WAZAZI WASEMA KLABU ZA VIPIMO ZIMEWAFUNGUA MACHO

Wazazi jijini Dodoma wamesema elimu ya vipimo inayotolewa kupitia Klabu za Vipimo katika shule za msingi imeanza kuleta mabadiliko ndani ya familia, baada ya watoto waliopatiwa mafunzo na Wakala wa Vipimo (WMA) kuanza kuwafundisha wazazi wao namna ya kutambua vipimo sahihi na kujilinda dhidi ya upunjaji katika manunuzi.

Wazazi wameyasema hayo  Septemba 18,2026  wakati wa mahafari ya wanafunzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Mtemi Mazengo jijini Dodoma ambapo  wanafunzi wa klabu ya vipimo walikuwa wakitoa elimu ya vipimo kwa wazazi na watu wengine mbalimbali waliohudhuria akiwemo Mgeni Rasmi.

Mzazi wa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mtemi Mazengo, Bertha Paulo Chipaga, amesema mtoto wake, Gloria Elisha Enock, amekuwa akimsaidia kuelewa matumizi sahihi ya mizani ya chakula, mita ya maji na vipimo vingine, jambo ambalo limempa uelewa na kujiamini zaidi kama mlaji.

Bi.Chipaga amesema awali hakuwa na uelewa mpana kuhusu namna ya kutambua kama kipimo kinachotumika katika biashara ni sahihi, lakini tangu mtoto wake ajiunge na Klabu ya Vipimo amekuwa akipata elimu hiyo nyumbani na sasa anaelewa umuhimu wa kuhakikisha bidhaa anayonunua inalingana na kiasi cha fedha anacholipa.

“Hatua hiyo inaonesha kuwa elimu inayotolewa kwa watoto haiishii shuleni, bali inasambaa hadi kwenye familia na jamii, hivyo akawataka wazazi wengine kutumia fursa hiyo kuwaelimisha watoto wao kuhusu haki za mlaji na matumizi sahihi ya vipimo.”amesema Bi.Chipaga

Akizungumza kuhusu umuhimu wa kuwaandaa watoto na elimu hiyo, mkazi wa Makao Mapya jijini Dodoma, Peter Daudi Mponzi, amesema mafunzo ya vipimo kwa wanafunzi ni uwekezaji muhimu kwa jamii kwa sababu yanawajengea uwezo wa kutambua mizani na vipimo visivyo sahihi wanapokuwa katika mazingira ya biashara.

Amesema mtoto anayeelewa vipimo anaweza kwenda dukani na kuangalia kama mzani unaotumika umehakikiwa, hivyo kupunguza uwezekano wa yeye au familia yake kupunjwa na wakati huo huo kueneza elimu hiyo kwa watu wengine.

Mponzi amesema kuanzia elimu hiyo katika umri mdogo kunaweza kujenga kizazi chenye uelewa mpana wa masuala ya vipimo na haki za walaji, kwa kuwa watoto wanakuwa na nafasi ya kutumia maarifa hayo katika maisha yao ya kila siku.

 “Watoto wanapotoka shuleni na kwenda majumbani, dukani na katika maeneo mengine ya jamii, wanakuwa sehemu ya mnyororo wa elimu unaoweza kuwafikia wazazi, ndugu na wananchi wengine, hivyo kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa vipimo sahihi.”amesema

Mwanafunzi wa Klabu ya Vipimo katika Shule ya Msingi Mtemi Mazengo, Gloria Elisha Enock, amesema WMA imewajengea uwezo wa kuelewa maana na umuhimu wa vipimo pamoja na jukumu la Wakala la kumlinda mlaji.

Amesema wamefundishwa kuwa WMA huhakiki vipimo mbalimbali, ikiwemo mizani, mita za maji na umeme, pamoja na bidhaa zilizofungashwa, huku mlaji akitakiwa kuangalia alama ya WMA kwenye mizani ili kuhakikisha kipimo  hicho kimehakikiwa na kinafanya kazi kwa usahihi.

Kwa upande wake, mwanafunzi mwenzake, Venosa Michael Simba, amesema elimu hiyo imemsaidia kubadilika kutoka kuwa mtoto anayekwenda dukani bila kuzingatia usahihi wa vipimo hadi kuwa mfuatiliaji na mtoa elimu kwa jamii.

