Bunge lasogezwa mbele kupisha sherehe za Maulid

Dar es Salaam. Baada ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kutangaza kuwa Jumanne Agosti 25 Agosti, 2026 itakuwa ni Sikukuu ya Maulid, mkutano wa nne wa Bunge umesogezwa mbele na sasa utaanza Jumatano Agosti 26.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Agosti 17,2026 na Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma ya  ofisi ya Bunge, imeeleza mabadiliko hayo yamefanyika ili kutoa fursa kwa Waislam wote na Watanzania kwa ujumla kusherehekea sikukuu hiyo ambayo kitaifa itafanyika Jijini Dar es Salaam.

“Kwa mujibu wa hoja iliyotolewa bungeni na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mwigulu  Nchemba Juni 26, 2026, mkutano wa nne wa Bunge la  13 umepangwa kuanza siku ya Jumanne Agosti , 2026.”

“ Hata hivyo, kufuatia taarifa ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kuutangazia umma kuwa siku ya Jumanne Agosti  25 Agosti, 2026 itakuwa ni Sikukuu ya Maulid.”

“Mheshimiwa Spika kwa mamlaka yake chini ya Kanuni ya 35 (4) na (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2025 anapenda kuwataarifu Waheshimiwa wabunge na umma wote wa Tanzania, kuwa mkutano wa nne wa Bunge utaanza siku ya Jumatano Agosti 26, 2026 saa 3:00 asubuhi,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari leo Agosti 17, 2026, Katibu Mkuu wa Bakwata, Nuhu Mruma, amesema Maulid hayo yatasomwa usiku wa Agosti 24, katika Viwanja vya Mnazi Mmoja.

Wakati Baraza la Maulid litafanyika Jumanne Agosti 25, 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) na mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Agizo la Chalamila Stendi ya Magufuli lapingwa

Dar es Salaam. Abiria wameendelea kupinga uamuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, wa kutaka mabasi ya mikoani kuanzia na kumalizia safari katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, wakitaka suala hilo litazamwe upya kwa kuzingatia masilahi ya abiria, hususan wanaoishi mbali na Mbezi Luis.

Uamuzi huo umeibua kumbukumbu ya agizo kama hilo lililowahi kutolewa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, ambalo pia lilikumbana na malalamiko kutoka kwa wananchi na hatimaye kubadilishwa.

Makalla, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, alitoa agizo hilo Julai 2021, akitaka mabasi yanayoingia na kutoka Dar es Salaam kutumia Kituo cha Mabasi cha Magufuli kwa ajili ya kupakia na kushusha abiria. Agizo hilo lilitolewa wakati akisikiliza kero za wafanyabiashara katika kituo hicho, ambao walilalamikia baadhi ya mabasi kupakia na kushusha abiria nje ya kituo, hivyo kupunguza wateja katika eneo hilo.

Hata hivyo, agizo hilo lilikutana na upinzani kutoka kwa wananchi waliodai kuwa kulazimisha abiria wote kufika Mbezi Luis kungeongeza gharama na usumbufu, hasa kwa wanaotoka au kuelekea maeneo ya kusini na katikati ya jiji.

Malalamiko hayo yalihusu pia abiria waliokuwa wakishushwa Magufuli baada ya safari ndefu, kisha kulazimika kutafuta usafiri mwingine kwenda maeneo yao ya makazi ilihali baadhi ya mabasi yanayowashusha yanaelekea wanakokwenda.

Hoja hiyo ilifikia Serikali Kuu, ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi kwa wakati huo, Innocent Bashungwa, Agosti 30, 2022, alimtaka Makalla kukutana na wadau na wamiliki wa mabasi, ili kuweka utaratibu shirikishi usiowaongezea wananchi adha.

Bashungwa alisema wakati huo kuwa baadhi ya abiria wanaoingia Dar es Salaam kupitia Magufuli walihitaji mabasi hayo kuendelea hadi vituo vya mabasi vilivyojengwa na sekta binafsi mjini ili kuwafikisha karibu na maeneo yao.

Alisisitiza kuwa lengo la Serikali la kutumia Kituo cha Magufuli linaweza kutekelezwa bila kuwaongezea wananchi gharama za kutafuta usafiri mwingine baada ya kushushwa Mbezi Luis.

Baadaye, Makalla aliruhusu vituo binafsi vilivyohakikiwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kuendelea kutoa huduma, kwa sharti la mabasi kuingia na kutoka Kituo cha Magufuli.

Chalamila alitoa agizo hilo Agosti 11, 2026, akizitaka kampuni za mabasi zinazotoa huduma nje ya Kituo cha Mabasi cha Magufuli kuhamia kituoni hapo na kuanza kutoa huduma zake kutoka eneo hilo.

Mkuu huyo wa Mkoa alitoa muda wa siku sita kwa kampuni hizo kutekeleza agizo hilo, akisisitiza kuwa ifikapo leo, Agosti 17, 2026, mabasi yote ya masafa marefu yanapaswa kuwa yameondoka katika vituo vingine na kurejea Kituo cha Magufuli.

Gazeti hili lilifika katika maeneo yenye ofisi za kampuni mbalimbali za mabasi, ikiwamo Ubungo, Shekilango, Manzese, Argentina na Magomeni, na kubaini kuwa shughuli za usafirishaji wa abiria bado zinaendelea kama kawaida.

Baadhi ya abiria waliozungumza na gazeti hili walipinga agizo hilo, akiwamo Leonard Munisi aliyesema viongozi wanapotoa maamuzi wanapaswa kuzingatia mabadiliko ya maisha na mahitaji ya abiria, akisema miundombinu ya usafiri iliyopo inapaswa kutumika kwa manufaa ya abiria.

