Global Publishers
September 22, 2026
0 views
0 Comments

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kufuatia kifo cha Mama Fatma Karume, mjane wa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, leo Septemba 22, 2026, imesema Rais Samia amepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mama Fatma Karume, ambaye pia alikuwa mjane wa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika salamu zake, Rais Samia ametoa pole kwa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dkt. Amani Abeid Karume, pamoja na familia, ndugu, jamaa na wananchi wote wa Zanzibar kutokana na msiba huo.
Aidha, Rais Samia amewaombea wafiwa wote subira na faraja katika kipindi hiki cha majonzi.
“Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi. Amin,” imeeleza sehemu ya salamu hizo.
Salamu hizo zimetolewa kwa niaba ya Rais Samia na Bakari S. Machumu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
