
Iran imewasilisha pendekezo jipya kuhusu masuala ya nyuklia kwa Marekani kupitia Qatar, huku ikiweka masharti saba ambayo inataka yatimizwe na Washington kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.
Afisa mmoja mwandamizi wa Iran asema tayari wametuma pendekezo hilo kwa Marekani, lakini hakutoa maelezo zaidi.
Hatua hiyo inakuja wakati juhudi za kidiplomasia zikiongezwa na wapatanishi wanaolenga kumaliza vita kati ya Iran na Marekani, huku kukiwa na hofu kuwa mapigano yanaweza kurejea baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani.
Hofu hiyo imeongezeka baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, Jumanne kukataa kuondoa uwezekano wa kurejea kwa operesheni za kijeshi baada ya uchaguzi huo, huku Iran nayo ikionya kuwa itapanua mashambulizi yake endapo vita vitaanza tena.
Akizungumza wakati wa ziara yake nchini Urusi Alhamisi, afisa mkuu wa usalama wa Iran, Mohsen Rezaei, amesema Tehran tayari imewasilisha masharti saba kwa Marekani na haitakuwa tayari kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz wala kuanza mazungumzo hadi masharti hayo yatakapotekelezwa.
Miongoni mwa madai ya Iran ni kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani, kurejeshwa kwa mali za Iran zilizozuiwa nje ya nchi pamoja na kulipwa fidia ya uharibifu uliotokana na vita.
Kwa upande wake, Washington imesisitiza kuwa suala la mpango wa nyuklia wa Iran lazima liwe sehemu ya mazungumzo yoyote ya awali, jambo linaloonyesha tofauti zilizopo kati ya pande hizo mbili kuhusu namna ya kuanza mchakato wa kutafuta suluhu.
Mgogoro huo ulianza Februari 28, 2026, baada ya Marekani na Israel kufanya mashambulizi dhidi ya Iran, hatua iliyosababisha Tehran kujibu kwa kushambulia maeneo ya Israel pamoja na mataifa ya Ghuba yanayohifadhi kambi za kijeshi za Marekani.
Mapigano hayo pia yalienea nchini Lebanon, ambako kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran liliingia katika mapambano na Israel. Baadaye mzozo huo ulifikia Yemen, ambako waasi wa Houthi, wanaohusishwa na Iran, walifanya mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati, viwanja vya ndege na maeneo mengine nchini Saudi Arabia.
Kwa sasa, juhudi za kidiplomasia kupitia Qatar zinaonekana kuwa sehemu muhimu ya kutafuta njia ya kumaliza vita hivyo, ingawa masharti yaliyowekwa na Iran na msimamo wa Marekani kuhusu mpango wa nyuklia vinaendelea kuwa vikwazo katika kufikia makubaliano.
Hatma ya mazungumzo hayo inatarajiwa kutegemea namna Washington itakavyojibu pendekezo la Tehran na iwapo pande hizo mbili zitakuwa tayari kufanya makubaliano kuhusu masuala ya nyuklia, vikwazo vya kiuchumi na usalama katika eneo la Mashariki ya Kati.
