufika hospitalini wakiwa na dalili zinazofanana na kiharusi, walibainika baada ya uchunguzi kuwa hawakuwa na kiharusi wala tatizo la ubongo na walisaidiwa kwa fiziotherapia.

“Nilikuwa na wagonjwa watatu vijana ambao walikuja wakiwa wamepooza upande mmoja wa uso. Baada ya kuwafanyia uchunguzi, tulibaini hawakuwa na kiharusi wala tatizo la ubongo. Walipewa fiziotherapia na wakapona,” anasema.

Kwa mujibu wa Dk Mpiri, fiziotherapia haiwahusu watu waliopata ajali au kufanyiwa upasuaji pekee, bali inaweza kusaidia changamoto mbalimbali zinazohusu misuli, mifupa, mishipa ya fahamu, mfumo wa upumuaji na utendaji wa mwili.

“Fiziotherapia ni kubwa zaidi ya tunavyofikiria. Kuna magonjwa ya upumuaji, kizunguzungu na matatizo ya misuli ya nyonga ambayo yanaweza kusaidiwa kwa tiba hii,” anasema.

Anasema udhaifu wa misuli ya nyonga unaweza kuhusishwa na changamoto za kudhibiti mkojo na kwamba, kwa baadhi ya watu, mazoezi maalumu yanaweza kusaidia kuimarisha misuli hiyo.

Hatari ya masaji ya nguvu

Wataalamu pia wanaonya matumizi ya nguvu kubwa wakati wa masaji, hasa kwa watu wenye maumivu ya mgongo ambayo chanzo chake hakijajulikana.

Baadhi ya watoa huduma hutumia uzito wa mwili, ikiwamo kukanyaga mgongo, kwa madai ya kumsaidia mteja kujisikia mwepesi.

Hata hivyo, wataalamu wanasema shinikizo kubwa linaweza kuwa hatari kwa mtu mwenye tatizo la mifupa, pingili za mgongo, mishipa ya fahamu au jeraha ambalo halijagundulika.

Dk Mpiri anawataka watu wenye maumivu ya muda mrefu au yanayorudia kutafuta ushauri wa kitaalamu badala ya kutegemea masaji kila wanapohisi maumivu.

Anasema hata uchovu wa mwili unaweza kusababishwa na mambo mbalimbali, yakiwamo kazi nzito, kukaa au kusimama kwa muda mrefu, kukosa usingizi na mkazo wa misuli.

Hata hivyo, anasema uchovu unaodumu au unaoambatana na dalili nyingine unaweza kuhitaji uchunguzi wa kitabibu.

Akizungumza na Mwananchi mwishoni mwa juma, mtaalamu mwingine wa fiziotherapia wa Medinova, Witney Lema, anasema huduma hiyo inahusika na tiba ya utengamao na mazoezi tiba bila kutumia dawa, huku ikilenga matatizo ya misuli na mifupa pamoja na magonjwa ya mfumo wa fahamu kwa watu wazima na watoto.

“Wengi wetu tunaonekana kusumbuliwa na matatizo ya misuli na mifupa. Tunaumwa migongo, shingo, miguu na tunapata ajali. Baada ya ajali au kuvunjika mifupa, baadhi hushindwa kutembea vizuri tena. Fiziotherapia imekuja kusaidia katika changamoto hizi,” anasema.

Anasema tiba hiyo hutumia mbinu mbalimbali, ikiwamo tiba kwa mikono na vifaa vya kielektroniki, kulingana na hali ya mgonjwa.

Dk Mpiri anawataka wananchi pia kutotumia mazoezi wanayoyaona kwenye Youtube kama mbadala wa tathmini ya mtaalamu.

“Tunatakiwa tujue kwamba mazoezi, ili yafae zaidi, yanatakiwa yawe individualized (yalengwe kwako). Mtaalamu wa fiziotherapia pia atakurekebisha unapofanya mazoezi vibaya,” anasema.

Anasema mazoezi yanapaswa kuzingatia umri, ukubwa wa mwili na hali ya kiafya ya mtu, hivyo mazoezi ya mtu mwenye miaka 20 hayawezi kutumika kwa mtu wa miaka 60 bila tathmini.

Dk Imran Asif Bajwa anasema fiziotherapia huanza kwa tathmini ya mgonjwa na wakati mwingine huhitaji ushirikiano wa wataalamu mbalimbali kulingana na tatizo litakalobainika.

“Kupona kwa mgonjwa hakutegemei daktari mmoja au wawili, bali timu kubwa. Mgonjwa anaweza kuja kwa mtaalamu, lakini wakati wa assessment (tathmini) tunaweza kubaini anahitaji kumuona daktari wa mifupa. Tutafanya kazi kwa pamoja,” anasema.

Kwa nini GB 128 za simu yako zinawahi kujaa? Fanya hivi…

Dar es Salaam. Miaka iliyopita, simu yenye nafasi ya kuhifadhi taarifa ya GB32 au GB64 ilionekana kuwa na uwezo mkubwa, lakini mabadiliko ya matumizi ya simu janja yamefanya nafasi hiyo kujaa kwa haraka.

Leo, hata simu yenye GB 128 inaweza kumlazimu mtumiaji kusafisha taarifa mara kwa mara, hasa anayepiga picha nyingi, kurekodi video, kucheza michezo mikubwa au kutumia mitandao ya kijamii kwa kiwango kikubwa.

Sababu kubwa ni ongezeko la ukubwa wa picha, video na programu. Simu nyingi za kisasa zina uwezo wa kurekodi video za ubora wa juu, huku baadhi zikiruhusu kurekodi video zenye ubora wa hali ya juu unaofikia (4K) na hata viwango vya juu zaidi kulingana na aina ya kifaa.

