NSSF YAJIVUNIA MIAKA MITANO YA MAFANIKIO MAKUBWA

 

Na Matukio DaimaMedia 

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeeleza kurekodi mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka mitano, huku thamani ya Mfuko ikipanda kwa asilimia 125 na kufikia Sh11.41 trilioni Juni 2026, kutoka Sh5.06 trilioni mwaka 2020/21.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu na mafanikio ya Mfuko huo mbele ya Wahariri wa Vyombo vya Habari.

Amesema ukuaji huo umeenda sambamba na ongezeko la wanachama, makusanyo ya michango, thamani ya vitega uchumi na kasi ya ulipaji wa mafao kwa wastaafu na wanufaika.

Kwa mujibu wa Mshomba, thamani ya vitega uchumi vya NSSF imeongezeka kwa asilimia 108, kutoka Sh4.62 trilioni mwaka 2020/21 hadi Sh9.60 trilioni mwaka 2025/26.

“Ukuaji huu mkubwa unathibitisha kuwa NSSF ipo imara na endelevu. Ongezeko hili limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa thamani ya vitega uchumi, michango ya wanachama pamoja na mapato yatokanayo na uwekezaji katika miradi mbalimbali ya kimkakati,” amesema.

Katika kipindi hicho, NSSF imeandikisha wanachama wapya 1,486,930, huku idadi ya wanachama wachangiaji ikiongezeka kwa asilimia 130, kutoka 932,112 Juni 2021 hadi 2,144,906 Juni 2026.

Ongezeko hilo limekwenda sambamba na kuimarika kwa makusanyo ya michango, ambayo yamepanda kwa asilimia 147 kutoka Sh1.17 trilioni mwaka 2020/21 hadi Sh2.90 trilioni katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2026.

Mshomba amesema NSSF pia imefanya maboresho katika viwango vya mafao, ambapo malipo ya mafao ya mkupuo yameongezeka kutoka asilimia 25 hadi 35.

Aidha, kima cha chini cha pensheni ya kila mwezi kimeongezeka kutoka Sh100,000 hadi Sh150,000, huku viwango vya pensheni kwa baadhi ya wastaafu vikiongezeka kati ya asilimia mbili na 20.

Malipo ya mafao kwa wastaafu na wanufaika yameongezeka kutoka Sh594.33 bilioni mwaka 2020/21 hadi Sh1.16 trilioni mwaka 2025/26.

Mshomba amesema NSSF pia imepunguza muda wa kushughulikia madai, ambapo wastani wa siku za kulipa madai yaliyokamilika umeshuka kutoka siku 63 mwaka 2021 hadi siku 19 Juni 2026.

Amesema asilimia 99 ya madai ya mafao yaliyofunguliwa yamelipwa ndani ya muda wa kisheria wa siku 60.

Katika uwekezaji, Mshomba amesema miradi kadhaa iliyokuwa imesimama, ikiwamo nyumba za makazi za Dungu, Toangoma, Mtoni Kijichi na Jengo la Mzizima, ilirejelewa mwaka 2023 baada ya kufanyika kwa ukaguzi maalum.

Miradi hiyo inatarajiwa kukamilika kati ya Desemba 2026 na Machi 2027.

Kuhusu Kiwanda cha Sukari Mkulazi, amesema kimezalisha tani 45,594 za sukari ya majumbani, kikiingiza mapato ya Sh107.90 bilioni na kupata faida ya Sh4.56 bilioni katika mwaka wa fedha 2025/26.

Akizungumzia mipango ijayo, Mshomba amesema kupitia Mpango Mkakati wa Nane wa NSSF wa 2026–2031, Mfuko unalenga kuongeza thamani yake hadi Sh24.75 trilioni na kuandikisha wanachama wapya milioni 5.8 ifikapo Juni 2031.

Awali, mwakilishi wa Msajili wa Hazina (TR), Sabato Kosuri, amesema mkutano huo ni sehemu ya mkakati wa Ofisi ya Msajili wa Hazina wa kuziwezesha taasisi za umma kukutana na wahariri na kueleza shughuli zake kwa Watanzania.

“Hii ni awamu ya pili ya mikutano hii na NSSF inakuwa taasisi ya kwanza kukutana na wahariri. Zipo taasisi zaidi ya 400 ambazo tutazifanyia mikutano kama hii ili kuwapa fursa Watanzania kujua taasisi hizi za umma zinatendaje kazi zake,” amesema Kosuri.