Waziri Katambi Atoa Ufafanuzi kuhusu Mfumo wa Alama za leseni

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Paschal Katambi Patrobass, amesema Serikali imeanza kufanya majaribio ya mfumo wa alama za leseni za udereva kwa lengo la kudhibiti makosa ya usalama barabarani na kupunguza ajali nchini.

Akizungumza kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa Septemba 19, 2026, Waziri Katambi amesema mfumo huo unatokana na Kanuni za Usalama Barabarani (Mfumo wa Alama za Leseni za Udereva) za mwaka 2014, ambazo zilirekebishwa mwaka 2025.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chini ya Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, Waziri mwenye mamlaka ya kutunga kanuni kuhusu masuala ya usalama barabarani anaweza kuweka mfumo wa kupunguza vifo na ajali zinazotokana na sababu mbalimbali, ikiwemo makosa yanayofanywa na madereva wa vyombo vya usafiri.

Serikali imeeleza kuwa imefanya kazi ya muda mrefu na imejiridhisha kuwa hakuna haja ya kuanza kutumia mfumo huo madhubuti wa kudhibiti usalama barabarani.

Aidha, Serikali imeeleza kuwa pamoja na miradi ya usalama barabarani inayoendelea, ikiwemo matumizi ya teknolojia za kamera za barabarani zenye uwezo wa kutumia akili unde (AI), imeanza majaribio ya mfumo wa alama za leseni za udereva.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa mfumo huo bado haujaanza kutumika rasmi, bali hatua ya sasa ni kufanya majaribio ili kubaini namna utakavyoweza kutumika kudhibiti madereva watakaokiuka Sheria na Kanuni za Usalama Barabarani.

Serikali imeonya madereva kuwa leseni zao zikiingizwa kwenye mfumo huo, alama zitakazotolewa kutokana na makosa ya barabarani zinaweza kuathiri uhalali wa leseni zao iwapo wataendelea kukiuka sheria.

Waziri Katambi amesema baadhi ya alama zinazoweza kuhusishwa na makosa ya barabarani ni pamoja na makosa ya mwendokasi, kutofuata alama za barabarani, kuzidisha abiria, kutoa mikanda, kuendesha vyombo hatarishi na makosa mengine kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168.

Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza ajali za barabarani zinazosababisha vifo na majeruhi, akieleza kuwa matumizi ya mifumo kama hiyo yamekuwa yakiongezeka katika nchi mbalimbali.

Ametolea mfano Rwanda, ambayo amesema imetumia mfumo huo na kuona kupungua kwa kiwango kikubwa cha ajali na vifo vinavyotokana na ajali za barabarani.

Waziri Katambi pia amesisitiza kuwa Kanuni za Usalama Barabarani (Mfumo wa Alama za Leseni za Udereva) za mwaka 2014, zilizorekebishwa mwaka 2025, bado hazijaanza kutekelezwa rasmi.

Amesema sababu mojawapo ya kutocheleweshwa kwa utekelezaji wake ni kuwa wataalamu wa mifumo kutoka Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Mapato wanaendelea kuunganisha mifumo hiyo ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi.

Sababu nyingine, kwa mujibu wa Waziri, ni kwamba Serikali iko katika kipindi cha utoaji elimu kwa umma kuhusu kanuni hizo. Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani linaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya madereva wa vyombo vya moto pamoja na wananchi kwa ujumla kuhusu mfumo huo na umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Waziri amesema Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani linaendelea kufikisha elimu hiyo kwa makundi mbalimbali ya madereva kupitia mikutano ya uelimishaji, pamoja na vyombo vya habari kama redio na Runinga, katika vituo vya mabasi, maeneo ya maegesho ya malori, mikusanyiko ya watu na maeneo mengine.

Ameongeza kuwa elimu hiyo inalenga kuwaelimisha wananchi kuhusu makosa yanayoweza kupewa alama na namna alama hizo zitakavyotumika.

Waziri Katambi amesisitiza kuwa mfumo huo bado haujaanza kutekelezwa rasmi, hivyo hakuna haja ya dereva ambaye leseni yake imeondolewa alama kutokana na kosa la barabarani kuwa na wasiwasi kwa sasa.

Amesema madereva watajulishwa rasmi pindi mfumo huo utakapoanza kutumika.

Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Paschal Katambi Patrobass, Septemba 19, 2026, jijini Dar es Salaam.

