
Vyombo vikubwa vya televisheni nchini Marekani vimesitisha kwa pamoja huduma ya kurusha picha za shughuli za Rais Donald Trump baada ya utawala wake kumzuia mtandao wa CNN kushiriki katika mfumo wa pamoja wa kuripoti shughuli za rais unaojulikana kama White House TV Pool.
Mfumo huo unahusisha ABC, CBS, CNN, Fox News na NBC, ambazo hubadilishana zamu ya kurekodi na kusambaza picha za shughuli za rais kwa vyombo vingine vya habari. CNN ilikuwa imepangwa kuwa mwakilishi wa mfumo huo Jumatatu, Septemba 21, lakini haikuruhusiwa kutekeleza jukumu hilo.
Baada ya CNN kuzuiwa, ABC, CBS, Fox News na NBC zilikataa kutuma mtandao mwingine kuchukua nafasi yake, hatua iliyosababisha kusitishwa kwa muda kwa huduma hiyo ya pamoja ya televisheni. Mitandao hiyo ilisema umma una maslahi ya kupata taarifa sahihi na huru kuhusu shughuli za serikali.
Hatua hiyo iliathiri pia matangazo ya baadhi ya shughuli za Trump. Katika tukio la uzinduzi wa helipad mpya katika Ikulu ya White House, watazamaji waliweza kuona picha za rais lakini bila sauti ya kawaida kutoka kwenye mfumo wa TV Pool.
CNN, MS NOW NA POLITICO ZAFUNGUA KESI
Mzozo huo umeibuka baada ya utawala wa Trump kuzuia waandishi wa CNN, MS NOW na Politico kuingia katika eneo la White House na kuondoa vitambulisho vyao vya waandishi.
Vyombo hivyo vitatu vimefungua kesi katika mahakama ya shirikisho dhidi ya utawala wa Trump, vikidai kuwa hatua hiyo inakiuka haki zao chini ya Marekebisho ya Kwanza ya Katiba ya Marekani, yanayolinda uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari, pamoja na haki za kisheria zinazohusiana na mchakato unaostahili.
Trump ametetea uamuzi huo, akisema vyombo hivyo vimekuwa vikitoa kile anachokiita taarifa za uongo kuhusu yeye na utawala wake. Utawala wake umesema suala hilo linahusu upatikanaji wa White House na kwamba vyombo vya habari havina haki ya kudumu ya kupata nafasi ndani ya Ikulu.
WHITE HOUSE YAZINDUA “TRUMP TV”
Wakati mvutano huo ukiendelea, White House imezindua kituo cha mtandaoni kinachoitwa “TRUMP TV: The Essentials Station.” Kituo hicho kilizinduliwa Septemba 21, 2026, na kinatoa video na maudhui yanayohusiana na Rais Trump na shughuli za utawala wake. (
Taarifa zilizochapishwa kuhusu kituo hicho zinaeleza kuwa kinatoa matangazo ya shughuli za rais, hotuba, taarifa za utawala pamoja na video za matukio mbalimbali ya Trump, huku huduma hiyo ikipatikana mtandaoni.
Uzinduzi wa TRUMP TV umefanyika siku hiyo hiyo ambayo mitandao mikubwa ya televisheni ilisimamisha huduma ya pamoja ya TV Pool, hivyo kuongeza mjadala kuhusu namna shughuli za rais zinavyopaswa kuripotiwa na vyombo huru vya habari.
Kwa sasa, mzozo huo unaendelea pia mahakamani, huku CNN, MS NOW na Politico zikiiomba mahakama kurejesha upatikanaji wao wa White House wakati kesi yao ikiendelea.
Stori na Ashura Karimu | GPL -TUDACO
