Unguja. Rais Samia Suluhu Hassan amefunga Tamasha la Kizimkazi akiwataka viongozi kuhakikisha fursa zinazozalishwa au kuibuliwa ndani ya tamasha hilo zinawagusa wananchi.
Amesema kutokana na tamasha hilo, Wilaya ya Kusini imechangamka, imefurahi, imekuwa na biashara na imepata fursa ilizokusudia katika kuboresha maisha na ustawi wa wananchi.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo, Agosti 14, 2026, wakati akihitimisha tamasha hilo katika Uwanja wa Mwehe, Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja.
“Tunaziunga mkono na kuzichochea kwa wananchi wetu, kama Rais wa Zanzibar (Dk Hussein Mwinyi) alivyoahidi. Kwa hiyo, shangwe iwe lango la fursa, na fursa hizo ziwe chanzo cha ustawi wa wananchi wetu na taifa kwa ujumla,” amesema Dk Samia.
Amesema miradi yote iliyozinduliwa au kujengwa kupitia tamasha hilo, ndiyo malengo hasa ya kuanzishwa kwa tamasha hilo.
“Mnakubaliana nami nyote mlioshiriki tamasha hili, mmeona ukweli huu kwamba Kizimkazi na Wilaya ya Kusini kwa ujumla ilinoga,” amesema.
Amesema baada ya shangwe hilo kumalizika, wananchi wabaki na huduma, miundombinu, biashara na fursa zinazoendelea kufanya kazi, huku akipongeza kaulimbiu ya mwaka huu akisema imetendewa haki.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi katika Kilele cha Tamasha la Kizimkazi (Kizimkazi Festival) lililofanyika, Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar Agosti 14, 2026.
“Kaulimbiu ya mwaka huu inasema ‘Kizimkazi kumenoga, shangwe na fursa’. Asanteni sana mlioshiriki kuileta shangwe hiyo Kizimkazi na maeneo ya jirani, na hatimaye fursa kuibuka,” amesema.
Rais Samia amesema Wilaya ya Kusini ya leo imebadilika, siyo kama ilivyokuwa miaka 10 au 15 iliyopita, tofauti na mwaka 2016 walipoanza tamasha hilo, ambapo Kizimkazi imekuwa na fursa nyingi za biashara na uwekezaji.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, miundombinu na miradi wanayoijenga imeendelea kuvutia wananchi na wawekezaji kuja kufanya shughuli zao katika eneo hilo.
“Nawaomba wale wote walioziona fursa ndani ya wilaya hii, waje kwa uwekezaji, tunawakaribisha. Rais wa Zanzibar ameweka mazingira mazuri sana ya uwekezaji. Karibuni sana kuja kuwekeza,” amesema Samia.
Katika kutengeneza fursa, Rais Samia amesema wanajenga uwanja wa michezo ambao ukikamilika utaweza kutumika katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) itakayofanyika Juni 2027.
Amesema: “Uwanja huo ni fursa kwenu wawekezaji kuja kuwekeza kwa ajili ya huduma zitakazotolewa kwa wachezaji na watu wote watakaoshiriki katika michuano hiyo.”
Rais Samia ametumia fursa hiyo kusisitiza suala la amani, usalama na utulivu ndani ya nchi. Amesema kila anapopata fursa ya kuzungumza na wananchi, imekuwa ni utaratibu wake kusisitiza na kuwakumbusha umuhimu wa kuendelea kuzilinda na kuzitunza tunu hizo kwa nguvu zote.
“Uwekezaji, maendeleo tunayoyaona hapa, uwekezaji, utalii, biashara, ajira na huduma za jamii, haya hayawezi kustawi katika mazingira ya vurugu na uvunjifu wa amani.
“Niwaombe Watanzania wenzangu, hususan vijana, msikubali kuharibu amani ya nchi yenu. Amani ndiyo kila kitu katika maisha yetu. Tukatae kwa nguvu zote wasiolitakia mema taifa letu, na tulinde Tanzania yetu na Muungano wetu kwa mustakabali wa kizazi chetu na kizazi kijacho,” amesema Rais Samia.
Kwa upande wake Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, amesema tamasha hilo lina mchango mkubwa katika kutangaza, kuhifadhi na kuenzi mila na utamaduni, na hivyo kuchochea na kuhamasisha shughuli za maendeleo ya wananchi wa Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja na Zanzibar kwa ujumla.
Amempongeza Rais Samia kwa maono yake ya kuanzisha tamasha hilo.
“Hakika, mwaka huu tamasha hili limefana sana, hongereni sana. Mheshimiwa Rais Samia, tamasha hili limekuwa ni jukwaa muhimu la kuhamasisha shughuli za maendeleo, kwani pamoja na shughuli za burudani na michezo,” amesema Dk Mwinyi.
Pia, amesema wameshuhudia uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo barabara, maji, elimu, afya, nyumba za makazi na viwanja vya michezo.
Ametumia fursa hiyo kuahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha miradi yote iliyozinduliwa na ile itakayojengwa baadaye inatunzwa na kuendelezwa ipasavyo kwa maendeleo na ustawi wa wananchi.
Dk Mwinyi ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha miundombinu inayojengwa inatumika na kutunzwa vizuri ili idumu na kutumika kwa muda mrefu kama ilivyokusudiwa.
Amesema Tamasha la Kizimkazi litaendelea kuwa chachu na kutoa mchango muhimu wa kuwavutia wageni Zanzibar, kuhamasisha utalii wa ndani na shughuli za uwekezaji Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Sherehe hizo zimehudhuriwa pia na Rais wa zamani wa Guinea-Bissau, Umaro Sissoco Embalo, Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, na viongozi wengine wa kidini na kisiasa.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis, amesema tamasha hilo limegusa maeneo yote ya kihuduma, ikiwemo afya, elimu na ujasiriamali.
Kwa mujibu wa Hamida, wajasiriamali wadogo wa Mkoa wa Kusini Unguja, maeneo ya Kizimkazi na shehia jirani, wamepata ajira na fursa mbalimbali.
“Mheshimiwa Rais Samia, tunakushukuru sana. Tamasha limewakutanisha na taasisi za fedha; sasa hivi wananchi wa maeneo haya wanakopesheka na wanakopeshwa na taasisi zetu, na wameanza kufanya biashara,” amesema Hamida.
Hamida amesema vijana wa mkoa huo sasa wamefikia fursa za kiutalii, uwekezaji na kujiajiri katika kazi mbalimbali za amali.
“Kupitia maonyesho ya mwaka huu, tumesajili jumla ya wafanyabiashara 129 waliohitaji kuonyesha biashara ama huduma.
“Pia, tulikuwa na wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo ambao hawakuingia kwenye mabanda ya maonyesho, wasiopungua 200, hata yule mdogo ambaye alikuwa akiuza karanga, mikate, kachori na vitu kama hivyo,” amesema.
Amesema tamasha limeendelea kuwaunganisha wanakusini, wana wa Kizimkazi na kuwakutanisha na watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Zanzibar.
“Tamasha hili, kwetu sisi wana wa Kusini, tunasema linaimarisha Muungano wetu. Tunaendelea kuungana, na ndiyo maana leo hii tuna wageni wengi kutoka Tanzania Bara. Hii inaonyesha kwamba tamasha limelenga kuimarisha Muungano wetu, na sisi tunajivunia hilo,” amesema.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, tamasha hilo limewafanya waone thamani ya fursa zilizomo ndani ya mkoa wao.



Leave a Reply