Amesema baada ya kupata mafunzo hayo aligundua hata nyumbani kwao kuwa mita ya maji ilikuwa haijahakikiwa na akaweza kutoa elimu kwa watu waliokuwa hawajui umuhimu wa kuhakiki vipimo.

 “kabla ya kupata elimu hiyo alikuwa akienda dukani bila kuangalia chochote, lakini sasa anaelewa kuwa mlaji ana wajibu wa kuhakikisha anapata kiasi sahihi cha bidhaa anayolipia.”amesema

Kwa ujumla, Klabu za Vipimo za WMA zimeanza kuwa darasa la vitendo la kuwaandaa watoto kuwa mabalozi wa ulinzi wa mlaji, huku elimu hiyo ikitoka shuleni na kuingia moja kwa moja katika familia na jamii.

Mpango huo unaongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya vipimo sahihi, unasaidia kujenga utamaduni wa kuhoji na kuthibitisha vipimo vinavyotumika katika biashara na, kwa muda mrefu, unaweka msingi wa kizazi kinachothamini uadilifu, usawa na uwazi katika shughuli za kiuchumi.

Fahamu Mambo Muhimu Yasiyotakiwa Kupuuzwa Katika Gari Lako

Global Publishers
September 20, 2026
5,756 views
0 Comments

Kila mmiliki wa gari anapaswa kuwa makini na alama ndogo ndogo zinazoweza kuashiria matatizo makubwa yanayoweza kusababisha ajali au gharama kubwa za matengenezo. Kupuuza tatizo dogo leo inaweza kumaanisha tatizo kubwa kesho. Hapa kuna mambo muhimu yasiyotakiwa kupuuzwa kwenye gari lako:

1️⃣ Breki – Moyo wa Usalama
Breki ni kila kitu barabarani. Kelele zisizo za kawaida, kuvuja kwa majimaji au breki zisizofanya kazi ni ishara ya hatari. Ukipuuzia, unajiwekea maisha yako na ya wengine hatarini.

2️⃣ Mataili
Mataili ni kinga ya gari lako kwenye dhoruba, mvua au barabara yenye changamoto. Angalia mataili mara kwa mara na ubadilishe pale inapohitajika. Usipuuze!

3️⃣ Maji ya Radiator (Rejeta) na Mafuta ya Engine (Oili ya gari)
Engine inahitaji Oili sahihi na maji ya radiator. Ukosefu wa mafuta au maji hupelekea engine kuchemka na kuharibiwa sehemu zingine, jambo linalogharimu pesa.

4️⃣ Taa na Viashiria – Usikose kuangalia
Taa za mbele, brake, na viashiria vya mwelekeo vitaleta usalama. Ukipuuzia tatizo lolote, hasa usiku au mvua, unajiwekea kwenye hatari kubwa ya ajali.

5️⃣ Viashiria vya Dashibodi – Onyo la Haraka
Taa ndogo za onyo kwenye dashibodi si za kupuuziwa. Kila mwanga ni ishara ya tatizo, iwe ni mafuta, betri, au breki. Chukua hatua mara moja.

6️⃣ Belt za Engine – Hatarishi Kuu
Belt zinapoharibika zinaweza kusababisha engine kushindwa kufanya kazi na kuharibu sehemu nyingi za gari. Angalia belt na ubadilishe pale inapohitajika.

7️⃣ Kichungi cha Mafuta na Mafuta
Kichungi kilichoziba au mafuta machache huathiri engine, kupunguza nguvu na kuongeza gharama ya matengenezo. Usisubiri hadi engine ishindwe kufanya kazi.

8️⃣ Mafuta ya Breki na Clutch
Breki na clutch zinahitaji lubrication sahihi. Ukosefu wa fluids huongeza hatari ya ajali na kuharibu mfumo mzima wa gari.

 

Norway ina Watu Milioni 5, Utajiri Wake Washangaza Dunia, Hii Ndiyo siri Yao

Norway ni miongoni mwa nchi zinazotajwa kuwa na kiwango cha juu cha maendeleo duniani. Licha ya kuwa na idadi ya watu isiyozidi milioni sita, nchi hiyo imejenga uchumi wenye nguvu, huduma bora za kijamii na mfuko mkubwa wa utajiri wa taifa unaotokana kwa kiasi kikubwa na mapato ya mafuta na gesi.

