WIZARA YA MADINI YAJA NA SHERIA KUSIMAMIA TAALUMA YA WAJIOLOJIA

*Sheria kuanzisha Bodi ya Wajiolojia kusimamia na kuratibu taaluma nchini*

*Serikali kutenga asilimia 10 ya mapato ya madini kwa utafiti wa jiosayansi*

*Taarifa sahihi za jiolojia kuimarisha uwekezaji na kuwalinda wadau wa madini*

Wizara ya Madini imewasilisha pendekezo la kuanzishwa kwa Sheria ya Usimamizi wa Wajiolojia nchini katika Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, hatua inayolenga kuweka mfumo madhubuti wa kusimamia taaluma hiyo na kuhakikisha taarifa za jiosayansi zinazotolewa nchini zinakuwa sahihi na zenye kuaminika.

Hayo yamebainishwa leo, Septemba 16, 2026, jijini Mwanza na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuiya ya Wajiolojia Tanzania (TGS).

Dkt. Kiruswa amesema endapo Sheria hiyo itapitishwa, itaanzishwa Bodi ya Wajiolojia itakayokuwa na jukumu la kusimamia, kuratibu na kuimarisha taaluma hiyo, ikiwemo kuweka viwango vya kitaaluma na kuhakikisha wataalamu wanaohusika na shughuli za jiosayansi wanatambulika na kuwajibika ipasavyo.

Amesema hatua hiyo ni muhimu kutokana na umuhimu wa taarifa za jiosayansi katika shughuli za utafutaji, uchimbaji na uwekezaji katika sekta ya madini, huku akieleza kuwa kumekuwa na baadhi ya taarifa zisizo sahihi zinazotolewa na watu wasio waaminifu au wasiokuwa na weledi na ujuzi unaohitajika, hali ambayo imekuwa ikisababisha hasara kwa baadhi ya wadau wa sekta hiyo.

“Ni muhimu kuwa na chombo kitakachosimamia taaluma hii ili kuhakikisha taarifa za jiosayansi zinazotokana na tafiti zinazofanywa nchini zinakuwa za uhakika na zinatolewa na wataalamu wenye sifa, weledi na uwajibikaji,” amesema Dkt. Kiruswa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa amesema Serikali imefanya uamuzi wa kutenga asilimia 10 ya makusanyo yatokanayo na mapato yasiyo ya kodi katika sekta ya madini kwa ajili ya shughuli za utafiti wa madini nchini, ambapo fedha hizo zinakadiriwa kufikia takribani Sh bilioni 140.

Amesema fedha hizo zitawezesha Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuongeza kasi ya tafiti za jiosayansi na kuzalisha taarifa nyingi na sahihi zitakazosaidia kubainisha rasilimali zilizopo nchini na kuweka msingi imara wa uwekezaji katika sekta ya madini.

Dkt. Kiruswa amesema Wizara ya Madini itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Wajiolojia Tanzania katika kuimarisha taaluma hiyo na kuhakikisha wataalamu wa ndani wanashiriki kikamilifu katika tafiti na shughuli za jiosayansi zinazolenga kuongeza manufaa ya rasilimali za madini kwa Taifa.

Ameeleza kuwa hatua hiyo inakwenda sambamba na vipaumbele vya Wizara vinavyotokana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 na Sera ya Madini, ambavyo ni pamoja na kuongeza utafiti na upatikanaji wa taarifa sahihi za jiolojia, kuongeza thamani madini, kuunganisha sekta ya madini na sekta nyingine za uchumi, kurasimisha na kuboresha uchimbaji mdogo, pamoja na kuimarisha usimamizi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Rais wa Jumuiya ya Wajiolojia Tanzania, Prof. Alisante Mshiu, amesema Mkutano Mkuu wa Mwaka ulianza Septemba 14, 2026, ukiwa na dhima ya “Matumizi ya Suluhisho za Jiosayansi kwa Ukuaji wa Viwanda, Uhakika wa Upatikanaji wa Nishati, Kuelekea Matumizi ya Nishati Safi na Maendeleo Stahimilivu Tanzania.”