MAKAMU WA RAIS AZITAKA TAASISI ZA MUUNGANO KUIMARISHA USHIRIKIANO, HUDUMA KWA WANANCHI

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, amezitaka Taasisi za Muungano kuimarisha ushirikiano, kubaini na kutumia fursa zilizopo pamoja na kushiriki kwa pamoja katika shughuli mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuongeza tija na kuleta manufaa zaidi kwa Watanzania.

 

Makamu wa Rais ametoa wito huo leo, Septemba 19, 2026 wakati akifungua kikao cha Wakuu wa Taasisi za Muungano kilichofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip, Zanzibar, na kuhudhuriwa na wakuu wa Taasisi 39 za Muungano.

 

Makamu wa Rais amewataka viongozi wa taasisi hizo kuelewa kwa kina wajibu wao katika kuwahudumia wananchi na kufanya kazi kwa mtazamo mmoja wa kujenga “nyumba moja”, huku maslahi ya Watanzania yakiwekwa mbele.

 

Amesema matarajio ya wananchi ni kuona Muungano na taasisi zake zikitoa matokeo yanayogusa maisha yao moja kwa moja, hususan katika kuboresha hali ya uchumi, afya, elimu na maeneo mengine muhimu ya kijamii.

 

Amezihimiza taasisi hizo kuondoa vikwazo vinavyoweza kudhoofisha ushirikiano na badala yake kutumia fursa zilizopo katika pande zote mbili za Muungano ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

 

Aidha, Mhe. Ndejembi ameahidi kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kuunga mkono jitihada za Taasisi za Muungano kwa kuratibu, kusimamia, kushauri na kuziwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi, kwa lengo la kuharakisha maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.

 

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema kikao hicho kinalenga kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za Muungano na Ofisi ya Makamu wa Rais; na kuongeza uelewa wa pamoja kuhusu masuala mbalimbali ya Muungano na majukumu yanayotekelezwa na taasisi hizo, sambamba na kuweka mwelekeo wa kuimarisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi.

 

Kikao hicho cha Wakuu wa Taasisi za Muungano ambacho pia kimehudhiriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mhe Hamza Hassan Juma, Makatibu Wakuu na Watendaji Wakuu wa Taasisi kinatoa  nafasi kwa viongozi hao kujadili namna ya kuimarisha uratibu, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja itakayoongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao kwa manufaa ya wananchi.

 

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

19 Septemba 2026

Zanzibar.

WAZIRI MKUU KUMWAKILISHA RAIS DKT. SAMIA KATIKA MKUTANO WA AFYA MOJA NCHINI ITALIA

 

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ameondoka nchini leo (Jumamosi, Septemba 19, 2026) kwenda Roma, Italia kumwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa siku tatu wa Kimataifa wa Kujadili Afya Moja na Mifumo ya Chakula na Kilimo.

 

Mkutano huo utakaofanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), jijini Roma, Italia kuanzia Septemba 21–23, 2026 unalenga kuimarisha utekelezaji wa dhana ya Afya Moja (One Health) inayotambua uhusiano kati ya afya ya binadamu, wanyama, mimea na mazingira, kwa lengo la kuhakikisha mifumo endelevu ya chakula na kilimo

 

Mkutano huo utahusisha viongozi wa nchi na Serikali, wakiwemo Marais kati ya watano hadi saba, Mawaziri kati ya 30 hadi 50, pamoja na wawakilishi wa taasisi za kikanda na kimataifa, wadau wa maendeleo, sekta binafsi, taasisi za utafiti na mashirika ya kimataifa.

 

Mambo muhimu yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni Ujumuishaji wa dhana ya Afya Moja (One Health) katika sera na uwekezaji wa mifumo ya chakula na kilimo; na uimarishaji wa ushirikiano wa kisekta kati ya sekta za kilimo, mazingira, afya, fedha na mipango ya miji.

 

Mengine ni ukuzaji wa ubunifu, sayansi na maarifa ya ndani ili kuboresha uzuiaji wa vihatarishi, ufuatiliaji na usimamizi endelevu wa rasilimali na kuhamasisha uwekezaji na ushirikiano ili kutafsiri ahadi kuwa hatua madhubuti zenye matokeo yanayopimika.