Kwa mujibu wa Apple Support, kwa mfano, inaonyesha kuwa baadhi ya iPhone zinaweza kurekodi video ya 4K na kwamba teknolojia ya ProRes inaweza kutumia nafasi kubwa ya kuhifadhi, kiasi kwamba baadhi ya uwezo wa kurekodi hutegemea ukubwa wa uhifadhi ‘storage’ wa simu.

WhatsApp nayo inakula nafasi

Kwa watumiaji wengi, si kamera pekee inayojaza storage. Programu za mawasiliano kama WhatsApp zinaweza kuhifadhi kwa muda mrefu picha, video, nyaraka, sauti na faili nyingine zinazotumwa kwenye makundi na mazungumzo binafsi.

Tatizo linaweza kuwa kubwa zaidi kwa mtu aliye kwenye makundi mengi yanayotuma video na picha kila siku ambapo itakulazimu uzime auto-download.

Kwa upande wa Android, Google inashauri watumiaji kuingia sehemu ya Settings > Storage ili kuona ni aina gani ya faili au programu zinazotumia nafasi kubwa na kuanza kuziondoa zisizo muhimu.

Google pia inaeleza kuwa (backup) za WhatsApp kwenye Android sasa zinahesabiwa katika nafasi ya kuhifadhi ya akaunti ya Google, huku video zikiwa miongoni mwa vitu vinavyoweza kuongeza ukubwa kwa haraka.

GB 128 haimaanishi nafasi yote ipo wazi

Jambo jingine ambalo mtumiaji anapaswa kulifahamu ni kwamba namba iliyoandikwa kwenye boksi, kama GB 128, si lazima iwe nafasi yote atakayoiona akiwa anaanza kutumia simu.

Sehemu ya nafasi hiyo hutumika na mfumo wa uendeshaji, programu zilizokuja na simu na mafaili mengine ya mfumo. Kadri mtumiaji anavyoongeza programu na taarifa zake nafasi iliyobaki hupungua.

Hivyo, mtu anayenunua simu ya GB 128 kwa sababu anaona ina nafasi kubwa anapaswa kujiuliza pia ataitumia kwa shughuli gani.

Njia rahisi ni kuanza kwa kuangalia sehemu ya Storage kwenye simu ili kubaini kinachotumia nafasi kubwa.

Picha na video muhimu zinaweza kuhifadhiwa kwenye huduma za cloud au kuhamishiwa kwenye kompyuta au kifaa kingine cha kuhifadhi. Google, kwa mfano, inaruhusu watumiaji wa Android kusimamia nafasi kwa kuondoa picha na video ambazo tayari zimehifadhiwa kwenye Google photos, pamoja na faili zilizopakuliwa na programu ambazo hazitumiki.

Google Help, pia kuna simu za Android zinazoweza ku-archive programu zisizotumiwa mara kwa mara, badala ya kuzifuta kabisa. Google inaeleza kuwa hatua hiyo inaweza kuondoa sehemu ya programu inayotumia nafasi huku taarifa na ikoni yake vikibaki ili iweze kurejeshwa baadaye.

Kwa mtumiaji anayefanya matumizi ya kawaida kama kupiga picha chache, kutumia WhatsApp, mitandao ya kijamii, kusoma habari na kupiga simu, GB 128 inaweza kutosha ikiwa atasimamia vizuri taarifa zake.

Lakini kwa mpiga picha, mtengeneza maudhui, mcheza michezo mikubwa au mtu anayerekodi video nyingi, GB 256 au zaidi inaweza kuwa chaguo lenye nafasi kubwa zaidi ya matumizi ya muda mrefu.

Kabla ya kununua simu, si muhimu kuangalia storage pekee. Mnunuzi anapaswa pia kuangalia aina ya kamera, ubora wa video, ukubwa wa programu anazotumia, kama kifaa kinaunga mkono memory card na kama kina uwezo wa kutumia huduma za cloud.

Kwa kifupi, GB 128 si ndogo moja kwa moja, lakini inaweza kuwa ndogo kulingana na matumizi ya mwenye simu. Kadri simu inavyotumika kama kamera, ofisi, burudani na kituo cha kuhifadhi mafaili, ndivyo nafasi kubwa ya kuhifadhi inavyokuwa muhimu zaidi.

Asimulia alivyojifungua katikati ya tetemeko la ardhi

Dar es Salaam. Maria Florida, 39, ameeleza furaha yake baada ya kujifungua salama mtoto wake wa nne kwa njia ya upasuaji, huku tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.7 likitikisa eneo la Nusa Tenggara Mashariki mwa Indonesia.

Florida alikuwa tayari ameshaanza kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Nagekeo wakati tetemeko hilo lilipoanza. Hata hivyo, madaktari waliendelea na huduma huo licha ya mazingira magumu yaliyosababishwa na mtikisiko huo.

Tetemeko hilo lilisababisha kukatika kwa umeme hospitalini hapo, hivyo madaktari walilazimika kutumia mwanga wa tochi kuendelea na upasuaji hadi kufanikisha kumleta duniani mtoto huyo.

Baada ya kujifungua mtoto wa kike, Florida alimpa jina Gempita Soli Wona,   linalohusishwa na neno la Kiindonesia linalomaanisha tetemeko la ardhi.

Mtoto huyo alizaliwa akiwa na uzito wa kilo 1.3 na kwa mujibu wa taarifa za madaktari afya yake inaendelea kuimarika.

Tetemeko hilo lilitokea Agosti 15, 2026 na kuleta madhara makubwa mashariki mwa Indonesia, likisababisha vifo vya watu wasiopungua 54, majeruhi zaidi ya 130 na kuwalazimisha maelfu ya wakazi kuondoka katika maeneo yaliyoathirika.