Amesema mkutano huo umelenga kutoa fursa kwa wataalamu kubadilishana uzoefu na maarifa katika nyanja mbalimbali za jiosayansi, kwa lengo la kuongeza matumizi ya taaluma hiyo katika kutatua changamoto za maendeleo, kukuza uchumi na kuongeza manufaa yatokanayo na rasilimali zilizopo nchini.

NIDA KUANZA KUWASAJILI WATOTO CHINI YA MIAKA 18″ – DKT MWIGULU.

*_● Awasihi Watanzania kuchukua Vitambulisho vyao vya Uraia._*

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) itaanza kuchukua hatua za kuwasajili na kuwatambua watoto walio chini ya umri wa miaka 18, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mfumo wa utambulisho wa Taifa.

Dkt. Mwigulu amesema hatua hiyo itamuwezesha kila Mtanzania kutambulika kuanzia hatua za mwanzo za maisha yake pamoja na kuondoa pengo lililokuwepo katika mfumo wa utambulisho kati ya mtoto anapozaliwa na anapofikisha umri wa miaka 18.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo, Jumatano, Septemba 16, 2026, wakati akiwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Utambulisho Duniani, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

“Mfumo huu utasaidia kupunguza usumbufu wa kutumia nyaraka au vitambulisho vingi wakati wa kupata huduma mbalimbali, kwa kuwa taarifa muhimu za mwananchi zitaendelea kutambulika na kuhifadhiwa katika mfumo mkuu wa Taifa wa utambuzi” amesema.

Aidha, Dkt. Mwigulu amewataka Watanzania ambao tayari wamesajiliwa na vitambulisho vyao vya Taifa vimekamilika kwenda kuvichukua, akisisitiza kuwa utambulisho ni msingi muhimu wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

“Kitambulisho chenyewe kama nchi tumeingia gharama, tumeahirisha baadhi ya shughuli za maendeleo ili tutoe vitambulisho. Lakini tunapokuwa tumetoa kitambulisho, halafu mhusika haendi kuchukua, haya ni mambo ambayo yanakwamisha malengo mapana,” amesema.

Amesema kwa sasa NIDA imeboresha utaratibu wa kuwafahamisha wananchi pale vitambulisho vyao vinapokuwa tayari, ikiwemo kupitia ujumbe mfupi wa simu (SMS), hivyo hakuna sababu kwa wananchi waliokwishaandikishwa kuacha vitambulisho vyao kwa muda mrefu bila kuvichukua.

“Niendelee kusisitiza wananchi wote ambao wako tayari na vitambulisho vyao, basi waende kuvichukua. Lengo letu ni kuona kuwa hakuna Mtanzania anayeachwa nyuma katika kupata vitambulisho vya Taifa,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amesema Serikali imeendelea kufanya maboresho katika mfumo wa utambulisho wa Taifa ili kuhakikisha unakidhi mahitaji ya sasa ya kiteknolojia, usalama wa taarifa na utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Serikali imeendelea kuboresha mfumo wa utambulisho ili kupunguza utegemezi wa vitambulisho vingi kwa huduma mbalimbali na kuelekea katika mfumo ambao taarifa muhimu za mwananchi zinapatikana kupitia mfumo mkuu wa Taifa wa utambuzi,” amesema.

Naye, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema NIDA imefanya mapitio ya jumla ya vitambulisho vilivyotolewa katika ofisi zake na vituo 10 vya usajili vilivyopo katika kila wilaya, bila kuhusisha vituo 156 vilivyotajwa awali.

Amesema hadi sasa jumla ya watu 27,520,835 wamesajiliwa, ambapo watu 23,515,667 wamekwishapatiwa Namba za Utambulisho wa Taifa. Aidha, vitambulisho 21,526,635 vimezalishwa, huku bado kukiwa na idadi ya vitambulisho ambavyo havijachukuliwa na wananchi waliostahili kuvipata.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, amesema jamii inapaswa kuacha dhana kwamba NIDA ni taasisi inayotoa kadi pekee, kwa kuwa utambulisho wa Taifa ni msingi wa upatikanaji wa huduma na utambulisho wa mwananchi katika maisha yake yote.