UBORESHAJI MIUNDO MBINU KUCHOCHEA SHUGHULI ZA UCHUMI NA BIASHARA – WAZIRI KAPINGA

Na Fadhili Abdallah, Kigoma

SERIKALI ya Tanzania imesema kuwa maboresho makubwa ya miundo mbinu ya usafiri na usafirishaji yaliyofanyika nchini yanalenga kuboresha shughuli za uchumi na biashara ili kuwafanya watanzania wengi kutumia fursa hizo katika kuimarisha shughuli zao za kiuchumi biashara.

Waziri wa viwanda na biashara, Judith Kapinga amesema hayo mkoani Kigoma  akifungua Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Ziwa Tanganyika yanayofanyika katika viwanja vya Mwanga Community mkoani Kigoma ambapo alisema kuwa serikali  inawekeza fedha nyingi katika kuboresha miundo mbinu ili kuweka mazingira yatakayowawezesha Watanzania  wengi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi na biashara  ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa yam waka 2025 hadi 2050

Katika hotuba ya Waziri Kapinga iliyotolewa kwa niaba yake na Naibu Waziri wa viwanda na biashara, Dennis Londo alisema kuwa serikali imefanya  uwekezaji mkubwa  katika miundombinu yaa reli, barabara, meli, reli na katika mazingira ya biashara ikilenga kuwawezesha wananchi kutumia fursa zilizopo ndani na nje ya nchi kufanya biashara kwa  masoko ya nchi za ukanda wa Maziwa Makuu.

Kupitia Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Ziwa Tanganyika Waziri Kapinga alitaka yawe  jukwaa muhimu la kuwaunganisha wafanyabiashara, wazalishaji, wawekezaji na wadau mbalimbali wa biashara kutoka ndani na nje ya Tanzania hivyo maonyesho hayo siyo tu kwa ajili ya kuonyesh bidhaa bali kutengeneza mtandao wa kushirikiana katika biashara na uwekezaji.

Awali Katibu Tawala wa mkoa Kigoma,Hassan Rugwa alisema kuwa mkoa Kigoma umekuwa mkoa Kimkakati kutokana na nafasi yake kupakana na nchii jirani za maziwa makuu ambazo zinatoa fursa kubwa ya kufanya biashara na shughuli za uchumi kwa ukubwa kwani ndiyo nchi ambazo hata asilimia 70 ya mizigo inayopitia bandari ya Dar es Salaam inapotia huku.

Rugwa alisema kuwa mikoa ya ukanda wa mashariki ya nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) inategemea kwa sehemu kubwa ya mahitajii yao ya chakula,matunda,bidhaa za  ujenzi na mahitaji mengine ya kibinadamu na maendeleo wanategemea kutoka Tanzania kupitia mkoa Kigoma hivyo maonyesho hayo yanafanyika kuwaweka pamoja wadau wa biashara kuzungumzia fursa hizo na mipango katika jambo hilo.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara  Tanzania (TNCC) alisema kuwa maonyesho hayo kwa mkoa Kigoma yanafanyika ili kuunga mkono Mpango wa serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuufanya mkoa Kigoma kuwa mkoa wa kimkakati wa uchumi na biashara hivyo maonyesho hayo yanawaleta pamoja wadau wa uchumi na biashara kutoka nchi hizo kukaa pamoja kuona namna ambavyo biashara na shughuli za uchumi zinavyoweza kufanyika kwa pamoja na tija kubwa.

Mwisho.

 

RC CHALAMILA AFIKA MTAA WA MADALE KINONDONI KUTATUA MGOGORO WA ARDHI

-Aagiza kukamatwa kwa familia ya Mushi kutokana na kushindwa kufika eneo la tukio.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila ameagiza familia ya Devid Mushi kukamatwa na kufikishwa kituo cha polisi cha Oysterbay hadi siku ya jumatatu septemba 21,2026 baada ya kudharau wito wake alipotembelea eneo la mtaa wa Madale wilaya ya Kinondoni ulipokuwa mgogoro wa ardhi baina ya familia hiyo na familia ya Abdallah Msham Kitwanga

RC Chalamila ametoa agizo hilo mara baada ya kufika kwenye eneo hilo la wananchi zaidi ya kaya 15 walioathiriwa na mgogoro wa ardhi  unaohusisha familia za marehemu Abdallah Msham Kitwanga na Marehemu na Devid Mushi kwenye mtaa wa madale wilaya ya Kinondoni ambao waliondoshwa kwenye nyumba zao na kutolewa vyombo vyao nje tokea septemba 3 ,2026 kufuatia familia ya Devid Mushi kupata ushindi wa kesi ya mgogoro huo mahakamani lakini familia hiyo ya Devid Mushi haikutii kuwepo eneo hilo.