 “Kama suala ni mapato ya Kituo cha Magufuli, Serikali inaweza kuangalia namna ya kuongeza tozo kidogo kwa mabasi yanayopakia au kushusha abiria nje ya kituo hicho. Serikali isiangalie tu mapato, iangalie pia ubinadamu na namna ya kuwasogezea wananchi huduma karibu,” amesema.

Naye William Makali amesema agizo hilo linaweza kuwaongezea abiria usumbufu, ikiwamo kuvutwa mabegi na wapiga debe, kutapeliwa na hata kuibiwa wanapofika Magufuli kutafuta usafiri.

“Sisi tunaishauri Serikali iangalie changamoto zilizopo na kufanya uamuzi kwa masilahi mapana ya abiria ili vituo vilivyo nje ya Magufuli viendelee kufanya kazi kwa kuwa vina faida nyingi kuliko hasara,” amesema.

Kwa upande wake, Elly Mumbungu, mkazi wa Mbagala, amesema agizo hilo litawaumiza wananchi wa kipato cha kawaida, akisema mabasi yanayowafikisha maeneo ya Mbagala, Mbande, Kigamboni na Chanika yamekuwa yakirahisisha maisha yao.

“Sasa ukiniambia nishuke Mbezi, gharama ya kutoka huko hadi nyumbani nani atabeba? Maisha ni magumu,” amesema.

Baadhi ya wamiliki na wadau wa usafirishaji wa mabasi nchini wameitaka Serikali kulitazama kwa jicho la ziada agizo hilo, wakisema utekelezaji wake unaweza kuwaongezea changamoto abiria.

Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustapha Mwalongo, amesema baada ya Kamati Tendaji kukutana, wamekubaliana kuwasiliana na viongozi wa Serikali ili kujadiliana kuhusu agizo hilo.

“Hadi sasa bado tunaendelea kufanya jitihada za kwenda kuzungumza nao, na barua tayari zilishatumwa. Kwa hiyo, bado hatuna msimamo tulioufikia kuhusu jambo hilo zaidi ya kwenda kukubaliana kuongea na viongozi,” amesema.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi ya Tilisho, John Tilisho, amesema Serikali inapaswa kuwapa kipaumbele wamiliki ambao wamewekeza katika kujenga vituo na ofisi zao, ili wananchi wapate huduma karibu na maeneo wanayoishi.

Amesema kauli ya Chalamila, si mbaya, lakini ingekuwa vyema viongozi kutembelea vituo mbalimbali na kujionea changamoto zilizopo.

“Kwenda Mbezi ni jambo zuri, lakini kwa watu wanaosafiri kwenda mikoa ya Kaskazini itakuwa changamoto kwa sababu ya njia,” amesema.

Tilisho amesema barabara ya Goba ambayo baadhi ya mabasi yatapaswa kutumia ina changamoto kutokana na kuwa nyembamba na ina matuta mengi, hali ambayo inaweza kuongeza muda wa safari.

“Ukisema unatoka Stendi ya Magufuli kufika Moshi muda fulani, hicho kitu hakipo. Changamoto itakuwa kubwa,” amesema.

Amesema Serikali inaweza kushirikiana na wamiliki wa vituo binafsi kwa kuwawekea utaratibu wa kulipa tozo au ada zinazostahili badala ya kuwalazimisha kuhamia Magufuli.

Kwa upande wake, mmiliki wa Kampuni ya Mabasi ya Esther Luxury, Joseph Ngelleuya, amesema hawapingani na Serikali na watafuata maelekezo yatakayotolewa, akisema mwisho wa siku anayebeba athari za uamuzi huo ni abiria.

“Tukishapewa maelekezo ni kuyafuata. Hatuwezi kupingana na Serikali. Tunawasikiliza na kutenda wanalolitaka, kwa sababu katika suala hili mwathirika ni mwananchi,” amesema.

Mmiliki wa Kampuni ya Mabasi ya Shabiby, Ahmed Shabiby, amesema agizo la kuondoa vituo visivyo rasmi katikati ya Jiji linapaswa kuungwa mkono, lakini amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria na masilahi ya abiria.

Amesema Latra inaruhusu mtu mwenye sifa na kituo kilichokidhi vigezo kuendesha shughuli hizo, hivyo vituo vilivyoidhinishwa vinapaswa kuruhusiwa kufanya kazi.

“Watu wakipata kituo ambacho kimekubaliwa na Latra waachwe waegeshe,” amesema.

Hata hivyo, Shabiby amesema mabasi yote yanapaswa kupitia Kituo cha Magufuli ili kukaguliwa na Serikali kukusanya mapato.

Ametoa mfano wa Dodoma, ambako mabasi huanzia katika vituo vyao, lakini hulazimika kupitia stendi kuu kwa ajili ya ukaguzi na malipo ya ushuru.

Amesema utaratibu huo unaweza kuleta usawa kwa Serikali kupata mapato huku abiria wakiruhusiwa kuanzia safari zao katika vituo vilivyo karibu nao.

Naye msemaji wa Kampuni ya Kimbinyiko, Hamisi Maneno, ameunga mkono agizo la Chalamila, akisema uegeshaji wa mabasi katika maeneo yasiyo rasmi umeongeza msongamano na kuhatarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara.

Amesema suluhisho ni kuwa na vituo maalumu, huku akitaka mabasi yote yalazimishwe kupitia stendi kwa ajili ya ukaguzi na ulipaji wa ushuru.

Ametolea mfano eneo la Urafiki, akisema limekuwa likitumika kama eneo la maegesho kwa namna inayosababisha changamoto kwa watumiaji wengine, huku baadhi ya vituo vikikosa huduma muhimu kwa abiria.

Kaimu Meneja wa leseni Latra, Pateli Ngereza, amesema kwa Mkoa wa Dar es Salaam mabasi yote yanayotoka Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati, Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Ziwa  yanapaswa kuishia kituo cha mabasi kilichopo Mbezi Louis (yaani Magufuli Bus Terminal).

