SHAKA: JESHI LA AKIBA LIWE NGUZO YA ULINZI NA MAENDELEO YA JAMII

 

Matukio Daima Media, Kilosa.

Wahitimu wa mafunzo ya Jeshi la Akiba wametakiwa kutotumia ujuzi walioupata kwa masuala ya kiusalama pekee, bali pia kuutumia kuimarisha ulinzi wa rasilimali za umma, kusimamia mapato ya halmashauri na kuhakikisha maeneo yao yanakuwa salama.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, wakati akifunga rasmi mafunzo ya Jeshi la Akiba Kundi la 21/26 katika uwanja wa Mpira wa Kilosa Town, yaliyodumu kwa miezi minne.

Shaka amesema usalama wa jamii unaanzia katika ngazi ya kijiji na kata, hivyo wahitimu hao wanapaswa kushirikiana na Polisi Kata na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha hakuna vitendo vinavyohatarisha amani, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda minada, masoko na mapato ya umma.

Amesema wajibu wa kulinda nchi si wa vyombo vya dola pekee, bali ni jukumu la kila raia kwa mujibu wa Ibara ya 27 ya Katiba, hivyo wahitimu hao wanapaswa kuwa mfano wa uzalendo, uaminifu na nidhamu wanaporejea katika kata na vijiji vyao.

Katika hatua nyingine, amewataka kuwa mstari wa mbele kupinga taarifa za uongo na uchochezi kwenye mitandao ya kijamii, akiwakumbusha kuwa jukumu lao ni kulinda umoja na mshikamano wa taifa badala ya kushiriki vitendo vinavyoweza kuvuruga amani.

Akifunga mafunzo hayo, Shaka amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha bajeti ya ulinzi na uwekezaji katika mafunzo, akieleza kuwa amani ndiyo msingi wa uzalishaji, uwekezaji, elimu na maendeleo ya wananchi.

Aidha, amewaonya wahitimu hao dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya na maambukizi ya VVU, akisisitiza kuwa wanapaswa kutambua kuwa afya zao ni sehemu muhimu ya uwezo wao wa kulitumikia taifa.