MWITIKIO MKUBWA TUZO ZA AKS 2026 KAZI 294 ZAINGIA FAINALI

Na Mwandishi wetu 

Dar es Salaam, Septemba 3, 2026: Kazi 294 zimefuzu kuingia hatua ya kupigiwa kura na wananchi katika msimu wa pili wa Tuzo za Samia Kalamu Awards (SKA 2026).

Kazi hizo zimechujwa kutoka katika kazi 3,003 zilizowasilishwa na waombaji 985 na kufanyiwa tathmini na jopo la majaji kwa kuzingatia ubora, ubunifu, utafiti, maadili ya taaluma, athari kwa jamii na mchango katika maendeleo ya nchi.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo, Septemba 3, 2026, Mwenyekiti wa Maandalizi ya tuzo ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mha. Peter Mwasalyanda, amewakaribisha wananchi kupiga kura kuchagua washindi kupitia tovuti https://www.samiaawards.tz/ au kutuma ujumbe mfupi wenye neno “SKA”, likifuatiwa na namba ya mshiriki kwenda namba 15200.

Zoezi la upigaji kura limeanza leo, Septemba 3, 2026, na litafungwa Septemba 30, 2026.

Naye Mwenyekiti Mwenza wa Mashindano hayo na Mkurugenzi wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, amesema mashindano hayo yamewaleta pamoja waandishi wa habari kutoka maeneo ya vijijini na mijini, akisisitiza kuwa washiriki watashindana kwa kuzingatia ubora wa kazi zao na si umaarufu wao.

Kwa mujibu wa mmoja wa majaji wa mashindano hayo, Bi. Beatrice Bandawe, amesema kuwa miongoni mwa maeneo yaliyopatiwa kipaumbele katika kazi zilizowasilishwa ni pamoja na afya, jinsia na makundi maalum, mazingira pamoja na elimu.

Samia Kalamu Awards ni tuzo za kitaifa zinazoratibiwa kwa ushirikiano wa TCRA, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB).

Aidha TCRA, TAMWA, na JAB zinaendelea kuwaomba wadau kujitokeza kudhamini tuzo za SKA 2026 kwa dhumuni la kutambua, kuenzi na kuhamasisha uandishi wa habari wenye ubora, weledi na ubunifu katika kuchochea maendeleo ya nchi.

MWIGULU AITAKA WIZARA YA FEDHA KUPANDISHA KIKOMO CHA MIRADI DODOMA.

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameitaka Wizara ya Fedha kufanya marekebisho ya sheria za ununuzi wa umma ili kuongeza kiwango cha thamani ya miradi inayoweza kutekelezwa na kampuni za Kitanzania, akipendekeza kiwango cha Sh bilioni 50 kipandishwe hadi zaidi ya Sh bilioni 100 au Sh bilioni 150.

Dkt. Mwigulu amesema kiwango cha Sh bilioni 50 kwa baadhi ya miradi kimekuwa kidogo kutokana na kukua kwa uchumi na kuongezeka kwa uwezo wa kampuni za ndani.

“Hii ya bilioni 50 imeshakuwa ya kawaida wekeni bilioni 100… au kama mnarekebisha sasa ikachukua muda, wekeni bilioni 150 Mambo yanaenda mbele. Tuwawezeshe Watanzania kushika uchumi wao,” amesema.

Amesema kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi ni muhimu katika kuongeza ajira, kukuza sekta binafsi, kuongeza mapato na kupunguza umaskini nchini.

Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo, Septemba 3, 2026, wakati akifungua Kongamano la Tano la Kitaifa la Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati na Uwekezaji, lililofanyika Dodoma.

Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira ya kisera, kisheria na kiutendaji yatakayowawezesha Watanzania kushiriki moja kwa moja katika shughuli za uchumi.

“Tuwawezeshe Watanzania kushika uchumi wao hii ndiyo njia ya kuongeza ajira, kuongeza vyanzo vya mapato na kujenga sekta binafsi yenye nguvu,” amesema.

Amesema lengo la kuwawezesha Watanzania si kuwazuia wawekezaji wa nje, bali kuongeza uwezo wa kampuni na wananchi wa ndani ili nao wanufaike na fursa zinazotokana na rasilimali na miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi (NEEC), Gwakisa Bapala, amesema takribani wadau 600 wameshiriki kongamano hilo la siku mbili lililoanza Septemba 2, 2026.