Idadi ya watu

Kwa mujibu wa Statistics Norway (SSB), Norway ilikuwa na watu 5,636,904 mwishoni mwa robo ya pili ya mwaka 2026. Hii inaifanya kuwa nchi yenye watu wachache ikilinganishwa na ukubwa wa uchumi wake.

Makadirio rasmi yanaonyesha idadi hiyo inaweza kufikia zaidi ya milioni 6.2 ifikapo mwaka 2050, kutegemea mwenendo wa uzazi, vifo na uhamiaji.

Uchumi wa Norway

Nguvu kubwa ya uchumi wa Norway imejengwa katika sekta mbalimbali, ikiwemo mafuta na gesi, usafirishaji wa baharini, viwanda, uvuvi, nishati na huduma.

Katika robo ya pili ya 2026, thamani ya GDP ya Norway kwa bei za sasa ilifikia takribani NOK trilioni 1.48, huku shughuli za mafuta na usafirishaji wa baharini zikichangia sehemu muhimu ya uzalishaji huo.

IMF inakadiria kuwa Norway itakuwa na ukuaji wa uchumi wa karibu 1.5% mwaka 2026, huku GDP kwa kila mtu ikikadiriwa kuwa zaidi ya dola 105,000 kwa bei za sasa.

Siri kubwa: Mafuta hayatumiki yote mara moja

Moja ya mambo yanayoifanya Norway kuwa ya kipekee ni namna ilivyotumia mapato ya mafuta.

Badala ya kutumia mapato yote ya mafuta na gesi katika matumizi ya kawaida, Serikali hupeleka mapato ya shughuli za petroli katika Government Pension Fund Global, maarufu kama Oil Fund, ambao unawekeza fedha hizo katika masoko ya kimataifa.

Mwisho wa mwaka 2025, thamani ya mfuko huo ilikuwa takribani NOK trilioni 21.3, sawa na karibu mara nne ya GDP ya Norway na takribani NOK milioni 3.8 kwa kila mtu aliyesajiliwa nchini humo.

Serikali ina utaratibu wa kifedha unaolenga kuhakikisha mapato ya mafuta yanawanufaisha wananchi wa sasa na vizazi vijavyo, badala ya kutegemea mafuta pekee wakati wa sasa.

Norway imeendeleaje kuwa nchi tajiri?

Tangu kuanza kwa uzalishaji wa mafuta na gesi katika Bahari ya Kaskazini miaka ya 1970, shughuli za petroli zimechangia zaidi ya NOK trilioni 28,000 katika GDP ya Norway kwa thamani za sasa. Serikali pia inasema takribani nusu tu ya rasilimali zinazokadiriwa kurejesheka katika rafu ya Norway zimezalishwa na kuuzwa.

Hata hivyo, mafanikio ya Norway hayawezi kuelezwa na mafuta pekee. Nchi hiyo imejenga taasisi imara, mfumo wa kodi, elimu, miundombinu na sera za muda mrefu za kusimamia rasilimali zake.

Maendeleo ya binadamu

Norway pia iko juu sana katika kipimo cha maendeleo ya binadamu. Kwenye takwimu za UNDP zilizotumika katika Human Development Report 2025, Norway ilikuwa na HDI ya 0.970, ikiwa katika nafasi ya pili duniani kwa pamoja na Uswisi. Matarajio ya maisha yalikuwa miaka 83.3, huku kipato cha taifa kwa mtu kikikadiriwa kuwa dola 112,710 za kimataifa za PPP.

HDI hupima mambo makuu matatu: afya, elimu na kiwango cha maisha.

Kwa nini Norway ni mfano wa kipekee?

Kwa ufupi, “maajabu” ya Norway yanatokana na mchanganyiko wa:

  • Idadi ndogo ya watu — karibu milioni 5.6.
  • Rasilimali nyingi za mafuta na gesi.
  • Mfuko mkubwa wa utajiri wa taifa unaowekeza nje ya nchi.
  • Uwekezaji katika elimu, afya na huduma za jamii.
  • Taasisi na mifumo ya usimamizi wa fedha za umma.
  • Uchumi wenye sekta nyingi, si mafuta pekee.
  • Kiwango cha juu sana cha maendeleo ya binadamu.

