Idris Sultan Kuiwakilisha Tanzania Kwenye Tuzo Kubwa Afrika Novemba 2026

Global Publishers
September 19, 2026
0 views
0 Comments

MTANZANIA Idris Sultan amepewa nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika moja ya majukwaa makubwa yanayotambua na kuenzi vijana wenye mafanikio barani Afrika.

Idris, ambaye ni mwigizaji, mchekeshaji na mtayarishaji, ametangazwa kuwa mmoja wa waandaji wa The Future Awards Africa (TFAA) 2026, hafla kubwa inayotarajiwa kufanyika mwezi Novemba 2026 katika Balmoral Events Centre, Lagos, Nigeria.

Idris atakuwa miongoni mwa waandaji watano kutoka nchi mbalimbali za Afrika, akiiwakilisha Tanzania katika jukwaa hilo pamoja na wawakilishi kutoka Nigeria, Kenya, Malawi na Botswana.

Waandaji wengine waliotangazwa ni mwigizaji wa Nigeria, Genoveva Umeh; mtangazaji wa Malawi, Priscilla Kayira; mtangazaji na mtayarishaji kutoka Botswana, Resego Motlhokathari; pamoja na mwanahabari na mwigizaji wa Kenya, Claudia Naisibwa.

Kwa mwaka huu, TFAA inaadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, huku waandaaji wakitumia mfumo wa kipekee wa kuwaleta pamoja waandaji watano kutoka mataifa matano tofauti ya Afrika kwenye jukwaa moja.

Kaulimbiu ya TFAA 2026 ni “Celebrating the Redefiners: Africa’s AI Generation,” inayolenga kuangazia kizazi kipya cha vijana wa Afrika wanaotumia teknolojia, ubunifu na mawazo mapya kubadilisha sekta mbalimbali.

Nafasi hiyo inampa Idris Sultan fursa ya kuendelea kuonekana katika jukwaa la kimataifa na kushiriki katika tukio linalolenga kutambua mchango na mafanikio ya vijana barani Afrika.

Stori na Razaku Ramadhan | GPL – TUDACO

Tuchel Awaonya Alexander-Arnold na Palmer Baada ya Kuwaita Tena England

Global Publishers
September 19, 2026
0 views
0 Comments

KOCHA wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel, amewajumuisha tena Trent Alexander-Arnold na Cole Palmer katika kikosi cha

Alexander-Arnold, anayekipiga Real Madrid, amerejea kwenye kikosi cha England kwa mara ya kwanza tangu Juni 2025. Beki huyo alikosa nafasi katika kikosi kilichoshiriki Kombe la Dunia, lakini kiwango kizuri alichoanza nacho msimu huu katika klabu yake kimemsaidia kurejea kwenye timu ya taifa.

Kwa upande wa Palmer, mchezaji huyo wa Chelsea pia ameitwa tena baada ya kukosa Kombe la Dunia kutokana na changamoto za kiwango na utimamu wa mwili msimu uliopita.

Palmer ameanza msimu mpya kwa kiwango kizuri, akiwa amefunga mabao manne na kutoa pasi mbili za mabao katika michezo sita.

Akizungumza kuhusu kurejea kwa wachezaji hao, Tuchel amesisitiza kuwa hakuna anayehakikishiwa nafasi ya kudumu kwenye kikosi, akiwataka kutumia fursa hiyo kuthibitisha uwezo wao.

Kwa Alexander-Arnold, kocha huyo amesema ushindani katika nafasi ya beki wa kulia bado ni mkubwa na mchezaji huyo atalazimika kupigania nafasi yake.

“Anapaswa kupigania nafasi yake,” Tuchel amesema, akisisitiza umuhimu wa kila mchezaji kuonyesha kiwango kinachohitajika ili kuendelea kuwa sehemu ya mipango yake.

England inajiandaa kuanza kampeni yake ya UEFA Nations League kwa mchezo dhidi ya mabingwa wa dunia Spain utakaochezwa katika Uwanja wa Wembley Septemba 26.

Baada ya mchezo huo, England itakutana na Czech Republic na Croatia katika michezo inayofuata, huku Tuchel akitarajiwa kutumia mechi hizo kutathmini kikosi chake na kuandaa timu yenye ushindani.

Stori na Erick Elibariki | GPL -TUDACO

Dereva Bodaboda Afungwa Miaka 30 Jela kwa Kumbaka Mwanafunzi Kigoma

Global Publishers
September 19, 2026
0 views
0 Comments

UVINZA, KIGOMA — Mahakama ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela, Rajabu Uhuru (36), dereva wa bodaboda na mkazi wa Kijiji cha Ilalangulu, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 13.