Huku yale mabasi yanayotoka Mikoa ya Kusini yakipaswa kuishia kituo cha mabasi Mbagala kilichopo Wilaya ya Temeke jijini humo.

Imeandikwa na Tuzo Mapunda, Nasra Abdallah, Habel Chidawali (Dodoma) na Janeth Joseph (Kilimanjaro)

TRA Songwe kuanzisha klabu za kodi shule za sekondari

Songwe. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Songwe imeanza mchakato wa kuanzisha klabu za kodi katika shule zote za sekondari mkoani humo, ikiwa ni mkakati wa kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu umuhimu wa kulipa kodi.

Klabu hizo zinalenga pia kuwawezesha wanafunzi kufahamu masuala ya kodi na kuyafikisha katika jamii, hususan umuhimu wa kudai na kutoa risiti wakati wa manunuzi na kufanya biashara.

Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Songwe, Angetile Kitalile, amesema hayo leo Jumatatu, Agosti 17, 2026, wakati wa uzinduzi wa klabu ya kodi katika Shule ya Sekondari Mlowo wilayani Mbozi.

Amesema hadi sasa mamlaka hiyo imefanikiwa kuanzisha klabu saba katika shule za sekondari mkoani humo na mpango ni kuzifikia shule zote katika halmashauri za mkoa huo.

“Mpaka sasa tumefanikiwa kufungua klabu saba za kodi katika shule za sekondari. Leo tumeifikia Shule ya Sekondari Mlowo iliyopo hapa Wilaya ya Mbozi, ikiwa ni mwendelezo wa mpango huu, tukiamini wanafunzi watasaidia kuifikisha elimu hiyo katika jamii wanayoishi,” amesema.

Kitalile amesema klabu hizo ni miongoni mwa njia zinazotumiwa na TRA kutoa elimu kwa walipa kodi wa sasa na kuwaandaa walipa kodi wa baadaye.

Amesema wanafunzi watakaopata elimu hiyo wataweza kuelewa wajibu wa kila mwananchi katika kulipa kodi na umuhimu wa kudai risiti wanaponunua bidhaa au kupata huduma.

Kwa mujibu wa Kitalile, elimu hiyo pia itasaidia kujenga utamaduni wa kufuata taratibu za kodi na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu mchango wa kodi katika maendeleo ya Taifa.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mlowo, Sophia Luoga, amepongeza hatua hiyo akisema itawajengea wanafunzi uzalendo na kuwafanya kuwa mabalozi wazuri wa masuala ya kodi katika familia na jamii.

Amesema matarajio yao ni kuona elimu inayotolewa kupitia klabu hizo ikisaidia kizazi cha sasa na kijacho kuelewa wajibu wa kulipa kodi wakati wa kununua au kuuza bidhaa.

“Wanafunzi wataelewa kuwa kila Mtanzania ana wajibu wa kulipa kodi na kwamba wakati wa kununua bidhaa au kufanya biashara, ni muhimu kutoa na kudai risiti ili Taifa lipate mapato ya kuendeleza miradi ya maendeleo,” amesema.

Baadhi ya wanafunzi walioshiriki kuanzishwa kwa klabu hiyo wamesema mpango huo utawasaidia kupata uelewa zaidi kuhusu masuala ya kodi, ikiwamo umuhimu wa kudai na kutoa risiti sahihi wanaponunua bidhaa au kufanya biashara.

Wamesema watatumia elimu watakayoipata kuwafikishia wazazi, ndugu na wananchi wengine ili kuongeza uelewa kuhusu ulipaji kodi na mchango wake katika maendeleo ya Taifa.

GLOBAL EDUCATION LINK YAPELEKA WANAFUNZI 198 CHINA NA 189 INDIA

 

 

Na Matukio Daima Media , Dar es Salaam

GLOBAL Education Link (GEL) imewakabidhi nyaraka rasmi za safari wanafunzi 387 wa Kitanzania wanaotarajia kwenda kuendelea na masomo ya elimu ya juu nchini China na India, huku wakihimizwa kutumia fursa hiyo kupata zaidi ya shahada kwa kujenga maarifa, ujuzi, teknolojia, mitandao ya kimataifa na uwezo wa kujitengenezea fursa za maisha.

Ukabidhi huo umefanyika kupitia mikutano miwili maalumu iliyofanyika Agosti 10 na 11, 2026 katika Ukumbi Mkuu wa Makao Makuu ya Global Education Link, Dar es Salaam, na kuhudhuriwa pia na wazazi na walezi wa wanafunzi hao.

Kati ya wanafunzi hao, 198 wanaelekea nchini China na 189 wanaelekea nchini India kwa ajili ya kuanza masomo katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu.

Wazazi na walezi waliohudhuria mikutano hiyo kwa ajili ya kushuhudia ukabidhi wa nyaraka na kupata maelekezo kuhusu safari na maisha ya watoto wao watakapokuwa nje ya nchi.

Lengo kuu la mikutano hiyo lilikuwa kuwakabidhi wanafunzi nyaraka muhimu za safari ambazo zimekamilishwa na GEL kama sehemu ya huduma inayofanywa nataasisi hiyo  katika hatua mbalimbali za maandalizi yao, zikiwemo pasipoti, visa, tiketi za ndege, NOC (No Objection Certificate), cheti au kijitabu cha chanjo ya homa ya manjano (Yellow Fever Certificate) pamoja na nyaraka nyingine zinazohitajika na mamlaka husika kulingana na nchi, chuo na masharti ya safari ya mwanafunzi katika chuo husika.

Mbali na kukabidhiwa nyaraka hizo, wanafunzi pamoja na wazazi na walezi wao walipata maelekezo ya mwisho kuhusu taratibu za safari, uhamiaji, mazingira ya vyuo, makazi, bima ya afya, usalama, matumizi ya fedha, nidhamu na namna ya kukabiliana na mazingira mapya watakapofika katika nchi wanazokwenda.