Amesema washiriki wamejadili changamoto na fursa zilizopo katika miradi ya kimkakati na uwekezaji, pamoja na kupewa mbinu za kushiriki na kunufaika na fursa zinazotokana na manunuzi ya umma.

Bapala amesema pamoja na Serikali kuweka mwongozo unaotaka angalau asilimia 30 ya wanufaika wa zabuni za manunuzi ya umma kuwa makundi maalum, ikiwemo vijana, bado ushiriki wa makundi hayo umebaki kuwa mdogo, ukiwa karibu asilimia moja pekee.

Amesema kongamano hilo limeweka maazimio yanayolenga kuwapa wadau mbinu za kunufaika na zabuni za manunuzi ya umma, fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali pamoja na maeneo mengine yanayotolewa na Serikali.

Kongamano hilo limefanyika chini ya kaulimbiu: “Ushiriki wa Watanzania ni Nguzo ya Uchumi Shindani na Jumuishi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

WATAALAMU WA UCHUMI WA BULUU KUKUTANA DAR

Wataalamu, watafiti, wanasayansi, watunga sera na wadau wa Uchumi wa Buluu kutoka Tanzania, Afrika na mataifa mbalimbali duniani wanatarajiwa kukutana jijini Dar es Salaam katika Kongamano la Tano la Kimataifa la Uchumi wa Buluu.

Kongamano hilo litafanyika Septemba 7 hadi 9, 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), huku Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam, Tumaini Gurumo, amesema kongamano hilo litatoa fursa kwa wadau kujadili namna rasilimali za maji zinavyoweza kutumika kuongeza ukuaji wa uchumi na kuchochea maendeleo endelevu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Septemba 3, 2026, Gurumo amesema washiriki watawasilisha tafiti na mawasilisho ya kitaalamu yatakayosaidia kubaini changamoto zinazoikabili sekta hiyo na kutafuta suluhisho.

“Lengo ni kuwakutanisha wabobezi wa masuala ya Uchumi wa Buluu pamoja na wadau mbalimbali, wakiwemo wale wenye uelewa mkubwa wa sekta hii na wale wanaotaka kujifunza zaidi,” amesema.

Amesema majadiliano yatahusisha fursa zinazopatikana kupitia bahari, mito, maziwa na rasilimali nyingine za maji, pamoja na namna ya kuzitumia kukuza ubunifu, ajira na shughuli za kiuchumi kwa kuzingatia matumizi endelevu.

Kwa mujibu wa Gurumo, kongamano hilo linaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika, ambazo zinasisitiza matumizi endelevu ya rasilimali katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Amesema washiriki kutoka nchi mbalimbali tayari wamethibitisha kushiriki, wakiwemo kutoka Kenya, Ghana, Afrika Kusini, Comoro, Seychelles na Uganda.

Kwa upande wa nje ya Afrika, amesema washiriki wanatarajiwa kutoka Japan, Sweden, Urusi na nchi nyingine, huku mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania, taasisi za kitaifa na kimataifa, viongozi wa Serikali na sekta binafsi, wanasayansi na watafiti wakitarajiwa kuhudhuria.

Mbali na wataalamu na wadau wa sekta hiyo, waandaaji wamewaalika vijana kutoka vyuo vikuu, shule za sekondari na shule za msingi kushiriki katika kongamano hilo.

Gurumo amesema ushiriki wa vijana ni muhimu katika kuwajengea uelewa kuhusu Uchumi wa Buluu na fursa zilizopo, ili waweze kuwa sehemu ya kizazi kitakachobeba na kuendeleza ajenda hiyo.

Amesema vijana wanapaswa kutambua nafasi yao katika kutumia fursa zinazotokana na rasilimali za maji, hususan katika maeneo ya ubunifu, utafiti, ajira na shughuli za ujasiriamali.

Amewataka Watanzania kutumia fursa hiyo kushiriki na kuongeza uelewa kuhusu Uchumi wa Buluu, pamoja na namna bahari, mito, maziwa na vyanzo vingine vya maji vinavyoweza kutumika kuchochea maendeleo endelevu nchini na barani Afrika.

*DKT. MWIGULU: TUWAWEZESHE WATANZANIA KUSHIKA UCHUMI WAO*

*_▪︎ Ataka wigo wa miradi kwa Watanzania kupanuliwa_*

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa wito wa kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu katika uchumi wa nchi yao, akisisitiza kuwa uwezeshaji wa wananchi ni msingi wa kuongeza ajira, kukuza sekta binafsi, kuongeza mapato na kupunguza umaskini.

Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 03, 2026) wakati akifungua Kongamano la Tano la Taifa la Ushiriki wa Watanzania katika Masuala ya Uchumi, lililofanyika Dodoma, lenye kaulimbiu inayosisitiza ushiriki wa Watanzania kama nguzo ya uchumi shindani na jumuishi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira ya kisera, kisheria na kiutendaji yatakayowawezesha Watanzania kushiriki moja kwa moja katika shughuli za kiuchumi, akisisitiza kuwa lengo si kuwazuia wawekezaji wa nje bali kuongeza uwezo na ushiriki wa Watanzania.

“Tuwawezeshe Watanzania kushika uchumi wao. Hii ndiyo njia ya kuongeza ajira, kuongeza vyanzo vya mapato na kujenga sekta binafsi yenye nguvu,” amesema.

Dkt. Mwigulu amesema Tanzania ina rasilimali nyingi na fursa kubwa za kiuchumi, hivyo ni muhimu kuhakikisha fursa hizo zinatafsiriwa kuwa ajira, biashara, uwekezaji na umiliki kwa Watanzania.

Dkt. Mwigulu ameiagiza Wizara ya Fedha kuhakikisha marekebisho yanayofuata ya sheria za ununuzi yanaongeza wigo wa miradi inayoweza kutekelezwa na kampuni za Kitanzania.

Amesema kiwango cha Shilingi bilioni 50 kwa baadhi ya miradi kimekuwa kidogo kutokana na kukua kwa uchumi na uwezo wa kampuni za ndani, hivyo akapendekeza kiwango hicho kipandishwe hadi zaidi ya Shilingi bilioni 100 au Shilingi bilioni 150.

“Hii ya bilioni 50 imeshakuwa ya kawaida. Wekeni bilioni 100… au kama mnarekebisha sasa ikachukua muda, wekeni bilioni 150. Mambo yanaenda mbele. Tuwawezeshe Watanzania kushika uchumi wao,” amesema.

Amesisitiza pia kuwa fursa zinazotolewa na Serikali zinapaswa kutumiwa kwa uwajibikaji, akizitaka kampuni za Kitanzania kuhakikisha fedha za miradi zinatumika kutekeleza kazi kwa kiwango na ubora unaostahili, na kuonya kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya watakaotumia vibaya fedha za umma.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amezindua rasmi Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Uwezeshaji Kiuchumi (NEMIS) unaolenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa kuhusu fursa mbalimbali za uwezeshaji kwa Watanzania.

Mfumo huo utasaidia kuwafikishia wananchi taarifa kuhusu fursa za mitaji kupitia mifuko na programu za uwezeshaji, zabuni za umma, fursa za uwekezaji pamoja na taarifa nyingine muhimu za kiuchumi.

Dkt. Mwigulu amehitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kuondoka kwenye mipango na sheria na kuelekea kwenye utekelezaji unaoleta matokeo kwa wananchi.

“Tanzania inasifika sana kwa mipango mizuri, inasifika sana kwa sheria hizi hizi tunazoziandika. Sasa tupige hatua twende kwenye kuhakikisha haya tunayotekeleza, haya tunayopanga, haya tunayoyaandika yanaonekana kwenye vitendo.”

Akizungumza katika kongamano hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Serikali imeendelea kuweka mifumo, sera na sheria zinazolenga kuongeza ushiriki wa Watanzania katika uchumi, akisisitiza umuhimu wa uratibu ili fursa hizo ziwafikie wananchi na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema manunuzi ya bidhaa na huduma katika sekta ya madini yanafikia Shilingi trilioni 5.1 kwa mwaka, ambapo Serikali imehakikisha asilimia 90 ya manunuzi hayo yanabaki nchini Tanzania, hatua inayoongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.

Kwa niaba ya Bunge, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Edwin Swale, amesema Bunge limeendelea kuunga mkono hatua za Serikali za kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia maboresho ya sheria, akibainisha kuwa Serikali imeweka mifuko zaidi ya 74 ya uwezeshaji na imeendelea kuchukua hatua za kupunguza vikwazo kwa wafanyabiashara na wajasiriamali.