Kutokana na mitikisiko kuendelea na baadhi ya miundombinu ya hospitali kuathirika, mtoto huyo amewekwa katika mashine maalumu ya kuhifadhi joto iliyowekwa nje ya jengo la hospitali.

Florida amewashukuru madaktari kwa kujitoa na kuendelea na upasuaji huo licha ya hatari iliyokuwapo.

Wakati tukio hilo likitoa simulizi ya matumaini, idadi ya watu waliofariki kutokana na tetemeko hilo imefikia 53, huku shughuli za uokoaji zikiendelea katika maeneo yaliyoathirika.

Waokoaji wamefanikiwa kupata miili mingine sita, hali iliyoongeza idadi ya vifo kutoka 47 hadi 53.

Zaidi ya watu 135 wameripotiwa kujeruhiwa, huku nyumba zaidi ya 900 zikiharibiwa na maelfu ya watu kulazimika kuondoka katika makazi yao kutokana na hofu ya mitetemeko zaidi.

Takriban watu 5,000 wamehama makazi yao na kuhamia maeneo salama likiwa la  Kisiwa cha Flores.

Tetemeko hilo pia limesababisha maporomoko ya ardhi na kuziba baadhi ya barabara, hali iliyowapa changamoto waokoaji kuwafikia watu waliokwama katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

Kukatika kwa umeme na mawasiliano kumeongeza ugumu wa shughuli za uokoaji, huku mamlaka zikiendelea kuratibu juhudi za kuwafikia waathirika na kutoa msaada wa dharura.

Misaada inayotolewa inajumuisha chakula, mahema na mahitaji mengine muhimu kwa watu walioathirika.

Jose Chameleone alivyoibua shangwe akitumbuiza kilele tamasha la Kizimkazi

Unguja. Msaanii wa kimataifa kutoka Uganda, Jose Chameleone ameibua shangwe wakati akitumbuiza katika kilele cha tamasha la Kizimkazi.

Katika tamasha hilo linalofanyika leo Agosti 14, 2026 viwanja vya Mwehe Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja, msanii huyo amepata fursa kutumbuiza nyimbo zake mbili, Jamila na Mama Mia.

Katika kibao chake cha Jamila, alishuka kutoka katika jukwaa la burudani na kusogelea meza kuu walipokaa viongozi wakuu wa kitaifa kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Baada ya kufika katika jukwaa hilo, Rais Samia Suluhu Hassan alishuka kutoka kwenye kiti chake alipokuwa amekaa na kuongea na msanii huyo kisha kucheza naye wimbo huo wa mbona umeniacha.

Baada ya hapo aliondoka huku akiibua shwangwe kubwa kwa wananchi na viongozi waliofurika katika viwanja hivyo kwa ajili ya kusherehekea sherehe hizo.

Katika tamasha hilo pia wasanii wengine wa ndani na nje ya Tanzania wamepata fursa ya kutumbuiza.

Miongoni mwa wasanii hao ni Mrisho Mpoto, Sholo Mwamba, kikundi cha ngoma kutoka Dodoma cha Mahenza na ngoma ya asili ya Kizimkazi ya Shomoo.

Rais Samia ahimiza amani, utulivu Tamasha la Kizimkazi

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewahimiza Watanzania, hususan vijana, kulinda amani, usalama na utulivu, akisema maendeleo ya Taifa hayawezi kustawi katika mazingira ya vurugu.

Amesema amani, usalama na utulivu ni nguzo muhimu zinazowezesha uwekezaji, utalii, biashara, ajira na utoaji wa huduma za jamii, ambazo haziwezi kustawi katika mazingira ya vurugu na uvunjifu wa amani.

“Niwaombe Watanzania wenzangu, hususan vijana, msikubali kuharibu amani ya nchi yenu, amani ndiyo kila kitu katika maisha yenu, niwaombe sana mumkatae kwa nguvu zote yeyote asiyeitakia mema Tanzania yetu, tulinde nchi yetu pamoja na Muungano wetu kwa mustakabali wa kizazi kijacho,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema hayo leo Ijumaa, Agosti 14, 2026, alipohitimisha Tamasha la Kizimkazi katika Uwanja wa Mwehe, Makunduchi, Zanzibar.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, akiwamo Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, pamoja na viongozi wa vyama vya siasa na taasisi za umma.

Akizungumzia tamasha hilo, Rais Samia amesema limeleta chachu ya maendeleo katika wilaya za Kusini mwa Zanzibar kwa kuchochea biashara na kuongeza fursa za kiuchumi zinazoboresha maisha ya wananchi.

“Ndugu zangu, shangwe siku zote ni nzuri. Zinatuleta pamoja, zinaimarisha mshikamano na umoja, zinatusaidia kutangaza utamaduni wetu na kuvutia wageni. Kazi yetu kama viongozi ni kuhakikisha fursa zinazoibuliwa kupitia shangwe hizi zinawagusa wananchi wetu na tunaziunga mkono,” amesema.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo na Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi katika Kilele cha Tamasha la Kizimkazi lililofanyika leo Agosti 14, 2026, Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

Amesisitiza kuwa, Tamasha la Kizimkazi linapaswa kuwa lango la fursa za kiuchumi na chanzo cha ustawi wa wananchi na Taifa kwa jumla.

Amesema Wilaya ya Kusini imepata mabadiliko makubwa ikilinganishwa na mwaka 2016, kutokana na kuongezeka kwa fursa za biashara na uwekezaji.

Ameongeza kuwa ujenzi wa miundombinu na utekelezaji wa miradi mbalimbali umeendelea kuvutia wananchi na wawekezaji kuwekeza katika eneo hilo.