Mtoa mada mkuu katika mikutano hiyo alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Bw. Abdulmalik Mollel, akishirikiana na wawakilishi wa vyuo kutoka China na India waliotoa ufafanuzi kuhusu masomo, huduma za vyuo na maisha ya mwanafunzi wa kimataifa.

Global Education Link ni wakala wa vyuo vikuu vya nje ya nchi mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 19 katika kusaidia wanafunzi wa Kitanzania pamoja na wazazi na walezi wenye watoto wenye ndoto ya kupata elimu ya juu nje ya nchi.

Katika kipindi hicho, taasisi hiyo imekuwa ikitoa mwongozo katika hatua mbalimbali kuanzia ushauri wa kielimu, uchaguzi wa programu na chuo, maombi ya udahili, maandalizi ya nyaraka, visa, safari na maandalizi ya mwanafunzi kabla ya kuondoka nchini.

Akizungumza katika mikutano hiyo, Mollel aliwataka wanafunzi kutokwenda China na India kwa lengo la kupata cheti au shahada pekee, bali kutumia mazingira ya vyuo watakavyosoma kujenga uwezo mpana utakaowasaidia baada ya kuhitimu.

Alisema kwenda kusoma nje ya nchi kunamfungulia mwanafunzi mazingira mapya yenye teknolojia, maabara, warsha, vituo vya ubunifu, wataalamu pamoja na wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali, hivyo ni jukumu la mwanafunzi mwenyewe kutumia fursa hizo kwa manufaa yake na Taifa.

Aliwataka vijana hao kwenda zaidi ya masomo yao ya darasani kwa kutembelea maabara, warsha na vituo vya ubunifu na kujifunza kwa vitendo namna teknolojia na bidhaa mbalimbali zinavyozalishwa na kutumika katika kutatua changamoto za jamii.

Akitolea mfano mwanafunzi anayesomea Business Administration, alisema haipaswi kutosha kujifunza nadharia za usimamizi wa biashara pekee, bali mwanafunzi huyo anapaswa kutafuta maarifa kuhusu bidhaa, teknolojia, uzalishaji na mifumo mbalimbali ya viwanda ili aweze kuelewa kile anachoweza kukisimamia au kukigeuza kuwa biashara

16 mbaroni kwa tuhuma za kuchoma moto shamba, matrekta ya mwekezaji

Babati. Wakazi 16 wa Kijiji cha Kiru, wilayani Babati, Mkoa wa Manyara, wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuvamia eneo la mwekezaji wa Dudumera Estate na kuchoma moto shamba pamoja na matrekta matatu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani, amethibitisha kushikiliwa kwa watu hao na kusema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati leo Jumatatu, Agosti 17, 2026, Makarani amesema tukio hilo lilitokea Agosti 15, 2026, katika Kijiji cha Kiru.

“Tunaendelea kuwashikilia watu 16 kwa tuhuma hizo na uchunguzi ukikamilika, hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa,” amesema kamanda huyo.

Baadhi ya wajumbe wa kamati ya usalama ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara, wakikagua maeneo ya kampuni ya Dudumera Estate yaliyochomwa moto na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kiru wilayani Babati mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo

Amesema watuhumiwa hao wanadaiwa kushiriki kuchoma mali mbalimbali, zikiwamo shamba na matrekta matatu.

Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Babati, ikiongozwa na katibu tawala wa wilaya hiyo, Thobias Abwaro, leo imefika eneo la tukio na kujionea madhara yaliyosababishwa na moto huo.

Hata hivyo, Abwaro amelipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua ya kuwakamata watu hao huku akisema Serikali inaendelea kuchukua hatua nyingine zaidi kuhusu tukio hilo.

“Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Agosti 15, 2026, baada ya kundi la watu kudaiwa kuvamia eneo la mwekezaji huyo na kuchoma moto shamba lenye ukubwa wa takribani hekta 15,” amesema na kuongeza kuwa shamba hilo lilikuwa likilimwa miwa na mtama.

Kwa mujibu wa Abwaro, chanzo kinachodaiwa kusababisha tukio hilo ni mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu kati ya wananchi wa eneo hilo na mwekezaji, licha ya jitihada za viongozi wa Serikali za kutafuta suluhisho kufanyika.

Mwekezaji wa Dudumera Estate, Radhika Jeta, amesema tukio hilo limemsababishia hasara kubwa kutokana na uharibifu wa mali na kuvurugika kwa shughuli za uzalishaji shambani.

Amesema matrekta matatu yameteketea pamoja na mashamba yaliyokuwa yamepandwa miwa na mtama.

“Nimesikitishwa na tukio hilo la uchomaji moto, kwani mara nyingi tumekuwa tukishirikiana na wananchi na viongozi wa eneo hili. Mimi huwa nashiriki kutoa michango mbalimbali ya maendeleo,” amesema Jeta.

Akizungumzia tukio hilo, mlinzi wa eneo hilo, Hussein Twabatari, amesema usiku wa tukio alishtushwa na kundi la watu waliobeba silaha za jadi lililovamia eneo hilo.

Amesema alihofia usalama wake kutokana na namna uvamizi huo ulivyofanyika.

Wakati huohuo, tukio hilo limeathiri pia huduma ya umeme katika baadhi ya maeneo ya Tarafa ya Mbugwe.

Ofisa Uhusiano wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Manyara, Samuel Mandari, amesema watu wasiojulikana walichoma nguzo ya umeme na kusababisha baadhi ya maeneo kukosa huduma hiyo.

“Watu wasiojulikana wamechoma nguzo ya Tanesco na tukio hilo limesababisha hasara kwa shirika, na wakazi wa maeneo ya Magugu na jirani wamekosa huduma ya umeme,” amesema Mandari.Akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati leo Jumatatu Agosti 17, 2026, Makarani amesema tukio hilo lilitokea Agosti 15, 2026 katika Kijiji cha Kiru.