Nae, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi, Prof. Aurelia Kamuzora, amesema uwezeshaji wa wananchi unapaswa kwenda sambamba na kujenga uwezo wa watu, upatikanaji wa mitaji, taarifa na ujuzi ili Watanzania waweze kushindana ndani na nje ya nchi.

Amesema Baraza limeweka mkazo katika kuwafikishia wananchi taarifa za fursa za kiuchumi na kuimarisha vituo vya uwezeshaji katika mikoa na wilaya.

*MAKAMU WA RAIS AMWAKILISHA RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN, UTOAJI WA TUZO ZA PYMA.*

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya utoaji wa tuzo za 19 za Rais za Wazalishaji Bora Viwandani, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Super Dome, Masaki Jijini Dar es Salaam.

 

Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu wa Rais ametoa wito kwa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na wazalishaji wa saruji nchini, kuhakikisha wanatafuta suluhu ya haraka ili kurejesha bei ya kawaida ya saruji kwa wananchi. Amesema maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona wananchi wanaweza kununua mfuko wa saruji kwa gharama nafuu hivyo ni lazima kuoanisha uzalishaji wa malighafi zote zinazochangia katika uzalishaji wa saruji ili bidhaa hiyo ipatikane kwa urahisi.

 

Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema ni muhimu kufanya tathimini ya ukuaji wa viwanda hapa nchini ili kutambua ukuaji huo kama unaviwezesha viwanda kuwa na ushindani wa masoko katika kanda, Afrika na Dunia kwa ujumla.

 

Makamu wa Rais amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria kwa wafanyabishaara wote wanaojihusisha na biashara haramu za uingizaji bidhaa bandia ambazo hukwepa kodi na tozo mbalimbali stahiki ambapo, zinaathiri ukuaji wa viwanda, kusababisha upotevu wa mapato ya serikali pamoja na kupunguza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi.

 

Amewataka wazalishaji wa viwandani hapa nchini, kufanya jitihada za kuongeza uchakataji wa malighafi ndani ya nchi kwa kuhakikisha wanaongeza thamani, hatua itakayosaidia katika kuongeza ajira kwa watanzania na ukuaji wa uchumi kwa kasi.

 

Aidha, Makamu wa Rais ameitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakiki takwimu sahihi za idadi ya viwanda vilivyopo ili kuweka mikakati ya namna ya kuongeza wanachama wa Shirikisho la Viwanda Tanzania, hali itakayorahisisha uwepo wa chombo kimoja kinachowawakilisha wazalishaji wa viwandani.

 

Makamu wa Rais amesema katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya watanzania, sekta ya viwanda ina nafasi kubwa kwa kuwa ndiyo chimbuko la maendeleo ya haraka na ni muhimili mkuu katika uongezaji thamani wa malighafi zilizopo, utoaji ajira kwa wananchi, kuongeza mapato ya Serikali pamoja na fedha za kigeni.  Pia, amesema sekta ya viwanda ni muhimu katika kuboresha sayansi na teknolojia na  kuongeza uzalishaji, na hivyo kukuza ubunifu, uvumbuzi, uchumi, na kuondoa umasikini nchini.

 

Amesema kutokana na wingi wa rasilimali zilizopo nchini ikiwemo misitu na madini mbalimbali, ni muhimu kukuza  sekta ya viwanda na kuendelea kujenga mahusiano kati ya sekta ya viwanda na nyingine ili kuongeza ufanisi, kuharakisha maendeleo jumuishi na hatimaye kuongeza kipato cha Watanzania walio wengi.

 

Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kufanya kazi kwa karibu na sekta binafsi ili kuharakisha maendeleo ya Taifa.

 

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga, amesema Wizara hiyo imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuhakikisha lengo lake la kuendeleza sekta ya viwanda linafanikiwa. Amesema Sekta hiyo imeendelea kujiimarisha ili kuongeza nafasi katika mchango wa pato la Taifa na kuongeza ufanisi kwa lengo la ukuaji wa sekta hiyo muhimu.

 

Amesema tayari Wizara imekamilisha na itazindua Sera ya Maendeleo endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025 na Sera ya Maendeleo ya jasiriamali ndogo na za kati ya mwaka 2003 Toleo la mwaka 2025 ikiwa na lengo la kwenda sambamba na Dira 2050 ambayo inategemea uendelevu wa Viwanda.