“Rais wa Zanzibar ameweka mazingira mazuri ya uwekezaji. Karibuni muwekeze. Tunaendelea kujenga uwanja wa michezo ambao utasaidia kufungua fursa mbalimbali wakati wa michuano ya AFCON itakayofanyika Juni 2027,” amesema.

Ameongeza kuwa uwanja huo utatoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza katika huduma zitakazohitajika na wachezaji pamoja na wageni watakaoshiriki mashindano hayo.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amemshukuru Rais Samia kwa kuanzisha Tamasha la Kizimkazi, akisema limekuwa na mchango mkubwa katika kutangaza utalii wa Zanzibar.

“Nawapongeza wananchi wote kwa mwamko mkubwa wa kushiriki tamasha hili na kutumia fursa zilizoambatana nalo, hakika mwaka huu tamasha limefana sana. Limekuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha shughuli za maendeleo,” amesema na kuongeza:

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na msanii wa Uganda, Jose Chameleone wakati wa tamasha la Kizimkazi linalofanyika leo Agosti 14, 2026 viwanja vya Mwehe Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja.

“Tumeshuhudia uzinduzi wa miradi mbalimbali ikiwamo ya maji, barabara, elimu, nyumba za makazi na viwanja vya michezo,” amesema.

Rais Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha miradi yote iliyozinduliwa na itakayotekelezwa baadaye inatunzwa na kuendelezwa ipasavyo.

Hoja ya uhamiaji kutikisa mkutano wa wakuu wa SADC

Dar es Salaam. Suala la uhamiaji linatarajiwa kutawala mjadala katika mkutano wa 46 wa kawaida wa wakuu wa nchi na serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaofanyika leo, Agosti 17, 2026, jijini Durban, Afrika Kusini.

Mkutano huo unaowakutanisha viongozi wa nchi 16 wanachama unafanyika katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Durban, chini ya uenyekiti wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa.

Ajenda rasmi ya mkutano huo ni pana na inahusisha maendeleo ya kiuchumi, usalama, ushirikiano wa kikanda, usalama wa chakula pamoja na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya SADC.

Hata hivyo, suala la uhamiaji limeibuka kama moja ya changamoto zinazoweza kuhitaji uangalizi wa viongozi, hasa kutokana na kuongezeka kwa mvutano kuhusu wahamiaji nchini Afrika Kusini na athari zake kwa uhusiano kati ya nchi wanachama.

Mjadala huo unakuja wakati Afrika Kusini ikiendelea kukabiliana na malalamiko ya baadhi ya raia wanaodai wahamiaji wanashindania ajira, huduma za jamii na fursa za kiuchumi.

Takwimu rasmi za serikali ya nchi hiyo zinaonyesha takribani watu milioni 2.4, waliozaliwa nje ya nchi wanaishi nchini humo , na utafiti mwingine ulionyesha  idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia milioni 3.1.

Wataalamu wanaonya kuwa changamoto ya uhamiaji haiwezi kutatuliwa na Afrika Kusini pekee kwa kuwa inahusishwa kwa kiasi kikubwa na tofauti za kiuchumi, ajira na fursa zilizopo kati ya nchi za SADC.

Mtazamo huo umeungwa mkono na Taasisi ya Institute for Security Studies (ISS), inayosisitiza kuwa uhamiaji unapaswa kushughulikiwa kama suala la kikanda kutokana na utegemeano wa nchi wanachama.

Kwa mtazamo huo, hatua za nchi moja katika kudhibiti wahamiaji zinaweza kuwa na athari kwa majirani zake, hasa kwa kuwa wananchi wa nchi za SADC wamekuwa wakivuka mipaka kutafuta ajira, biashara, usalama na fursa nyingine za kiuchumi.

Kwa mujibu wa Associated Press (AP), Afrika Kusini imetumia karibu dola milioni 18 kugharamia kuwarejesha  wahamiaji katika nchi zao, huku zaidi ya watu 80,000 wakirudishwa au kusaidiwa kurejea katika mataifa yao.

Serikali pia imesema imewakamata karibu watu 60,000 waliokuwa nchini humo bila vibali, wakiwamo zaidi ya 16,000 kwa Julai pekee.

Rais Ramaphosa amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kuonya dhidi ya mgongano kati ya ajenda ya ushirikiano wa kikanda na matendo yanayoweza kuwabagua wahamiaji.

Katika hotuba yake ya Agosti 14, alisema Afrika Kusini haiwezi kuzungumzia ushirikiano katika mikutano ya kikanda wakati ikifanya kinyume chake mitaani, akisisitiza umuhimu wa mshikamano uliojengwa katika historia ya ukombozi wa eneo hilo.

Kauli hiyo inaweka shinikizo zaidi kwa mkutano wa Durban, ambao unafanyika wakati suala la uhamiaji likiwa tayari limezua mijadala mikali ndani ya Afrika Kusini na katika baadhi ya nchi jirani.

Imeandaliwa na Salma Hamis kwa msaada wa mitandao.

NBC kuchochea nguvu ya uchumi Zanzibar

Zanzibar. Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imesema itaendelea kuwa mshirika wa kimkakati katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar kwa kuwawezesha wafanyabiashara, wawekezaji na wajasiriamali kutumia fursa zinazotokana na uwekezaji, maendeleo ya miundombinu na ukuaji wa sekta ya utalii.

Benki hiyo imesema itaendelea kutoa huduma na suluhisho za kifedha zitakazowawezesha wafanyabiashara kupata mitaji, kupanua shughuli zao, kuongeza uzalishaji na kuwekeza katika fursa mpya za biashara, hususan maeneo yenye kasi ya ukuaji wa uchumi kama Kizimkazi.