Shamba la miwa la kampuni ya Dudumera Estate lililochomwa moto na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kiru wilayani Babati mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo

“Tunaendeleo kuwashikilia watu 16 kwa tuhuma hizo na uchunguzi ukikamilika hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa,” amesema kamanda huyo.

Amesema watuhumiwa hao wanadaiwa kushiriki kuchoma mali mbalimbali, zikiwamo shamba na matrekta matatu.

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Babati, ikiongozwa na Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Thobias Abwaro, leo imefika eneo la tukio na kujionea madhara yaliyosababishwa na moto huo.

Hata hivyo, Abwaro amelipongeza Jeshi la Polisi  kwa hatua ya kuwakamata watu hao huku akisema Serikali inaendelea kuchukua hatua nyingine zaidi kuhusu tukio hilo.

“Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Agosti 15, 2026 baada ya kundi la watu kudaiwa kuvamia eneo la mwekezaji huyo na kuchoma moto shamba lenye ukubwa wa takribani hekta 15,” amesema na kuongeza kuwa shamba hilo lilikuwa likilimwa miwa na mtama.

Kwa mujibu wa Abwaro, chanzo kinachodaiwa kusababisha tukio hilo ni mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu kati ya wananchi wa eneo hilo na mwekezaji, licha ya jitihada za viongozi wa Serikali za kutafuta suluhisho kufanyika.

Mwekezaji wa Dudumera Estate, Radhika Jeta amesema tukio hilo limemsababishia hasara kubwa kutokana na uharibifu wa mali na kuvurugika kwa shughuli za uzalishaji shambani.

Matrekta ya kampuni ya Dudumera Estate yaliyochomwa na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kiru wilayani Babati mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo

Amesema matrekta matatu yameteketea pamoja na mashamba yaliyokuwa yamepandwa miwa na mtama.

“Nimesikitishwa na tukio hilo la uchomaji moto kwani mara nyingi tumekuwa tukishirikiana na wananchi na viongozi wa eneo hili, mimi huwa nashiriki kutoa michango mbalimbali ya maendeleo,” amesema Jeta.

Alizungumzia tukio hilo, mlinzi wa eneo hilo, Hussein Twabatari amesema usiku wa tukio alishtushwa na kundi la watu waliobeba silaha za jadi lililovamia eneo hilo.

Amesema alihofia usalama wake kutokana na namna uvamizi huo ulivyofanyika.

Wakati huohuo, tukio hilo limeathiri pia huduma ya umeme katika baadhi ya maeneo ya Tarafa ya Mbugwe.

Ofisa Uhusiano wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Manyara, Samuel Mandari amesema watu wasiojulikana walichoma nguzo ya umeme na kusababisha baadhi ya maeneo kukosa huduma hiyo.

“Watu wasiojulikana wamechoma nguzo ya Tanesco na tukio hilo limesababisha hasara kwa shirika na wakazi wa maeneo ya Magugu na jirani wamekosa huduma ya umeme,” amesema Mandari.

UBORA WA SHULE ZA ST DOMINIC SAVIO ,WAPONGEZWA NA WAZAZI

NA MATUKIO DAIMA MEDIA

IRINGA

WAZAZI wa wanafunzi wanaosoma katika Shule za St. Dominic Savio mkoani Iringa wamepongeza uongozi wa shule hizo kwa kuandaa ziara za kielimu zinazowawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo na kuongeza uelewa nje ya mazingira ya darasa.

Wazazi hao wamesema ziara hizo ni sehemu muhimu ya elimu, kwa kuwa zinawapa wanafunzi fursa ya kujionea na kuelewa kwa vitendo mambo wanayofundishwa darasani, ikiwemo historia, utamaduni na uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi wengine, Shukuru Mpelele, mkazi wa Zanzibar, amepongeza juhudi za shule hiyo za kuwapeleka wanafunzi kutembelea maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuongeza maarifa na ujuzi.

“Wazazi tuna wajibu wa kuendelea kushirikiana na walimu katika kugharamia na kuunga mkono programu za kielimu kama hizi, kwa kuwa manufaa yake kwa watoto ni makubwa na yanaweza kuwasaidia katika maisha yao ya baadaye,” alisema Shukuru.

Alisema fursa hizo zikienziwa na kuendelea kutolewa, wanafunzi wengi zaidi wataweza kujifunza mambo mbalimbali yanayoongeza maarifa na kuwaandaa kukabiliana na changamoto za maisha ya baadaye.

Aidha, Shukuru ameipongeza St. Dominic Savio kwa kuweka mazingira rafiki ya kujifunzia, kusimamia nidhamu na kuwa na walimu wanaowasimamia wanafunzi kwa karibu, akisema mambo hayo yanachangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi kufanya vizuri kitaaluma.

Ziara hiyo imewashirikisha jumla ya wanafunzi 117 pamoja na walimu saba kutoka Shule ya St. Dominic Savio ya mkoani Iringa, ambao wameelekea Zanzibar kwa ziara ya kielimu yenye lengo la kuwapa wanafunzi fursa ya kujifunza kwa vitendo.

Wakati wa ziara hiyo, wanafunzi wanatarajiwa kutembelea maeneo mbalimbali yenye umuhimu wa kihistoria, kiutamaduni na kimazingira, huku wakipata fursa ya kujifunza moja kwa moja kutoka katika mazingira wanayoyatembelea.TAZAMA MAHOJIANO YOTE BOFYA LINK HII

Akizungumza na Matukio Daima, Mratibu wa Shule za St. Dominic, Mussa Myula, alisema ziara hiyo imehusisha makundi ya wanafunzi yanayoongozwa na walimu wao katika maeneo mbalimbali yaliyopangwa kwa ajili ya kujifunza.