Akizungimza mara baada ya kufika kwenye eneo hilo la mgogoro Chalamila amesema alitoa taarifa ya kufika kwenye eneo hilo ili akutane na familia zote mbili za mgogoro huo pamoja na wahanga lakini familia ya Devid Mushi imedhatau wito huo huku akisisitiza kuwa hakuwa na mpango wa kuvunja hukumu iliyotolewa na mahakama bali alitamani kuwakutanisha ili kama itaawezekana kuwe na maridhiano ya wananchi kuweza kununua maeneo hayo

Aidha RC Chalamila amesema amehuzunishwa na kitendo cha familia hiyo kutotii maelekezo  na ameendelea kuweka msisitizo wa marufuku kwa mabaunsa kutumika kwenye migogoro ya ardhi kwa kuwa hawana mafunzo husika badala yake jeshi la polisi ndio litumike

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe Saad Mtambule ameeleza kiini cha mgogoro huo kuwa hapo awali mwaka 2015 Abdallah Msham Kitwanga alipeleka shauri hilo mahakamani dhidi ya Devid Mushi na kupata ushindi na baadaye kuwauzia wananchi maeneo hayo.

Vilevile Mtambule ameongeza kuwa baada ya wananchi kununua na kujenga nyumba zao baadae familia ya Devid Mushi ilipeleka shauri hilo tena mahakamani na kupata ushindi mwaka 2022 na ndipo wananchi hao zaidi ya kaya 15 kuanza kusimbuliwa wakitakiwa kuondoka na kumekuwa na mazungumzo mara kadhaa ili kufikia suluhu ya sakata hilo. 

Nao baadhi ya wananchi waliopata fursa ya kuongea mbele ya Mkuu wa Mkoa wameiomba Serikali kuwasaidia kufikia maridhiano ili walipie ardhi kwa bei itakayoridhiwa na pande zote

 

CHONGOLO AITAKA TOSCI KURATIBU BEI ZA MBEGU NCHINI

Na Matukio daima App 

Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, ameiagiza Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kuhakikisha inaratibu na kusimamia bei za mbegu nchini ili kuwawezesha wakulima kupata taarifa sahihi za bei na kununua mbegu bora kwa bei zinazozingatia taratibu zilizowekwa.

Chongolo ametoa agizo hilo leo jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha wadau wa tasnia ya mbegu akisema mbegu ni miongoni mwa pembejeo muhimu katika uzalishaji wa mazao, hivyo kuna umuhimu wa kuwepo kwa mfumo utakaomwezesha mkulima kufahamu bei ya mbegu kabla ya kufanya manunuzi.

Amesema TOSCI, kwa nafasi yake ya kusimamia ubora wa mbegu nchini, inapaswa pia kuhakikisha kampuni zia mbegu zinasambaza na kuuza mbegu kwa ushindani kwa bei ambazo TOSCI itazisimamia.

“Tumekuwa na utaratibu kwenye mbolea ambapo TFRA ndiyo inayoratibu na kusimamia bei za mbolea”. Mbegu nazo ni pembejeo za kilimo, hivyo hapa TOSCI ina wajibu wa kuratibu,” amesema Mheshimiwa Chongolo.

Aidha, amezitaka kampuni za mbegu kuhakikisha mbegu bora zinawafikia wakulima kwa wakati kupitia mawakala wanaokidhi vigezo, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa mbegu nchini. Amesema Tanzania ina ardhi na mazingira bora yanayowezesha kuongeza uzalishaji wa mbegu ndani ya nchi na hivyo kupunguza utegemezi wa mbegu kutoka nje ya nchi.

 

Waziri Mkuu Mwigulu kumwakilisha Rais Samia katika Mkutano wa Afya Moja Italia

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameondoka nchini leo Jumamosi, Septemba 19, 2026, kuelekea Roma, Italia, kumwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Kimataifa wa Afya Moja (One Health) na Mifumo ya Chakula na Kilimo.

Mkutano huo utafanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), jijini Roma, kuanzia Septemba 21 hadi 23, 2026.