Amesema NIDA inaendelea kuboresha kitambulisho cha Taifa ili kiwe cha kidijitali na kiweze kuhusisha taarifa muhimu za huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo cheti cha kuzaliwa, bima ya afya, TIN, leseni ya udereva na taarifa nyingine muhimu, huku taarifa za kiafya kama kundi la damu zikitarajiwa kusaidia wakati wa dharura, kwa kuzingatia uthibitisho wa kitabibu.

Kanji amesema usajili wa watoto tangu wanapozaliwa ni muhimu kwa sababu utamwezesha kila mtoto kutambulika na kupata huduma za kijamii kwa urahisi katika hatua zote za maisha. Amesema zoezi hilo litaanza kwa majaribio katika wilaya za Kilolo, Lungu na Kusini Unguja, kabla ya kupanuliwa katika maeneo mengine nchini

 

WAZIRI MKUU AWASILI ARUSHA, KUFUNGUA KONGAMANO LA WANAMIPANGO

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewasili mkoani Arusha leo Jumatano, Septemba 16, 2026, ambapo amepokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Arusha na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, pamoja na viongozi wengine wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali.

Dkt. Mwigulu yupo mkoani Arusha kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kikazi, ikiwemo kufungua rasmi Kongamano la Kitaifa la Wanamipango, litakalofanyika kesho Alhamisi, Septemba 17, 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).

 

MAKAMU WA RAIS MHE. NDEJEMBI AENDELEZA DIPLOMASIA YA TANZANIA – VIENNA

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi amefanya mikutano miwili ya pande mbili (bilateral meetings) pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 70 wa Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu (IAEA) Jijini Vienna, Austria, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Tanzania kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.

 

Katika mkutano wake na Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Bw. Rafael Mariano Grossi, mazungumzo yalijikita katika kuimarisha ushirikiano katika matumizi ya sayansi na teknolojia ya nyuklia kwa madhumuni ya amani na maendeleo, hususan matibabu ya saratani, kilimo na usalama wa chakula, lishe, maendeleo ya wataalamu pamoja na maandalizi ya Tanzania kuelekea matumizi ya nishati ya nyuklia kama nyongeza ya vyanzo vya uzalishaji umeme nchini siku zijazo.

 

Aidha, Makamu wa Rais amefanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa Vienna (UNOV) na Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), Dkt. Monica Juma. Mazungumzo yaliyolenga kuendeleza ushirikiano baina ya Tanzania na UNODC katika juhudi za kudhibiti dawa za kulevya.

 

Makamu wa Rais, Mhe. Ndejembi, yuko Jijini Vienna, Austria, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano Mkuu wa 70 wa Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu (IAEA), unaowakutanisha Viongozi na Wawakilishi wa Nchi wanachama kujadili masuala mbalimbali yanayohusu matumizi salama na ya amani ya sayansi na teknolojia ya nyuklia.

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

16 Septemba 2026

Vienna – Austria

 

DCI Kingai Kutinga Ijumaa Hii Kutoa Ushahidi Kesi ya Lissu, Heche Amaliza..

Mshtakiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amemaliza kumuuliza maswali ya re-examination shahidi wake, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche, katika kesi inayosikilizwa mbele ya Jopo la Majaji watatu wa Mahakama Kuu, likiongozwa na Jaji Dustan Ndunguru.

Baada ya kumaliza kumuuliza Heche maswali ya re-examination, Lissu aliliomba Jopo la Majaji maelekezo kuhusu mashahidi ambao Mahakama ilitoa summons kwa ajili yao.

“Waheshimiwa Majaji, niliomba summons kwa ajili ya mashahidi, kwa hiyo nataka kujua majibu kuwa mashahidi hao wako wapi na tunakwendaje mbele,” alisema Lissu.

Lissu alieleza pia kuwa anahitaji kukutana na mashahidi hao kabla hawajafika mahakamani ili kuwaandaa kwa ajili ya kutoa ushahidi.

Alisema hawezi kuwaweka mashahidi kizimbani bila kwanza kukutana nao na kuwaelekeza namna ya kuendesha ushahidi wao.

Kwa mujibu wa Lissu, Mahakama ndiyo eneo pekee analoweza kukutana na mashahidi hao kwa kuwa hana sehemu nyingine ya kuwaandalia, huku akisema hawezi kwenda maofisini kwao au gerezani.