Myula alisema miongoni mwa maeneo yatakayotembelewa ni misitu ya Zanzibar, ambapo wanafunzi watapata fursa ya kujifunza kuhusu mazingira, uhifadhi wa misitu na umuhimu wa rasilimali hizo katika maisha ya jamii.

“Ziara hii pia inalenga kuwafanya wanafunzi wajifunze historia ya Zanzibar kwa kujionea wenyewe maeneo mbalimbali ambayo wamekuwa wakiyasoma katika vitabu na masomo ya darasani,” alisema.

Alisema elimu ya darasani pekee haitoshi, hivyo wanafunzi wanapopewa nafasi ya kutembelea maeneo wanayojifunza, huwa rahisi kuelewa zaidi kile wanachofundishwa na kupata maarifa kupitia uzoefu wa moja kwa moja.

Kwa mujibu wa Myula, wanafunzi hao pia wanatarajiwa kukutana na viongozi pamoja na wawakilishi wa makundi mbalimbali ya vijana Zanzibar, hatua ambayo itawapa fursa ya kujifunza namna vijana wanavyoshiriki katika shughuli za kijamii na maendeleo katika maeneo yao.

“Lengo kubwa la Shule ya St. Dominic katika kuandaa ziara kama hizi ni kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujifunza mazingira mapya, kufahamu historia na tamaduni za maeneo mbalimbali, pamoja na kupata ujuzi ambao unaweza kuwasaidia katika maisha yao ya baadaye,” alisema Myula.

Aliongeza kuwa shule itaendelea kuwapa wanafunzi fursa za kutembelea maeneo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania, akisisitiza kuwa ziara za kielimu ni sehemu muhimu ya kuwasaidia watoto kupanua uelewa, kujifunza kwa vitendo na kutambua fursa mbalimbali zilizopo katika jamii.

KUJIUNGA NA SHULE ZETU TAZAMA HABA CHINI ⬇️⬇️

TANGAZO LA ST DOMINIC BOFYA HAPA

FEASSA 2026 KUFANYIKA MOROGORO, WANAFUNZI 6,800 KUSHIRIKI MASHINDANO

Na Lilian Kasenene, Morogoro

Matukio DaimaApp

JUMLA ya wanafunzi takribani 6,800 kutoka nchi za Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda na wenyeji Tanzania wanatarajiwa kushiriki Mashindano ya Michezo ya Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSA) 2026, yanayotarajiwa kufanyika katika Mkoa wa Morogoro.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, wakati akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 12 hadi 23, 2026, katika Manispaa ya Morogoro.

Kwa upande wa Tanzania, jumla ya wanafunzi 1,510 kutoka mikoa 26 wanatarajiwa kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo, hali ambayo inaweka rekodi ya idadi kubwa ya ushiriki wa Tanzania katika historia ya mashindano ya FEASSA.

Mashindano hayo yanafanyika kwa mara ya 23 katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku Tanzania ikiwa mwenyeji kwa mara ya tano, na ni mara ya kwanza kwa Mkoa wa Morogoro kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, FEASSA ni mashindano makubwa ya michezo kwa wanafunzi katika ukanda wa Afrika Mashariki, yenye lengo la kukuza vipaji vya vijana katika michezo, wakiwemo wanafunzi wenye mahitaji maalum na wasio na mahitaji maalum.

Aidha, mashindano hayo yana nafasi muhimu katika kujenga umoja, mshikamano, urafiki na mahusiano mema miongoni mwa vijana wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Katika mashindano hayo, jumla ya michezo 20 itashindaniwa kwa upande wa shule za sekondari, michezo sita (6) kwa shule za msingi, pamoja na michezo minne (4) kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Mkoa wa Morogoro umejipanga kikamilifu kuhakikisha unakuwa mwenyeji bora wa mashindano hayo, ambapo jumla ya viwanja 21 ndani ya Manispaa ya Morogoro vitatumika katika mashindano hayo.

Aidha, maeneo manane (8) yametengwa kwa ajili ya malazi ya wanafunzi watakaoshiriki mashindano hayo.

Mkuu wa Mkoa amesema maandalizi yamezingatia maeneo muhimu ikiwemo usalama, afya, usafi wa mazingira, usafiri, chakula, malazi na huduma nyingine muhimu, huku Serikali kupitia Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiendelea kuhakikisha kila eneo linakuwa tayari kabla na wakati wa mashindano.

Mashindano ya FEASSA 2026 yanatarajiwa kuwa zaidi ya tukio la michezo, kwani yanatoa fursa kubwa kwa wananchi wa Morogoro kunufaika kiuchumi, kiutalii na kiutamaduni.

Kuwapo kwa maelfu ya wanafunzi, walimu, viongozi, waamuzi na wageni kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki kunatarajiwa kuongeza shughuli za kiuchumi kwa wafanyabiashara na watoa huduma katika sekta za usafiri, chakula, malazi, bidhaa mbalimbali na huduma nyingine.

Aidha, wageni watapata fursa ya kuifahamu zaidi Morogoro, ikiwemo vivutio vyake vya utalii, pamoja na utamaduni na ukarimu wa wananchi wa Mkoa huo.

Mashindano hayo pia yanatarajiwa kutoa fursa ya mabadilishano ya kiutamaduni miongoni mwa vijana kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki, hatua ambayo itasaidia kuimarisha uhusiano na mshikamano wa kikanda.

Mashindano ya FEASSA 2026 yataanza rasmi Agosti 12, 2026, huku hafla ya ufunguzi rasmi ikitarajiwa kufanyika Agosti 16, 2026.

Mgeni Rasmi katika hafla hiyo anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Mwigulu Nchemba.

Mashindano hayo yatahitimishwa Agosti 23, 2026, yakitarajiwa kuwakutanisha vijana kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki katika michezo, kujenga urafiki na kuimarisha mshikamano wa kikanda.