Mkutano huo unalenga kuimarisha utekelezaji wa dhana ya Afya Moja, inayotambua uhusiano uliopo kati ya afya ya binadamu, wanyama, mimea na mazingira, kwa lengo la kujenga mifumo endelevu ya chakula na kilimo.

Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi na Serikali, wakiwemo Marais kati ya watano hadi saba, Mawaziri kati ya 30 hadi 50, pamoja na wawakilishi wa taasisi za kikanda na kimataifa, wadau wa maendeleo, sekta binafsi, taasisi za utafiti na mashirika ya kimataifa.

Miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa ni namna ya kuingiza dhana ya Afya Moja katika sera na uwekezaji wa mifumo ya chakula na kilimo, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta za kilimo, mazingira, afya, fedha na mipango miji.

Aidha, mkutano huo utajadili ukuzaji wa ubunifu, sayansi na maarifa ya ndani kwa ajili ya kuboresha uzuiaji wa vihatarishi, ufuatiliaji na usimamizi endelevu wa rasilimali.

Pia, washiriki watajadili namna ya kuhamasisha uwekezaji na ushirikiano ili kutafsiri ahadi zilizotolewa kuwa hatua madhubuti zenye matokeo yanayoweza kupimika.

Waziri Katambi Atoa Ufafanuzi kuhusu Mfumo wa Alama za leseni

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Paschal Katambi Patrobass, amesema Serikali imeanza kufanya majaribio ya mfumo wa alama za leseni za udereva kwa lengo la kudhibiti makosa ya usalama barabarani na kupunguza ajali nchini.

Akizungumza kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa Septemba 19, 2026, Waziri Katambi amesema mfumo huo unatokana na Kanuni za Usalama Barabarani (Mfumo wa Alama za Leseni za Udereva) za mwaka 2014, ambazo zilirekebishwa mwaka 2025.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chini ya Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, Waziri mwenye mamlaka ya kutunga kanuni kuhusu masuala ya usalama barabarani anaweza kuweka mfumo wa kupunguza vifo na ajali zinazotokana na sababu mbalimbali, ikiwemo makosa yanayofanywa na madereva wa vyombo vya usafiri.

Serikali imeeleza kuwa imefanya kazi ya muda mrefu na imejiridhisha kuwa hakuna haja ya kuanza kutumia mfumo huo madhubuti wa kudhibiti usalama barabarani.

Aidha, Serikali imeeleza kuwa pamoja na miradi ya usalama barabarani inayoendelea, ikiwemo matumizi ya teknolojia za kamera za barabarani zenye uwezo wa kutumia akili unde (AI), imeanza majaribio ya mfumo wa alama za leseni za udereva.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa mfumo huo bado haujaanza kutumika rasmi, bali hatua ya sasa ni kufanya majaribio ili kubaini namna utakavyoweza kutumika kudhibiti madereva watakaokiuka Sheria na Kanuni za Usalama Barabarani.

Serikali imeonya madereva kuwa leseni zao zikiingizwa kwenye mfumo huo, alama zitakazotolewa kutokana na makosa ya barabarani zinaweza kuathiri uhalali wa leseni zao iwapo wataendelea kukiuka sheria.

Waziri Katambi amesema baadhi ya alama zinazoweza kuhusishwa na makosa ya barabarani ni pamoja na makosa ya mwendokasi, kutofuata alama za barabarani, kuzidisha abiria, kutoa mikanda, kuendesha vyombo hatarishi na makosa mengine kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168.

Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza ajali za barabarani zinazosababisha vifo na majeruhi, akieleza kuwa matumizi ya mifumo kama hiyo yamekuwa yakiongezeka katika nchi mbalimbali.

Ametolea mfano Rwanda, ambayo amesema imetumia mfumo huo na kuona kupungua kwa kiwango kikubwa cha ajali na vifo vinavyotokana na ajali za barabarani.

Waziri Katambi pia amesisitiza kuwa Kanuni za Usalama Barabarani (Mfumo wa Alama za Leseni za Udereva) za mwaka 2014, zilizorekebishwa mwaka 2025, bado hazijaanza kutekelezwa rasmi.

Amesema sababu mojawapo ya kutocheleweshwa kwa utekelezaji wake ni kuwa wataalamu wa mifumo kutoka Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Mapato wanaendelea kuunganisha mifumo hiyo ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi.