Kwa hiyo, somo kubwa la Norway si kwamba ina mafuta mengi tu, bali ni jinsi ilivyoweka mfumo wa kuhakikisha utajiri wa rasilimali unabadilishwa kuwa mali ya muda mrefu kwa taifa na vizazi vijavyo

Yanga Yatozwa Faini ya Milioni 5, Afisa Usalama Apelekwa Kamati Ya Maadili

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetoa adhabu mbalimbali kwa klabu, viongozi na waamuzi kufuatia mwenendo wa michezo ya Ligi Kuu ya NBC na Championship, katika kikao chake kilichofanyika Septemba 18, 2026.

Katika Ligi Kuu ya NBC, Young Africans SC imetozwa faini ya Sh milioni 5 kwa kosa la mashabiki wake kuwarushia chupa benchi la ufundi la Geita Gold katika mchezo uliomalizika kwa Yanga kushinda 1-0.

Mbali na faini hiyo, Yanga imepewa onyo kali kwa kutofuata mtiririko wa matukio ya mchezo (Match Countdown), ambapo wachezaji watatu waliingia uwanjani kwa ajili ya kupasha misuli joto saa 12:00 jioni badala ya saa 12:10 jioni kama ilivyopangwa.

Aidha, Afisa Ulinzi na Usalama wa Yanga, Eddie Evance, amepelekwa Kamati ya Maadili ya TFF kwa kosa la kukaidi maamuzi ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi. Evance alionekana uwanjani wakati wa mchezo huo licha ya kuwa anatumikia adhabu ya kutoruhusiwa kuingia uwanjani kwa kipindi cha miezi sita, adhabu iliyotolewa Juni 8, 2026.

Katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu ya NBC kati ya Azam FC na Simba SC uliomalizika kwa Simba kushinda 2-0, Azam FC imepewa onyo kali kwa kutofuata mtiririko wa matukio ya mchezo.

TPLB imesema wachezaji wa Azam waliingia uwanjani kwa ajili ya kupasha misuli joto saa 12:07 jioni badala ya saa 12:10 jioni kama ilivyokuwa imeelekezwa na Mratibu wa Mchezo.

Kwa upande mwingine, Afisa Ulinzi na Usalama wa Azam FC, Masoud Fupe, amepelekwa Kamati ya Maadili ya TFF kwa kosa la kuvuruga utaratibu wa kuingia uwanjani kwa benchi la ufundi na wachezaji.

Fupe anatuhumiwa kuwaingiza viongozi wa benchi la ufundi la Azam, akiwemo Kocha Mkuu Frolent Ibenge, Kocha Msaidizi Anicet Makiadi pamoja na mchezaji Himid Mao, kupitia mlango usio rasmi, licha ya makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha maandalizi ya mchezo kuhusu mlango uliopaswa kutumika.

Katika mchezo wa Kagera Sugar na Fountain Gate uliomalizika kwa sare ya 1-1, waamuzi Hassan Mhina na Soud Hussein wameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitatu kutokana na kuonyesha mapungufu ya kiuchezeshaji yaliyotokana na kushindwa kutafsiri vizuri sheria za mpira wa miguu katika mchezo huo.

CHAMPIONSHIP

Katika Ligi ya Championship ya NBC, Bigman FC imepewa onyo kali kwa kosa la kuwakilishwa na wajumbe watatu badala ya watano katika kikao cha kitaalamu cha maandalizi ya mchezo dhidi ya IAA FC.

Aidha, Songea United imetozwa faini ya Sh milioni 5 kwa kushindwa kuvaa jezi zenye nembo ya mdhamini mkuu wa Ligi ya Championship ya NBC, licha ya kukumbushwa kufanya hivyo.

Maamuzi hayo yametolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Septemba 19, 2026.

Raphinha Acharuka, Afunga Hat-Trick, Barca Yaendeleza Mwendo wa Ushindi

Raphinha amefunga hat-trick na kuisaidia Barcelona kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Sevilla katika mchezo wa La Liga uliochezwa Jumamosi, Septemba 19, 2026.

Ushindi huo umeifanya Barcelona kuendeleza rekodi yake ya ushindi katika michezo yote minane iliyocheza msimu huu kwenye mashindano yote.

Sevilla ilianza kwa kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya 19 kupitia Youssouf Fofana, aliyefunga kwa kichwa baada ya kupokea krosi ya Felix Correia.

Barcelona ilisawazisha kupitia Raphinha kabla ya mapumziko, akitumia ustadi wake kumzidi beki na kufunga kwa shuti la chini.