MWISHO

Vijana wa Mwanjelwa walivyogeuza kucha, rangi kuwa dili

Mbeya. Soko la Mwanjelwa lililopo jijini Mbeya ni miongoni mwa masoko yanayowakutanisha wafanyabiashara wa bidhaa na huduma mbalimbali, lakini ndani yake kuna kundi la vijana lililogeuza upakaji rangi na ubandikaji kucha kuwa chanzo cha kipato.

Kwa vijana hao, kazi hiyo imekuwa fursa ya kujitafutia kipato halali na kujikwamua kiuchumi, huku wakikabiliana na changamoto mbalimbali, ikiwamo vishawishi kutoka kwa baadhi ya wateja na mazingira ya kazi.

Kwa nyakati tofauti, Mwananchi imefika sokoni hapo na kuzungumza na baadhi yao kuhusu kazi hiyo na maisha yao kwa ujumla.

Twabi Mawea, mkazi wa Tunduru mkoani Ruvuma, anasema tangu alipowasili Mbeya miaka miwili iliyopita, kazi hiyo imekuwa mkombozi kwake.

Anasema aliacha masomo ya sekondari kutokana na changamoto za maisha na kuamua kujikita katika shughuli hiyo.

“Kwa siku naingiza takriban Sh50,000, kutegemea aina ya huduma anayohitaji mteja. Kiwango cha chini ni Sh28,000 kwa mtu mmoja. Sijutii kazi hii, imenipa heshima kifamilia,” anasema.

Rafael Jackson, mkazi wa Ikuti anayefanya kazi hiyo kwa mwaka mmoja sasa, anasema imebadilisha maisha yake ikilinganishwa na alipokuwa akiendesha bodaboda.

“Nina uhakika wa mahitaji muhimu ya familia. Kwa siku naweza kuondoka na Sh60,000 baada ya kugawana na bosi wangu, ingawa wakati mwingine kipato huongezeka kulingana na mzunguko,” anasema.

Kijana mwingine, Erick Samuel, anasema kazi hiyo imemwezesha kufungua kituo cha uwakala wa fedha na hana mpango wa kuacha kwa kuwa anaona fursa kubwa ya kujikwamua.

Anasema kazi hiyo haihitaji elimu kubwa na inafanywa na watu wenye viwango tofauti vya elimu.

Hata hivyo, vijana hao wanasema baadhi ya wateja huleta changamoto, hasa wanapohitaji huduma nyumbani.

Mawea anasema wakati mwingine mavazi na mienendo ya baadhi ya wateja huwaweka katika mazingira magumu.

“Tunakutana na vishawishi vingi. Mteja anakuita nyumbani kwake, lakini mazingira unayokutana nayo yanaweza kukupa ugumu. Kwa kuwa tumeamua kutafuta riziki kupitia kazi hii, tunavumilia,” anasema.

Jackson anasema kwa kuwa sehemu kubwa ya wateja wao ni wanawake, baadhi ya mazingira wanayokutana nayo yanahitaji umakini mkubwa.

Vijana hao pia wanasema wanachukua tahadhari dhidi ya maambukizi kwa kutumia barakoa na glovu, hasa wanapokutana na wateja wenye michubuko.

Samuel anasema pia huwa makini na vumbi linalotokana na kucha bandia pamoja na harufu ya rangi wanazotumia.

“Tunashika miili ya watu tofauti na wengine huwa na michubuko. Pia hatujui madhara ya baadhi ya rangi tunazotumia, hivyo tunashauriwa kuvaa barakoa na glovu,” anasema.

Akizungumzia suala la mitaji, Mawea anasema licha ya kipato wanachopata, bado wanakabiliwa na changamoto ya mitaji na hawakuwa na taarifa za kutosha kuhusu mikopo inayotolewa na Serikali kupitia halmashauri.

“Bado hatujawahi kuomba mikopo kwa sababu hatukujua mapema. Sasa tutashirikiana na wenzangu kuomba. Hii ni kazi halali na tunalipa kodi, tatizo ni mtaji tu,” anasema.

Emmy Casian, mteja wa huduma hizo, anasema vijana hao wanafanya kazi muhimu inayosaidia kuwabadilisha wateja mwonekano.

Happy Sanga anasema baadhi ya wateja wanapaswa kuepuka kuingiza masuala binafsi wakati wa kupata huduma kwa kuwa hali hiyo inaweza kuwaathiri wahudumu.

Mbunge wa Mbeya Mjini, Patrick Mwalunenge, anasema atatembelea makundi mbalimbali ya wajasiriamali, likiwamo kundi hilo, kusikiliza changamoto zao na kutafuta namna ya kuboresha mazingira ya biashara.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Mkuu wa Kitengo cha Maliasili, Utalii na Hifadhi ya Mazingira, Anamary Joseph, anasema Serikali imetenga asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya mikopo kwa vijana, wanawake na makundi maalumu.

Anasema kikundi cha watu kuanzia watano kinaweza kukopa hadi Sh150 milioni kwa ajili ya shughuli za kiuchumi, hivyo kuwataka vijana kutumia fursa hiyo.

MAGAZETINI LEO JUMATANO AGOSTI 12/2026:TANZANIA NA MAREKANI KUENDELEA KUSHIRIKIANA,RC KHERI APONGEZA UWEKEZAJI HOTELI YA GOLDEN GLOW ..


















MAGAZETINI LEO JUMATANO AGOSTI 12/2026:TANZANIA NA MAREKANI KUENDELEA KUSHIRIKIANA,RC KHERI APONGEZA UWEKEZAJI HOTELI YA GOLDEN GLOW .. – Matukio Daima Habari










GIZ YAAHIDI KUTOA EURO MILIONI 39.8 KWA AJILI YA KUIMARISHA BIASHARA YA KIKANDA.