Hukumu hiyo imetolewa Septemba 17, 2026 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Uvinza, Misana Majula.

Katika hukumu hiyo, Hakimu Majula amesema Mahakama imejiridhisha bila kuacha shaka yoyote kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo, kutokana na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, tukio hilo lilitokea Juni 12, 2026, majira ya saa 3 usiku, katika eneo la Kigulwe, Kijiji cha Ilalangulu, Kata ya Mtego wa Noti, Tarafa ya Nguruka, Wilaya ya Uvinza.

Mahakama ilielezwa kuwa baada ya kutenda kosa hilo, mshtakiwa alikimbilia jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujificha na kukwepa mkono wa sheria.

Hata hivyo, alikamatwa baada ya Jeshi la Polisi kufanya msako uliomwezesha kunaswa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Majula amesema adhabu hiyo ni fundisho kwa wengine na sehemu ya juhudi za Serikali katika kulinda haki na usalama wa watoto pamoja na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Mahakama imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu wanaokiuka haki na usalama wa watoto.

Stori na Mwajabu Abdallah | GPL -TUDACO

Niffer Afunguka Kuhusu Hali Ya Kiredio “Hayuko Sawa Kwa Sasa”

Global Publishers
September 19, 2026
0 views
0 Comments

Baada ya shabiki kumuomba mfanyabiashara maarufu nchini, Jennifer Bilikwija, anayefahamika zaidi kwa jina la Niffer, atafute namna ya kuwasiliana na mtangazaji na mtayarishaji wa maudhui, Vicent Njau, maarufu kama Kiredio, ili arejee kupost mitandaoni kama alivyokuwa akifanya awali, Niffer ametoa ufafanuzi kuhusu hali yake.

Kupitia Instagram, Niffer alijibu ombi hilo kwa kusema:

“Hayuko sawa kwa sasa but he will be back! Yanini nifiche? Muombeeni ❤️”

Kauli hiyo imeibua mjadala miongoni mwa mashabiki wanaofuatilia kutokuwepo kwa Kiredio kwenye mitandao ya kijamii, huku Niffer akiwaomba kumuombea na kusubiri kurejea kwake.

Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wamehusisha kutokuwepo kwa Kiredio mitandaoni na tetesi za kuachana na aliyekuwa mpenzi wake, Vee Dollarz.

Mpaka sasa, taarifa hizo za kuhusisha kutokuwepo kwake mitandaoni na suala hilo zimeendelea kuwa tetesi, huku Niffer akieleza tu kwamba Kiredio “hayuko sawa kwa sasa” bila kufafanua zaidi kuhusu kinachoendelea.

SGR na JKCI Waanzisha Ushirikiano wa Kutoa Huduma Za Afya Kwa Abiria

Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) zimeingia katika ushirikiano wa kimkakati wa kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi, hatua itakayoanza kwa utoaji wa huduma za uchunguzi na vipimo vya afya ya moyo bila malipo kwa abiria wanaosafiri kwa treni ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) kati ya Dar es Salaam na Dodoma.

Kupitia ushirikiano huo, huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza zitatolewa ndani ya treni za SGR kuanzia Septemba 21 hadi 27, 2026, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Afya ya Moyo kuelekea Siku ya Moyo Duniani inayoadhimishwa Septemba 29 kila mwaka.

Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 18, 2026, katika Stesheni ya SGR jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa JKCI, Dkt. Peter Kissenge, alisema wataalamu na mabingwa wa afya watasafiri ndani ya treni hizo kutoa huduma za uchunguzi, ushauri na elimu ya afya kwa abiria watakaohitaji huduma hizo.

Alisema vipimo vitakavyotolewa ni pamoja na Echo, ECG, vipimo vya sukari na mafuta kwenye damu, ambavyo kwa kawaida vina gharama kubwa vinapotolewa hospitalini.

“Vipimo hivi vyote vinaweza kugharimu zaidi ya shilingi 500,000 vinapofanyika hospitalini, lakini katika kipindi hiki cha Wiki ya Afya ya Moyo vitatolewa bila malipo kwa abiria wote watakaosafiri kwa SGR,” alisema Dkt. Kissenge.

Aliongeza kuwa mpango huo unalenga kuhamasisha wananchi kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini mapema magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza ambayo yanaendelea kuongezeka nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Masanja Machibya, alisema ushirikiano huo unaashiria mwanzo wa hatua mpya ya kuunganisha huduma za usafiri na afya kwa manufaa ya wananchi.

