Taasisi ya Pamoja Tutashinda Tanzania (PATUTA) inatarajia kufanya tamasha la Mzizima Festival kuanzia Desemba 11 hadi 13 mwaka huu katika Viwanja vya Kijitonyama, jijini Dar es Salaam, likilenga kufufua na kurithisha mila, desturi na utamaduni wa Watanzania kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Tamasha hilo litahusisha vikundi 26 vya ngoma za asili kutoka makabila mbalimbali nchini, michezo ya jadi, burudani pamoja na mijadala kuhusu historia ya jamii na maadili.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya tamasha hilo, Mkurugenzi Mkuu wa PATUTA, Dk. Aidan Ndaombwa, amesema waandaaji wanaendelea kuwasiliana na vikundi vya ngoma za asili kuhakikisha vinashiriki katika tukio hilo.
Amesema tamasha hilo litatoa fursa kwa vijana kujifunza michezo ya jadi ikiwemo bao, iliyokuwa sehemu ya maisha ya wazee wao, pamoja na historia ya usafiri wa umma jijini Dar es Salaam, kuanzia UDA, daladala hadi usafiri wa mwendokasi.
Ameongeza kuwa historia ya Dar es Salaam kama kitovu cha biashara itajadiliwa, ikiwemo chimbuko na maendeleo ya Soko la Kariakoo pamoja na mchango wa wafanyabiashara kutoka maeneo na makabila mbalimbali nchini.
Dk. Ndaombwa amesema kutakuwa pia na mijadala itakayowakutanisha vijana na wazee waliowahi kushiriki katika shughuli za siasa, utamaduni na majeshi ili kueleza historia na uzoefu wao kwa kizazi kipya.
Amesema moja ya malengo ya tamasha hilo ni kukabiliana na changamoto ya kushuka kwa maadili katika jamii, akieleza kuwa michezo na shughuli za kitamaduni zilikuwa zikijenga mshikamano na kuimarisha mahusiano baina ya watu.
Kwa upande wake, Mratibu wa tamasha hilo, Mayasa Jabiri, amesema jina Mzizima linabeba historia ya Dar es Salaam na utamaduni wa ukarimu, hivyo tamasha hilo ni fursa ya kuitangaza Tanzania kama nchi yenye amani, fursa za kiuchumi na utamaduni unaowakaribisha wageni.
Amesema waandaaji wanashirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kuhakikisha tamasha hilo linafanikiwa na kuonyesha utamaduni halisi wa Tanzania.
Naye Afisa Sanaa wa BASATA, Gabriel Awe, amesema baraza hilo limeunga mkono maandalizi ya tamasha hilo baada ya waandaaji kufika ofisini kupata mwongozo kuhusu taratibu za kuandaa na kuendesha matamasha nchini.
Amesema tamasha hilo lina umuhimu katika kuimarisha utamaduni na maadili, hususan kwa vijana wanaohitaji kufahamu misingi ya maisha iliyokuwa ikifuatwa na wazee wao, huku akitoa wito kwa wadau na wadhamini kujitokeza kulisaidia.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa VOT Afrika Limited, Everest Oende, ameyahimiza makampuni na taasisi mbalimbali kuunga mkono tamasha hilo kwa kutumia jukwaa hilo kuonyesha mchango wao katika shughuli za kijamii na uhifadhi wa urithi wa taifa.
Amesema ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika kushirikiana na Serikali kuendeleza utamaduni wa Watanzania, hivyo kuzitaka kampuni kujitokeza kuiunga mkono PATUTA.
Amesema shughuli za tamasha hilo zitaanza asubuhi na kuendelea hadi usiku katika siku zote tatu, huku kukitarajiwa kuwepo kwa mgeni rasmi ambaye ni mtu mkubwa nchini.
Aidha, Watanzania, wadau na wanahabari wametakiwa kujitokeza kushiriki tamasha hilo ili kupata fursa ya kujifunza na kushuhudia historia na utamaduni wa jamii mbalimbali nchini.
