Watu 63 Wafunguliwa Mashtaka ya Uhalifu wa Uchaguzi Marekani

Global Publishers
November 4, 2026
18 views
0 Comments

Wizara ya Sheria ya Marekani (Department of Justice – DOJ) imetangaza kufunguliwa kwa mashtaka dhidi ya watu 63 wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo mbalimbali vya ukiukwaji wa sheria za uchaguzi nchini humo, ikiwemo kupiga kura kinyume cha sheria na kufanya udanganyifu katika usajili wa wapiga kura.

Taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo Novemba 2, 2026, imeeleza kuwa miongoni mwa watuhumiwa hao wapo raia wanne wa kigeni ambao kwa mujibu wa mamlaka hiyo wanaishi nchini Marekani bila kuwa na vibali halali vya ukaazi.

Kwa mujibu wa DOJ, makosa yanayohusishwa na watuhumiwa hao ni pamoja na raia wasio na uraia wa Marekani kushiriki katika uchaguzi wa Shirikisho, kutoa taarifa za uongo kuhusu uraia wa Marekani ili kujisajili kama wapiga kura na kuwasilisha maombi ya usajili wa wapiga kura kwa njia za udanganyifu.

Akizungumzia hatua hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Todd Blanche, amesema tangazo hilo linaashiria ongezeko kubwa la hatua za kukabiliana na udanganyifu wa uchaguzi tangu Rais Donald Trump arejee madarakani.

Blanche amesisitiza kuwa Wizara ya Sheria itaendelea kuchunguza na kuwafikisha mahakamani wote watakaobainika kukiuka sheria za uchaguzi ili kurejesha imani ya wananchi katika mfumo wa uchaguzi nchini humo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa katika kipindi cha wiki tisa zilizopita, Wizara hiyo imewafungulia mashtaka raia 195 wa kigeni katika majimbo 25 kwa makosa yanayohusiana na upigaji kura na usajili wa wapiga kura kinyume cha sheria.

Hata hivyo, Wizara ya Sheria imeweka wazi kuwa mashtaka yaliyotangazwa ni tuhuma ambazo bado zinapaswa kuthibitishwa mahakamani, hivyo watuhumiwa wote wanachukuliwa kuwa hawana hatia hadi pale watakapothibitika kuwa na hatia kwa mujibu wa sheria.

Kim Kardashian Arejea Kwenye Msimu wa Pili Wa ‘All’s Fair’ Licha ya Kukosolewa Vikali

Mwigizaji na mfanyabiashara maarufu wa Marekani, Kim Kardashian, amerejea katika msimu wa pili wa tamthilia ya kisheria ya All’s Fair, licha ya msimu wake wa kwanza kukumbwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa wakosoaji wa filamu na televisheni.

Kardashian, ambaye anacheza nafasi ya Allura Grant katika tamthilia hiyo iliyoundwa na mtayarishaji Ryan Murphy, amesema timu ya utayarishaji imeamua kukubali maoni ya watazamaji na kuelekeza zaidi tamthilia hiyo katika vichekesho.

Awali, All’s Fair ilikusudiwa kuwa tamthilia nzito inayohusu masuala ya sheria, lakini badala yake ilijikuta ikivutia mjadala mkubwa kutokana na uigizaji, mavazi na mazungumzo yaliyotumiwa na waigizaji wake.

Baadhi ya wakosoaji waliikosoa vikali, huku gazeti la The Times likiielezea kama moja ya tamthilia mbaya zaidi kuwahi kutengenezwa.

Hata hivyo, ukosoaji huo haukuzuia mafanikio yake kwa upande wa watazamaji. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tamthilia hiyo iliweka rekodi ya kuwa mwanzo uliotazamwa zaidi kwa tamthilia zilizoandaliwa na Hulu katika kipindi cha miaka mitatu.

Kardashian amesema badala ya kukata tamaa kutokana na maoni hasi, wameamua kuyatumia kama sehemu ya kuboresha msimu unaofuata.

Amesema kurejea kwao kumewapa nafasi ya kuendeleza vichekesho na matukio ya kusisimua ambayo watazamaji walionekana kuyafurahia.

Kwa upande wake, mwigizaji mwenzake Naomi Watts amesema Kardashian ameonyesha maendeleo katika uigizaji wake kwenye msimu wa pili, akibainisha kuwa amekuwa akijiamini zaidi na kuonyesha uwezo wa kubuni mazungumzo wakati wa kurekodi.