Alisema TRC inaendelea na maandalizi ya mradi wa mabehewa maalumu ya matibabu yatakayokuwa na vifaa vya kisasa pamoja na vitanda kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa mahututi na wanaopewa rufaa kutoka mikoani kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa haraka na usalama zaidi.

“Mabehewa haya yatasaidia kupunguza muda wa usafirishaji wa wagonjwa kutoka mikoa mbalimbali, hususan Dodoma na Morogoro, na kuwafikisha kwa haraka zaidi katika vituo vya matibabu vya rufaa ikilinganishwa na usafiri wa barabarani,” alisema Machibya.

Alibainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza ndani ya miezi sita ijayo, hatua inayotarajiwa kuimarisha huduma za afya na mfumo wa rufaa nchini.

Aidha, wananchi na abiria wote watakaosafiri kwa SGR katika kipindi hicho wamehimizwa kutumia fursa hiyo ya kupata uchunguzi wa afya ya moyo na ushauri wa kitaalamu bila gharama, ili kubaini mapema changamoto za kiafya na kuchukua hatua stahiki za matibabu.

Cardi B Avunja Ukimya Kuhusu Uvumi wa Kurudiana na Offset

Global Publishers
September 19, 2026
0 views
0 Comments

RAPA kutoka Marekani, Cardi B, amevunja ukimya kuhusu uvumi unaodai kuwa anajaribu kurejesha uhusiano wake wa kimapenzi na aliyekuwa mume wake, Offset.

Uvumi huo uliibuka Septemba 16, 2026, baada ya mwanamitindo Melanie Jayda, ambaye amewahi kuhusishwa kimapenzi na Offset, kudaiwa kuchapisha ujumbe kwenye mtandao wa X uliosababisha mjadala kuhusu uhusiano wa wawili hao.

Cardi B alijibu madai hayo kupitia chapisho ambalo baadaye lilifutwa, akisisitiza kwamba hakuna ushahidi wa yeye kujaribu kumfuatilia au kurejesha uhusiano na Offset.

“Kamwe maishani mwako, kamwe katika maisha haya… mnaweza kupitia jumbe za simu za jamaa huyo (Offset) au chochote kile… lakini kamwe hutaona nikifanya hivyo. Weka hata mpelelezi binafsi anifuatilie, naapa kwa jina la Yesu, hutapata ushahidi wowote!” aliandika Cardi B.

Kauli hiyo imekuja wakati ambapo historia ya uhusiano wa Cardi B na Offset imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu na mashabiki wao.

Julai 2024, Cardi B aliwasilisha ombi la talaka dhidi ya Offset kwa mara ya pili baada ya kuwa pamoja kwa miaka kadhaa.

Wawili hao wana watoto watatu, Kulture, Blossom na Wave, huku mchakato wa talaka yao ukiendelea kukumbwa na changamoto za kisheria.

MAKAMU WA RAIS MHE. NDEJEMBI AAGIZA DAMPO LA PUGU LIBORESHWE, KERO ZA WANANCHI ZITATULIWE*

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Halmashauri zake kuhakikisha hali ya Dampo la Pugu inaboreshwa, huku akielekeza maeneo ya makazi yanayozunguka dampo hilo kupuliziwa dawa ili kuwalinda wananchi dhidi ya wadudu na kupunguza hatari ya magonjwa, hususan katika kipindi cha mvua.

 

Makamu wa Rais ametoa maelekezo hayo leo, Septemba 18, 2026, alipofanya ziara katika Dampo la Pugu linalotumika kukusanya taka za Mkoa wa Dar es Salaam ili kujionea hali halisi ya eneo hilo na kusikiliza kero za wananchi wanaoishi maeneo ya jirani.

 

Aidha, ameelekeza kuandaliwa kwa mpango kazi wa pamoja utakaoainisha hatua za haraka na za muda mrefu za kukabiliana na changamoto za uendeshaji wa Dampo la Pugu pamoja na kero zinazowakabili wananchi wanaoishi katika maeneo yanayolizunguka, ikiwemo kutopuliziwa dawa za kuua wadudu.

 

 

Akiwa katika dampo hilo, Mhe. Ndejembi ameonesha kutoridhishwa na kutofautiana kwa takwimu kuhusu kiasi cha taka zinazokusanywa na kupelekwa katika Dampo la Pugu kila siku kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam.