Sababu nyingine, kwa mujibu wa Waziri, ni kwamba Serikali iko katika kipindi cha utoaji elimu kwa umma kuhusu kanuni hizo. Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani linaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya madereva wa vyombo vya moto pamoja na wananchi kwa ujumla kuhusu mfumo huo na umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Waziri amesema Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani linaendelea kufikisha elimu hiyo kwa makundi mbalimbali ya madereva kupitia mikutano ya uelimishaji, pamoja na vyombo vya habari kama redio na Runinga, katika vituo vya mabasi, maeneo ya maegesho ya malori, mikusanyiko ya watu na maeneo mengine.

Ameongeza kuwa elimu hiyo inalenga kuwaelimisha wananchi kuhusu makosa yanayoweza kupewa alama na namna alama hizo zitakavyotumika.

Waziri Katambi amesisitiza kuwa mfumo huo bado haujaanza kutekelezwa rasmi, hivyo hakuna haja ya dereva ambaye leseni yake imeondolewa alama kutokana na kosa la barabarani kuwa na wasiwasi kwa sasa.

Amesema madereva watajulishwa rasmi pindi mfumo huo utakapoanza kutumika.

Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Paschal Katambi Patrobass, Septemba 19, 2026, jijini Dar es Salaam.

Chalamila Aagiza Familia ya Mushi Itafutwe, Ikamatwe – Video

Global Publishers
September 19, 2026
0 views
0 Comments

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Mtatiro Kitwinkwi, kuhakikisha wanafamilia ya David Mushi wanatafutwa na kukamatwa baada ya kutofika kwenye mkutano aliouitisha Septemba 19, 2026, kwa ajili ya kujadili mgogoro wa ardhi uliopo Mtaa wa Madale, Kata ya Wazo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Nipashe, Chalamila amesema aliwaita wanafamilia hao kwa lengo la kuzungumza nao na kutafuta namna ya kumaliza mgogoro huo kwa amani, akisisitiza kuwa Serikali haikulenga kutengua uamuzi wa Mahakama.

Amesema kutofika kwa familia hiyo katika mkutano huo, licha ya kuitwa, amekitafsiri kama dharau kwa Serikali, huku akimtaka Kamanda wa Polisi kuwatafuta na kuwahifadhi kituoni.

Chalamila amesema mgogoro huo unahusisha familia za Abdallah Kitwanga na David Mushi, ambapo Mahakama imewahi kutoa maamuzi katika vipindi tofauti. Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa katika mkutano huo, uamuzi wa mwaka 2022 uliipa ushindi familia ya Mushi.

Mgogoro huo unahusu eneo lenye ukubwa wa takribani hekta 10 katika Mtaa wa Madale, huku taarifa zikieleza kuwa kati ya kaya 13 na 15 zimehusishwa na eneo hilo.

Wakati huo huo, wawakilishi wa familia ya Mushi wamesema walinunua maeneo hayo kwa kufuata taratibu, lakini tangu Septemba 3, 2026 baadhi ya wakazi wamezuiwa kuingia katika nyumba zao na kulazimika kuishi katika mahema.

Chalamila amewataka wahusika kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea kutafuta suluhisho la mgogoro huo, huku akisisitiza kuwa matumizi ya mabango katika eneo hilo yanaweza kuongeza taharuki.

WAJASIRIAMALI WADOGO WAFAIDIKA USHIRIKI WA TBS MAONESHO YA MADINI NA FURSA ZA UWEKEZAJI LINDI 2026.

 Na Mwandishi Wetu.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kuwa karibu na wajasiriamali wadogo nchini kwa kutoa elimu kuhusu viwango na ubora wa bidhaa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha kuzalisha bidhaa salama, zenye ubora na zinazoweza kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

TBS imetoa elimu hiyo katika Maonesho ya Madini na Fursa za Uwekezaji Lindi 2026, yanayofanyika Wilaya ya Ruangwa, Mkoa wa Lindi, ambapo wadau mbalimbali wamepata fursa ya kujifunza kuhusu viwango, taratibu za ubora wa bidhaa pamoja na umuhimu wa kuzingatia matakwa ya viwango katika uzalishaji na biashara.

Akizungumza katika maonesho hayo, Eng. Hemedy Hamim, Mkaguzi wa TBS Kanda ya Kusini, amesema TBS imeendelea kuwafikia wajasiriamali wadogo kwa kuwapatia elimu inayolenga kuwawezesha kuboresha bidhaa zao na kuingia katika masoko yenye ushindani.