Mbali na kazi yake ya uigizaji, Kardashian pia amezungumzia safari yake ya kutaka kuwa mwanasheria. Ameeleza kuwa bado hajaachana na ndoto hiyo licha ya kushindwa kufaulu mtihani aliokuwa akiutarajia baada ya miaka sita ya masomo kupitia mfumo wa mafunzo ya sheria.

Amesisitiza kuwa kushindwa katika jambo fulani hakumaanishi mwisho wa safari, akisema ataendelea kujitahidi hadi atakapofikia lengo lake.

Kardashian pia amesema amejifunza kukabiliana na ukosoaji baada ya kuwa kwenye uangalizi wa umma kwa zaidi ya miaka 20.

Kwa sasa, msimu wa pili wa All’s Fair unatarajiwa kuendeleza mchanganyiko wa mitindo ya mavazi ya kifahari, drama na vichekesho, huku Kardashian na waigizaji wenzake wakijaribu kuendeleza umaarufu wa tamthilia hiyo licha ya changamoto ilizokutana nazo awali.

MAKAMU WA RAIS MHE NDEJEMBI AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZONA RAIS WA UGANDA MHE YOWERI MUSEVENI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Bomba la Mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Tanga Tanzania.

 

Mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu ya Entebbe nchini Uganda, yanalenga kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Uganda katika miradi ya kimkakati ikiwemo sekta ya mafuta na gesi.

 

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe, Balozi wa Tanzania nchini Uganda Mhe. Meja Jenerali Marco Gaguti, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia mafuta na gesi Dkt. James Mataragio, Kamishna wa Mafuta na Gesi Bw. Goodluck Shirima pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mussa Makame.

 

DCP LYIMO AHIMIZA MIRADI YENYE TIJA KWA WANACHAMA WA MTANDAO WA WANAWAKE

DODOMA.

Mwenyekiti wa Mtandao wa wanawake wa Jeshi la Magereza, Naibu Kamishna wa Magereza (DCP) Lipina Lyimo, leo Novemba 4, 2026, ameongoza kikao cha majumuisho ya tathmini ya Mkutano Mkuu wa Mtandao wa Wanawake wa Jeshi la Magereza, kilichowakutanisha washiriki kutoka Mkoa wa Dodoma. Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Msalato, jijini Dodoma.

Akizungumza katika kikao hicho, DCP Lyimo amewashauri wanawake hao kupendekeza miradi yenye tija itakayoongeza thamani ya michango ya wanachama wa mtandao huo. Aidha, ameitaka Sekretarieti kupokea na kufanyia kazi maoni ya wanachama ili kuwezesha tathmini, majumuisho na maandalizi bora ya mkutano mkuu ujao.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Edith Mbogo amewataka washiriki kuzingatia usalama na faragha zao kwa kuepuka kurekodi na kusambaza picha binafsi kwenye mitandao ya kijamii. Ushauri huo ameutoa akishirikisha uzoefu alioupata wakati wa kuhudhuria mafunzo ya uongozi nchini Indonesia.

Naye Mhandisi wa Jeshi la Magereza, Mrakibu Mwandamizi wa Magereza (SSP) Bonaza Malata, amewasilisha taarifa kuhusu mafunzo ya uongozi yaliyowashirikisha viongozi wanawake wanane kutoka Jeshi la Magereza, yaliyofanyika katika Shule ya  Uongozi Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha kwa Mfipa Pwani

Mafunzo hayo yalijikita katika maeneo mbalimbali, yakiwemo uongozi binafsi na kitaasisi, usimamizi wa rasilimali watu, uongozi wa kimkakati, utatuzi wa migogoro, usimamizi wa miradi, mawasiliano, matumizi ya Akili Mnemba (AI), teknolojia za kidijitali, usalama wa taarifa na uwezeshaji wa wanawake katika uongozi.

Akitoa ufafanuzi kuhusu uendeshaji wa mtandao huo, Katibu wa Mtandao wa Wanawake wa Jeshi la Magereza, INSP Scholastica Ndunguru, amesema mtandao una Katiba inayoweka mwongozo wa uendeshaji wa vikao na mikutano mbalimbali. Aidha, amewahimiza wanachama kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha utekelezaji wa majukumu ya mtandao huo.