 

Kutokana na hali hiyo, amezitaka mamlaka zote zinazohusika kukaa pamoja, kuhakiki na kuweka takwimu sahihi zitakazokuwa msingi wa kupanga na kutekeleza hatua madhubuti za kuboresha usimamizi wa taka jijini Dar es Salaam.

 

“Hatuwezi kutatua changamoto za eneo hili bila kuwa na taarifa na takwimu sahihi. Hawa wananchi mnaowaona wamechoka na stori; wanataka kuona kazi,” alisisitiza Makamu wa Rais.

 

Makamu wa Rais amesema wananchi wanatarajia kuona matokeo ya moja kwa moja ya hatua zinazochukuliwa na Serikali, hivyo amewataka viongozi na taasisi husika kuharakisha utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha kero za wananchi zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

 

Makamu wa Rais amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Serikali sikivu inayojali maslahi ya Watanzania na itahakikisha changamoto za watanzania zinatatuliwa kwa wakati.

 

Katika hatua nyingine, Mhe. Ndejembi ametoa siku saba kwa mawaziri wanaohusika na TAMISEMI, Maliasili na Utalii pamoja na Ardhi kufika katika maeneo husika na kutatua mgogoro wa muda mrefu unaohusu mipaka ya kiutawala na mpaka wa Msitu wa Kazimzumbwi, ambao umekuwa ukiwaathiri wananchi wa Pugu na maeneo ya jirani.

 

Changamoto hiyo imesababisha baadhi ya wananchi kutokuwa na uhakika kuhusu maeneo yao ya makazi kutokana na kutofahamika kwa mipaka ya kiutawala pamoja na mpaka wa Msitu wa Kazimzumbwi.

 

Makamu wa Rais ameelekeza mawaziri hao kufika wenyewe katika maeneo yenye mgogoro na, kwa kushirikiana na wananchi pamoja na wataalamu, kusoma ramani na matangazo rasmi ya Serikali (GN) ili kuweka wazi mipaka na kuwawezesha wananchi kutambua kwa uhakika maeneo yao.

 

“Waheshimiwa Mawaziri, nataka mfike wenyewe kwenye eneo hili kutambua GN za mikoa na mipaka ya Msitu wa Kazimzumbwi, kwani hii imekuwa kero ya muda mrefu. Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anataka tutatue kero za wananchi; kwa hiyo naelekeza hili mkalifanyie kazi ndani ya siku saba liwe limeisha,” alisema Mhe. Ndejembi.

 

Awali, wananchi wa maeneo ya Mstafa, Viwege na Kinyamwezi walitumia fursa ya ziara hiyo kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili, zikiwemo athari zinazotokana na uwepo wa dampo, kutopuliziwa dawa za kuua wadudu katika maeneo yao, ukosefu wa maji kwa muda mrefu pamoja na migogoro ya ardhi.

 

 

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, ameahidi kusimamia kikamilifu utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa na Makamu wa Rais.

 

Miongoni mwa hatua zitakazotekelezwa ni kuboresha usimamizi wa Dampo la Pugu, kuweka utaratibu wa kila Halmashauri kutenga bajeti mahsusi kwa ajili ya uendeshaji wa dampo hilo, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa vifaa na kuboresha miundombinu muhimu ili shughuli za dampo ziendeshwe kwa kuzingatia matakwa ya kimazingira na kiafya.

 

Hatua hizo zinalenga kuimarisha usimamizi wa taka katika Mkoa wa Dar es Salaam na kuhakikisha changamoto za mazingira, afya na mipaka ya ardhi zinazowakabili wananchi wa Pugu na maeneo ya jirani zinapatiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu.

 

 

Katika ziara hiyo, Makamu wa Rais ameambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI Mhe. Prof Riziki Shemdoe, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Masauni, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, Wakuu wa Wilaya pamoja na viongozi kutoka Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam.

 

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

18 Septemba 2026

Dar es Salaam.

Ndejembi Aagiza Dampo la Pugu Liboreshwe, Kero za Wananchi Zitatuliwe – Picha

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Deogratius Ndejembi akiongea na wananchi katika Dampo la Pugu.

DAR ES SALAAM — Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na halmashauri zake kuhakikisha hali ya Dampo la Pugu inaboreshwa na kero za wananchi wanaoishi maeneo ya jirani zinapatiwa ufumbuzi.

Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo leo, Septemba 18, 2026, alipofanya ziara katika Dampo la Pugu linalotumika kukusanya taka za Mkoa wa Dar es Salaam, kwa lengo la kujionea hali halisi ya eneo hilo na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi wanaoishi jirani na dampo hilo.