Kauli hiyo ilitolewa jana Jumapili, Agosti 16, 2026, na Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, wakati wa hitimisho la Tamasha la Kizimkazi mwishoni mwa wiki. Mgeni rasmi katika hitimisho hilo alikuwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Sabi alisema benki hiyo inaona fursa kubwa katika mabadiliko yanayoendelea Zanzibar na imejipanga kushirikiana na sekta binafsi kuzigeuza fursa hizo kuwa shughuli endelevu za kiuchumi.

“NBC itaendelea kuwa mshirika wa wafanyabiashara na wawekezaji katika kutumia fursa zinazopatikana Zanzibar, ikiwemo Kizimkazi. Tumejipanga kutoa suluhisho mbalimbali za kifedha zitakazowasaidia kupata mitaji, kukuza biashara zao na hatimaye kuchangia katika ukuaji wa uchumi,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi (kulia), akizungumza na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba wakati wa hafla ya kuhitimisha Tamasha la Kizimkazi lililoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Sabi alisema uwezeshaji wa kifedha ni muhimu katika kujenga mazingira yanayowezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi, kwa kuwa ukuaji wa biashara unaweza kuongeza uzalishaji, ajira na fursa za kipato kwa wananchi.

Kauli hiyo imekuja wakati Zanzibar, hususan maeneo ya Kusini, ikiendelea kushuhudia ongezeko la shughuli za kiuchumi linalochochewa na uwekezaji katika sekta ya utalii na maendeleo ya miundombinu.

Akihitimisha tamasha hilo Agosti 14, 2026, Rais Samia Suluhu aliwahimiza wafanyabiashara na wawekezaji kutumia fursa zinazozidi kujitokeza Zanzibar.

Rais Samia alisema Wilaya ya Kusini imepiga hatua kubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita kutokana na ongezeko la uwekezaji, hasa katika sekta ya utalii.

“Wilaya ya Kusini imepata mabadiliko makubwa sana ikilinganishwa na mwaka 2016 kutokana na kuongezeka kwa fursa za biashara zilizotokana na uwekezaji, hususani kwenye maeneo ya utalii. Tamasha la Kizimkazi limekuwa chachu muhimu kuelekea mafanikio hayo. Hivyo, tunawakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutumia fursa hizi,” alisema.

Akizungumzia wito huo, Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa na Uwekezaji wa NBC, Elvis Ndunguru, alisisitiza nafasi ya sekta binafsi katika kunufaika na mnyororo wa thamani unaotokana na ukuaji wa utalii.

Alisema fursa hizo zinahusisha biashara za huduma, usafirishaji, malazi, chakula na vinywaji, bidhaa za ndani, burudani, sanaa na huduma nyingine zinazohusiana na utalii.

“Dhamira ya NBC ya kushirikiana na wafanyabiashara na wawekezaji ipo wazi na inaakisi umuhimu wa upatikanaji wa huduma na mitaji inayowawezesha wadau wa sekta binafsi kuchangamkia fursa hizo na kuzifanya kuwa shughuli za kibiashara zenye tija na endelevu,” alisema.

Ndunguru alisema ushiriki huo unaonesha dhamira ya NBC kwenda zaidi ya utoaji wa huduma za kifedha kwa kushirikiana na wadau katika masuala yenye umuhimu kwa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kimazingira.

Katika hafla hiyo, Rais Samia aliwashukuru wadau mbalimbali walioshiriki na kuchangia kufanikisha Tamasha la Kizimkazi, akiwemo NBC kwa mchango wake.

Samia: Fursa zinazoibuliwa Kizimkazi ziwaguse wananchi

Unguja. Rais Samia Suluhu Hassan amefunga Tamasha la Kizimkazi akiwataka viongozi kuhakikisha fursa zinazozalishwa au kuibuliwa ndani ya tamasha hilo zinawagusa wananchi.

Amesema kutokana na tamasha hilo, Wilaya ya Kusini imechangamka, imefurahi, imekuwa na biashara na imepata fursa ilizokusudia katika kuboresha maisha na ustawi wa wananchi.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo, Agosti 14, 2026, wakati akihitimisha tamasha hilo katika Uwanja wa Mwehe, Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja.

“Tunaziunga mkono na kuzichochea kwa wananchi wetu, kama Rais wa Zanzibar (Dk Hussein Mwinyi) alivyoahidi. Kwa hiyo, shangwe iwe lango la fursa, na fursa hizo ziwe chanzo cha ustawi wa wananchi wetu na taifa kwa ujumla,” amesema Dk Samia.

Amesema miradi yote iliyozinduliwa au kujengwa kupitia tamasha hilo, ndiyo malengo hasa ya kuanzishwa kwa tamasha hilo.

“Mnakubaliana nami nyote mlioshiriki tamasha hili, mmeona ukweli huu kwamba Kizimkazi na Wilaya ya Kusini kwa ujumla ilinoga,” amesema.

Amesema baada ya shangwe hilo kumalizika, wananchi wabaki na huduma, miundombinu, biashara na fursa zinazoendelea kufanya kazi, huku akipongeza kaulimbiu ya mwaka huu akisema imetendewa haki.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi katika Kilele cha Tamasha la Kizimkazi (Kizimkazi Festival) lililofanyika, Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar Agosti 14, 2026.

“Kaulimbiu ya mwaka huu inasema ‘Kizimkazi kumenoga, shangwe na fursa’. Asanteni sana mlioshiriki kuileta shangwe hiyo Kizimkazi na maeneo ya jirani, na hatimaye fursa kuibuka,” amesema.