Amesema mtandao huo ulianzishwa mwaka 2018 ukiwa na malengo mbalimbali, ikiwemo kuongeza uelewa wa wanawake kuhusu masuala yanayohusu mazingira yao ya kazi, pamoja na kusimamia haki na stahiki za makundi maalumu ya wahalifu wa kike, wakiwemo wajawazito, wanawake wenye watoto na watoto walio katika mgogoro na sheria.

TNCC yasisitiza uaminifu kuimarisha biashara – HabariLeo

KIGOMA: CHEMBA ya Taifa ya Biashara (TNCC) mkoani Kigoma imewataka wafanyabiashara wa mkoa huo kuzingatia uaminifu na uadilifu wanapofanya biashara na raia kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ili kuimarisha uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili.

Meneja wa TNCC Mkoa wa Kigoma, Prosper Guga, amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma, akieleza kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya wafanyabiashara wa DRC kuhusu changamoto ya uaminifu Kigoma.

Amesema suala hilo hivyo vinaweza kudhoofisha imani na kuathiri ushirikiano wa kibiashara baina ya wafanyabiashara wa nchi hizo mbili.

Guga amesema wafanyabiashara wanapaswa kuzingatia maadili, kutimiza makubaliano na kujenga uaminifu, kwa kuwa biashara za kuvuka mipaka zinahitaji mahusiano ya muda mrefu na kuaminiana.

Ameeleza kuwa TNCC imeingia makubaliano na Chemba ya Biashara ya DRC kwa lengo la kukuza biashara na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa nchi hizo.

Katika hatua nyingine, amesema TNCC imeanza kushughulikia malalamiko ya mfanyabiashara mmoja kutoka DRC aliyedai kutapeliwa zaidi ya Sh milioni 90 na mfanyabiashara wa Kigoma mwaka 2024.

Amesema kupitia ufuatiliaji uliofanywa na taasisi hiyo, mfanyabiashara anayedaiwa kuhusika na deni hilo ameanza kurejesha fedha hizo, ambapo hivi karibuni alilipa Sh milioni 20.

Kwa upande wake, mfanyabiashara kutoka DRC, Anne Shilwalwa Maombi, amesema alikuwa akishirikiana na mfanyabiashara mmoja wa Kigoma aliyekuwa akimletea unga wa ngano kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma, kisha yeye kuusafirisha kwenda DRC.

Amesema kutokana na ushirikiano huo, alimwamini mfanyabiashara huyo na kumpatia Sh milioni 90 mwaka 2024 ili awe wakala wao, lakini fedha hizo zilitumika kwa manufaa yake binafsi badala ya kutekeleza makubaliano yao.

 

TANGA NA MKAKATI WA KUINUA ZAO LA MACHUNGWA

Mkoa wa Tanga ni maarufu kwa uzalishaji wa matunda nchini. Machungwa ni miongoni mwa matunda yanayozalishwa kwa wingi katika wilaya za Muheza, Korogwe na Handeni mkoani humo.

Wakulima wa zao hili hufanya jitihada kubwa za uzalishaji, lakini bado hawajafaidi vya kutosha jasho lao. Wakulima hutegemea baada ya kuvuna, wauze machungwa kwa bei nzuri ambayo itarejesha gharama za uendeshaji.

Aidha, wakulima hao hutegemea kupata faida kwani kwao kilimo hicho ni ajira kwa ajili ya kuendesha maisha yao na kufanya mambo mengine ya maendeleo kama kusomesha watoto, kujenga nyumba, kufungua biashara, kununua vyombo vya moto za usafiri, kutaja kwa uchache.

Miongoni mwa changamoto katika kilimo cha machungwa ni bei ndogo na kukosa soko la uhakika. Hili limesababisha wakulima kuuza machungwa yao mashambani kwa madalali.

Kwa kufanya hivyo, wakulima wamejikuta wakiuza machungwa yao kwa bei ndogo huku madalali wakinufaika pasi na kumwaga jasho kama walivyomwaga wakulima.

Kutokana na changamoto hizi, serikali ya mkoa wa Tanga chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa, Balozi Dk. Batilda Buriani, umejizatiti kuinua zao hili ili libadili hali za maisha ya wakulima na kuchangia katika maendeleo.

Novemba 1, 2026, katika kikao cha viongozi wa mkoa na wilaya, Dk. Buriani alisema, mkoa wa Tanga huzalisha asilimia 60 ya machungwa yote nchini, hivyo ni muhimu kuweka mazingira mazuri ya biashara hiyo ili iwanufaishe wakulima.

