Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda Rebecca Kadaga anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki yatakayofanyika Novemba 12 mwaka huu katika makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Arusha.
Rais wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) Jaji Nestory Kayobera, akizungumza na waandishi wa habari, ameyasema maadhimisho hayo yanaadhimishwa kwa lengo la kuangazia mafanikio ya Mahakama hiyo walikotoka,walipo na wanapoelekea katika kuhakikisha wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanapata haki.
Maadhimisho hayo yatafanyika chini ya Kauli mbiu isemayo “Kutoka misingi hadi mustakabali.” yataenda sambamba na mijadala mbalimbali katika masuala ya mchango wa Mahakama kwenye maendeleo ya Jumuiya, usuluhishi wa migogoro ya kibiashara na ushirikiano wa kikanda.
Amesema Mahakama hiyo imekuwa nguzo muhimu ya utoaji wa haki kwa wananchi wa Jumuiya hiyo kwa kutoa fursa kwa watu binafsi, mashirika ya kiraia, vyama vya siasa, vyombo vya habari na serikali kuwasilisha mashauri, na kuonyesha hatua ambazo Mahakama imepiga katika kutenda haki.
Aidha jumuiya hiyo yenye jumla ya nchi 8 wanachama ina zaidi ya watu Milioni 350 ambapo katika utekelezaji wa majukumu yake ndani ya miaka yote 25, Mahakama hiyo imefanikiwa kutatua kesi ambazo zimekuwa zikifikishwa kwao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Mahakama hiyo inakuwa imara.
Ameongeza kuwa maadhimisho hayo yatahusisha wageni zaidi ya 200 kutoka ndani na nje ya nchi wanachama wakiwrmo majaji wakuu, mawaziri wa Sheria, wanasheria wakuu wa serikali pamoja na wasomi kutoka Afrika na Marekani.