 

Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) Hussein Suphian Ally ameipongeza Serikali kwa mafanikio mbalimbali yanayoendelea kuimarisha mchango wa sekta ya viwanda nchini ikiwemo uwekezaji mkubwa unaofanywa katika miradi ya kimkakati ambayo imeendelea kuongeza ushindani katika sekta ya viwanda.

 

Amesema CTI inapongeza juhudi za Serikali za kuendelea na ujenzi wa miradi ya Reli ya Kisasa (SGR), ujenzi na upanuzi wa Bandari, ujenzi wa mitandao ya barabara pamoja na uwekezaji katika nishati na miundombinu mingine ya kiuchumi ambayo kwa pamoja imeendelea kupunguza gharama za usafirishaji, kurahisisha biashara na kuongeza uwezo wa bidhaa zinazozalishwa nchini kufikia masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.

 

Katika hafla hiyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezawadia tuzo ya heshima kwa kutambua mchango wake katika uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na viwanda nchini.

 

Hafla hiyo imewakutanisha wazalishaji wakubwa, wakati na wadogo, wafanyabiashara pamoja na wadau wengine wa sekta ya viwanda na biashara, huku tuzo hizo zikiendelea kuwa jukwaa la kuhamasisha ubora, ubunifu, uwekezaji, matumizi ya teknolojia na uzalishaji endelevu nchini.

 

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

03 Septemba 2026

Dar es Salaam.

MBUNGE KIGOMA KASKAZINI AOMBWA KUBORESHA VIWANJA VYA MICHEZO

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

WAPENZI wa soka katika jimbo la Kigoma Kaskazini mkoani Kigoma wamemuomba mbunge wa jimbo hilo Kiza Mayeye  kuboresha viwanja vya soka katika jimbo hilo ikiwemo kuzungumzia uzio ili kuwezesha michezo kufanya kwa usalama na kulata tija katika kuibua vipaji.

Wito huo wa wapenzi wa soka wa jimbo hilo umetolewa katika uzinduzi wa ligi ya mpira wa miguu inayoandaliwa na Mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini, Kiza Mayeye inayojumuisha jumla ya timu 32 ikijulikana kama Mayeye Cup.

Mmoja wa wapenzi hao wa soka Hussein Suleiman wa Mwandiga alisema kuwa jimbo hilo lina wapenzi wengi wa soka lakini viwanja vingi haviko kweny hali nzuri akitolea mfano Uwanja wa Tarafa kwenye mji mdogo wa Mwandiga maarufu kwa mashindano mbalimbali lakini uwanja huo hauna uzio na magari,pikipiki, baiskeli zimekuwa zikipita sambamba na kuwa na mifereji mikubwa wakati wa mvua.

Hoja hiyo imeunga mkono na Shaban Mambo Mshauri wa mbunge wa jimbo hilo Kigoma Kaskazini ambaye alisema kuwa amepokea maombi mengi ya vijana ya kutaka kuboreshwa kwa viwanja vyao ukiwemo uwanja maarufu wa Tarafa Mwandiga ambao umekuwa ukitumika kwa michezo mbalimbali.

Mambo alisema kuwa binafsi ameshafikisha suala hilo kwa mbunge na kwa kuanza kwa ligi hiyo ni wazi atatekeeleza ombi hilo ili kuwezesha michezo kufanyika mahali pazuri, salama na kuleta tija kwenye suala la michezo kuwa ajira.

 Akizungumza katika uzinduzi huo kwa niaba ya Mbunge wa jimbo hilo Katibu wa Mbunge,Ilaki Issa  alisema kuwa kufanyika kwa mashindano hayo kunatokana na maombi ya vijana wengi kuomba kufanyika kwa mashindano ambayo yatashirikisha timu mbalimbali za jimbo hilo na kwamba ametimiza ahadi hiyo.

 Issa alisema kuwa Mshindi wa kwanza atapata Zawadi ya pesa taslim shilingi milioni mbili na jezi seti moja, Mshindi wa pili atanyakua pesa taslim shilingi milioni moja na seti moja ya jezi ambapo mshindi wa tatu ataondoka na jezi Seti mbili huku kukiwa pia na zawadi kwa Mchezaji bora, mfungaji bora na golikipa bora.