Kipindi cha pili kilikuwa cha Raphinha na Lamine Yamal. Yamal alitoa pasi ya krosi iliyomuwezesha Raphinha kufunga bao la pili kwa kichwa na kuipa Barcelona uongozi.

Raphinha alikamilisha hat-trick yake baada ya Yamal kumpa pasi iliyomweka katika nafasi nzuri, kabla ya Mbrazil huyo kumtungua kipa kwa kumpiga mpira juu yake na kuufanya mchezo kuwa 3-1.

Raphinha, ambaye msimu huu ameanza kucheza zaidi kama mshambuliaji wa kati, sasa amefikisha mabao 12 katika mechi saba za La Liga, huku pia akiwa amefunga mabao mawili katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kocha wa Barcelona, Hansi Flick, amemsifu Raphinha kwa uwezo wake wa kuzoea nafasi mbalimbali na mchango wake mkubwa katika timu.

Ushindi huo umeifanya Barcelona kufikisha ushindi wa nane mfululizo katika michezo yote msimu huu na kuendelea kuongoza La Liga kwa tofauti ya pointi sita dhidi ya Real Madrid, ambao wanatarajiwa kucheza dhidi ya Atletico Madrid katika derby ya Madrid leo Jumapili.

Kwa upande wa Sevilla, ilikuwa ni kipigo cha pili msimu huu, licha ya kuonyesha ushindani mkubwa hasa katika kipindi cha kwanza.

Katika michezo mingine ya La Liga, Celta Vigo iliichapa Racing Santander mabao 5-0, Athletic Bilbao na Alaves zilitoka sare ya 0-0, huku Osasuna na Rayo Vallecano zikifungana 1-1.

Raphinha Acharuka Sevilla, Barca Yaendeleza Mwendo Wa Ushindi

Raphinha amefunga hat-trick na kuisaidia Barcelona kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Sevilla katika mchezo wa La Liga uliochezwa Jumamosi, Septemba 19, 2026.

Ushindi huo umeifanya Barcelona kuendeleza rekodi yake ya ushindi katika michezo yote minane iliyocheza msimu huu kwenye mashindano yote.

Sevilla ilianza kwa kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya 19 kupitia Youssouf Fofana, aliyefunga kwa kichwa baada ya kupokea krosi ya Felix Correia.

Barcelona ilisawazisha kupitia Raphinha kabla ya mapumziko, akitumia ustadi wake kumzidi beki na kufunga kwa shuti la chini.

Kipindi cha pili kilikuwa cha Raphinha na Lamine Yamal. Yamal alitoa pasi ya krosi iliyomuwezesha Raphinha kufunga bao la pili kwa kichwa na kuipa Barcelona uongozi.

Raphinha alikamilisha hat-trick yake baada ya Yamal kumpa pasi iliyomweka katika nafasi nzuri, kabla ya Mbrazil huyo kumtungua kipa kwa kumpiga mpira juu yake na kuufanya mchezo kuwa 3-1.

Raphinha, ambaye msimu huu ameanza kucheza zaidi kama mshambuliaji wa kati, sasa amefikisha mabao 12 katika mechi saba za La Liga, huku pia akiwa amefunga mabao mawili katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kocha wa Barcelona, Hansi Flick, amemsifu Raphinha kwa uwezo wake wa kuzoea nafasi mbalimbali na mchango wake mkubwa katika timu.

Ushindi huo umeifanya Barcelona kufikisha ushindi wa nane mfululizo katika michezo yote msimu huu na kuendelea kuongoza La Liga kwa tofauti ya pointi sita dhidi ya Real Madrid, ambao wanatarajiwa kucheza dhidi ya Atletico Madrid katika derby ya Madrid leo Jumapili.

Kwa upande wa Sevilla, ilikuwa ni kipigo cha pili msimu huu, licha ya kuonyesha ushindani mkubwa hasa katika kipindi cha kwanza.

Katika michezo mingine ya La Liga, Celta Vigo iliichapa Racing Santander mabao 5-0, Athletic Bilbao na Alaves zilitoka sare ya 0-0, huku Osasuna na Rayo Vallecano zikifungana 1-1.