Jaji Ndunguru alisema Mahakama ilitarajia upande wa Lissu kutoa taarifa iwapo ana shahidi au hana, kwa kuwa summons tayari zilitolewa na Mahakama.

Jaji alisema Mahakama ingepumzika ili Msajili awasilishe taarifa kuhusu utekelezaji wa summons hizo.

Baada ya mapumziko, Lissu alirejea mahakamani na kueleza kuwa alikuwa amekutana na Msajili wa Mahakama ambaye alimpatia taarifa kuhusu summons za mashahidi.

Kwa mujibu wa Lissu, Msajili alimweleza kuwa mashahidi wote walipelekewa summons Dodoma, ingawa nakala za summons hizo hazikuweza kuhifadhiwa baada ya kubainika kuwa baadhi ya mashahidi walikuwa nje ya nchi.

Lissu alisema mmoja wa mashahidi hao, ambaye ni Kamishna wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi katika Jeshi la Polisi (DCI), alitarajiwa kurejea nchini siku hiyo.

Alisema Msajili alimwahidi kuwa siku ya Ijumaa Kamishna huyo atakuwepo Mahakamani kwa ajili ya kutekeleza wito uliotolewa na Mahakama.

Lissu alieleza kuwa mashahidi wengine wawili waliotajwa ni Mkuu wa Majeshi, Jenerali Jacob Mkunda, na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camillius Wambura, ambao wakati huo haikufahamika ni lini wangerejea nchini.

Kutokana na hali hiyo, Lissu alipendekeza kesi hiyo iahirishwe hadi Ijumaa saa 8:30 mchana, ili muda wa asubuhi autumie kukutana na kushauriana na shahidi anayetarajiwa kufika, pamoja na kuchukua maelezo yake.

Alisema endapo mashahidi hao hawatakuja kabisa, suala hilo litakuwa mikononi mwa Mahakama kwa kuwa ni Mahakama iliyotoa summons hizo.

Aidha, Lissu alieleza kuwa anafahamu ratiba ya shauri hilo ilivyo na kwamba yeye pia anatamani shauri hilo lifikie hatua ya final submissions ili Mahakama ipate muda wa kutafakari na kutoa uamuzi.

Alisema iwapo mashahidi watafuata wito wa Mahakama, anaamini ushahidi wao hautachukua muda mrefu.

Upande wa mashtaka, kupitia Wakili Nassor Katuga, ulisema hauna pingamizi kuhusu kuahirishwa kwa kesi hiyo.

“Hata hivyo, tunaomba Mahakama hii imsisitize mshtakiwa mashahidi wake wafike kwa wakati,” alisema Katuga.

Kauli hiyo ilisababisha hali vicheko mahakamani, kabla ya Jaji Ndunguru kusisitiza kuwa mashahidi hao si “mashahidi wake” kwa maana ya kwamba ni jukumu la Mahakama kuhakikisha summons zinazingatiwa, huku akimkumbusha Lissu kuwa yeye ndiye anayetarajiwa kuwaleta mashahidi hao mahakamani.

Hatimaye, Jaji Ndunguru alitangaza kuwa shauri hilo limeahirishwa hadi Ijumaa tarehe 18, ambapo shahidi anayetarajiwa kufika mahakamani anatarajiwa kuendelea na hatua inayofuata ya ushahidi.

Katika hatua hiyo, Ramadhan Kingai anatarajiwa kufika Mahakamani Ijumaa kwa ajili ya kutoa ushahidi, ikiwa ni sehemu ya mwenendo wa shauri hilo.

Saudi Arabia Yatungua Drone ya Houthi Iliyolenga Anga ya Makkah

RIYADH, Saudi Arabia — Mfumo wa ulinzi wa anga wa Saudi Arabia umefanikiwa kutungua ndege isiyo na rubani (drone) iliyokuwa ikijaribu kuelekea katika anga ya mji mtakatifu wa Makkah, mamlaka za Saudi Arabia zimesema.

Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa Muungano wa Kurejesha Uhalali nchini Yemen, Meja Jenerali Turki Al-Malki, drone hiyo ilidunguliwa majira ya saa 6:50 jioni kwa saa za Saudi Arabia, kusini mwa Makkah, kabla haijaingia katika anga ya mji huo.

Al-Malki amesema jaribio hilo ni hatua kubwa na limevuka kile alichokiita “mstari mwekundu”, kutokana na umuhimu wa Makkah kwa Waislamu duniani.

Makkah ni mji mtakatifu zaidi katika Uislamu na hutembelewa na mamilioni ya Waislamu kila mwaka kwa ajili ya ibada za Hajj na Umrah. Pia ni eneo ambalo lina umuhimu mkubwa katika utekelezaji wa moja ya nguzo tano za Uislamu, Hajj.

Muungano huo umeitaja hatua hiyo kama jaribio la makusudi la kuchochea hisia za mamilioni ya Waislamu, na kusema kuwa tukio hilo litaendelea kuwa sehemu ya rekodi ya ukiukaji unaodaiwa kufanywa na kundi la Houthi.

Tukio hilo si la kwanza kuhusisha shambulio linalolenga eneo la Makkah. Mwaka 2017, Saudi Arabia ilisema vikosi vyake vya ulinzi wa anga vilifanikiwa kulitungua kombora la balestiki lililorushwa kuelekea Makkah kutoka Yemen.

Kwa mujibu wa mamlaka za Saudi Arabia wakati huo, kombora hilo lilitunguliwa katika eneo la Al-Wasliya, mkoani Taif, na hakukuwa na taarifa za watu kujeruhiwa wala uharibifu wa mali.

Mvutano huo umeendelea huku Saudi Arabia ikiripoti mashambulizi mengine yanayohusishwa na Houthi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Siku ya Jumatatu, Saudi Arabia ilisema raia 13 walijeruhiwa baada ya maeneo ya raia katika Khamis Mushait, Abha na Taif kulengwa kwa makombora ya balestiki.

Wiki iliyopita, shambulio jingine lililoripotiwa katika miji na maeneo mbalimbali nchini Saudi Arabia lilisababisha zaidi ya watu 70 kujeruhiwa, wakiwemo wanawake na watoto.

Aidha, Saudi Arabia ilitangaza Ijumaa kusitisha kwa muda shughuli za East-West Pipeline, baada ya bomba hilo kulengwa katika mfululizo wa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika maeneo ya Riyadh na Madinah.

Mashirika ya nchi za Ghuba pamoja na taasisi mbalimbali za Kiislamu yalilaani shambulio hilo dhidi ya bomba na kueleza mshikamano wao na Saudi Arabia.

FCC YATAJWA CHACHU YA SOKO HURU NA USHINDANI WA HAKI

SOMALIA YAIPONGEZA FCC KWA UTENDAJI BORA

SOMALIA YAONA UFANISI MKUBWA WA FCC KATIKA KULINDA SOKO

Na.Matukio Daima Media 

Tume ya Ushindani ya Somali  imefanya ziara ya siku moja nchini Tanzania kwa lengo la kujifunza uzoefu na mbinu zinazotumiwa na Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) katika kusimamia ushindani wa kibiashara, kudhibiti bidhaa bandia na kulinda maslahi ya walaji.

Ziara hiyo imefanywa na Mkurugenzi wa Masuala ya Uchumi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Jamhuri ya Shirikisho la Somalia na Kamishna wa Mamlaka ya Ushindani ya Afrika Mashariki (EACA), Bw. Ahmed Warsame pamoja na Mkurugenzi wa Biashara na Upatikanaji wa Masoko wa Wizara ya Biashara na Viwanda ya Jamhuri ya Shirikisho la Somalia, Bw. Abdihalim Osman.

Katika ziara hiyo, ujumbe huo umekutana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, pamoja na uongozi wa Tume, ambapo walipata fursa ya kujifunza namna FCC inavyotekeleza majukumu yake ya kukuza na kulinda ushindani, kumlinda mlaji na udhibiti wa bidhaa bandia.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, uongozi wa ujumbe wa Somalia umepongeza utendaji wa FCC, ukieleza kuwa uzoefu wa Tanzania katika kusimamia ushindani na kulinda mlaji ni muhimu kwa Somalia katika kuimarisha mifumo yake ya usimamizi wa soko na kukuza mazingira bora ya biashara.