Katika utekelezaji wa jukumu hilo, TBS imewatembelea na kuwapatia elimu wajasiriamali wanaojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa za korosho, mafuta ya mwani, sabuni za mwani pamoja na Shower Jelly zinazotokana na mwani, huku ikiwahamasisha kuzingatia viwango vya ubora katika uzalishaji wao.

Eng. Hemedy amesema elimu hiyo pia inalenga kuwawezesha wajasiriamali kuelewa taratibu za kupata Alama ya Ubora ya TBS, ambayo ni muhimu katika kujenga uaminifu wa bidhaa kwa watumiaji na kuongeza uwezo wa bidhaa kufikia masoko mbalimbali.

TBS imeeleza kuwa kwa wajasiriamali wadogo, upatikanaji wa Alama ya Ubora unatolewa bila malipo, jambo linalolenga kuwawezesha wafanyabiashara hao wadogo kupata huduma za viwango na kuimarisha ubora wa bidhaa zao.

Katika kuwafikia kwa urahisi zaidi wajasiriamali hao, TBS imeshirikiana na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), ambapo ushirikiano huo umewezesha elimu ya viwango kuwafikia wajasiriamali wadogo wanaozalisha bidhaa mbalimbali, ikiwemo zile zinazotokana na mazao yanayopatikana katika maeneo yao.

TBS imewasisitiza wajasiriamali kutumia fursa hiyo kwa kuhakikisha bidhaa zao zinafuata taratibu zinazotakiwa na kupata Alama ya Ubora, kwani hatua hiyo inaweza kuongeza uaminifu wa bidhaa kwa walaji na kuwawezesha kutafuta fursa za masoko mapana zaidi.

Mmoja wa wajasiriamali walionufaika na elimu na huduma za TBS ni Bi. Zena Adam, mbanguaji wa korosho kutoka Nachingwea, ambaye baada ya kufuata taratibu zilizowekwa na TBS alifanikiwa kupata Alama ya Ubora kwa bidhaa yake.

Bi. Zena ameishukuru TBS kwa elimu na maelekezo aliyopatiwa katika hatua mbalimbali, akieleza kuwa mafunzo hayo yamemsaidia kuelewa umuhimu wa ubora na taratibu zinazotakiwa katika uzalishaji.

Kwa mujibu wa Bi. Zena, kupata Alama ya Ubora ya TBS ni hatua muhimu kwake kama mjasiriamali, kwani anaamini itasaidia kuongeza uaminifu wa bidhaa zake na kumfungulia fursa za masoko kutoka nje ya Mkoa wa Lindi hadi katika masoko ya kimataifa.

Kwa upande wake, Bi. Fatma Machalila, ambaye ni miongoni mwa wajasiriamali walionufaika na elimu hiyo, ameipongeza TBS kwa kuendelea kuwafikia wajasiriamali wadogo na kutoa elimu kuhusu uzalishaji wa bidhaa bora.

Bi. Fatma ameomba TBS iendelee na programu za elimu kama hiyo, hususan katika maeneo ya vijijini, ili wajasiriamali wengi zaidi waweze kupata uelewa wa viwango na kuzalisha bidhaa bora na salama.

Amesema elimu hiyo ni muhimu kwa sababu inawasaidia wajasiriamali kuelewa namna ya kuboresha bidhaa zao, kulinda afya na usalama wa wananchi, pamoja na kukuza biashara zao katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Ushiriki wa TBS katika Maonesho ya Madini na Fursa za Uwekezaji Lindi 2026 umeendelea kuonyesha umuhimu wa taasisi hiyo kuwa karibu na wazalishaji na wajasiriamali, si kwa kutoa huduma za viwango pekee, bali pia kwa kutoa elimu inayowawezesha kuelewa namna ubora unavyoweza kuwa sehemu muhimu ya ukuaji wa biashara zao.

Kwa wajasiriamali wadogo wanaozalisha bidhaa za korosho, mwani na bidhaa nyingine, elimu hiyo inatoa fursa ya kuelewa kwamba ubora wa bidhaa ni zaidi ya mahitaji ya kisheria; ni sehemu ya kujenga uaminifu wa mlaji, kuongeza ushindani wa bidhaa na kufungua milango ya masoko mapana zaidi.