“Tumepiga marufuku madalali kununua machungwa mashambani, machungwa yatauzwa katika vituo maalum, hii itasaidia machungwa kuuzwa kwa bei nzuri,” amesema Dk. Buriani.

Katika hatua nyingine, Dk. Buriani amesema, serikali mkoani humo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), watajenga vituo vinne ambapo wanunuzi wa machungwa watakwenda kununua moja kwa moja katika vituo hivyo kwa bei elekezi.

Kimsingi, ujenzi wa vituo hivi na kuwa na bei elekezi ya machungwa ni mkakati mzuri wa kuinua zao hili. Ni wakati muafaka sasa kwa wakulima kufaidi jasho lao na kuona fahari kulima machungwa kwani sasa kilimo hicho kitalipa na chenchi itabaki.

Wataalamu watakiwa kutumia teknolojia akili unde kuboresha utendaji – HabariLeo

ARUSHA; Wataalamu wa kada mbalimbali wametakiwa kujifunza na kutumia teknolojia ya akili unde (AI) katika kuboresha utendaji wa majukumu yao.

Aidha walimu na wahadhiri wamehimizwa kuiboresha mifumo ya ufundishaji na tathmini ili kuhakikisha wanafunzi wanaitumia teknolojia hiyo kama nyenzo ya kujifunzia, badala ya kutegemea kufanya kazi zinazopaswa kutekelezwa na wao wenyewe.

Mwito huo umetolewa na Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Profesa Eliamani Sedoyeka katika kongamano la kitaaluma lililoandaliwa na chuo hicho na kuwakutanisha wanafunzi wa shahada ya uzamili, wanataaluma na wadau mbalimbali kwa lengo la kujadili changamoto zinazoikabili jamii na kuangalia namna ya kuzitatua kupitia tafiti na maarifa yao jijini Dar es Salaam leo.

“Mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea duniani hayawezi kuzuiliwa, hivyo ni muhimu kwa walimu, wahadhiri na wataalamu wa kada mbalimbali kujifunza namna ya kuitumia AI katika kuboresha utendaji wao wa kitaaluma,” alisema.

Alisema wataalamu wanapaswa kuhakikisha wanapata mafunzo ya teknolojia hiyo ili kuelewa namna inavyoweza kutumika katika fani zao na kuongeza ufanisi katika majukumu wanayotekeleza.

Akizungumzia matumizi ya AI katika elimu, Profesa Sedoyeka alisema teknolojia hiyo inaweza kusaidia katika tafiti kwa kubaini maeneo ambayo tayari yamefanyiwa utafiti na yale ambayo bado yana mapengo ya maarifa yanayohitaji kuchunguzwa huku akisisitiza kuwa matumizi hayo yanaweza kuwawezesha wanafunzi na watafiti kutambua maeneo mapya ya kufanyia tafiti na kurahisisha mchakato wa kupata taarifa za kitaaluma.

Alisisitiza kuwa changamoto kubwa ni baadhi ya wanafunzi kutumia AI kufanya kazi zao na kuwasilisha matokeo kana kwamba wamezifanyia wao wenyewe, jambo linaloweza kudhoofisha malengo ya elimu ya kuwajengea maarifa, ujuzi, weledi na kubadili tabia.

Alisema walimu wanapaswa kubuni namna mpya za kutoa kazi na mitihani zitakazohakikisha wanafunzi wanapata ujuzi unaokusudiwa hata wanapotumia teknolojia hiyo.

Kwa upande wake Mhitimu wa Shahada ya Uzamili ya Uongozi na Utawala Bora kutoka IAA, Sharfani Zuberi amewataka wanafunzi hasa wa vyuo vikuu kuepuka matumizi mabaya ya AI katika kufanya tafiti na kuandika kazi za kitaaluma, bali watumie maarifa na uwezo wao binafsi ili kulinda ubora na uadilifu wa taaluma.

“Naomba wanafunzi waache kutumia AI kwa namna hasi, kwa sababu taaluma haina udanganyifu. Tujaribu kutumia akili zetu darasani, tunapoandika makala na tunapochapisha tafiti zetu,” alisema.

Katika utafiti aliouwasilisha, Zuberi alisema alijikita kuchunguza nafasi ya mawasiliano kati ya menejimenti na wafanyakazi, akieleza kuwa mawasiliano ni nyenzo muhimu katika kufanikisha malengo ya taasisi.