Ujumbe huo umeeleza kuwa kujifunza kutoka FCC kutasaidia kuongeza uelewa na uwezo wa taasisi za Somalia katika kukabiliana na changamoto zinazohusu ushindani usio wa haki, bidhaa bandia na vitendo vinavyoweza kuwadhuru walaji.

Kwa upande wake,Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, amesema  kuwa Tanzania ipo tayari kuendelea kushirikiana na taasisi za Somalia na nchi nyingine katika kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu bora za usimamizi wa ushindani na ulinzi wa walaji.

Ziara hiyo ya siku moja imekuwa fursa muhimu kwa Somalia kujifunza uzoefu wa Tanzania katika eneo la ushindani wa kibiashara, udhibiti wa bidhaa bandia na ulinzi wa mlaji, hatua inayotarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi na kuchangia katika ujenzi wa masoko yenye ushindani wa haki na biashara endelevu.

 

KUPIGA KURA ZA SAMIA KALAMU AWARDS 2026 KWA MATUKIO DAIMA PEKEE INGIA HAPA

 

 

MATUKIO DAIMA IMETEULIWA KUSHIRIKI TUZO ZA UMAHIRI WA VYOMBO VYA HABARI NA WANAHABARI TANZANIA TUZO HIZI ZIMETOLEWA NA TCRA NA TAMWA 

 MAARUFU KWA JINA LA SAMIA KALAMU AWARDS (SKA2026)

1:TUZO YA CHOMBO CHA HABARI -MATUKIO DAIMA MEDIA 

2:TUZO YA JINSIA ,WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM 

3:TUZO YA AFYA

 

4:TUZO YA MPIGA PICHA 

AHSANTE KWA KUPIGIA KWA KUENDELEA KUTUPIGIA KURA MATUKIO DAIMA MEDIA ENDELEA KUTUPIGIA KURA KILA BAADA YA SAA 24 HADI SEPT 30 KASI YAKO YA KUPIGA KURA NDIO USHINDI .

DKT. MWIGULU: NDANI YA WIKI MOJA TUTACHUKUA HATUA KUSHUSHA BEI YA SARUJI

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema ndani ya wiki moja, Serikali itachukua hatua ya kuhakikisha bei ya saruji inakuwa himilivu kwa wananchi, baada ya kubaini malalamiko ya kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Simiyu.

Ametoa kauli hiyo jana (Jumanne, Septemba 15, 2026) wakati akizungumza na wananchi wa Bariadi Mjini, mkoani Simiyu katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya CCM Saba Saba.

“Serikali tumeliona hilo. Serikali sikivu tumesikia hilo. Nimewatuma wataalamu ndani ya wiki moja wawe wameshapata ufumbuzi. Tutatoa tamko la njia ya kushusha bei ya saruji ili kila Mtanzania aweze kumudu. Katika baadhi ya maeneo bei ya saruji imefikia zaidi ya sh. 26,000 na katika baadhi ya mikoa ya mipakani imefikia sh. 32,000,” amesema na kusisitiza kuwa Serikali inataka wananchi waweze kumudu gharama za ujenzi wa nyumba na miradi mingine ya maendeleo.

Kuhusu zao la pamba, Waziri Mkuu amesema ameielekeza Wizara ya Kilimo ikutane na wadau wa pamba ndani ya mwezi mmoja na ifikapo Oktoba 15, 2026 apelekewe mapendekezo rasmi kuhusu bei na mfumo bora wa ununuzi wa zao hilo ili kuhakikisha wakulima wananufaika zaidi.

“Nimeipokea hoja hii. Nimeelekeza Wizara ya Kilimo ikae na wadau wa pamba ndani ya mwezi mmoja. Ifikapo tarehe 15 mwezi wa 10, niwe nimeshapata mapendekezo rasmi yaliyorejea mifumo ambayo tumeshaitumia na kubaini upi ni mfumo bora ili tuweze kuhakikisha kwamba wakulima wananufaika,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema pia Serikali imebadilisha utaratibu wa kodi kwa wenye biashara mpya, ambapo mfanyabiashara anayeanzisha biashara atapewa muda wa kuimarisha biashara yake kabla ya kuanza kubeba mzigo wa kodi. “Zamani ilikuwa mtu akianzisha tu biashara, siku hiyo hiyo anaanza kudaiwa kodi. Sasa tumefuta, atasubiriwa mwaka mzima ili biashara yake iimarike,” amesema.