Rais Samia amesema Wilaya ya Kusini ya leo imebadilika, siyo kama ilivyokuwa miaka 10 au 15 iliyopita, tofauti na mwaka 2016 walipoanza tamasha hilo, ambapo Kizimkazi imekuwa na fursa nyingi za biashara na uwekezaji.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, miundombinu na miradi wanayoijenga imeendelea kuvutia wananchi na wawekezaji kuja kufanya shughuli zao katika eneo hilo.

“Nawaomba wale wote walioziona fursa ndani ya wilaya hii, waje kwa uwekezaji, tunawakaribisha. Rais wa Zanzibar ameweka mazingira mazuri sana ya uwekezaji. Karibuni sana kuja kuwekeza,” amesema Samia.

Katika kutengeneza fursa, Rais Samia amesema wanajenga uwanja wa michezo ambao ukikamilika utaweza kutumika katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) itakayofanyika Juni 2027.

Amesema: “Uwanja huo ni fursa kwenu wawekezaji kuja kuwekeza kwa ajili ya huduma zitakazotolewa kwa wachezaji na watu wote watakaoshiriki katika michuano hiyo.”

Rais Samia ametumia fursa hiyo kusisitiza suala la amani, usalama na utulivu ndani ya nchi. Amesema kila anapopata fursa ya kuzungumza na wananchi, imekuwa ni utaratibu wake kusisitiza na kuwakumbusha umuhimu wa kuendelea kuzilinda na kuzitunza tunu hizo kwa nguvu zote.

“Uwekezaji, maendeleo tunayoyaona hapa, uwekezaji, utalii, biashara, ajira na huduma za jamii, haya hayawezi kustawi katika mazingira ya vurugu na uvunjifu wa amani.

“Niwaombe Watanzania wenzangu, hususan vijana, msikubali kuharibu amani ya nchi yenu. Amani ndiyo kila kitu katika maisha yetu. Tukatae kwa nguvu zote wasiolitakia mema taifa letu, na tulinde Tanzania yetu na Muungano wetu kwa mustakabali wa kizazi chetu na kizazi kijacho,” amesema Rais Samia.

Kwa upande wake Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, amesema tamasha hilo lina mchango mkubwa katika kutangaza, kuhifadhi na kuenzi mila na utamaduni, na hivyo kuchochea na kuhamasisha shughuli za maendeleo ya wananchi wa Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja na Zanzibar kwa ujumla.

Amempongeza Rais Samia kwa maono yake ya kuanzisha tamasha hilo.

“Hakika, mwaka huu tamasha hili limefana sana, hongereni sana. Mheshimiwa Rais Samia, tamasha hili limekuwa ni jukwaa muhimu la kuhamasisha shughuli za maendeleo, kwani pamoja na shughuli za burudani na michezo,” amesema Dk Mwinyi.

Pia, amesema wameshuhudia uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo barabara, maji, elimu, afya, nyumba za makazi na viwanja vya michezo.

Ametumia fursa hiyo kuahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha miradi yote iliyozinduliwa na ile itakayojengwa baadaye inatunzwa na kuendelezwa ipasavyo kwa maendeleo na ustawi wa wananchi.

Dk Mwinyi ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha miundombinu inayojengwa inatumika na kutunzwa vizuri ili idumu na kutumika kwa muda mrefu kama ilivyokusudiwa.

Amesema Tamasha la Kizimkazi litaendelea kuwa chachu na kutoa mchango muhimu wa kuwavutia wageni Zanzibar, kuhamasisha utalii wa ndani na shughuli za uwekezaji Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Sherehe hizo zimehudhuriwa pia na Rais wa zamani wa Guinea-Bissau, Umaro Sissoco Embalo, Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, na viongozi wengine wa kidini na kisiasa.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis, amesema tamasha hilo limegusa maeneo yote ya kihuduma, ikiwemo afya, elimu na ujasiriamali.

Kwa mujibu wa Hamida, wajasiriamali wadogo wa Mkoa wa Kusini Unguja, maeneo ya Kizimkazi na shehia jirani, wamepata ajira na fursa mbalimbali.

“Mheshimiwa Rais Samia, tunakushukuru sana. Tamasha limewakutanisha na taasisi za fedha; sasa hivi wananchi wa maeneo haya wanakopesheka na wanakopeshwa na taasisi zetu, na wameanza kufanya biashara,” amesema Hamida.

Hamida amesema vijana wa mkoa huo sasa wamefikia fursa za kiutalii, uwekezaji na kujiajiri katika kazi mbalimbali za amali.

“Kupitia maonyesho ya mwaka huu, tumesajili jumla ya wafanyabiashara 129 waliohitaji kuonyesha biashara ama huduma.

“Pia, tulikuwa na wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo ambao hawakuingia kwenye mabanda ya maonyesho, wasiopungua 200, hata yule mdogo ambaye alikuwa akiuza karanga, mikate, kachori na vitu kama hivyo,” amesema.

Amesema tamasha limeendelea kuwaunganisha wanakusini, wana wa Kizimkazi na kuwakutanisha na watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Zanzibar.

“Tamasha hili, kwetu sisi wana wa Kusini, tunasema linaimarisha Muungano wetu. Tunaendelea kuungana, na ndiyo maana leo hii tuna wageni wengi kutoka Tanzania Bara. Hii inaonyesha kwamba tamasha limelenga kuimarisha Muungano wetu, na sisi tunajivunia hilo,” amesema.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, tamasha hilo limewafanya waone thamani ya fursa zilizomo ndani ya mkoa wao.

Jaji Warioba atoa kauli sakata la Lissu

Dar es Salaam. Mwanasiasa mkongwe, Jaji Joseph Warioba amesema busara za kisiasa zinatakiwa kutumika ili kumwezesha Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia (Chadema), Tundu Lissu anayekabiliwa na kesi ya uhaini kuachiwa huru.