TANZANIA, DRC KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI NA KIUSALAMA

 

Na Hamida Ramadhan, Dodoma Matukio Daima Media Dodoma

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Judith Suminwa Tuluka, ameishukuru Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kushirikiana na nchi hiyo katika masuala ya usalama na maendeleo ya kiuchumi, akisema ushirikiano huo ni muhimu katika kulinda maslahi ya mataifa hayo mawili.

Akiongea leo Novemba 4 Mara baada ya kumaliza ziara ya  kutembelea mji wa Serikali Mtumba Dodoma, Waziri Mkuu huyo, amesema Tanzania na DRC zina uhusiano wa muda mrefu uliojengwa katika misingi ya undugu na ujirani mwema, hivyo ni muhimu kuendelea kuimarisha ushirikiano huo ili kulinda usalama na kukuza uchumi wa nchi hizo.

Ameeleza kuwa ushirikiano huo utaendelea kuimarishwa kupitia maeneo mbalimbali yenye maslahi ya pamoja, ikiwamo juhudi za kuendeleza miji na kuboresha mazingira ya maendeleo kwa wananchi wa nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi wa DRC, John Banza Lunda, amesema amevutiwa na hatua za maendeleo ya miundombinu zilizofikiwa na Tanzania, akieleza kuwa ziara yake nchini imempa fursa ya kujionea uwekezaji uliofanywa na Serikali katika sekta hiyo.

Banza Lunda amesema safari yake kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma imemwezesha kushuhudia maendeleo ya miundombinu ya usafiri, pamoja na uwekezaji katika majengo ya umma, ikiwamo Bunge na Mji wa Serikali wa Mtumba.

Amesema Tanzania imepiga hatua katika kuimarisha miundombinu, jambo ambalo ni muhimu katika kurahisisha usafiri, kuboresha utoaji wa huduma na kukuza uchumi wa taifa.

Ameeleza kuwa serikali ya nchi yake pia inaendelea kuweka juhudi katika kujenga na kuimarisha miundombinu ndani ya DRC ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, amesema anatarajia kutumia Treni ya Reli ya Kisasa (SGR) kusafiri kurejea Dar es Salaam ili kujionea zaidi uwekezaji uliofanywa na Tanzania katika sekta ya usafiri wa reli.

Waziri huyo ameishukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ukarimu na mapokezi mazuri aliyoyatoa kwa ujumbe wa DRC wakati wa ziara yao nchini.

“Katika kuimarisha miundombinu ya usafirishaji, Banza Lunda amesema DRC inaendelea na juhudi za kuendeleza bandari katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, ambayo inatarajiwa kuanza kufanya kazi Machi 2027,” Amesema.

Na Kuongea “mesema bandari hiyo itakuwa muhimu katika kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kukuza biashara katika maeneo yanayozunguka Ziwa Tanganyika, hususan katika kuimarisha shughuli za kiuchumi za wananchi wa maeneo hayo, ” Amesema waziri Lunda

Naye Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, amesema Tanzania imefurahi kupokea ujumbe kutoka DRC kwa ziara ya kindugu na kirafiki inayolenga kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya mataifa hayo.

Kairuki amesema mahusiano ya Tanzania na DRC hayajaanza leo, bali yamejengwa kwa muda mrefu kutokana na historia ya undugu, ujirani na ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo mbili.

Amesema ziara hiyo ni fursa muhimu ya kuendeleza urafiki na kuimarisha mahusiano yaliyopo, huku akieleza kuwa Tanzania inathamini uhusiano huo na itaendelea kujenga mazingira mazuri ya ushirikiano na taifa hilo.

Ameongeza kuwa ziara za aina hiyo zina nafasi kubwa katika kuimarisha mshikamano wa mataifa hayo na kufungua fursa zaidi za kushirikiana katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na DRC.

NCHI ZA EAC ZATAKIWA KUJIPANGA KUKABILIANA NA ATHARI ZA EL NIÑO

Na, Mwandishi Wetu – Nairobi, Kenya

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimetakiwa kuimarisha ushirikiano na kuchukua hatua za haraka kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa za El Niño, zikiwemo mafuriko, maporomoko ya ardhi, uharibifu wa miundombinu na kuathirika kwa biashara na maisha ya kawaida ya wananchi.

Wito huo umetolewa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Dharura wa Wataalamu wa Sekta Mbalimbali kuhusu Maandalizi na Mwitikio wa Kikanda dhidi ya Mvua Zinazotarajiwa za El Niño Kali, unaofanyika Nairobi, Kenya, kuanzia Novemba 4 hadi 6, 2026.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo wa wataalamu  umeongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Brigedia Jenerali Hosea Ndagala.