Na,Jusline Marco;Arusha

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jamhuri ya Shirikisho ya Ujerumani zimethibitisha upya nia yao ya kuendeleza ushirikiano wa kikanda kufuatia kuhitimishwa kwa majadiliano ya 

Ushirikiano wa Maendeleo, huku Ujerumani ikiahidi kutoa ruzuku mpya ya Euro milioni 39.8 kwa ajili ya kuimarisha biashara ya kikanda na ushirikiano wa kiuchumi katika eneo hilo.

Akizungumza wakati wa mkutano wa pande mbili na ujumbe huo wa kusaini makubaliano ya fedha hizo, Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Balozi Stephen P.  Mbundi ameushukuru uongozi wa Jamhuri ya Shirikisho ya Ujerumani kwa kuwa mshirika wa muda mrefu wa EAC, huku akibainisha kuwa ushirikiano endelevu wa nchi hiyo umechangia kwa kiasi kikubwa katika safari ya Jumuiya hiyo ya ushirikiano wa kikanda.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia Masuala ya Forodha, Biashara na Fedha, Bi. Annette Ssemuwemba, mbali na kuushukuru ujumbe huo kwa dhamira yao ya kuiunga mkono Jumuiya hiyo, alibainisha kuwa mazungumzo hayo yalifanyika wakati mwafaka ambapo EAC inaanzisha utekelezaji wa Mkakati wake wa 7 wa Maendeleo.

” Tunaishukuru Ujerumani kwa kukaa nasi mezani ili kupitia upya vipaumbele vyetu na kubainisha maeneo ambayo tunaweza kushirikiana ili kupata matokeo, hii ndiyo roho ya ushirikiano na uwajibikaji wa pamoja ambayo ni muhimu katika kufikia malengo ya ajenda yetu ya ushirikiano wa kikanda,” alisema Bi. Ssemuwemba.

Mazungumzo hayo yalilenga katika kuunga mkono Mkakati wa 7 wa Maendeleo wa EAC, wakati wa majadiliano hayo, Ujerumani na EAC zilikubaliana kuwa jukumu kuu ni kuendeleza zaidi Biashara ya Afrika Mashariki na ushirikiano wa kiuchumi wa kanda hiyo ambapo Ujerumani imeahidi kutoa ruzuku ya euro milioni 39.8 kwa ajili ya lengo hili.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Afrika Mashariki na Kati katika Wizara ya Shirikisho ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (BMZ), Joachim Schmitt, akizungumza alisema kuwa “Afrika Mashariki ndiyo kanda inayokua kwa kasi zaidi, ikishuhudia ongezeko la asilimia 14 katika biashara ya ndani ya EAC, pamoja na kukua kwa kiasi cha biashara ndani ya AfCFTA na nje ya bara hilo, amesema kanda hiyo ni kitovu cha kuvutia  uwekezaji kwa sekta binafsi ya Ujerumani na Ulaya inayopenda kujihusisha na biashara na uendelezaji wa mnyororo wa thamani.

Aliongeza kuwa kupitia ushirikiano huo wamelenga kuunga mkono ushirikiano wa kibiashara unaozingatia kanuni na sheria, maendeleo ya kiuchumi ya kikanda, pamoja na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi ambapo fedha zilizotengwa zitalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa biashara ndogo ndogo na za kati katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupitia ushirikiano kati ya benki ya maendeleo ya Ujerumani na Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki huku sehemu ya fedha hizo zitaboresha upatikanaji wa fedha kwa biashara hizo kupitia ushirikiano kati ya  Benki hizo.

Sambamba na hayo washirika wote wawili walisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu na uratibu na asasi za kiraia, sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kuimarisha ushirikiano wa kikanda ambapo Ujerumani itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Umoja wa Ulaya pamoja na nchi zote wanachama zinazoshiriki, ili kusaidia mipango ya kikanda katika nyanja za biashara, mabadiliko ya kidijitali, afya, usimamizi wa maji ya mipakani, asasi za kiraia na maendeleo endelevu ya kiuchumi.

Aliongeza kuwa katika mgao wa fedha hizo,  kiasi cha Euro milioni 4.8 kimetengwa kama msaada wa ziada ili kukabiliana na mlipuko wa Ebola unaoendelea ambapo fedha hizi zitaelekezwa kwenye hatua za moja kwa moja za kujiandaa, kuzuia na kukabiliana na Ebola, pamoja na kuimarisha kwa ujumla uwezo na uratibu wa kikanda, shughuli hizo ambazo zitatekelezwa kupitia mradi wa EAC/GIZ unaoitwa “Support to Pandemic Preparedness in the EAC Region” (PanPrep), ambao umekuwa ukilisaidia eneo hilo tangu mwaka 2017.

Rasilimali hizo za ziada zitagharamia hatua mahususi za kukabiliana na Ebola, ikiwa ni pamoja na mafunzo ya kivitendo ya kuzuia na kudhibiti maambukizi (IPC) kwa wahudumu wa afya walio mstari wa mbele, ununuzi na usambazaji wa vifaa maalum vya kujikinga (PPE) dhidi ya Ebola, kuimarisha utayari wa kikanuni ili kuharakisha upatikanaji wa chanjo zinazoweza kutumika dhidi ya Ebola, dawa na hatua nyingine za kimatibabu, pamoja na shughuli za kuielimisha jamii ili kupunguza kusita kupokea chanjo na kuunga mkono kampeni zijazo za chanjo dhidi ya Ebola.

Alibainisha kuwa hatua zote zitatekelezwa kwa ushirikiano wa karibu na Sekretarieti ya EAC pamoja na nchi husika wanachama, na zitaendana na Mpango wa Bara wa Kujiandaa na Kukabiliana na Ebola unaoongozwa na Africa CDC na WHO, ili kuhakikisha kunakuwa na ufanisi unaokamilisha juhudi za kikanda na kimataifa za kukabiliana na janga hilo.