Kauli ya Jaji Warioba imekuja baada ya siku mbili tangu wadau wa siasa na haki za binadamu, kueleza hatua nne za kiutu, ikiwemo kumuachia Lissu, katika kulirejesha Taifa pamoja baada ya matukio ya Oktoba 29, 2025.

Jaji Warioba, mwanasheria na jaji wa siku nyingi na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia Novemba 5, 1985 hadi Novemba 9, 1990, amesema hayo katika Mahojiano la Mwandishi wa siku nyingi, Jenerali Ulimwengu.

Amesema mamlaka aliyonayo Rais ya kutoa msamaha kwa wafungwa hayamaanishi kuingilia uhuru wa Mahakama, akieleza kuwa Rais anaweza kutumia mamlaka hayo pale anapoona kuna sababu za msingi za kuponya majeraha au kulinda masilahi mapana ya nchi.

Amesema Mahakama inapomhukumu mtu, hata kwa adhabu kubwa kama kifungo cha muda mrefu au hukumu ya kifo, uamuzi huo unabaki kuwa wa Mahakama, lakini Katiba inampa Rais mamlaka ya kusamehe au kupunguza adhabu katika mazingira yanayofaa.

“Mahakama imeamua, lakini Rais anaweza kusema huyu hapana. Ndiyo maana kila mwaka wakati wa siku ya Uhuru, hutolewa orodha ya watu ambao Rais amewasamehe. Anao uwezo huo,” amesema.

Warioba amesema mamlaka hayo yanaweza kutumika pia katika mazingira ambayo nchi inahitaji kutuliza hali, kuponya majeraha na kufungua nafasi ya mazungumzo, akisisitiza kuwa hatua hiyo si kuingilia Mahakama, bali ni kutumia mamlaka aliyopewa Rais.

“Mbowe alitiwa ndani lakini kwa sababau ya public interest (masilahi ya umma) na mambo yalivyokuwa, wakasema tumtoe ili tuweze kujadiliana, haikutoka sababu kwamba suala hili liko mahakamani hivyo hawawezi kuingilia mahakama.

Akitoa mfano mwingine, amesema: “Mwaka jana wakati vijana wengi walikamatwa na kufikishwa mahakamani kutokana na vurugu za uchaguzi, Rais aliweza kuingilia kwa kuzingatia hali ya nchi na kuamua kuwa waachiliwe.”

“Kwa nini katika hali Lissu ishindikane? Kwa sababu nchi iko katika hali fulani. Unaona ili tuponye majeraha haya, tuzungumze, ni vizuri huyu akaachwa kwa sababu ni mtu muhimu katika haya,” amesema.

Amesema Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza kutumia mamlaka hayo, akitoa mfano wa Afrika Kusini wakati wa utawala wa makaburu, ambapo baadhi ya watu walifungwa kutokana na misimamo yao ya kisiasa.

Kauli ya Warioba inaungana na ile iliyowahi kutolewa na Julai 13, 2026 na mwanasiasa mkongwe na mwanazuoni wa uchumi, Profesa Anna Tibaijuka, aliyemshauri Rais Samia Suluhu Hassan kutumia hekima, busara na kuzingatia falsafa yake ya 4R aliyoasisi, kumwachia huru Lissu.

Rais Samia alipoingia madarakani Machi 19, 2021 alitangaza kuongoza kwa kutumia falsafa za R nne, Reconciliation, Resilience, Reforms and Rebuilding, akimaanisha maridhiano, mabadiliko, ustahimilivu na kujenga upya.

Kwa mujibu wa Tibajuka, kuendelea kwa kesi ya Lissu, na simulizi zinazoripotiwa na vyombo vya habari vya kimataifa, vinazidi kuibua hisia tofauti miongoni mwa vijana na kuathiri taswira ya Tanzania pamoja na masilahi yake katika jumuiya ya kimataifa.

Ushauri huo wa Profesa ulienda sambamba na ule uliotolewa na Baraza la Mawaziri (CMAG) wa Jumuiya ya Madola, lililoipa Serikali ya Tanzania muda wa siku 30 kutafuta suluhisho la kisiasa na kisheria kuhusu kesi inayomkabili Lissu. Taarifa hiyo ilitolewa baada ya kikao cha 73 cha dharura cha CMAG kilichofanyika Julai 10, 2026.

Katika mahojiano yake juzi yaliyofanywa na mwanahabari mkongwe Jenerali Ulimwengu na kurushwa na JU Post, Jaji Warioba amejenga hoja yake akirejea namna baadhi ya wanasiasa waliowahi kuwekwa gerezani, lakini Rais Samia akawatoa.

Jaji Warioba alieleza namna Rais Samia alivyomtoa gerezani Mwenyekiti wa zamani wa Chadema, Freeman Mbowe aliyekuwa akikabiliwa na mashitaka ya ugaidi.

“Mbowe aliwekwa ndani, kwa sababu ya masilahi ya umma na mambo yalivyokuwa, akatoka ili kujadiliana,” ameeleza Warioba.

Julai 21, 2021 Mbowe alikamatwa na Polisi jijini Mwanza kisha kusafirishwa hadi Dar es Salaam kwa tuhuma za ugaidi.

Agosti 16, 2021 Mbowe alishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam kwa makosa mbalimbali ikiwemo kufadhili vitendo vya ugaidi na alikaa ndani kwa miezi minane.

Baadhi ya viongozi wa kisiasa walimwomba Rais Samia kumwachia Mbowe, miongoni mwao alikuwa Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe wakitaka kuingilia kati sakata la Mbowe, wakisema Rais anao uwezo huo.