Arsenal Yapokea Kichapo cha 3-0, Spurs Waendelea Kuteseka dhidi ya Aston Villa

Global Publishers
September 20, 2026
6 views
0 Comments

Arsenal imeanza kupoteza kasi katika mbio za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu England baada ya kuchapwa mabao 3-0 na Brighton katika mchezo uliochezwa Septemba 19, 2026.

Arsenal iliingia kwenye mchezo huo ikiwa na rekodi ya ushindi katika mechi zote saba ilizocheza msimu huu kwenye mashindano yote, lakini Brighton ilivunja rekodi hiyo kupitia mabao ya Pascal Groß dakika ya 31, Charalampos Kostoulas dakika za mwisho za kipindi cha kwanza na Chema Andrés dakika ya 60.

Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, amekiri kuwa Brighton ilistahili ushindi, akisema timu yake ilishindwa kufanya mambo ya msingi kwa muda mrefu wa mchezo.

Kipigo hicho ni cha kwanza kwa Arsenal msimu huu na kikubwa zaidi katika mashindano yote tangu Aprili 2023.

Kwa upande mwingine, Tottenham Hotspur imeendelea kusuasua baada ya kupoteza kwa mabao 3-2 dhidi ya Aston Villa, hivyo kubaki bila ushindi katika michezo yake ya ligi.

Villa ilipata mabao yake kupitia Johan Manzambi, Nicolas Jackson na Emi Buendía, huku Tottenham ikijibu kupitia Conor Gallagher na Jan Paul van Hecke.

Kocha wa Tottenham, Roberto De Zerbi, amesema timu yake imekuwa “dhaifu sana” katika nyakati ambazo inapaswa kujilinda.

Katika michezo mingine, Newcastle United iliifunga Hull City 2-1, huku Everton ikiibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Ipswich Town.

Manchester City ilikuwa na nafasi ya kuongeza uongozi wa pointi tatu kileleni ilipokuwa ikitarajiwa kuikaribisha Sunderland, huku Manchester United ikitarajiwa kucheza dhidi ya Fulham leo Jumapili.

Fahamu Njia 5 za Vijana Kujipatia Kipato Kikubwa na Kujenga Maisha Bora

Fedha ni sehemu muhimu ya maisha ya kila mtu, lakini kupata mafanikio ya kifedha kunahitaji zaidi ya kutamani kuwa na pesa. Vijana wanahitaji kujenga ujuzi, kufanya kazi kwa bidii, kuwa wabunifu na kutumia fursa zinazopatikana katika dunia ya sasa.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya elimu na maendeleo ya vijana, Isma’il Muhammad Anchau, kuna mambo muhimu ambayo yanaweza kuwasaidia vijana kujenga kipato na maisha bora ya baadaye.

1. Jifunze Ujuzi Unaoweza Kukuletea Kipato

Katika dunia ya sasa, ujuzi ni mtaji mkubwa. Vijana hawapaswi kutegemea ajira pekee bali wanapaswa kujifunza stadi zitakazowawezesha kujiajiri.

Baadhi ya ujuzi unaoweza kuleta kipato ni pamoja na:

  • Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT)
  • Matengenezo ya simu
  • Upigaji picha na utengenezaji wa video
  • Ushonaji
  • Useremala
  • Ubunifu na kazi za sanaa
  • Fani mbalimbali za ufundi

Ujuzi mzuri unaweza kuwa chanzo cha kipato cha kudumu ikiwa utatumika kwa ubunifu na kujituma.

2. Anzisha Biashara

Biashara ni moja ya njia zinazoweza kumsaidia mtu kuongeza kipato. Vijana wanaweza kuanza hata kwa mtaji mdogo kulingana na uwezo wao.

Mifano ya maeneo ya kuanzia ni:

  • Biashara mtandaoni
  • Uuzaji wa bidhaa mbalimbali
  • Kilimo cha kibiashara
  • Ufugaji wa mifugo
  • Huduma zinazohitajika kwenye jamii

Muhimu ni kufanya utafiti wa soko na kuanza na jambo linaloeleweka.

3. Jifunze Teknolojia na Sayansi ya Kompyuta

Teknolojia imefungua milango mingi ya kupata kipato bila mipaka ya kijiografia.

Vijana wanaweza kujifunza:

  • Utengenezaji wa programu za kompyuta
  • Masoko ya kidijitali (digital marketing)
  • Uundaji wa maudhui mtandaoni
  • Ubunifu wa michoro (graphic design)
  • Uchambuzi wa data

Ujuzi wa teknolojia unaweza kutoa nafasi za kazi na biashara katika soko la ndani na kimataifa.