Akifungua mkutano huo Mratibu wa Mradi wa Pamoja wa Sekta Mbalimbali wa Usalama wa Chakula na Lishe wa Uganda, Bw.Julius Twinamatsiko amesema utabiri unaonesha uwezekano wa mvua kunyesha kwa kiwango kikubwa kuliko kawaida katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2026, hali inayohitaji maandalizi ya haraka na hatua za pamoja.

Amezitaka nchi wanachama kubaini maeneo hatarishi katika miundombinu ya usafirishaji, kuandaa njia mbadala, kuhakikisha upatikanaji wa chakula na malisho ya mifugo, pamoja na kuimarisha huduma za afya na ufuatiliaji wa magonjwa yanayoweza kuenea kutokana na mafuriko.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Sekretarieti ya EAC amesisitiza kuwa athari za El Niño zinaweza kuhatarisha amani, usalama na maendeleo ya kiuchumi, hivyo juhudi za kila nchi zinapaswa kuunganishwa kupitia mpango wa pamoja wa kikanda.

Mkutano huo unalenga kutathmini uwezo wa nchi wanachama kukabiliana na athari zinazotarajiwa, kubaini mapungufu na kuandaa mpango wa uratibu wa kikanda utakaosaidia kulinda maisha ya wananchi, huduma muhimu na shughuli za biashara katika Afrika Mashariki.

=MWISHO=

 

NECTA 2026: HIZI HAPA SHULE 48 ZILIZOFANYA MTIHANI WA DARASA LA SABA MANISPAA YA IRINGA

 

NA MATUKIO DAIMA MEDIA, IRINGA

Orodha ya shule 48 pamoja na nafasi zake katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kumaliza Elimu ya Msingi, Darasa la Saba mwaka 2026, katika Manispaa ya Iringa imeonesha ushindani wa kitaaluma kati ya shule mbalimbali za serikali na binafsi.

Kwa mujibu wa orodha ya matokeo ya NECTA Iringa Manispaa 2026, Shule ya St Dominic Ngelewala imeongoza kwa kupata wastani wa alama 279.0455, ikifuatiwa na Shule ya Good Victory iliyoshika nafasi ya pili kwa wastani wa alama 277.2344.

Nafasi ya tatu imechukuliwa na St Dominic Mkim­bizi kwa wastani wa alama 264.2247, huku St Dominic Kigon­zile ikishika nafasi ya nne kwa wastani wa alama 258.4597.

Shule ya SIPTO imechukua nafasi ya tano kwa wastani wa alama 258.4167, ikifuatiwa na Gangilonga iliyoshika nafasi ya sita kwa alama 254.069.

Shule nyingine zilizoingia katika kumi bora ni St Dominic Main nafasi ya saba, Moria nafasi ya nane, Star nafasi ya tisa na Legacy iliyoshika nafasi ya kumi.

Kwa mujibu wa orodha hiyo, shule zilizoshika nafasi ya 11 hadi 48 ni Mapinduzi, Peace Flame, TY Ndendya, Hyperlink, Jordan, St Charles, Sun, Lugalo, Ukombozi, Ummusalama, Highland, Wilolesi, Tumaini, Mungano, Umoja, Jitegemee, Igeleke, Kigamboni, Ugele, Njia Panda, Nyumbatatu, Igumbilo, Sabasaba, Kihesa, Maendeleo, Mlangali, Zizi, Ngome, Nduli, Mawelewele, Itamba, Hoho, Kitasengwa, Mkim­bizi, Mshikamano, Mtwivila, JJ Mungai na Mlande­ge.

Orodha hiyo inaonesha nafasi ya kila shule pamoja na wastani wa alama zilizopatikana, ikiwa ni sehemu ya tathmini ya mwenendo wa ufaulu wa shule katika Manispaa ya Iringa.

Hata hivyo, matokeo hayo yanaendelea kuwa sehemu muhimu kwa wazazi na walezi katika kufuatilia maendeleo ya elimu na kujua nafasi zilizopatikana na shule za watoto wao.

JE, MTOTO WAKO ANASOMA SHULE IPI NA SHULE HIYO IMESHIKA NAFASI YA NGAPI KATIKA ORODHA HII?

Tuandikie kwenye sehemu ya maoni.