Makamu wa Rais ameelekeza maeneo ya makazi yanayozunguka Dampo la Pugu kupuliziwa dawa za kuua wadudu, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuwalinda wananchi dhidi ya wadudu na kupunguza hatari ya magonjwa, hususan wakati wa kipindi cha mvua.

Aidha, ameagiza kuandaliwa kwa mpango kazi wa pamoja utakaobainisha hatua za haraka na za muda mrefu za kukabiliana na changamoto za uendeshaji wa dampo hilo pamoja na kero zinazowakabili wananchi wanaoishi maeneo yanayolizunguka.

Akiwa katika eneo hilo, Mhe. Ndejembi ameonesha kutoridhishwa na kutofautiana kwa takwimu zinazotolewa kuhusu kiasi cha taka kinachokusanywa na kupelekwa Dampo la Pugu kila siku kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.

Kutokana na hali hiyo, amezitaka mamlaka zote zinazohusika kukaa pamoja, kuhakiki na kuweka takwimu sahihi zitakazotumika kama msingi wa kupanga na kutekeleza hatua madhubuti za kuboresha usimamizi wa taka jijini.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Deogratius Ndejembi akiwa na wananchi mbalimbali wanaofanya shughuli za biashara na kutenganisha taka katika Dampo la kukusanyia taka la mkoa wa Dar es Salaam, lililopo Pugu Kinyamwezi wakati wa ziara maalum aliyoifanya leo tarehe 18 Septemba 2026.

“Hatuwezi kutatua changamoto za eneo hili bila kuwa na taarifa na takwimu sahihi. Hawa wananchi mnaowaona wamechoka na stori; wanataka kuona kazi,” amesisitiza Makamu wa Rais.

Amesema wananchi wanatarajia kuona matokeo ya moja kwa moja kutokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali, hivyo amewataka viongozi na taasisi husika kuharakisha utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu kutatua kero za wananchi.

Mhe. Ndejembi amesisitiza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Serikali inayosikiliza wananchi na inayojali maslahi yao, akiahidi kuwa changamoto zinazowakabili zitaendelea kushughulikiwa kwa wakati.

Ndejembi Aagiza Dampo la Pugu Liboreshwe, Kero za Wananchi Zitatuliwe

DAR ES SALAAM — Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na halmashauri zake kuhakikisha hali ya Dampo la Pugu inaboreshwa na kero za wananchi wanaoishi maeneo ya jirani zinapatiwa ufumbuzi.

Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo leo, Septemba 18, 2026, alipofanya ziara katika Dampo la Pugu linalotumika kukusanya taka za Mkoa wa Dar es Salaam, kwa lengo la kujionea hali halisi ya eneo hilo na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi wanaoishi jirani na dampo hilo.

Makamu wa Rais ameelekeza maeneo ya makazi yanayozunguka Dampo la Pugu kupuliziwa dawa za kuua wadudu, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuwalinda wananchi dhidi ya wadudu na kupunguza hatari ya magonjwa, hususan wakati wa kipindi cha mvua.

Aidha, ameagiza kuandaliwa kwa mpango kazi wa pamoja utakaobainisha hatua za haraka na za muda mrefu za kukabiliana na changamoto za uendeshaji wa dampo hilo pamoja na kero zinazowakabili wananchi wanaoishi maeneo yanayolizunguka.

Akiwa katika eneo hilo, Mhe. Ndejembi ameonesha kutoridhishwa na kutofautiana kwa takwimu zinazotolewa kuhusu kiasi cha taka kinachokusanywa na kupelekwa Dampo la Pugu kila siku kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.

Kutokana na hali hiyo, amezitaka mamlaka zote zinazohusika kukaa pamoja, kuhakiki na kuweka takwimu sahihi zitakazotumika kama msingi wa kupanga na kutekeleza hatua madhubuti za kuboresha usimamizi wa taka jijini.

“Hatuwezi kutatua changamoto za eneo hili bila kuwa na taarifa na takwimu sahihi. Hawa wananchi mnaowaona wamechoka na stori; wanataka kuona kazi,” amesisitiza Makamu wa Rais.

Amesema wananchi wanatarajia kuona matokeo ya moja kwa moja kutokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali, hivyo amewataka viongozi na taasisi husika kuharakisha utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu kutatua kero za wananchi.

Mhe. Ndejembi amesisitiza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Serikali inayosikiliza wananchi na inayojali maslahi yao, akiahidi kuwa changamoto zinazowakabili zitaendelea kushughulikiwa kwa wakati.