4. Weka Akiba na Wekeza

Kupata fedha pekee haitoshi, muhimu ni kujua namna ya kuzitunza na kuzizalisha.

Vijana wanashauriwa:

  • Kutenga sehemu ya kipato kwa ajili ya akiba
  • Kuepuka matumizi yasiyo ya lazima
  • Kujifunza kabla ya kuwekeza
  • Kuweka fedha kwenye biashara au miradi yenye uelewa nayo

Uwekezaji mzuri huanza na maarifa na mipango sahihi.

5. Jenga Mahusiano Mazuri na Watu

Mtandao wa watu una nafasi kubwa katika mafanikio. Vijana wanapaswa kujenga mahusiano na watu wenye uzoefu na maarifa.

Njia za kufanya hivyo ni:

  • Kushiriki mafunzo na semina
  • Kuomba ushauri kutoka kwa wajasiriamali
  • Kujifunza kutoka kwa viongozi wa biashara
  • Kushirikiana na watu wenye malengo chanya

Mambo ya Kuepuka Ili Kulinda Kipato

Vijana wanapaswa kuepuka:

  • Kutumia fedha bila mpango
  • Kukopa bila mpango wa kurejesha
  • Kununua vitu visivyo vya lazima
  • Kutegemea kamari au njia za kupata pesa haraka
  • Kuacha kujifunza na kutafuta fursa mpya

Mafanikio ya kifedha hayaji kwa bahati pekee, bali yanajengwa kupitia maarifa, nidhamu, uvumilivu na kutumia fursa kwa wakati sahihi.

Serikali Yatoa Tahadhari Athari za El Niño Katika Mvua Za Vuli

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imetoa tahadhari kuhusu uwezekano wa kutokea kwa athari zinazohusishwa na hali ya El Niño katika kipindi cha mvua za Vuli za miezi ya Oktoba hadi Desemba 2026.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo, tarehe 18 Agosti 2026, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Vuli (Oktoba–Desemba 2026), ambao unaashiria kuwepo kwa viwango vikubwa vya hali ya El Niño kwenye eneo kubwa la Bahari ya Pasifiki.

Hali hiyo inatarajiwa kuchangia ongezeko la mvua za Vuli za mwaka 2026 kuwa juu ya wastani katika baadhi ya maeneo nchini.

Wizara imesema baadhi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na hali hiyo ni pamoja na mafuriko, maporomoko ya ardhi, kujaa kwa mito na mifereji, uharibifu wa miundombinu ya barabara, reli, madaraja na majengo, pamoja na uharibifu wa mali na mazao.

Aidha, imeonya kuwa kuna uwezekano wa kuongezeka kwa hatari ya magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo salama.

Kutokana na hali hiyo, Wizara imetoa wito kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii kutoa elimu na tahadhari kwa wananchi kuhusu athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño.

Maafisa hao wametakiwa pia kuwatambua wananchi walio katika mazingira hatarishi, hususan watoto, wazee na watu wenye ulemavu, pamoja na kufanya maandalizi ya utoaji wa msaada wa kisaikolojia na kijamii kwa wananchi watakaoathiriwa na mvua hizo.

Kwa upande wa wazazi, walezi, walimu na jamii kwa ujumla, Wizara imewataka kuchukua tahadhari mapema kwa kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa, kuepuka kuvuka mito au maeneo yaliyofunikwa na maji na kutoa usaidizi kwa watu wenye ulemavu na wazee wasiojiweza.

Wananchi pia wametakiwa kutoruhusu watoto kucheza karibu na mifereji, mitaro, mito, makalavati, madaraja na maeneo ambayo maji yanapita kwa kasi.

Aidha, wametakiwa kusafisha mitaro na mifereji ya kupitisha maji ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo, pamoja na kuhakikisha wanapata maji salama ya kunywa na kupikia wakati wote.

Wizara imewataka pia wakazi wanaoishi katika maeneo ya mabondeni, karibu na mito na maeneo yenye historia ya mafuriko au maporomoko ya ardhi kuwa waangalifu zaidi na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, ikiwemo kuhama mapema endapo wataelekezwa kufanya hivyo.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Charles F. Komba, Septemba 19, 2026.