Novemba 13, 2025 akihutubia Bunge Rais Samia Suluhu aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo ofisi ya DPP kuchuja makosa ya vijana wanaoshtakiwa kwa makosa ya uhaini baada ya maandamano yaliyosababisha vurugu wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Rais Samia alisema kwa wale vijana waliofanya makosa kwa kufuata mkumbo waachiwe huru.

“Natambua kuna vijana wengi wamekamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini, hawakujua wanachokifanya,”

“Wengine walifuata mkumbo, nikiwa kama mama navielekeza vyombo vya kisheria kuangalia makosa yaliyofanywa na vijana wetu, kwa wale waliofanya mambo kwa kufuata mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu wawafutie makosa yao,” alisema Rais Samia.

Kiswahili chazidi kujitanua duniani, watafiti kukutana Kampala

Dar es Salaam. Watafiti na wanataaluma wa Kiswahili wamepewa fursa ya kushiriki katika mjadala wa kimataifa kuhusu maendeleo ya lugha hiyo kupitia kongamano la Kiswahili litakalofanyika Kampala, nchini Uganda, wakati Kiswahili kikizidi kupanua ushawishi wake katika elimu, diplomasia, utamaduni na mawasiliano ya kimataifa.

Fursa hiyo imetolewa na Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (Chaukidu), ambacho kimeongeza hadi Agosti 26, 2026, muda wa kutuma ikisiri za makala kwa ajili ya kongamano hilo.

Uamuzi huo umetokana na maombi kutoka kwa wanachama na wadau mbalimbali wa Kiswahili waliotaka muda zaidi wa kukamilisha kazi zao na kuziwasilisha.

Katika taarifa iliyosainiwa leo, Agosti 17, 2026, na Mkurugenzi wa Chaukidu, Dk Mussa Hans, chama hicho kimewataka wanachama na wadau ambao bado hawajawasilisha ikisiri kutumia muda huo wa nyongeza kukamilisha kazi zao na kuzifikisha kabla ya tarehe hiyo.

Dk Hans amesema uamuzi huo umezingatia maombi yaliyowasilishwa na wanachama, huku akisisitiza kuwa muda huo unapaswa kutumiwa vizuri na wale ambao bado wanakamilisha kazi zao.

Mbali na kuwasilisha ikisiri, Chaukidu imewakumbusha wanachama kuendelea kuimarisha uanachama wao kwa kulipa ada ya mwaka 2026, hatua inayolenga kuwezesha chama kuendelea na shughuli zake za kukuza na kuendeleza Kiswahili.

Kongamano hilo linakuja wakati Kiswahili kikizidi kupata nafasi katika majukwaa ya kimataifa, hali inayoongeza hitaji la tafiti na mijadala ya kitaaluma kuhusu namna ya kukiendeleza na kukifanya kiendane na mabadiliko ya dunia.

Akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika Makao Makuu ya Unesco jijini Paris, Ufaransa, Julai 7, 2026, Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba alisema kuna haja ya kutafuta mbinu mpya za kukieneza Kiswahili baada ya lugha hiyo kupata hadhi kubwa kimataifa.

“Kadiri Kiswahili kinavyoendelea kupata hadhi ya kimataifa, ni muhimu sasa kuanza kutazama hatua inayofuata ya kukieneza duniani,” alisema.

Alisema Serikali itaendelea kuimarisha matumizi ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania kupitia elimu, tafiti, uchapishaji, tafsiri, teknolojia za kidijitali na diplomasia ya lugha, kwa kushirikiana na Unesco, vyuo vikuu, nchi mbalimbali na taasisi za kimataifa.

Kauli hiyo inaonesha umuhimu wa majukwaa ya kitaaluma kama kongamano la Chaukidu, ambayo huwapa watafiti nafasi ya kuwasilisha matokeo ya tafiti zao, kubadilishana maarifa na kujadili changamoto na fursa zinazolikabili Kiswahili katika dunia ya sasa.

Kwa upande wa Unesco, Mkurugenzi Mkuu Khaled El-Enany amesisitiza nafasi ya Kiswahili katika kuwaunganisha watu na kuongeza fursa za elimu na maarifa.

Katika Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani ya mwaka huu, Unesco iliweka mkazo katika kaulimbiu “Kiswahili kwa Amani, Mshikamano na Diplomasia ya Kiuchumi Duniani,” ikieleza kuwa lugha hiyo ina nafasi katika kukuza amani, mazungumzo, utambulisho wa kitamaduni, elimu, ushirikiano wa kikanda na mahusiano ya kimataifa.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Saidi Othman Yakub, alisema maadhimisho hayo yaliwakutanisha zaidi ya washiriki 300 kutoka nchi 16 duniani, huku shughuli mbalimbali zikilenga kuendeleza na kukitangaza Kiswahili kimataifa.

Unesco inaeleza kuwa Kiswahili kina zaidi ya wazungumzaji milioni 200 katika Afrika Mashariki, Kati na Kusini na maeneo mengine duniani, huku Siku ya Kiswahili Duniani ikiwa sehemu ya jitihada za kuongeza uelewa na matumizi ya lugha hiyo kimataifa.

Kwa msingi huo, watafiti na wanataaluma wanaoshiriki kongamano hilo wanatarajiwa kuwa sehemu ya mjadala mpana kuhusu mustakabali wa Kiswahili, ikiwamo nafasi yake katika elimu, teknolojia, uchumi, utamaduni na diplomasia.

Kwa Chaukidu, kuongeza muda wa kuwasilisha ikisiri hadi Agosti 26 ni nafasi kwa watafiti ambao bado hawajakamilisha kazi zao kujiunga na jukwaa hilo na kuchangia maarifa mapya yanayoweza kuimarisha nafasi ya Kiswahili ndani na nje ya Afrika.