PBPA YAWAWEZESHA MAMA LISHE KURASINI KUHAMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

 

Dar es Salaam, Septemba 3, 2026

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mhandisi Bruno Tarimo, amewahimiza mama na baba lishe kuachana na matumizi ya kuni na mkaa wa kawaida na kuhamia katika nishati safi ya kupikia ili kulinda afya zao, kuhifadhi mazingira na kuongeza ufanisi wa biashara zao.

Mhandisi Tarimo ametoa wito huo leo, Septemba 3, 2026, wakati wa mafunzo ya matumizi ya nishati safi ya kupikia yaliyotolewa na PBPA kwa mama na baba lishe wa Kikundi cha Jitihada, yaliyofanyika Kurasini jijini Dar es Salaam. Katika tukio hilo, PBPA imewakabidhi mama na baba lishe 70 jumla ya tani 1.7 za mkaa mbadala.

Akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa PBPA, Mhandisi Tarimo amesema mafunzo hayo ni sehemu ya ushiriki wa Wakala katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa miaka 10, uliozinduliwa mwaka 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mkakati huo unalenga kuhakikisha kuwa, ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania watakuwa wamehama kutoka katika matumizi ya nishati zisizo safi na salama na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia.

“Tumekuja kushirikiana na mama na baba lishe pamoja na watoa huduma wa teknolojia za nishati safi ili kuwapatia elimu kuhusu matumizi yake na kuwasaidia kuachana na nishati zisizo safi na salama,” amesema Mhandisi Tarimo.

Ameeleza kuwa PBPA imeanza na mama na baba lishe wa Kurasini kwa sababu eneo hilo lina makampuni mengi ya mafuta ambayo ni miongoni mwa wadau wakuu wa Wakala. Wafanyakazi wa makampuni hayo hupata huduma za chakula kutoka kwa mama na baba lishe wanaofanya biashara katika maeneo ya Kurasini na Kigamboni.

“Wafanyakazi wanapokuja kula wataona chakula kimepikwa katika mazingira safi, hakina moshi na kina ladha nzuri. Wanaweza pia kuifikisha elimu hii kwa ndugu, jamaa na marafiki. Kwa namna hiyo, tunaendelea kuchangia utekelezaji wa lengo la kuwafikia asilimia 80 ya Watanzania,” amesema.

Mhandisi Tarimo amesema, katika mafunzo hayo, washiriki walipata fursa ya kuona na kujifunza matumizi ya majiko ya kisasa ya umeme, majiko banifu na mkaa mbadala. Pia walishuhudia kwa vitendo namna teknolojia hizo zinavyoweza kutumika kupika chakula kwa haraka, bila kutoa moshi mwingi wala kuchafua vyombo vya kupikia.

Amesema matumizi ya kuni na mkaa wa kawaida yana madhara kwa afya za watumiaji, hususan mama na baba lishe ambao hukaa karibu na moshi kwa muda mrefu. Aidha, matumizi ya nishati hizo yanachangia uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti.

PBPA pia inaendelea kuzihamasisha taasisi zinazohudumia au kuandaa chakula kwa zaidi ya watu 100 kwa siku kuhamia katika matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kikundi cha Jitihada, Bw. Lugano Mwaiswelo, amesema mafunzo hayo yamewapatia washiriki maarifa yatakayowasaidia kulinda afya zao na kuboresha mazingira wanamofanyia biashara.

“Tunaishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kuwakumbuka mama na baba lishe kupitia jitihada za kuhamia katika nishati safi ya kupikia inasaidia kuboresha mazingira na kulinda afya zetu. Tumepokea elimu hii kwa furaha, tutazingatia tuliyofundishwa na tutakuwa mfano kwa vikundi vingine kwa kutumia majiko banifu, mkaa mbadala na majiko ya umeme,” amesema Bw. Mwaiswelo.

Mmoja wa mama lishe walioshiriki mafunzo hayo, Bi. Joyce Benjamin Mtweve, amesema maonesho ya upishi yaliyofanyika yamewathibitishia kuwa matumizi ya nishati safi yanaweza kurahisisha kazi zao na kuboresha mazingira ya biashara.

“Tumefurahi sana kwa ujio wenu na kwa kutuonesha majiko ya nishati safi. Tumeshuhudia yakipika vizuri, bila moshi na bila kuchafua sufuria. Tuko tayari kuunga mkono juhudi hizi,” amesema Bi. Mtweve.

