Mashabiki Kukutana Uso Kwa Uso na Wachezaji wa Taifa Stars

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limezindua tukio la ‘Mashabiki Open Day’, litakalowapa mashabiki na wadau wa soka nchini fursa ya kukutana kwa karibu na wachezaji pamoja na benchi la ufundi la Timu ya Taifa, Taifa Stars.

Tukio hilo linatarajiwa kufanyika kesho Jumatano, Septemba 23, 2026, kuanzia saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa TFF, hatua hiyo inalenga kuwawezesha mashabiki kushuhudia kwa karibu mazoezi ya Taifa Stars, huku ikiwa sehemu ya maandalizi ya timu kuelekea michezo ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 pamoja na mchezo wa kirafiki.

Mashabiki watakaohudhuria watapata fursa ya kuona maandalizi ya timu kwa karibu, huku pia wakipewa nafasi ya kupiga picha na kujipiga selfie pamoja na wachezaji na benchi la ufundi.

TFF imeeleza kuwa tukio hilo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uhusiano kati ya Taifa Stars na mashabiki wake, pamoja na kuongeza morali kwa wachezaji na benchi la ufundi kuelekea michezo ijayo.

Stori na Peter Jinanai| GPL -TUDACO

The post Mashabiki Kukutana Uso Kwa Uso na Wachezaji wa Taifa Stars appeared first on Global Publishers.