Mr. Cheeks wa Lost Boyz Kutua Arusha Septemba 19, Miaka 30 Ya Bongo Flava

Global Publishers
August 31, 2026
36 views
0 Comments

ARUSHA — Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Flava imethibitisha ujio wa rapa mkongwe kutoka nchini Marekani, Mr. Cheeks, ambaye anatarajiwa kutumbuiza katika tamasha hilo litakalofanyika jijini Arusha Septemba 19, 2026.

Mr. Cheeks, ambaye ni mwanachama wa kundi maarufu la Hip Hop duniani, Lost Boyz, anatarajiwa kuwasili nchini kwa ajili ya kushiriki katika tamasha hilo linalolenga kuadhimisha safari ya miaka 30 ya muziki wa Bongo Flava.

Ujio wa rapa huyo unatatajwa kuwa sehemu muhimu ya historia ya muziki kati ya Tanzania na Marekani, kutokana na uhusiano wa muda mrefu wa kundi la Lost Boyz na mashabiki wa muziki nchini.

Kundi hilo lilifanya historia mwaka 1998 baada ya kuwa miongoni mwa makundi ya kwanza ya Hip Hop kutoka Marekani kutumbuiza nchini Tanzania, tukio lililofungua ukurasa mpya katika mahusiano ya muziki kati ya wasanii wa Tanzania na Marekani.

Baada ya miaka 28, ujio wa Mr. Cheeks nchini unatarajiwa kuhuisha kumbukumbu hiyo huku akijiandaa kupanda jukwaani Arusha katika tamasha maalum la kuadhimisha miaka 30 ya Bongo Flava.

Tamasha hilo linatarajiwa kukutanisha wasanii na wadau mbalimbali wa muziki, likiwa sehemu ya kusherehekea safari, maendeleo na mchango wa Bongo Flava katika tasnia ya muziki Tanzania na kimataifa.

STORI NA GABBY MTANZANIA | GPL