Naye Rais wa Mama Lishe Tanzania, Bi. Latifa Habibu Masasi, amesema upatikanaji wa gesi, majiko ya umeme, majiko banifu na mkaa mbadala umewapa mama lishe fursa ya kuchagua teknolojia inayolingana na mahitaji pamoja na uwezo wao.

“Nishati safi ni muhimu sana. Teknolojia hizi zinaongeza thamani katika mnyororo wa biashara ya chakula kwa sababu zinawawezesha mama lishe kupika kwa haraka, kwa wakati na katika mazingira salama zaidi,” amesema Bi. Masasi.

Mafunzo hayo yanaashiria kuanza kwa kampeni ya PBPA ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia miongoni mwa mama na baba lishe nchini. Kampeni hiyo inatarajiwa kuendelea katika maeneo mengine yenye mama na baba lishe wanaotoa huduma za chakula kwa wadau wa PBPA.

UJENZI SPORTS CLUB YATOA MSAADA KWA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUM DODOMA

Timu ya Ujenzi Sports Club imeendelea kuunga mkono juhudi za kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa kutoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mlezi jijini Dodoma.

Msaada huo umetolewa Jumatano, Septemba 2, 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Ujenzi Sports Club kuunga mkono kazi inayofanywa na shule hiyo katika kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na wanafunzi wengine kupata mazingira bora ya kujifunzia.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na madaftari, vyombo vya kulia chakula, vifaa vya usafi, sabuni, ndoo pamoja na fedha kwa ajili ya ununuzi wa mipira ya michezo.

Akikabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa Ujenzi Sports Club, Arch. Ibrahim Chatila, amesema klabu hiyo inatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na walimu katika kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kutimiza ndoto zao kielimu na katika maisha kwa ujumla.

Amesema msaada huo ni sehemu ya jitihada za Ujenzi Sports Club kuunga mkono juhudi zinazofanywa na shule hiyo, huku akiahidi kuwa klabu itaendelea kushirikiana na kuwahamasisha wadau wengine, hususan katika sekta ya ujenzi, kujitokeza na kusaidia juhudi hizo.

“Tunatambua kazi kubwa inayofanywa na walimu katika kuwalea na kuwawezesha watoto hawa. Msaada huu ni sehemu ya mchango wetu katika kuunga mkono juhudi hizo, na tutaendelea kuwahamasisha wadau wengine kujitokeza na kusaidia,” amesema Arch. Chatila.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mlezi, Bi. Magreth Kisanga, ameishukuru Ujenzi Sports Club kwa ukarimu na moyo wa kujitolea uliouonyesha kwa kuwasaidia wanafunzi hao.

Amesema msaada huo utasaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa baadhi ya vitendea kazi vinavyohitajika katika kuwawezesha wanafunzi kupata mazingira bora ya kujifunzia na kuishi shuleni.

Kwa upande wake, mwalimu anayesimamia kitengo cha wanafunzi wenye mahitaji maalum, Mwl. Hashim Msemo, amesema wanafunzi hao wamekuwa wakifanya vizuri katika masomo yao na wameendelea kufanya vyema katika mitihani yao.

Ametoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza na kuunga mkono juhudi za shule hiyo ili kuongeza fursa na mazingira bora kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Shule ya Msingi Mlezi ni shule jumuishi inayotoa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na wanafunzi wengine, kwa lengo la kuhakikisha kila mtoto anapata fursa sawa ya elimu na maendeleo

Friji Bovu: Libasse Gueye Mmoja ni Sawa na Mawinga Wote wa Ligi Kuu – Video

Global Publishers
September 3, 2026
0 views
0 Comments

Mchambuzi wa soka, David Pascol, maarufu kama ‘Friji Bovu’.

Mchambuzi wa soka, David Pascol, maarufu kama ‘Friji Bovu’, amesema atashangaa endapo kiungo mshambuliaji wa Simba SC, Libasse Gueye, hatashinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi kutokana na kiwango alichoonyesha katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara mwezi huu.

Akizungumza kupitia Global TV, Pascol amesema Libasse ni mchezaji bora na ameonyesha uwezo mkubwa ndani ya uwanja, huku akitoa kauli kali kwamba:
“Libasse Gueye mmoja ni sawa na mawinga wote wa Ligi Kuu Tanzania Bara.”

Kauli hiyo ameitoa alipofanyiwa mahojiano na mtangazaji wa Global TV, @officialcosmo_, huku akisisitiza ubora wa mshambuliaji huyo wa Simba katika kipindi hiki.