Amesema hatua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050 inayolenga kujenga uchumi shirikishi, ambapo sekta binafsi inatarajiwa kutekeleza sehemu kubwa ya shughuli za maendeleo.

Mapema, akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Bariadi Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Andrea Mathew, amemshukuru Waziri Mkuu kwa ziara hiyo na kueleza kuwa Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo ikiwemo inayogusa sekta za maji, elimu, afya na barabara. 

Mhandisi Kundo amesema mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria wenye thamani ya sh. bilioni 440 unaendelea kutekelezwa mkoani humo, huku Serikali ikiwa imetoa sh. milioni 460 kupitia TARURA kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Majaida–Munambala katika Mto Ndoba.

Kuhusu ujenzi wa soko la kisasa la Bariadi mjini, Mhandisi Kumndo amesema ujenzi wake unaendelea, huku akiomba kasi ya mkandarasi iongezwe ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

Akigusia barabara za Bariadi Mjini, Mhandisi Kundo amesema Serikali imeweka mpango wa kuhakikisha kilomita zote 8.6 zilizotengewa ujenzi zinajengwa kwa awamu mbili, ambapo kilomita tano zitajengwa katika awamu ya kwanza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda, amesema Serikali ya Mkoa itasimamia na kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu wakati wa ziara hiyo na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Maagizo na maelekezo yako uliyoyatoa katika ziara yako hii tunayasimamia, tuyatekeleze, na kuleta ripoti ya utekelezaji katika ofisi yako ya Waziri Mkuu,” amesema.

Lissu Ataka Kukutana na IGP Wambura, CDF Mkunda na Kingai Kupanga Mkakati wa Ushahdi wa Kesi

Global Publishers
September 16, 2026
492 views
0 Comments

Dar es Salaam. Tundu Lissu ameiambia Mahakama kuwa John Heche ndiye shahidi wake wa mwisho kutoka miongoni mwa mashahidi raia, akieleza kuwa anatarajia kukamilisha hatua ya re-examination ya shahidi huyo kesho ndani ya muda usiozidi saa moja.

Lissu alitoa kauli hiyo wakati shauri hilo likiendelea Mahakamani, akieleza pia kuwa bado ana mashahidi wengine watatu ambao anahitaji kukutana nao kabla ya kuendelea na hatua inayofuata ya ushahidi.

Kwa mujibu wa Lissu, anahitaji kupata nafasi ya kukutana na mashahidi hao ili kupanga namna ya kuendesha ushahidi uliosalia. Kauli hiyo ilizua vicheko ndani ya ukumbi wa Mahakama.

Awali, Jaji Ndunguru alimweleza Lissu kuwa upande wa utetezi bado una mashahidi watatu na kwamba Mahakama ilitarajia kupokea final submissions siku ya Ijumaa.

Hata hivyo, Lissu aliomba muda wa kukutana na mashahidi hao, akisema hatua hiyo ni muhimu kwa ajili ya kupanga namna ya kuendelea na kesi.

Mashahidi watatu waliobaki ni IGP Camillius Wambura, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania; CDF Jenerali Jacob John Mkunda, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania; na DCI Ramadhan Kingai, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo, Jaji Ndunguru aliahirisha shauri hadi kesho saa tatu kamili asubuhi.

Mahakama pia imebainisha kuwa John Heche bado hajamaliza kutoa ushahidi wake, hivyo hatua ya re-examination ya shahidi huyo inatarajiwa kuendelea kabla ya upande wa utetezi kuwasilisha mashahidi wake wengine.

Hatua hiyo inaendelea huku Mahakama ikiwa imeweka Ijumaa kuwa siku inayotarajiwa kwa upande wa utetezi kuwasilisha hoja zake za mwisho (final submissions), endapo ushahidi utakuwa umekamilika.